SoC02 Sababu kuu za changamoto ya ajira kwa wahitimu wa vyuo nchini Tanzania

Stories of Change - 2022 Competition

Mohan Ksan

New Member
Jul 29, 2022
4
1
UTANGULIZI
Ufinyu wa ajira kwa sasa nchini Tanzania imekua ni changamoto kubwa. Wahitimu wa vyuo vikuu na vya kati ni wengi na wamekua wakiongezeka kila uchao. Mahali walipo vijana kumi sasa hivi vijana saba kati yao ni wahitimu wa vyuo mbalimbali nchini Tanzania lakini jambo la kushangaza vijana hawa wamekosa jambo la kufanya ili kujiingizia kipato na badala yake wamezidi kuwa tegemezi kwenye familia zao. Hii yote ni kutokana na uchache wa ajira.

Uhalisia ni kwamba, mhitimu wa chuo kikuu leo hii yuko tayari kufanya kazi kwa kujitolea yaani bila ujira wowote na hii hutokana na kuchoshwa kukaa bila kazi yoyote ya kufanya, lakini bado hata hizo nafasi za kujitolea yawezekana ikawa hazipatikani.

Changamoto ya uchache wa ajira nchini Tanzania imekua ni tatizo na lawama kubwa kwa serikali, huleta msongo wa mawazo kwa wahitimu ambao ndio wahanga wa tatizo hili. Serikali kupitia bodi ya mikopo imekua ikipata hasara kifedha kwa wanufaika wa mikopo kushindwa kurejesha pesa baada ya kukosa ajira. Wazazi wanakosa msaada kutoka kwa waliowasomesha na hatimaye kupoteza matumaini na elimu ya mtoto wao, vilevile wanakosa moyo wa kusomesha zaidi.

SABABU KUU ZA CHANGAMOTO YA AJIRA KWA WAHITIMU WA VYUO
Kuhusu changamoto ya ajira kwa wahitimu wa vyuo nchini Tanzania kumekua na sababu mbalimbali zinazozungumzwa ikiwa ni pamoja na Ongezeko kubwa la ufaulu shuleni na Ongezeko la Udahili vyuoni na pia Ongezeko la taasisi za kutoa elimu lakini sababu kuu ni mbili nazo ni ukosefu wa sera ya elimu na mabadiliko katika mfumo wa ajira. Sababu mbili hizi ndio chanzo cha tatizo la ajira kwa wahitimu wa vyuo Tanzania.

Sera ya elimu ndio dira ambayo ingeweza kutoa uelekeo wa maisha ya wanafunzi baada ya kuhitimu. Kukosekana kwa sera ya elimu kumefanya kila mmoja aamimi anachokiamini. Wapo wanaoamini katika kusoma ili wafanikiwe, japo pia hawaelezi wazi kua wafanikiwe kwenye suala gani. Wapo wanaoamini katika kusoma ili watimize ndoto zao, ila cha kushangaza mtu ana ndoto ya kuwa rubani halafu ana shahada ya kilimo cha mazao ya bustani.

Vilevile wapo wanaoamini katika kusoma ili kupata ajira na hapa ndipo tatizo lilipoanzia. Kwa kujenga dhana hii ya kusoma ili kupata ajira, tatizo hili halitaweza kuisha kamwe kwani haitawezekana kwa wahitimu wote kupewa ajira. Lakini wahitimu hawana kosa ila kosa ni Kukosekana kwa sera ya elimu.

Mfumo wa ajira kwa sasa nchini Tanzania ni sababu nyingine iliyopelekea changamoto ya ajira kwa wahitimu wa vyuo. Mfumo wa ajira unalenga kuajiri wataalamu kwa kuangalia vyeti vya elimu na uzoefu wa miaka kadhaa katika fani anayoomba mhitimu. Kuhusu suala la vyeti sio tatizo maana kila mhitimu nina imani ana vyeti vyake lakini kigezo cha uzoefu ndicho ambacho huwa kinawakosesha wasomi wengi ajira. Kwa kuzingatia kigezo hiki waajiriwa watakua walewale kila siku, mtu anaacha kazi sehemu moja leo, kesho anaajiriwa pengine kwakua ni mzoefu.

