Sababu Kubwa 2 za Kuukataa Mchakato huu wa Katiba Mpya

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,476
39,995
Watanzania wameweza kusubiri kwa karibu miaka ishirini sasa kuweza kuanza mchakato wa kuandika Katiba Mpya. Bahati mbaya subira hii ya Watanzania inataka kuchukuliwa kama papara au haraka ya kukubali kila kinachowekwa mezani. Nina uhakika wa kutosha kabisa kuwa Watanzania wanaweza kusubiri miaka mingine mitano ili kije chama na uongozi ambao utasimamia mchakato wa Katiba Mpya kwa misingi ya usawa, uwazi, haki na kukubali kuwa wananchi ndio msingi wa utawala wote na ambao kwao madaraka yote hutoka.

Bahati mbaya sana kuna watu ambao wanaamini kabisa kuwa kwa vile tumeshakubaliana kama taifa tunastahili Katiba Mpya basi mchakato wa kufikia Katiba hiyo uwe ule ambao wao wameamua bila kujali kanuni za msingi za kuandika Katiba Mpya. Matokeo yake ni kuwa mswada wa kwanza uliopendekezwa na watawala wetu kusimamia mchakato wa kuandika Katiba Mpya tuliupiga vita na kulazimisha urudishwe na kufikiriwa upya. Sasa watu makini wangetarajia kuwa waandishi wa mswada ule wangefikiria vizuri na kusikiliza kwanini tulipinga awali. Kinyume chake wameandaa mswada mwingine ambao japo umefanyiwa mabadiliko bado una matatizo yale yale na hivyo unatuachia uchaguzi mmoja tu - yaani kuupinga.


Sasa tusiupinge bila kuanisha sababu hasa za kuupinga ni nini. Kuna kanuni kubwa mbili ambazo naamini mtu yeyote ambaye atapitia mswada huo wa sheria anaweza kuziona zikiwa zimevunjwa toka mwanzo kabisa wa mchakato unaopendekezwa. Kwanza ni kutoheshimu mamlaka ya wananchi kujitungia katiba yao na pili vipengele vingi vya mswada unaopendekezwa vinathibitisha hilo la kwanza.

Kutoheshimu mamlaka ya wananchi
Hili jambo nimewahi kuliandika huko nyuma lakini kwa vile kuna uwezekano kwamba baadhi ya watu haamini jambo hili si vibaya kurudia tena. Katika nchi ya kidemokrasia mamlaka yanatoka kwa wananchi. Yaani, madaraka hayo kwa Rais, kwa Bunge au kwa Jeshi bali kwa wananchi. Ni wananchi ndio wanaamua serikali gani wanataka wawe nayo, iweje, na iongoze vipi. Wananchi ndio msingi wa madaraka yote nchini. Kwa maneno mengine Katiba inatakiwa itoke kwa wananchi.

Siyo katika kuipigia kura tu bali katika uandikaji wake. Katiba ambayo haitoki kwa wananchi na ambayo haiweki ushiriki wa juu kabisa wa wananchi toka mwanzo haiwezi kudai kuwa ni katiba ya wananchi hao. Sheria hii inaweka nguvu kubwa sana mikononi mwa Rais - hili watu wengi wameishalionesha. Kwa upande hata hivyo tatizo ni zaidi ya kuwa "Rais anapewa madaraka makubwa" tatizo langu kubwa ni kwamba Rais anachukua madaraka ya wananchi kuandika Katiba.

Hili ni kweli kwa kuangalia vipengele mbalimbali vya mswada huo:

