Riwaya: Lidake tena chozi langu

SEHEMU YA KUMI

Ilikuwa ni baada ya siku mbili za kupewa taarifa na
daktari kuwa kuna tetesi kuwa bwana mmoja
anayetaka kujiingiza katika siasa katika uchaguzi
ujao.
Ikiwa ni saa mbili usiku tukiwa tunafurahia kwa
pamoja chakula cha usiku ule tukiwa familia nzima,
mara tulipata ugeni wa ghafla.
Na mgeni mwenyewe hakuna aliyekuwa anamjua.
Alipokaribishwa hakutaka kuketi badala yake alimuita
daktari kiurafiki tu daktari akamfuata wakazungumza
waliyozungumza kisha wakaagana juu kwa juu.
Nilichokisikia ni kitu kimoja tu yule bwana alimsisitiza
kuwa afike kesho yake walipokubaliana.
Daktari aliingia ndani akiwqa na uso ambao ulionyesha
mashaka sana.
Na hakuweza tena kuendelea kula kile chakula alifika
na kunywa maji mengi sana. Alikuwa ameshikilia
bahasha mkonononi.
“Hebu washa feni!” alimwambia mkewe, mke akawasha
na kumuelekezea lile feni.
Licha ya kuelekezewa feni bado aliendelea kujipepea
kwa kutumia ile bahasha.
“Mume wangu kwani kuna nini… na huyo alikuwa ni
nani sasa” aliuliza mke wa daktari huku naye akiwa
ameacha kula na kunilisha mimi pia.
Badala ya kujibu daktari alishusha pumzi kwa nguvu
sana.
Akanitazama mimi kisha akamtazama mkewe,
akashusha tena pumzi.
“Eti kesho kutwa natakiwa mahakamani kuna bwana
mmoja ameniletea samasi eti nimemdhalilisha.”
Alijieleza huku akitutazama.
“Unamfahamu huyo mtu ama…” nilimuuliza kwa
utulivu.
Akanitazama na kisha akamgeukia mkewe.
“Mama Sikudhani, umezungumza na mtu yeyote
kuhusiana na lile jambo?” daktari alimuuliza mkewe
kwa makini sana.
“Jambo gani tena mume wangu….” Mkewe aliuliza
huku akijiweka sawa kwenye kiti.
“Ama… au achana nalo hebu ngoja kesho
tutazungumza….” Alisema na hapo akasimama na
kuelekea chumbani kwake. Mkewe hakungoja
akamfuata kwa nyuma hukohuko chumbani, sikuwa
tena na mtu wa kunilisha chakula. Nilikitamani sana
chakula kile lakini nisingeweza kula mwenyewe
nilihitaji kulishwa.
Kwa unyonge kabisa na mimi nikasimama na kutoweka.
Nikaenda kulala.
Nililala huku nikimuwaza mama yangu, nilijiuliza sana
juu ya mapokeo yake katika hali yangu ile ya kuumiza
nafsi.
Nikapitiwa na usingizi nikimuwaza mama yangu. Mama
Majaliwa!!
Asubuhi daktari aliwahi sana kuamka, akaondoka
kuelekea kazini akituaga sote mimi na mke wake kuwa
atawahi kurejea.
Hakurejea kama alivyoahidi badala yake mkewe
alipokea simu majira ya saa saba simu ambayo ilizua
mtafaruku.
Aliniita kwa sauti ya juu huku akihangaika kuifunga
vyema kanga yake kiunoni.
Licha ya kwamba nilikuwa karibu yake sana lakini
alikuwa akiongea kwa sauti ya juu nikaziona dalili za
mwanamke yule kuchanganyikia.
“Mama kuna nini kwani kinatokea.”nikamuuliza lakini
hakunijibu badala yake aliendelea kutokwa na maneno
mengi.
“Majaliwa natoka, natoka kidogo mume wangu ana
matatizo kidogo sijui niseme matatizo makubwa sasa
njoo huku nifuate” alinielekeza pa kumfuata
nikafanya hivyo hadi chumbani kwake.
“Ingia katika mlango huu, usitoke hata mtu agonge
vipi. Wewe utatoka ukitaka mwenyewe, nikifika mimi
nitakuita kwa jina la Steve hapo ndo utatoka lakini
isiwe vinginevyo sawa. Nakusihi hivi kwa sababu
hakuna adui yetu hata mmoja kati ya wale
waliotuvamia ambaye amekamatwa tunaamini bado
wanatuwinda lakini ukiwa katika sehemu hii hawawezi
kamwe kufungua bi9la wewe kutaka. Tunakupenda
sana Majaliwa…”alimaliza akanibusu shavuni.
Nikaingia katika kifaa kile ambacho kilifanana na
kabati lakini lilikuwa kubwa sana, sikuweza kuelewa ni
kwanini kifaa kile kilikuwa pale chumbani.
Mama akaondoka huku mashaka yakijitangaza
waziwazi katika uso wake. Lazima kulikuwa kuna
tatizo kubwa tu.
Tatizo gani sasa?
Sikuweza kupata jibu hadi mama aliporejea baadaye
jioni. Alikuwa analia sana, na aliponiona kile kilio cha
kimyakimya kikakatika na kuanza kulia kwa sauti ya
juu sana.
Alinifikia na kunikumbatia na hapo akaanza kunieleza
kijuu juu kuhusu tukio lililotokea.
Akanieleza kuwa mume wake alikuwa ametiwa kizuizini
kwa kosa la kumzalilisha mfanyabiashara mkubwa
wilayani pale kwa kupakaza kuwa anahusika na mauaji
ya Albino.
Huku akiwa analia bado aliendelea kunieleza kuwa kwa
hofu ya Mungu kabisa ni heri asiseme uongo.
Akanieleza kuwa ni kweli baada ya kuelezwa jambo lile
na daktari juu ya muhusika wa viungo vya albino na
yeye alitamani pakuche akamueleze.