SULUHISHO LA TATIZO LA AJIRA KWA WAHITIMU WA VYUO
Yafuatayo ni mambo muhimu kufanyika ili kudhibiti au kupunguza changamoto ya ufinyu wa ajira kwa wahitimu wa vyuo nchini Tanzania;

. Serikali inapaswa kuunda Sera ya elimu na kusimamia utekelezaji wake. Sera ambayo binafsi niliiweka akilini ni ile ya enzi za Mwalimu iliyosomeka kwa kiingereza "Education For Self Relience" ikiwa imelenga kutoa elimu itakayosaidia vijana kujitegemea wenyewe. Kuna jambo la kujifunza kwenye sera ya enzi za Mwalimu Julius Nyerere na siyo hii leo mtu anasoma ili aongeze vigezo vya kupewa ajira.

. Kuanzishwe taasisi unganishi kati ya vyuo na sekta za ajira. Ingependeza sana endapo kungelikua na taasisi inayounganisha vyuo na sekta za ajira kama ilivyo TCU ambayo huunganisha vyuo na bodi ya mikopo. Taasisi unganishi itasaidia sana kuwajengea raia ufahamu juu ya uhitaji wa wataalamu kazini na uhakika wa mahali pa kuwapata wataalamu yaani vyuoni.

. Kufuta dhana potofu ya kusoma ili kupata ajira. Imekua ni dhana potofu kwa sasa watanzania kudhani kwamba elimu ndio mkombozi wa maisha yao. Wanafunzi wengi wanawaza sana kuajiriwa na wanaamini wakihitimu vyuoni watapata ajira ilehali mambo yameshabadilika. Hivyo wanafunzi wanapaswa kufuta hiyo dhana na badala yake wasomee fani ambazo wanaweza kujiajiri pindi wasipoajiriwa.

. Vyombo vya habari kutoa elimu na kuhabarisha umma kuhusu mwenendo wa soko la ajira nchini. Watanzania sasa hivi wanapaswa kufahamu kua soko la ajira nchini limekua ni changamoto hivyo wanapaswa kufikiria zaidi namna ya kujiajiri na siyo kutegemea kuajiriwa. Ni jukumu la vyombo vya habari kutoa elimu na kuwahamasisha raia kufikiria zaidi kujiajiri kuliko kuajiriwa.

. Serikali kutoa kipaumbele kwa vyuo vya ufundi. Vyuo mbalimbali vya ufundi hususan VETA vimekua vikiwaandaa na kuwajengea wanafunzi wake uwezo wa kujiajiri kwa kutoa ujuzi kwenye fani mbalimbali kama vile udereva, ufundi bomba, ufundi umeme, useremala na wahitimu wa vyuo hivi hawajawa wahanga wa tatizo hili.

Hivyo serikali inapaswa kuviwezesha zaidi na kuvipa kipaumbele ili viweze kusaidia vijana wengi zaidi.

Kurekebisha kanuni na taratibu za kustaafu waajiriwa. Kutokana na uhaba wa ajira kwa sasa, kuna umuhimu wa kufanyika mabadiliko kwenye umri wa kustaafu waajiriwa, isiwe lazima mpaka mwajiriwa afikie miaka sitini, ikiwezekana iwe miaka arobaini na tano. Vilevile isiwe lazima mkataba wa ajira uwe wa maisha, ikiwezekana iwepo mikataba ya miaka kumi ya kazi, kisha mwajiriwa aweze kustaafu ili kuruhusu watu wengine kuajiriwa. Hii itapunguza changamoto ya uchache wa ajira nchini Tanzania.

HITIMISHO
Kwa kuhitimisha andiko hili ni muhimu kuzingatia mambo makuu mawili, kwanza kabisa ni kufuta dhana hii ya kusoma ili kupata ajira na badala yake watu wasome ili wapate ujuzi utakaowawezesha kuendesha maisha yao ya kila siku na ikiwezekana wanafunzi kabla ya kuanza masomo ya vyuo, wachague fani ambazo wakimaliza kusoma wataweza kujiajiri wenyewe endapo wakikosa kuajiriwa.

Pia, wahitimu wa vyuo wasibweteke kwa kigezo hiki cha kukosa ajira na badala yake wanapaswa wawe wabunifu kwa kujitengenezea ajira wao wenyewe kwa kujishughulisha.

Kwa mawasiliano; 0684125580
 
Back
Top Bottom