  • Rais, baada ya kushauriana na kukubaliana na Rais wa Zanzibar, na kwa ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar…ataunda tume (Ibara ya 5);
  • Rais, baada ya kushauriana na kukubaliana na Rais wa Zanzibar atateua wajumbe wa Tume (Ibara ya 6.1);
  • Katika kufanya uteuzi wa wajumbe wa tume Rais atazingatia masuala yafuatayo…(e)vigezo vingine ambavyo Rais ataona vinafaa;
  • Hadidu za rejea za tume zitatolewa na Rais kwa makubaliano na Rais wa Zanzibar (Ibara ya 8.1 na 8.1 inasema Rais kwa makubaliano na Rais wa Zanzibar anaweza kuongeza muda wa tume kukamilisha ripoti yake kwa muda usiozidi miezi mitatu;
  • Kabla ya kuanza kutekeleza majukumu yake kila mjumbe wa tume na Katibu ataapa au kula yamini mbele ya Rais (Ibara ya 11);
  • Katibu wa Sekretariati ya tume atateuliwa na Rais baada ya kukubaliana na Rais wa Zanzibar (Ibara 13.2);
  • Baada ya Tume kumaliza kazi yake itawasilisha ripoti yake kwa Rais na Rais wa Zanzibar (Ibara ya 18.1);
  • Baada ya kushauriana na kukubaliana na Rais wa Zanzibar … Rais atamuagiza Waziri kuwasilisha mswada wa Katiba katika Bunge la Katiba (Ibara ya 18.2);
  • Rais, baada ya kushauriana na kukubaliana na Rais wa Zanzibar, na kwa ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar…ataunda Bunge la Katiba (Ibara ya 20.1);
  • Rais atachapisha majina ya watu atakaowateua kuwa wajumbe wa wa Bunge la Katiba(Ibara ya 20.4);
  • Katibu na Naibu Katibu wa Bunge la Katiba kabla ya kushika madaraka yao wataapa au kula yamini mbele ya Rais (Ibara ya 20.5)
Sasa, kwa mtu yeyote ambaye amewahi kupita kwenye majengo ya shule anaweza kukiona kitu kimoja kilicho wazi sana - mchakato wa Katiba Mpya unamhitaji Rais ili kufanikiwa na kuwa halali. Lakini siyo kumhitaji Rais tu bali kumfanya Rais kuwa ndiye kiini cha mchakato mzima. Naweza kusema kwa ujasiri wa ukweli mchakato unaopendekezwa ukikubaliwa utamfanya Rais kuwa ndiye mwanzo na mwisho wa mchakato wa kuandika Katiba mpya na siyo wananchi.

Sasa swali ambalo litaundwa mara moja ni kuwa "sasa unataka tume aunde nani au iundwe vipi bila Rais?" Kwa wengine hili ni swali la kiakili lakini ukitambua kuwa Katiba tunayotaka kuiandika ni ya wananchi basi jibu haliwezi kuwa mbali hivyo. Ninaamini kuwa tuna uwezo na watu ambao wanaweza kuangalia ni jinsi gani tutengeneze mfumo mzuri wa kusimamia uandikishaji wa Katiba Mpya bila kuwanyang'anya wananchi madaraka hayo. Binafsi nina mapendekezo yangu lakini ninaamini kuwa wapo watu katika nchi yetu wenye uwezo wa kufikiria namna gani mchakato uwe bila kumfanya Rais mfalme wa mchakato huu.

Ili kuweza kufikia hilo maswali mawili yanatakiwa yajibiwe na hapo ndipo mapendekezo mbalimbali yanaweza kutolewa. La kwanza - je tunaweza vipi kuunda tume ya kusimamia mchakato wa kuandika Katiba Mpya bila kumpatia Rais madaraka ya kufanya hivyo? Jibu la swali hili litaonesha tuna uwezo gani wa kufikiria nje ya vile tulivyozoea. Kwa muda mrefu imekuwa ni rahisi kwa watu kumrundukia madaraka na majukumu Rais kwa sababu hatuoni njia nyingine ya kufanya mambo.

Swali pili ni je katika mchakato huo tutahakikisha kuwa wananchi wanashiriki kwa kiwango cha juu kabisa (maximum participation of the people) badala ya ilivyo sasa. Kwa mfano, mswada huu ukikubaliwa Katiba mpya itapitishwa na kwa asilimia 50 ya wapiga kura ya maoni. Yaani, nusu tu ya wananchi wakisema "ndiyo" kwenye kura ya maoni basi tutakuwa na Katiba Mpya. Na kuna mtu aliamini kabisa kuwa hiyo ni ‘brilliant idea'!