Baada ya kumweleza huyo rafiki hajui kama na yeye
amezisambaza sana ama kulikuwa na lolote kati ya
huyo msambazji
Kesi ile ilienda kwa kasi na wakati huo ikiwa imechukua
nafasi kubwa sana hapo wilayani.
Nilikuwa sijui cha kuzungumza. Nikajiuliza maswali
makuu ambayo yanaweza aidha chanzo cha kesi ile
kwenda kasi kiasi kile.
Hapakuwa na jibu moja nilibaki kuamini kuwa pesa ndo
chanzo….
Pesa ilikuwa ikihusika katika kuifanya isokuwa halali
ionekane kuwa halali.
Daktari alinyimwa dhamana, daktari hakupewa nafasi
ya kuongea na mkewe eti kisa tu upelelezi
utaharibika.
Na hatimaye daktari akageuziwa kesi eti yawezekana
anahusika katika tukio la kuikata mikono yangu na
sikio.
Ilianza kama tetesi na baadaye ikatapakaa wilayani
kuwa daktari amenikata mikono yangu.
Nilishangaa kilichokuwa cha ajabu ni kwamba
sikutafutwa ili kutoa ushahidi wowote.
Majuma mawili yakapita daktari akiwa mahabusu. Si
kwa kesi ya kumdhalilisha mtu bali kesi ya kuhusika
katika kukata viungo vya albino na kuvifanyia
biashara.
Kitendo cha kuendelea kuishi katika nyumba ya mtu
mwema yule huku nikishindwa kumtetea kwa jambo
lolote lile katika shutuma hizi za uongo mkubwa
kilinifanya nijisikie fedheha sana, hasahasa mbele ya
mkewe ambaye hakuchoka kunilisha kila siku.
Yaani mzigo aliotakiwa kuubeba mama yangu yeye
aliubeba kwa mikono yake yote miwili.
Sikutaka siku ziendelee kwenda mbele huku kila mara
nikiwa nafungiwa katika chumba kile chenye mlango
wa chuma ili nisiweze kujeruhiwa na kisha kuuwawa
kabisa na wale watu wabaya walioukata mkono wangu
pamoja na sikio.
Nilitambua wazi kuwa nikimshirikisha mke wa daktari
kuwa nahitaji kwenda kumtetea daktari ili akiepuke
kitanzi kinachomkabili waziwazi atakataa katakata.
Nikafikiria kuwa liwalo na liwe, nitatoroka na kisha
kupambana ili ukweli umweke huru daktari yule.
Mke wa daktari alikuwa akinitia moyo kila kukicha
kuwa kesi inendelea vyema tu, hakuwahi kabisa
kuniambia kuwa mumewe amegeuziwa kesi. Habari hizo
nilizipata kupitia redio.
Mke wa daktari hakujua kabisa kuwa hatimaye
nilikuwa naweza kuwasha simu na kubofya vitufe
kadhaa kwa kutumia vidole vya mguu wangu.
Naam!! Nilitambua kuwa hakutaka niumie na kisha
kukata tamaa kabisa.
Aliendelea kukonda kila siku na tabasamu likitoweka
usoni mwake.
Ni hapo nilipogundua kuwa jukumua langu kuu kabisa
ni kulirejesha tena tabasamu lililokuwa limetoweka na
kisha kuuleta tena uhuru wa daktari.
Siku aliyopanga kwenda mahakamani kusikiliza kesi ya
mumewe nd’o siku hiyo niliyopanga na mimi kuifanya
kuwa siku ya tukio. Liwalo na liwe!!
Kweli baada ya siku mbili baada ya kunilisha akaniaga
kuwa anaenda mahakamani yawezekana siku hiyo
ikatolewa hukumu. Alizungumza nami huku macho yake
yakionyesha kabisa dalili ya uoga mkubwa na ni kama
alikesha huku analia.
Nikajiuliza… nilikatwa mikono yangu yote bila ganzi,
nikakatwa sikio langu na kidole cha mguu bila ganzi.
Nina kitu gani cha kuhofia kupoteza katika maisha
haya.
Kama ni pumzi zangu wanazozitafuta basi na
wazichukue nilikuwa nimeridhia.
Alipotoka na kunipa angalizo la kila siku kuwa nisitoke
wala kumuitikia mtu.
Nilimkubalia kama kawaida na kumuaga.
Alipotoka na mimi nyuma nikatoka.
Nilipolifikia geti nikazitazama mbingu.
Na hapa nikaongea na aliyeniumba ambaye dunia nzima
ipo chini yake.
“Baba… wewe ndiye baba yangu pekee, yule baba
uliyemteua kuwa baba yangu hapa duniani alinikataa.
Sina baba mwingine ila wewe. Sina wa kumuomba kwa
lolote lile ila wewe. Wewe ni baba yangu mwaminifu,
nakuamini hata kama umeruhusu mikono yangu
kukatwa, wewe ni muaminifu kwa sababu haujawahi
kunitoza kwa kuvuta pumzi zako. Kama uliweza kunipa
pumzi zako bure bila kunibagua, baba naomba unipe
hekima na ikiwa umenipa nafasi ya kushuhudia miujiza
mingi bila mimi kukuomba miujiza hiyo naomba leo sasa
unipe muujiza. Nipatie kwa sababu na uhitaji, lakini
kama ikiwa utazinyakua pumzi ambazo ni mali yak
oleo… mkumbuke mama yangu mpe maono mwambie
Majaliwa mimi mwanaye ninampenda sana. Asante
baba”
Sikurudi nyuma nikalifungua geti nikatoweka. Nilikuwa
napajua mahakamani vizuri sana.
 
SEHEMU YA KUMI NA MOJA

Nilifika mahakamani na kukuta kesi kadha wa kadha
zikiendelea. Niliendelea kuwa mtulivu hadi nilipomuona
daktari akipandishwa kizmbani.
Masikini wa Mungu alikuwa amevimba uso, alikuwa
akitembea huku akichechemea.
Na wakati anapanda pale kizimbani watu
walimnyooshea kidole huku wengine nikiwasikia
wakisemezana kuwa yule ndiye muuaji wa Albino na
lazima ahukumiwe kunyongwa la si nhivyo
wanaandamana.
