Serikali yaifutia TANESCO deni la Tsh. Trilioni 2.4

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,379
8,123
Kwa kuwa bei ya umeme haiendani na uhalisia wa mauzo, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limesema halipati mtiririko mzuri wa mapato, hivyo kushindwa kulipa madeni yake ya muda mfupi, hali inayowakimbiza wawekezaji.

Hali hii inatokana na ukweli kwamba mara nyingi, Serikali huwa inakopa kisha kuipa Tanesco fedha hizo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi yake.

Ili kuondokana na utegemezi huu na kuipa Tanesco uwezo na uhuru mkubwa wa kuzalisha, kusambaza na kusafirisha umeme, shirika hilo limeiomba Serikali kuifutia madeni yake ili iweze kukopesheka na wawekezaji wa muda mfupi.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Maharage Chande, mahitaji ya umeme yanaongezeka kwa asilimia 10 kila mwaka, tofauti na kukua kwa asilimia sita kulikokuwapo kabla ya mwaka 2020.

Chande alisema kasi ya kukua kwa mahitaji ya umeme, imetokana na ongezeko la vijana wanaohamia mjini kusaka ajira na viwanda vinavyozidi kujengwa kila uchao.

“Kwa sasa Tanzania ina uwezo uliosimikwa wa kuzalisha megawati 3,815. Malengo yetu mpaka mwaka 2025 ni kuzalisha megawati 5,000 na megawati 18,000 mwaka 2044. Kufanikisha haya yote Shirika linahitaji fedha iwe za mkopo au kwa ubia na sekta binafsi (PPP),” alisema Chande.

Mkurugenzi huyo alisema mwenendo wa mapato na matumizi ya shirika, hauko vizuri kuliwezesha kukopa kwa kuwa kuna wakati hushindwa kulipa makandarasi na wazabuni waliolihudumia kwa wakati.

Hata hivyo, alisema kuanzia mwakani, Tanesco inatarajia kuwa na mapato chanya Sh800 bilioni zitakazoongezeka mpaka Sh1 trilioni mwaka 2025/26.

Uwiano wa madeni na mali ya shirika, Chande alisema ni asilimia 80 ambao ni mkubwa kuliko inavyotakiwa na iwapo Serikali italifutia madeni yake kwa kuyaingiza kwenye hisa inazomiliki, taarifa zake za fedha zitasomeka vizuri kuliko ilivyo sasa, hivyo kuliwezesha kutanua shughuli zake kwa urahisi.

“Hali ya mtiririko wa mapato inakatisha tamaa wawekezaji na hata wakopeshaji kwa hofu kwamba Tanesco itashindwa kuwalipa kutokana na vihatarishi vilivyopo,” alisema Chande.

Gazeti hili, lilimtafuta Waziri wa Nishati, Januari Makamba kuhusu hoja hiyo ya Tanesco, alisema: “Serikali tayari imekwisha kulifuta au kulichukua deni hilo zaidi ya Sh 2.4 trilioni.”

Waziri huyo alisema si kwamba Serikali itakuwa na mzigo mkubwa, akitolea mfano, Serikali hukopa fedha Benki ya Dunia kisha kuipa Tanesco fedha kama za kusambaza umeme. “Sasa hilo deni linakuwa katika vitabu vya deni la Serikali na deni hilo hilo linakuwa katika vitabu vya Tanesco, yaani deni moja linakuwa katika vitabu viwili,” alisema January.

“Kwa maana hiyo kwa uamuzi huu wa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, unaifanya Tanesco kuweza kujiimarisha, kukopesheka kwani vitabu vyake viko safi.” Msemaji wa Kisekta wa Wizara ya Nishati, Issihaka Mchinjita alisema ni hatua nzuri kwa Serikali kufuta deni hilo, kwa kuwa baadhi ya wadau, wakiwamo wanasiasa walilizungumzia suala hilo, lakini sasa limewezekana.

“Hatua hii itasaidia Tanesco kujiendesha kwa ufanisi, kikubwa shirika hili lijipange namna ya kutekeleza majukumu yake bila kuzalisha hasara. Inabidi wajijengee uwezo wa namna bora ya kukusanya madeni ambapo ilikuwa miongoni mwa changamoto,” alisema Mchinjita.

“Changamoto nyingine, miundombinu ya usafirishaji wa umeme sio rafiki, ndiyo maana mvua ikinyesha umeme unakatika, sasa Tanesco ijipange namna ya kukabiliana na suala hili. Tanesco wahakikishe hawazalishi madeni makubwa, maana sasa wamefutiwa deni na Serikali,” alisema Mchinjita.

Deni lililopo

Mpaka Juni 2022 deni la mikopo iliyoiva ya Serikali kwa Tanesco lilikuwa Sh2.4 trilioni, zinazojumuisha fedha zilizokopwa pamoja na riba.

Kwa mapendekezo ya Tanesco, Chande alisema deni hili linaweza kubadilishwa kuwa mtaji kwa hatua mbili. Kwanza ni Serikali kutumia Sh1.27 trilioni kulipia hisa zake zaidi ya bilioni 63.43 ambazo haijalipia.

“Pili ni Tanesco kuongeza hisa (right issue) za thamani ya deni lililobaki, kiasi cha Sh1.15 trilioni.

“Kwa kufanya hivyo, uwiano wa mali na madeni utafika 27:73 kutoka 20:80 na ule wa mtaji na madeni utaimarika mpaka 25:75 wa sasa. Mabadiliko haya hayataihitaji Serikali kutoa hela wala kuongeza deni bali ni mabadiliko ya kihasibu katika kitabu cha mizania cha Tanesco,” alisema.

Mkazi wa Mingoi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, alisema, “nilikuwa sijui kama Tanesco wanatuwekea gharama za riba na deni la Serikali kwenye umeme tunaoutumia. Ndio maana bei ya Luku inakuwa haieleweki.

“Kuna kipindi unapata uniti nyingi na wakati mwingine zinapungua kwa hela ileile unayolipa. Umeme ni kitu muhimu, Serikali iangalie uwezekano wa kuipunguzia mzigo Tanesco ili kumpa unafuu mwananchi.”

MWANANCHI
 
Aisee haya mzigo anapewa mwananchi alipe Hilo deni Kwa miaka yote tozoooooo,ATM,Kodi kila eneo ,ni hatari
 
Kila siku Makamba team mnabadili sababu na visingizio tu.

Mlianza na kusema Magufuli alichakaza mitambo.
Mkaja na wahindi kwa mkataba fisidi.

Makamba akapangua kuanzia Bodi ya Tanesco mpaka uongozi wa Tanesco woote!

Mkaja na ukame,Makamba tena akaruka na helkopta kukagua mito.

Mkarudi na kuondoa bei za REA alizoacha Magufuli .

Sasa visingizio vimeisha,mnageukia kwenye Madeni?
 
Back
Top Bottom