CCM itatunga na kupitisha Katiba Mpya
Hili linatuleta kwenye sehemu ya pili ambayo kimsingi ni kuwa kile kipengele cha kusimamia mchakato wa Katiba kinavunja ile kanuni ya kwanza hapo juu - kwamba vinaondoa madaraka ya wananchi kuandika Katiba. Mswada huu ukipita Chama cha Mapinduzi kitakuwa kimeuteka rasmi mjadala wa Katiba kwani kitasimamia mchakato mzima kupitisha peke yake tena kwa kutegemea wananchi wake tu - wananchi wengine wote watakuwa wasindikizaji. Angalia mambo haya mawili yaliyofichwa kiaina ndani ya mswada huu.

  • - Katiba Mpya kuwa halali ikipitishwa na asilimia 50 tu ya wapiga kura ya maoni
  • Mswada huu unatuambia kuwa matokeo ya kura ya maoni yataamuliwa kwa wingi wa kura zitakazopigwa kwenye kura hiyo ya maoni. Kwamba, matokao hayo yataamuliwa "kwa msingi wa kuungwa mkono kwa asilimia inayozidi hamsini ya jumla ya kura zote" zitakazopigwa Zanzibar na Tanzania bara. Yaani, asilimia 50 ya Watanzania wanaweza kubadilisha kabisa mwelekeo wa taifa letu na tukasema ni uamuzi wa "Watanzania". Katiba Mpya si uchaguzi wa rais au mbunge ni kuamua kubadilisha kwa kiasi kikubwa sana maisha yetu na ya watoto wetu. Kweli tunataka asilimia hamsini kati yetu waamue hatima hiyo?
  • - Mfumo wa hilo linaloitwa "bunge la Katiba" ukikubaliwa CCM itakuwa imeteka rasmi mchakato mzima wa Katiba na kwa kweli hakuna kitakachowazuia kuupeleka wanavyotaka wao. Fikiria kuwa pendekezo la sasa hivi lilivyo ni kuwa wabunge wote wa Jamhuri ya Muungano na Wawakilishi wote wa Zanzibar watakuwemo kwenye Bunge la Kutunga Katiba. Hii ina maana ya kwamba, tayari Chama cha Mapinduzi kitajipa uwiano usio wa kawaida katika baraza hilo.
  • Bunge letu linatakiwa liwe na wabunge 357; kati ya hawa 258 wanatoka Chama cha Mapinduzi na Upinzani unao 80. Tukiwajumlisha na wale 10 wanaoteuliwa na Rais ambapo mmoja ni kutoka CUF tunaweza kuona kuwa wabunge wenye kuhusiana na Rais ni wengi zaidi. Kwa vile Wawakilishi wote kutoka Zanzibar nao wanapendekezwa kuwa wajumbe wa Bunge la Katiba ni wazi kuwa CCM inajiongezea wajumbe wengine 30 na upinzani 19 kutoka Zanzibar. Hapa sijali muafaka kati ya CCM na CUF.
Kwa misingi hiyo, kwenye baraza la kutunga Katiba Chama cha Mapinduzi kitakuwa na wajumbe wasiopungua 297. Upinzani utakuwa na wajumbe 110. Kwa kuangalia uwiano huo tu ni kuwa CCM tayari itakuwa na wingi wa wajumbe kwa uwiano wa karibu 3:1. Sasa tunaambiwa pia kuwa kutakuwa na wajumbe wengine 116 kutoka taasisi mbalimbali kwa mujibu wa Ibara ya 20 ya mswada huo. Sasa cha kutufanya tufikirie ni kuwa ni Rais ndiye atakayewateua watu hao 116. Je itakuwa ni makosa sana kufikiria kuwa Rais atachagua watu ambao wanakubaliana naye au wale wenye mrengo wa chama chake? Je akiwateua watu wengi (kati ya hao 116) ambao wanaelekea kukubaliana naye kuna mtu anaweza kumuuliza?