Amakweli wema huwa hawaishi siku nyingi na hii ni kwa
sababu moja tu!! Wabaya wengi wanawazunguka hivyo
kuwagandamiza sana.
Niliendelea kusubiri hadi pale aliposoimewa mashtaka
yake na kuyakana. Alikuwa hawezi kuongea kwa sauti
ya juu na alionekana wazi kuwa alikuwa amekata
tamaa.
Ile hali yake ya kukata tamaa ikanikumbusha na mimi
njilivyokuwa nimekata tamaa akanishika mkono na
kunipa tumaini jipya sasa ilikuwqa zamu yangu
kumwonyesha kuwa nazilipa fadhila zake hapahapa
duniani na liwalo na liwe.
Nikaamua kutofuata utaratibu wa mahakama
nikaamua kuipaza sauti yangu ilimradi tu wachache
wanisikie wakaitangazie Tanzania na dunia kwa
ujumla.
Nikaingia katikati ulinzi haukuwa imara sana kwa
sababu mahakama ile ilikuwa haiwezi kutoa hukumu
kwa kesi ya jinai kama ile basi walikuwa wanatoa
tamko la kuifikisha kesi ile katika mahakama ya
makosa ya jinai.
Nikasimama katikati ya mahakama nikiwa sina mikono
yote miwili. Nikiwa sina sikio na sikuwa na kidole
changu mguuni.
“Naitwa Majaliwa… naomba nisikilizwe!!” niliipaza
sauti na mahakama nzima ikatulia badala ya kuchukua
hatua za kunitoa pale.
Bila shaka kila mmoja alikuwa amepigwa na
bumbuwazi!!
“Huyu mbele yenu anayetuhumiwa kuwa ni muuaji wa
albino si kweli badala yake mwenye haki
anagandamizwa kama muonavyo…. Huyu si muuaji bali
mtetezi wa haki zetu sisi walemavu wa ngozi.
Ameniokoa mara mbili bwana huyu, si mtu mbaya na
ninatamka mbele yenu kuwa wakati akiwa katika
harakati za kumtambua muuaji wa albino na
kufanikiwa kumpata ndipo hapo amegeuka kuwa mtu
mbaya. Nikataja jina la yule kiongozi ambaye daktari
alitueleza kuwa anahusika na unyama huo. Na hapo
nikawa kimya nikisubiri muujiza nilioumba kutoka kwa
muumba wa nchi na ardhi.
Nilitazamana na daktari walau alionyesha uhai katika
macho yake na alionekana kujaribu kutabasamu lakini
akaishia katika maumivu. Naam! Ukawa muujiza kweli
ulioambatana na kizaazaa…..
Askari wakanifuata pale waweze kuniondoa pale
mahakamani, yule kiongozi alikuwa pale mahakamani.
Watu wakaanza kumzongazonga na kumuuliza
kulikoni.
Nguvu ya umma!! Iache iitwe nguvu ya umma.
Askari walikuwa wachache raia wakamvuta yule bwana
njer na sijui kilichofuata ni kitu gani zaidi niliyasikia
tu mabomu ya machozi yakifyatuliwa na kikazuka
kizungumkuti kila mmoja akijitafutia usalama wake.
Polisi waliokuwa wamenidhibiti wakaniachia na mimi
nikawaponyoka kwa kasi na kuelekea popote ambapo
ningeweza kuwa salama.
Lakini sikufika mbali nikaanguka chini, nilichokiona ni
umati mkubwa ukija upande wangu na kisha kupita
kwa kasi wakinikanyaga kana kwamba hapakuwa na
mtu pale chini. Nilijaribu kuwasihi kuwa
wasainikanyage lakini haikuwezekana.
Nikaanza kukosa hewa palepale chini, nikatambua
kuwa iwe isiwe kwa safari ile siwezi kupona tena.
Nikayafumba macho yangu na kumtukuza Mungu kwa
kila jambo lililotokea na hapo kiza kinene kikatanda.
Fahamu zilirejea tena!! Mungu yu wa ajabu sana!!!
Sawa nilikuwa hai lakini nilipokuwa hapakuwa sehemu
sahihi.
Kweli ilikuwa nyumba nzuri haswa na nilikuwa
nimevalishwa nguo nyingine kabisa.
Lakini nilipotazama ukutani nikaiona picha fulani
ambayo haikuwa ngeni hata kidogo.
Ilikuwa sura mbayo nimewahi kuiona kabisa,
nikaitazama vyema sana na hatimaye nikakumbuka
kuwa sura ile niliiona pale mahakamani.
Ilikuwa ni sura ya yule bwana mwanasiasa ambaye
alikuwa akimtuhumu daktari kuwa anahusika katika
harakati haramu kabisa za kuwaua maalbino.
Nikiwa bado pale ndani niliusikia mwili wangu ukiwa
katika maumivu makali sana. Nikajitahidi kujiweka
sana, nikaweza kuuona mguu wangu ukiwa katika
bandeji gumu maarufu kama P.O.P.
Nikatambua kuwa nilikuwa nimevunjika mguu wangu.
Bila shaka nilipoanguka pale chini kisha watu
wakanipandia juu yangu.
“Naona umeamka mwanaharakati..” nikaisikia sauti
ikitokea nyuma yangu.
Nilipojitahidi kugeuka nikakutana na sura ya yule
mwanasiasa.
Sikujibu kitu chochote kwa sababu swali lake lilikuwa
la kinafiki haswa.
Nikajilaza na kusubiri kitu ambacho ataamua juu
yangu. Mwili wangu ulikuwa umeingia ganzi tayari na
sikuwa mwenye hofu kama awali nilijiona mimi kama
mtu wa kufa tu ambaye sina haki ya kuishi tena.
Yule bwana alizungumza mambo mengi sana
alinitukana kila aina ya tusi ambalo kinywa chake
kilihimiri kuweza kulitamka. Akanitukania mama
aliyenizaa na ukoo wangu kwa ujumla. Akawatukana
walemavu wote wa ngozi na kisha akaanza kujisifia
kuwa yeye na nguvu alizonazo, nguvu zake dhidi ya
viongozi wa serikalini, nguvu zake dhidi ya mahakama
na penginepo ambapo alijisikia fahari kupataja.
