Sekta ya elimu nchini China yapata maendeleo makubwa

ldleo

JF-Expert Member
Jan 9, 2010
1,010
1,036
VCG41483327542.jpg


Mkutano mkuu wa 20 wa Chama cha Kikomunisti cha China CPC utafanyika tarehe 16 Oktoba hapa Beijing. Lakini kabla ya kufanyika kwa Mkutano huo, ikiwa sasa watu wa China wanakuwa katika mapumziko ya siku saba ya kusherehekea miaka 73 ya kuzaliwa kwa taifa la China, siku ya taifa inayoangukia tarehe mosi, Oktoba, tuangazie mafanikio ambayo China imeyapata katika miaka hii 10 tangu Xi Jinping achaguliwe kuwa katibu mkuu wa Kamati Kuu ya CPC, leo hii tukiangazia suala la ujenzi wa miundombinu. Leo tutaangazia suala zima la maendeleo makubwa ambayo China imepata katika sekta ya elimu.

Kuna kauli ambayo ni maarufu sana kwa watu wengi, nayo ni kwamba, elimu ni msingi wa maisha. Ni kweli kwamba, wengi wetu tumesikia kauli hiyo, pamoja na ile inayosema, urithi mkubwa ambao mtu anaweza kumwachia mtoto wake ni elimu, na elimu, haina mwisho. Elimu pia ni moja ya misingi muhimu ya maendeleo ya taifa lolote duniani, bila ya elimu, si rahisi kupata maendeleo ambayo ni endelevu.

China, ikiwa nchi ya pili kwa ukubwa wa uchumi duniani, imetilia maanani sana sekta ya elimu, hususan elimu ya msingi ya lazima. Kupitia sera hiyo, watoto wote nchini China, wakiwemo wale walioko vijijini, wote wanapata elimu ya bure ya shule ya msingi kwa miaka 6, na kisha sekondari miaka mitatu.

Kutokana na mfumo huu wa elimu, China imeweza kupata mafanikio makubwa katika sekta hiyo, na kuweza kupata idadi kubwa ya wanafunzi wanaojiunga na vyuo vikuu baada ya kumaliza elimu ya sekondari ya juu. Sera hii ya elimu ya lazima nchini China imezalisha watu wenye uelewa mkubwa, na hivyo kudumisha maendeleo ya kiuchumi katika miongo miwili iliyopita.

Ikumbukwe kuwa, mwaka 1949 wakati Jamhuri ya Watu wa China ilipoanzishwa, kiwango cha ujinga nchini humo kilikuwa asilimia 80, na hata katika miaka ya 1980, bado kiwango hicho kilikuwa cha juu zaidi kuliko nchi nyingi. Lakini hii leo, kiwango cha ujinga nchini China ni cha chini zaidi kuliko kiwango cha dunia, na hii yote ni kutokana na serikali kuu kuweka msisitizo mkubwa katika elimu.

Mamlaka husika zilifuatilia na kugundua kuwa wanafunzi, hasa wa shule za msingi na sekondari ya chini, wanakuwa na kazi nyingi za shule wanazotakiwa kufanya nyumbani, lakini pia, wengi wao walikuwa wanakwenda kupata mafunzo ya ziada (tuition) katika vituo mbalimbali. Ni kwa sababu hiyo, mwezi Julai mwaka 2021, mamlaka nchini China zilitambulisha mwongozo mpya ili kupunguza mzigo wa kazi za nyumbani na mafunzo ya ziada kwa wanafunzi.

Sera hiyo inayojulikana kama “Punguzo mara mbili” inalenga kukabiliana na matatizo makuu katika elimu ya lazima, ambayo ni mzigo mkubwa wa masomo kwa wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari ya chini, na pia mafunzo ya ziada nje ya shule, ambayo pia yamekuwa mzigo wa kifedha na kiakili kwa wazazi na walezi, na hivyo kuwa kikwazo cha matokeo mazuri ya mageuzi katika sekta hiyo. Kutokana na sera hiyo, kazi wanazopewa wanafunzi kufanya nyumbani zimekuwa na mabadiliko makubwa, na zimepungua kwa wingi na kuongezeka kwa ubora.

Mwezi Desemba mwaka 2021, Wizara ya Elimu ya China ilisema kuwa, kiwango cha wanafunzi wanaoweza kumaliza kazi wanazopewa kufanyia nyumbani imeongezeka kutoka asilimia 46 kabla ya sera hiyo mpya kuanza kutekelezwa, mpaka zaidi ya asilimia 90 kwa sasa.

Kutokana na hatua hiyo, pamoja na hatua nyingine kadhaa, sekta ya elimu nchini China imeendelea kuwa na ubora wa juu na kukubalika kimataifa, na hivyo, lengo la China la kuwa nchi yenye nguvu kielimu itakapofika mwaka 2035 bila shaka litatimia.
 
Hakika elimu bora ina changia kwa kiwango kikubwa ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja moja na taifa kwa ujumla, jamii inayo kosa elimu bora hutumbukia katika wimbi kubwa la umasikini na ujinga.
 
Back
Top Bottom