Kimsingi kwa mfumo unaopendekezwa ni wazi kuwa Bunge la Katiba litakuwa na wajumbe wasiopungua 523. Hii ni idadi ndogo sana ya Baraza la Kutunga Katiba. Binafsi naamini kwanza kabisa wabunge na mawaziri wasiwe sehemu hii kwa sababu moja kubwa tayari wao wanawajibika na majukumu yao ya Kikatiba na majimbo yao. Kuwaongezea hili ni kuwapa majukumu zaidi yasiyo na sababu. Baraza la kutunga Katiba lisiwe na watu wasiopungua 2000 ambao watatoka miongoni mwa wananchi na wakiwakilisha sehemu kubwa ya wananchi wetu (cross section). Kwa mtindo ambao unapendekezwa na mswada kuna uwezekano mkumbwa kwamba baraza hili litakuwa ni la wasomi watupu!

Fikiria kuwa hao wajumbe 116 watatoka kwenye makundi matano yaani asasi zisizo za kiserikali, asasi za kidini, vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu, taasisi za elimu ya juu na makundi yenye mahitaji maalum. Sasa nina uhakika kuna mtu amejiaminisha huko waliko kuwa Katiba Mpya inahitaji kuandikwa na wasomi peke yao. Ndugu zangu, tukikubali hili tutakuwa tumenyang'anya haki ya wananchi kujiandikia katiba yao. Wananchi wengi wa Tanzania siyo wasomi sana na siyo wote wako kwenye hizo taasisi tano! Binafsi ninaamini ni lazima chombo kitakachoandika Katiba kiwe kinawakilisha jamii nzima yetu (must represent the cross-section of our society). Je, wakulima na maskini wanawakilishwa vipi, je makundi madogo (minority groups) wanawakilishwa vipi n.k Tusije kugeuza mchakato wa Katiba kuwa mchakato wa watu ambao tayari wana kiu ya madaraka na wameonja madaraka wakatutengenezea kitu cha kuzidi kuwapa wao madaraka ya kuwatawala wengine.

Hivyo basi, hata kama nisingeingia ndani na kuvichambua vipengele vyote vya mswada huo naweza kusema kwa uhakika wa dhamira yangu kuwa ni miongoni mwa miswada mingine mibovu ambavyo inaandikwa na watu ambao tunaamini wana akili timamu, na wasomi. Na kama hawa ndio ambao watakuja kutuandikia Katiba Mpya basi tunajitumbukiza wenyewe kwenye shimo ambalo tunajua hatuwezi kutoka. Lakini kubwa zaidi ni kwamba kwa vile CCM haijawahi kuwa na ajenda ya Katiba Mpya na sasa inaonekana wamekusudia kabisa kuliburuza taifa zima kama mtu huru nakataa kuburuzwa hivyo na binafsi ninaukataa mchakato huu unaoongozwa na CCM kwa misingi ya geresha ya kisiasa. Nakataa mara moja na daima mchakato mzima ambao unapendekezwa na mswada huu na ni matumaini yangu wengine nao wataukataa hivyo hivyo.

Kama CCM haiwezi kubuni mfumo bora wa kusimamia mchakato wa Katiba Mpya na badala yake kuturudishia kitu kile kile ambacho tumekikataa miezi michache iliyopita ni jukumu letu kukataa siyo tu kuunga mkono mchakato huu bali pia kushiriki endapo utapitishwa - na uwezekano wa kupita ni mkubwa kwani wao ni wengi, rais wao na vyombo vyote vyao.

Ninachoweza kusema ni kwamba kama CCM na serikali yake watalazimisha kutulisha katiba mpya kama kwa nguvu. Ni wajibu wetu kukataa kushiriki kwenye mijadala yao na kwa hakika kwenye kura ya maoni watakayoitisha. Kama tumeweza kusubiri miaka 20 nina uhakika tunaweza kusubiri miaka mingine mitano kwani tunajua ni kina nani kweli walipigania Katiba Mpya. Wanaotaka Katiba Mpya ya CCM waendelee na mchakato wao, wanaotaka Katiba Mpya kwa ajili ya Watanzania wote wasubiri wakati wao. Kwani miaka minne iliyobakia si mingi.