Katika maongezi yake kuna kitu alisema nikajikuta
natabasamu. Alisema eti anamshukuru Mungu kuwa
utajiri wake amepambana mwenyewe kuupata na si wa
kurithi kutoka kwa wazazi wake.
Nilitabasamu kwa sababu nilitambua kuwa hata watu
wakatili wanatambua kuwa Mungu yu hai. Sasa kama
wanatambua hili ni kwanini wanathubutu kufanya uasi
mkuu kama huu ilihali wakitambua wazi kuwa siku ya
kiama tunahukumiwa kutokana na matendo yetu??
“Unanicheka eeh!!” alinichimba mkwara alipoona
natabasamu wakati yeye anazungumza.
“Hapana sikucheki mkuu, natabasamu kwa sababu
stori ya maisha yako inatia hamasa sana!!” nilimjibu
vile kwa lengo la kumtia hasira. Ikiwezekana achukue
maamuzi hata ya kunipiga risasi nife kuliko kuendelea
kuwa pale kisha aendelee kukata viungo vyangu na
nilitambua wazi kuwa sasa wangenikata sehemu zangu
za siri!!
Ndugu msikilizaji damu ilinienda kasi sana baada ya
kufikiria jambo hili, ule uoga ukarejea upya kabisa na
kujikuta nikiwa katika mtetemeko wa ajabu!!
“Ujue kijana ulijifanya mjuaji sana ulipojitokeza
mahakamani ukiamini kuwa utaniumbua. Ni vile tu
hauuijui serikali yetu vizuri wewe… serikali yetu
katika ngazi za chini imejaa ubadhjilifu mkubwa. Pesa
ina nguvu kuliko hiyo haki uliyokuja kuitafuta. Dah!
Ulinitisha kweli ulipojitoikeza pale nikasema sasa leo
nd’o mwisho wangu lakini nilipokumbuka kuwa pesa
inazungumza hofu ikapungua. Najua ulipoteza fahamu
hata hujui kilichotokea hadi sasa upo hapa…” alisita
kidogo kisha akaiendea glasi ya maji na kugida kwa
kipimo alichoridhika kisha akaitua glasi.
Alipotaka kuendelea kuzungumza nikamuuliza swali.
“Samahani kaka… kwani umnaamini kuwa Mungu
yupo?”
Lile swali likawa zito kwake na lilionekana kumkera
kwa sababu nilimuuliza ukweli kabisa.
Nilimuona akipumua kwa kasi bila shaka ishara ya
hasira. Nikaona niendelee kumpandisha hasira ili
afanye maamuzi kwa kutumia hasira yake.
“….tazama nilikatwa mkono mmoja, ukafuata mkono
mwingine, nikakatwa sikio kisha dole gumba langu,
sikia nilikanyagwa na watu hadi kupoteza fahamu na
kuvunjika mguu pia….. ni kitu gani unajifunza kupitia
maisha niliyopitia. Unadhani Mungu unayemshukuru
kwa kukupatia maisha bora anapendezwa na haya??
Naomba unijibu tafadhali la si hivyo jicho langu
litakushuhudia siku ya kiama ukiteketea na mto
usiopungua makali na sitasita kukuuliza tena ikiwa
unayo hofu na Mungu!!!” nilitokwa na maneno yake
kwa mtiririko usiokoma.
Maneno yale yakamkera sana kwa sababu moja tu,
nilikuwa nasema ukweli mtupu.
Akanifuata pale nilipokuwa!! Kabla hajanigusa
nikamchokonoa tena.
“Labda uniue lakini kama ni kunipiga nimepigwa sana
moyo na mwioli wangu vimekufa ganzi, tazama
usivichafue vigaye vyako kwa damu kwa jambo
linaloewpukika!!! Mtanzania mtaka madaraka na
hatendi haki kwa baadhi ya wananchi wake….. kiti cha
uongozi utakachokikalia kitakuhukumu viobaya
sana…..” nilimaliza kisha nikamfanyia ishara kluwa
anaruhusiwa kufanya jambo ambalo alikuwa anataka
kulifanya!!
Upesi akaondoka na kurejea akiwa na panga kali sana,
makali yale yalinitonesha moyo upya na kutambua
kuwa nilikuwa naenda kufa kile kifo ambacho nilikuwa
nakikataa kila siku.
Huyu bwana angenicharanga mapanga na kuniua!!!
Nakufa bila kumuona mama yangu!!
“Unajifanya unajua sana kutoa ushauri sivyo, hebu
lishauri panga hili lisikukate sasa….” Alisema huku
akijilazimisha kutabasamu. Nilimtazama kisha
nikafumba macho yangu!!
Nafsi ilikuwa katika unyonge mkubwa sana.
Alifika na kuanza kunivua ngua zangu.
Dah! Nilichowaza kukatwa sehemu zangu za siri
kilikuwa kinaenda kutimia!!
Hofu ikanitetemesha zaidi na kujikuta koo likinikauka.
Alifanikiwa kunivua nguo hovyohovyo na kujikuta
nikiwa uchi wa mnyama!!
Yule bwana alikuwa amenuia kabisa kuniumniza…
Sikuwa na mikono ya kujitetea…. Mtanzania
mwenzangu anaenda kunipa maumivu ambayo yeye
binafsi hatamani kuyapata na hawezi kuyahimili!!!
Nikafumba macho nikijilamisha kupoteza fahamu lakini
haikuwezekana nilimsikia kila alichokuwa akisema na
kutenda!!!
 
Uwiii jaman inasikitisha sana hii story hadi chozi limenitoka
Ee Mungu warehemu albino wote waliopitia maumivu kama haya
Ameeen
 
SEHEMU YA KUMI NA MBILI
Nikiwa nimeyafumba macho yangu huku nikitambua
fika kuwa iwe isiwe lazima tu yule bwana ataniua.