Facebook: "Mimi Mwanakijiji"
 
Na kuna kipengele ambacho wenzetu wa zanzibar watafanya muswada uchanwe tena ni cha kusema bado zbar na pemba ni sehemu ya JMT kitu ambacho wenzetu hawakitaki kusikia rejea katiba mpya zbar ambayo inatambua zbar kama nchi ndani ya JMT na si sehemu!!!
 
Mkuu ulichonena kila mtanzania hata wa shule ya primary, ataona upuuzi huo. Anywy katiba mpya haikuwa ahadi ya ccm. Wamedakia kitu wasichukijua hvyo tutaupinga na nahc hapo ndio damu itamwagika! Tuungane kupinga kwa nguvu zetu zote
 
  • Thanks
Reactions: Ame
Well said tuko pamoja. Hivi la katiba lazima tulisimamie japo Tuwe na kizuri kimya cha kuachia watoto. Labda watatusamehe madudu tulioacha yaharibu nchi
 
Muungano uwepo katika suala la katiba. Kwani baraza la mawaziri, bunge na serikali ya Tanganyika vina utata. Tusikubali kupelekwa nusunusu. Katika suala hili Raisi apumzishwe, wacha wana wa nchi watengeneze katiba ya kumuajiri raisi. Kamati iapishwe na Wachungaji na Mashehe na Mapadri NK. Tuanze upya kabisa.
 
  • Thanks
Reactions: Ame
Mkuu Mwanakijiji huenda siku hizi Uzee unakufanya uanzae kuzisahau hesabu. Unapozungumzia Idadi ya Wapinzani 110 Sijakuelewa una maana gani! Uenda umesahau kwamba CUF nao ni Chama tawala kule Zanzibar!
Nakumbuka enzi zile za uhaba wa sukari, tulikuwa tunapanga foleni ili tuweze kununua. Ikatolewa amri kwamba kuwepo na foleni mbili tu, yaani ya moja ya Wanawake na Nyingine ya Wanaume. Jamaa mmoja akaropoka, Sasa wewe unasema wanawake na Wanaume tu, na sisi W.a.s.e.n.g.e tukae wapi?! Kumbe alikuwa amesahau kuwa kuna watu ambao si wanawake wala Wanaume. Ikabidi nao wapewe foleni yao.
Sasa hata hawa CUF inabidi nao sasa wawekwe kwenye kundi lao maana Zanzibar ni Watawala na huku Bara ni Wapinzani. Labda wajigawe, wale wa Zanzibar wawe upande wa Wajumbe upande wa Utawala na hawa wa Bara wawe upande wa Upinzani. Wanatuchanganya sana!
 
Muungano uwepo katika suala la katiba. Kwani baraza la mawaziri, bunge na serikali ya Tanganyika vina utata. Tusikubali kupelekwa nusunusu. Katika suala hili Raisi apumzishwe, wacha wana wa nchi watengeneze katiba ya kumuajiri raisi. Kamati iapishwe na Wachungaji na Mashehe na Mapadri NK. Tuanze upya kabisa.
Nimesikia mara nyingi katika viapo mwisho hutamkwa maneno "EE MWENYEZI MUNGU NISAIDIE". Nakubaliana na wewe kimsingi kwamba wanaojua habari za Mwenyezi Mungu ni watu wa dini hivyo suala la kiapo si lazima kifanywe chini/mbele ya Rais kwani kiapo kinatoka nafsini mwa tu, yaani nafsi iliyoumbwa na Mwenyezi Mungu. Ni suala la kutengeneza utaratibu tu.
 
Watanzania tusitegemee hata siku moja kama ccm wanaweza kuendesha mchakato wa katiba na ukawa wa haki na kukidhi haja ya watanzania walio wengi.CCM wanataka kuteletea katiba ambayo sio shirikishi na itakayo halalisha uwepo wao madarakani kwa njia za panya wanazotumia mara zote.Huu mswada umeletwa kama geresha ya kisiasa.Kama sababu mojawapo ya mabadiliko ya katiba ni kutaka kupunguza madaraka ya rais,inakuaje katika mchakato wa katiba hiyo hiyo tunayotaka rais apunguziwe madaraka,amepewa mamlaka kubwa kiasi hiki.Kwa muswada ulivo katika kila stage ya mchakato wake utategemea sana nguvu ya rais ambayo at the end tutajikuta CCM wametuletea katiba wanayotaka wao na sio katiba ya wananchi.TUKATAE KUBURUZWA
 
  • Thanks
Reactions: Ame
Mwanakijiji,

Uliyosema mengi ni sawa kabisa: Kukosoa mchakato wa katiba kwa sababu zote ulizoziweka.

Ninachopinga mimi ni kusubiri miaka 4 mingine. Bila shaka ni kweli kuwa Katiba ni mali ya wananchi. Wakiamua iwepo INAKUWEPO. Wakiamua vinginevyo, INAKUWA! Sidhani kama Katiba ni zawadi.
 
Asante kwa makala yako MM. Maoni yako ni mazuri sana na yanafanya tufikiri zaidi nje ya box. Kuongezea:

I) Mchakato wa katiba mpya usimamiwe na kuratibiwa na chombo huru chenye uwakilishi kutoka kila wilaya.

II) Wajumbe wa chombo hicho waapishwe na majaji wa mahakama kuu.

III) Kura ya maoni iandaliwe na kuratibiwa na chombo maalum kitakachopewa uwezo wa kisheria wa kusimamia kura hiyo, na wajumbe wote lazima waapishwe mahakama kuu.

IV) Mamlaka ya raisi yasiruhusiwe kuingilia maoni ya wananchi. Yaani pawe na utaratibu wa kupinga maamuzi ya rais pale inapotokea amekwenda kinyume na matakwa ya wananchi.

Mchakato huu uwe mwanzo wa wananchi kujiamulia mambo yao na watawala waheshimu maamuzi ya wananchi.

Nawasilisha.
 
  • Thanks
Reactions: Ame
Mkuu Mwanakijiji huenda siku hizi Uzee unakufanya uanzae kuzisahau hesabu. Unapozungumzia Idadi ya Wapinzani 110 Sijakuelewa una maana gani! Uenda umesahau kwamba CUF nao ni Chama tawala kule Zanzibar!
Nakumbuka enzi zile za uhaba wa sukari, tulikuwa tunapanga foleni ili tuweze kununua. Ikatolewa amri kwamba kuwepo na foleni mbili tu, yaani ya moja ya Wanawake na Nyingine ya Wanaume. Jamaa mmoja akaropoka, Sasa wewe unasema wanawake na Wanaume tu, na sisi W.a.s.e.n.g.e tukae wapi?! Kumbe alikuwa amesahau kuwa kuna watu ambao si wanawake wala Wanaume. Ikabidi nao wapewe foleni yao.
Sasa hata hawa CUF inabidi nao sasa wawekwe kwenye kundi lao maana Zanzibar ni Watawala na huku Bara ni Wapinzani. Labda wajigawe, wale wa Zanzibar wawe upande wa Wajumbe upande wa Utawala na hawa wa Bara wawe upande wa Upinzani. Wanatuchanganya sana!

Hakuwasahau CUF bali ameamua kuchukua conservative assumption kwamba wao ni wapinzani lakini hata baada ya kuwajumlisha kwenye kundi la upinzani bado mizani ikaegemea upande wa chama cha mafisadi (CCM ninayoifahamu mimi ilienda na azimio la Zanzibar kama ilivyo binafsishwa bank ya CRDB; kwamba imebaki na jina la zamani lakini ni mali ya raia wa nchi nyingine)...

Hakuna jinsi kwa mfumo uliopo katiba itakayo andikwa ikawa represenative kwa watu wote lazima itaegemea kwa mafisadi maana ndiyo wanaotengeneza serikali ambayo kwa practice imeshajipambanua ni ya chama kimoja kushika hatamu vingine ni vya kiharakati zaidi kuliko kisiasa. Mbaya zaidi chama hiki kilichoshika hatamu kina wanachama si zaidi ya millioni tano tu na kwa mujibu wa matokeo ya uchaguzi ndiyo takribani idadi iliyopiga kura halali ukiweka error margine kubwa ya plus or minus washabiki wao kupata idadi ya 9M (hao waweza kuwa members in a family ambao pengine hawana kadi), almost less than 55% ya all voters ambao tuliambiwa wako about 20M; sijui hapo tunapata implication gani!