Nikajiona mzembe kufa kirahisi bila hata kuparangana
kana kwamba ni haki ya yule bwana kuniua.
Nikayafumbua macho ghafla na kumkuta akiwa
anajiandaa kunifanyia alichotaka kunifanyia. Bila
kutarajia nikajikuta nafanya kitendo cha kijasiri bila
kuwa na mikono yangu.
Ningetumia silaha gani kama sio meno yangu.
Mpenzi msikilizaji, hii sio simulizi ya kutungwa
ukalichukulia lililotokea kama jambo la kawaida.
Ni kweli yalinitokea.
Nikamrukia yule bwana nikiwa nimeyaandaa meno
yangu na kutua vyema katika shingo yake. Ikawa
bahati nzuri kwangu na mbaya zaidi kwake.
Meno yakainasa shingo ipasavyo.
Nilitumia nguvu zangu zote zilizokuwa zimebakia
mwilini kumjeruhi yule bwana, nikayaunganisha meno
yangu, kwa sikio langui moja nikakisikia kisu
alichokuwa amekuja nacho kikidondoka chini na yowe
kubwa likimtoka.
Nikazidi kumtafuna shingo yake huku nikijua kuwa ule
ndio ulikuwa mwisho wangu. Sikujali damu iliyokuwa
inaruka nilichotazama ni kwamba na yeye anaumia
kama tulivyokuwa tunaumia sisi.
Nikiwa nimemng’ang’ania yule bwana hadi sauti ikawa
imekatika. Nikasikia mtu akijaribu kunivuta kwa
nyuma, wakati huo yule bwana alilegea na kutua chini,
nikiwa nimelowa damu vibaya mno na mguu wangu
wenye lile hogo gumu kabisa, nikamtandika tege kwa
kutumia ule mguu wenye hogo.
Kimyaa!! Hakutikisika!!
Nikageuka nikakutana na mwanamke ambaye alikuwa
akijaribu kunizuia nisiendelee kumsulubu yule bwana.
Sikujali lolote sasa nilikuwa kama kichaa, nilimvaa yule
mwanamke nikaanguka nay echini.
Wakati naanguka nikakutana na picha ukutani yule
mwanamke akiwa na yule mwanasiasa.
Kumbe ni mke wake!!!
Hasira maradufu ikanipanda tena, nikaendelea
kutumia silaha ya meno. Nikamng’ata mkono wake
kwa nguvu zote akatapatapa na kunirusha huku na
kule.
Naam! Akafanikiwa kunitoa katika mkono lakini sasa
nikatua katika paja lake, bahati iliyoje. Niliingiza
meno yangu pale kwa jinsi yalivyopenya nikahisi ni kwa
namna gani alikuwa akiumia yule mama.
Na aumie tu kwa sababu nilitaka aumie sikumg’ata ili
afurahie.
Alipiga kelele kubwa sana na kisha akapoteza fahamu.
Upesi nikatoka katika chumba kile nikiwa natamani
sana kuwa ningekuwa na mkono nilichukue bisu lile na
yeyote atakayekuja mbele yangu awe halali yangu.
Lakini sikuwa na mikono tena. Nikaifungua milango
kwa kutumia miguu na mikono.
Hatimaye nikalifikia geti na huko nikakutana na
mlinzi.
Bila shaka alipagawa kuniona nikiwa nimevuja damu
kiasi kile.
Akaanza kunionya kuwa nisimsogele.
Ebwana eeh!b nikaisikia lafudhi yake, alikuwa na
lafudhi ya kabila langu.
Aikwambie mtu kuwa kabila halina thamani tafadhali
sana jifunze lugha mbalimbali jifunze makabila
mbalimbali pia ukiweza. Wakati mwingine ukizungumza
na mtu kwa kabila lake ama lugha yake anajikuta
anakusikiliza na kukupa nafasi ya kujitetea.
Palepale nikatumia faida ile ya lafudhi ya mlinzi
nikamsemesha kikabila.
“Naitwa Majaliwa mwenyeji wa Dodoma, Mgogo halisi
kabisa… ikiwa sawa kushiriki katika kuniua mimi ndugu
yako basi uniue kwa kutumia hilo gobole lakini kama si
sawa kushuhudia mimi ndugu yako nikifa tafadhali
nisaidie, nimeteseka imetosha sikuzaliwa unavyoniona
nilivyo, wamenikata viungo vyangu, tafadhali
usishiriki dhambi hii…’ nilizungumza kiujasiri sana.
Na kweli kabila likaleta uzito akaniuliza ni kipi
kimetokea hadi nimelowa damu vile. Nikamweleza kuwa
ilikuwa niuwawe. Ni Mungu tu ameniokoa.
Kweli ikawa yale ya damu nzito kuliko maji.
Akanisogelea huku akionekana kuwa na hofu
akanichukua na kunitoa nje, huko akaniambia kuwa
yeye ni mlinzi na huwa hajui ni kitu gani kinaendelea
pale.
Lakini kuna watu ambao huwa anawaona wakija eneo
lile na kuondoka. Na yale sio makazi ya mtu bali kwa
msimu tu.
Aliposema kauli hizi akanifanya nitambue kuwa eneo
lile ni la siri sana na ni maalumu kwa maovu kama
haya.
Ajabu sasa akanieleza kuwa eneo lile lilikuwqa lipo
Dodoma!!
Nilistaajabu mpenzi msikilizaji, yaani kumbe nilikuwa
nimepelekwa kufia katika ardhi yangu ya nyumbani.
Yule mlinzi akanieleza kuwa sitakiwi kuwa pale na hata
yeye pia hawezi kuwa salama ikiwa watafika watu
wengine ambao huja katika nyumba ile na kutambua
kuwa kuna kitu anakijua kilichotokea pale ndani.
Wakati anamalizia haya mara ikasikika gari iija kwa
kasi.
Akaniamrisha nipotee, na hapoi akaqongoza njia na
mimi nikimfuata nyuma.
Msikilizaji, sikio la mwanadamu hutumika katika
kubalansi mwendo, kwa jinsi nilivyosoma shuleni ni
kwamba mtu asipokuwa na masikio hawezi kuendesha
baiskeli wala hawezi kukimbia mwendo mrefu.
Sasa nilikuwa katika kuona kwa macho yangu, nilikuwa
naanguka hovyo hovyo yule mlinzi akawa
ananinyanyua na kuendelea kukimbia sikujua hata ni
wapi tulikuwa tunaenda.
Ila sikuchoka kwa sababu nilijua kuwa Mungu yu
pamoja nasi na ni yeye aliyeniokoa hadi kufikia pale
nilipokuwa.
Baadaye yule mlinzi mzee ambaye ndiye aliyekuwa
anaongoza njia alishikwa na kichomi, akaapa kuwa
hawezi kuendelea kukimbia. Nilitamani basi mimi
nimbebe lakini ningeanzaje sasa.
Akanisemesha kilugha akanisihi nikimbie tu na nikifika
kijiji cha tatu kutoka hapo niulizie kwa mzee
anayeitwa Chilongani. Nikishampata nimeweleze kila
kilichotokea na kisha yule bwana akajitambulisha kwa
jina la Gaspa.
Nikaendelea kukimbia huku nikiamini kuwa utakuwa
muujiza tu kufika salama.
Nilikimbia huku nikiendelea kuburuza mguu wangu
wenye bandeji gumu.
Ilikuwa ngumu lakini ningefanya nini, walau nilikuwa
katika ardhi niliyozaliwa huenda nilikuwa nimeikaribia
mikono salama.
Sikuwa hata naelewa ni umbali gani kukimaliza kijiji
kimoja hadi kingine lakini nilikimbia tu bila kukoma.
Hatimaye na mimi nilichoka hadi hatua ya mwisho.
Lakini bado niliendelea kutembea mwendo wa taratibu
sana.
Na hatimaye nikaamua kucheza pata potea.
Nikaiendea nyumba fulani nikaugonga mlango.
Niligonga kama mara tatu, hatimaye mlango
ulifunguliwa na mwanaume aliyekuwa na panga kali.
Akauliza kikabila, na mimi nikajibu kikabila. Nikataja
jina la Chilongani!!
Akaniuliza iwapo mimi ni mwenyeji eneo lile
nikamwambia kuwa ni mwenyeji kiasi kiasi fulani.
Akaniuliza jina la ukoo wangu, nikamjibu!!
Nilipojibu jina langu la ukoo, ghafla nikasikia kilio
kikubwa sana kutoka ndani.
Kilikuwa ni kilio cha mwanamke…..
Na mara yule mwanaume pale mlangoni akasukumwa
na kuangukia mbali na hapo nikajikuta natazamana
ana kwa ana na mama Majaliwa!!
Akanikimbilia kwa nguvu sana na kunikumbatia
tukaanguka chinbi wote.
Nilibaki tu kuita mama mama… nisijue ni kitu gani
naweza kusema.
Yaani usiku mnene kama ule nikiwa nahitaji msaada
mkubwa kabisa nakutana na mama yangu mzazi??
Nilistaajabu msikilizaji, nililia sana….
Mama yangu naye alilia sana!!
Wakati haya yakiendelea yule bwana aliyekuwa
ameanguka mbali alikuwa sasa amesimama akishangaa
kilichokuwa kinaendelea!!
Na tukiwa bado pale chini mama yangu alikoma kulia
kisha akaanza kuzungumza.
“Maiko nilikwambia ukabisha, nilikwambia mwanangu
anateseka, nilikwambia kuwa moyo wangu hauna
amani hata kidogo ukasema niache imani potofu.
Mungu alikuwa anasema na mimi, angali wamenitesea
mwanangu, angali wamemkata mikono… yaani… yaani
kweli wameniumizia mtoto wangu hivi..” mama
hakuendelea kuzungumza tena akaanza kulia kwa
sauti ya juu sana.
Sikuhitaji kuwaza juu ya nini kinachopita katika moyo
wa mama yangu. Nilijua ni misumari mikali sana
inaupasua moyo wake!! Mama yangu alikuwa anaumia
sana!!!
 
SEHEMU YA KUMI NA TATU
Mama aliendelea kulia kwa uchungu mkubwa sana
akiwa bado yupo pale chini. Alilalamika sana mama
yangu, nililisikia kila neno ambalo alizungumza yule
mama ambaye umri nao ulikuwa unamtupa mkono.
Aliilaumu serikali kuwa huenda haitulindi ipasavyo,
akailaumu nchi kwa ujumla huenda haituhitaji watu
kama sisi na hatimaye akaanza kumlaumu yule
mwanaume ambaye alimpachika mimba na baada ya
kujifungua mtoto mwenye ulemavu wa ngozi
akakimbilia mbali na kuitelekeza familia akaoa mke
mwingine.
Alimlaumu kwa yote mema aliyowahi kumuahidi na
kumsababisha apate uhakika kuwa mtoto
atakayezaliwa atalelewa vyema lakini mwisho wa siku
akaishia kutelekezwa, mama akalia sana akijilaumu na
yeye kwa kutowasikiliza wazazi wake waliomsihi kuwa
asikurupukie mapenzi.
“Labda nipo katika kuitumikia adhabu sasa, adhabu ya
kilio cha wazazi wangu. Lakini mbona sasa imekuwa
adhabu nzito kuliko uwezo wangu, mbona imekuwa
suluba isiyofanana na yote niliyowahi kufanya.
Mwanangu Majaliwa, sijawahi kukuchukia mtoto
wangu, sijawahi hata kufikiria kukuchukia nd’o maana
hadi umekuwa mtu mzima nikiwa nakulinda.
Nilishauriwa mara nyingi sana ulipokuwa mdogo kabisa
kuwa nikutelekeze kwa sababu utaniletea mikosi…
sikuwahi kukubaliana na hilo jambo hata siku moja.