Hatari zaidi nikuwa hata katika hao waliopewa fursa adimu yakura zao kutambuliwa (halali) karibu nusu walikataa hicho chama kisichukue dhamana ya kuongoza nchi; alafu leo hii hao watu waliochaguliwa na chini ya nusu ya watu wote wenye haki ya kupiga kura eti watuamulie mustakabali wa maisha yetu kwa miaka isiyopungua 30 kwa uchache...Tukilikubali hili watanzania nitaanza kuamini maneno ya mtaani kuwa huo mwenge unaokimbizwa kila mwaka moshi wake una polute minds zetu!
 
Tusiwe na haraka ya kufanya mchakato wa katiba mpya.

Kwanza kama huu mchakato utaendeshwa bila kuwashirikisha wananchi kikamilifu mwisho wananchi wataweza kuja kupiga kura ya HAPANA. Na hili likitokea katiba ya mwaka 1977 itaendelea kutumika kama kinavyosema kifungu 32(4) cha huu mswaada. Sasa hii haitasaidia maana nchi itakuwa imetumia raslimali nyingi sana kufanya huo mchakato. Kwa kweli tutakuwa tunajaza maji kwenye gunia tu.

Sasa ili kuondoa hili tatizo, mimi napendekeza kuwa mchakato wa katiba usimamiwe na tume maalum ya katiba ambayo itatokana na wawakilishi wawili(au idadi itakayofaa) kutoka kila kundi la kijamii. Hawa ndio wataanda hadudu za rejea na kusimamia maoni ya wananchi kwa ujumla. Sasa kutakuwa na swali la makundi ya kijamii ni yapi na yako mangapi? Nadhani kuna watanzania wanaweza kutoa hilo jibu ( Kwa mfano kuna makundi yalisajiliwa kwa vile vyama vya siasa, NGOs, vikundi vya kidini nk)
 
Raisi wetu anaogopa nini kuwapa umma uandike katiba?? Above all he has nothing to loose, sababu lazima baada ya kipendi chake cha miezi mi 5 ataachia tu ngazi na atamwachia raisi mwingine,.Yatakayo andikwa ktk katiba mpya haatamhusu kama raisi.
 
MKJJ,

Well said, mimi huo mswaada baada ya kuupitia nilishiwa nguvu na matumaini kufa. Naamini CCM kuna kitu wanakitafuta!!! Ngoja tuone mkutano ujao wa bunge, si ni wiki ijayo tu!!!
 
Mwanakijiji,
Makala yako imenigusa sana. Natamani sana kama ungeweza kutengeneza video au audio tukaisambaza kwa watanzania itakayokuwa imebeba maneno yote yaliyomo kwenye makala hii. Hii itawasaidia watanzania wakulima na wafugaji kujua ukweli na ujanja unaotaka kufanywa ili kuhujumu mchakato wa katiba mpya.

Hongera sana mana kila mstari umetulia.

Hongera sana kwa umakini wako wa kuandika. Kila mstari una mashiko. Assume kuwa ndo
 
Mimi naona hawa watu wanacheza na Akili zetu kabisa...kama tumewapa muda wote huo afu wanakuja na huu utumbo maana yake nini kwanza Wametudharau kwamba sisi wananchi si lolote si chochote na wanafanya wanavyotaka na sio tunachotaka Wananchi.Jambo moja la msingi sana ambalo tunamtaka Muheshimiwa Rais afanye ni kumwajibisha Waziri wa Sheria pa1 na Mwanasheria Mkuu ili tuendelee kumuamini juu ya mchakato mzima coz hawa walishapinga toka awali ndo maana wanatufanyia mazingaumbwe.
 
Hili la kura kwa asilimia hamsini..halifai kabisa. Mimi napendekeza ili katiba iwe ya watu..basi ikubaliwe na 2/3 ya wapiga kura yaani 66.67%.
 
Back
Top Bottom