Tazama nipo nawe hapa tena nakuambia tena neno hili
na liishi nawe kila utakapokuwa aidha kwa uhai ama
uzima. Nakupenda sana mwanangu wa pekee…”
Maneno haya ya mama yalikuwa mfano wa suluba
kubwa sana katika nafsi yangu, nililia sana kumsikia
mama yangu mzazi akiyasema yale tukiwa katika giza
lile.
Wakati tukiwa pale kwa mbali tukawasikia mbwa
wakibweka.
Nikamweleza mama kwa ufupi sana juu ya kilichokuwa
kikitokea huko nilipotoka, upesi akishirikiana na yule
mwanaume ambaye alikuwa ni mdogo wake yaani
mjomba wangu.
Wakaniingiza ndani na kuniambia niingia chini ya
uvungu na kisha nitulie tuli.
Kweli nilidumu pale kwa takribani dakika kumi kabla ya
kusikia mlango ukigongwa, yule mjomba akajikausha
kama aliyelala na baadaye akaamka. Akatoka nje na
nikawa nayasikia mazungumzo ambayo walikuwa
wakizungumza.
Nilijikuta natabasamu kwa ujanja alioutumia mjomba
wangu, yule mgeni aliuliza Kiswahili na yeye akamjibu
kigogo. Hivyo ikawa hakuna kuelewana!!
“Wewe jifanye haujui Kiswahili, nakuuliza hivi kuna
ugeni wowote mmepokea hapa mkwenu usiku huu….”
Akauliza kwa ukali sana lakini mjomba aliendelea
kujibu kikabila.
Bila shaka yule bwana alichukizwa nikasikia akiongea
maneno maneno kisha ni kama aliondoka. Maana
mjomba aliingia ndani na kuufunga mlango.
Baada ya dakika takribani mbili mlango uligongwa
tena, safari hii sasa hakuwa mtu mmoja bali watatu.
Wakajitambulisha kuwa wao ni watu kutoka jeshi la
polisi Tanzania, wanahitaji kufanya upekuzi kuna
jambazi ametoroka hivyo msako unafanyika kijiji
kizima kwa sababu wanaamini kuwa bado yupo hapo
kijijini.
Hapo sasa nilianza kutetemeka sana, mjomba alijaribu
kuweka ngumu akijifanya aelewi wanachomaanisha na
mara wakamsukuma akaangukia pale ndani. Wakaanza
kumurika na tochi zao. Nilitulia kama gunia ambapo
limehifadhiwa pale ndani.
Wakakifikia chumba alichokuwa amelala mama
wakamuamsha nikamsikia akilalamika kikabila pia kuwa
anasumbuliwa. Hatimaye akaamka na yeye akaendelea
kujifanya hajui Kiswahili.
Bila shaka jambo hili lilisaidia sana watu hawa
kupunguza umakini katika kufanya ukaguzi.
Hawakufika kabisa uvunguni nilipokuwea,
qwakaondoka huku wakijiuliza kuwa nitakuwa
nimekimbilia wapi.
Na hapo nikaamini kuwa uwepo wangu hai ulikuwa
unaenda kuwaweka watu wengi sana matatani.
Na ilikuwa ni heri kabisa katika mtazamo wao kuwa
nife na wao wabaki na uhuru wao. Mtazamo wqa kiuaji
kabisa na usiokuwa wa kibinadamu!!
Usiku ule ulipita kimashaka sana na kisha ukakuchwa
ule wakati wa kuanza rasmi harakati za kufichua
maovu yote.
Harakati ambazo zilijawa na ushuhuda wa damu za
wenzangu wengi. Nilivishuhudia vifo vyao kwa macho
yangu!!
Usiombe kupambana na adui mwanadamu mwenye roho
yap aka ambaye hana huruma kabisa.
Nami nilijikuta katika vita hivi baada ya kuanza
harakati hizi na niseme neno moja laiti kama
wasingekuwa mama na mjomba kujitolea hata uhai
wao nisingekuwa hapa kukusimulie hiki kilichonitokea.
Niliishi pale kijijini nikiwa nimefungiwa ndani muda
wote na eneo langu la kulala likiwa ni palepale
uvunguni. Yalikuwa maisha yanayostaajabisha lakini
ilibidi tu kuwa vile. Sikuwa na mikono hivyo ilimlazimu
mjomba wangu kuniogesha usiku na nilipohitaji
kwenda haja kopo lilikuwa pale ndani hivyo ni kama tu
nilikuwa mfungwa.
Ilifikia wakati nikazungumza na mama yangu na
kumuuliza mambo mengi sana kuhusu mimi na familia
yangu na pia juu ya watu wenye ulemavu wa ngozi,
nilimuuliza mama ambaye ni mwanamke pekee
ninayemuamini kupita wote hivyo hata jibu lake ni
lazima tu ningeliamini.
Nilimuuliza na kumtaka anieleze ukweli ikiwa sisi
albino tulikuwa nayo haki ya kuishi ama la!!
Mama alitabasamu kisha akajisogeza karibu yangu na
kunieleza maneno yaliyonitia moyo. Yalikuwa
machache lakini yalitosha kuwa tiba kwa jinsi
nilivyokuwa nimekata tamaa.
“Majaliwa ulipotoweka hata na nilipopatwa hisia kuwa
utakuwa hatarini baada ya vyombo vya habari
kutangaza juu ya miili ya albino waliokutwa
wamekatwa viungo vyao na kisha kufukiwa. Nilipiga
goti na nilimuuliza Mungu swali hilo, nikamwambia
kuwa ikiwa mwanangu Majaliwa na maalbino wengine
wamekuja duniani bahati mbaya basi naomba iwe kwa
heri kabisa kwa sababu wamerejeshwa sehemu
waliyostahili lakini ikiwa wapo sawa kabisa na sisi na
ule mzigo wa miezi tisa nilioubeba sikuubeba kuzaa
kiumbe kisichokupendeza wewe basi nipe nafasi ya
kumuona mwanangu tena akiwa hai. Upo nami hapa
majaliwa unadhani Mungu wetu huwa anaongopa??”
alimaliza kwa kuniuliza swali. Nikatabasamu kisha
nikamkumbusha mama ya kuwa nampenda sana.
Naye akanambia kuwa ananipenda zaidi!!
Akasimama na kuniacha pale ndani!!
****
Siku iliyofuata mjomba alishughulikia mpango wa mimi
kutoroshwa kimyakimya kutoka pale kijijini.
Nakumbuka siku ile nilimwambia mama kuwa ipo siku
haya yanayonitokea mama yangu nitayasimulia siku
moja huku nikiwa natabasamu kabisa tena tabasamu
kutoka moyoni.
Naam! Leo hii nawasimulia huku natabasamu.
Harakati za kutoroka hazikuwa nyepesi ilibidi mjomba
na mama wasaidizane kunipaka masizi usoni ili
nionekane kuwa ni mweusi wakanipaka na miguuni.
Nilipowekewa kioo mbele na kujitazama, nililia sana
lakini leo hii nikiikumbuka ile hali niliyokuwanayo
nacheka tu kwa sababu kiukweli nilikuwa kituko.
Lakini ningefanya nini kwa wakati ule na hali tayari
ilikuwa mbaya sana.
Nikaondoka mimi mama na mjomba tukapita njia za
hapa na pale na hatimaye tukapata gari ambalo
lilikuwa likifanya safari zake kuelekea jijini Dar es
salaam.
Hata kabla sijafika jijini nikakabiliana na balaa kubwa
barabarani.
Nasema tena kama usingekuwa uimara wa mama
yangu na mjomba basi mimi Majaliwa nisingekuwa
hapa.
Mungu awajaze nguvu zaidi watu hawa!!
Baada ya kupanda gari na kuchukua siti, mita
takribani mia sita mbele tairi ikapata pancha,
ikatengenezwa tukaendelea na safari baada ya muda
kidogo tena gari likachemsha. Yaani gari lilikuwa
linaharibika mara kwa mara. Sijui ila nahisi tangu
awali gari lile lilionekana kuwa bovu tu lakini kama
kawaida huwa hakosekani mbuzi wa kafara. Abiria
wakaanza kulalamika kuwa kuna kitu ndani ya gari
ambacho si sawa kabisa.
Wengine wakasema patakuwepo na mtu amebeba
maiti, wengine wakasema hili na lile.
Na mwisho ikakubalika kuwa gari likiharibika tena
itabidi mbuzi wa kafara atafutwe ilimradi tu safari
iweze kuendelea vizuri!!
Ilikuwa baada ya nusu kilomita tu, gari likazima tena.
Sasa ikawa kwamba kila abiria amkague mwenzake na
akihisi kama kuna utofauti wowote ule atoe taarifa
na baada ya hapo itakaguliwa mizigo yote.
Pembeni yangu alikuwepo mzee mmoja mkimya sana.
Akanigeukia!!! AKAANZA kunitazama kwa mashaka
huku akijaribu kunikaribia zaidi.
 
SEHEMU YA 14

YULE mzee pembeni yangu alinitazama katika namna
ya kunitilia mashaka. Awali nilidhani ataishia
kunitazama mara moja na kuachana na mimi lakini
ajabu sasa alizidi kukazia kuwa anamashaka na mimi.
Ubaya ni kwamba huyu hakuwa wa kabila langu labda
ningeweza kumsihi na angeweza kuwa ha huruma.
Nilijaribu kumpuuzia yule mzee lakini sasa alimgusa
bega abiria mwingine. Alipogeuka akamwonyeshea
kidole kuja kwangu.
Wakagusana kadhaa na kisha mmoja akasimama na
kunifuata pale nilipokuwa.
“Msinigusie mwanangu nasema….” Mama alikaripia
baada ya wale watu walipoanza kunizongazonga
wakidai wana mashaka juu yangu.
“Watu wanabeba misukule wanatuletea mikosi tu
safarini.” Ilikuwa sauti ya kondakta wakati huo
akiwapangua abiria kadhaa na kunifikia.
Sasa mjomba wangu alisimama na kunikingia kifua,
akadai kuwa ikiwa kondakta anataka shari basi
athubutu kunigusa.
Hapo zikaanza vurugu, kundi kubwa likitupinga,
nadhani walikuwa sawa kabisa kutuona kuwa sisi ni
watu wabaya lakini wangejua magumu yote
niliyoyapitia si wanawake si wanaume wote
wangefunikwa nyuso zao na machozi.
Kondakta alifika na kumsukuma mjomba wangu na
hapa ndipo nikaelewa nini maana ya damu nzito kupita
maji.
Mjomba alifyatuka na kumtandika kichwa kikali sana
yule kondakta.
Palepale akaanza kuvuja damu na hapo watu wengine
wakatishika.
“Wapumbavu wakubwa nyie.,.. wapuuzi kabisa na
imani zenu dhaifu kabisa. Gari lenu bovu mnaanza
kubughudhi watu… sasa mwingine anayejiamini
amsogelee mpwa wangu!!” aling’aka. Nikayakumbuka
maneno ya mama ambayo aliwahi kunieleza zamani
sana kuwa ana mdogo wake ambaye ni mpole sana
lakini ukitaka kumkera wewe mguse tu ndugu yake
ama rafiki yake. Hasira yake haipoozwi kwa namna
yoyote na yupo radhi ajeruhiwe lakini si mwepesi
kukubali kushindwa.
Hakuna mtu aliyesogea, yule kondakta akajaribu
kumtupia teke mjomba. Kilichomtokea akadakwa mguu
na kisha kutupwa mbali. Kikasikika kilio cha maumivu!!
“Tupatie nauli yetu na tutashuka!! Tuwaache na gari
lenu bovu!!” alizidi kuwaka mjomba wangu ambaye
mwili wake ulikuwa wa wastani tu.
Mjomba akiwa hajui hili wala lile mara ghafla dereva
wa lile basi aliingilia kati, akarusha ngumi mjomba
akaikwepa akarusha teke likampata mjomba. Mjomba
akiwa hajatulia mara nikashuhudia yule dereva
akijipekua na kutoka na bisibisi, nikapiga kelele lakini
nilikuwa nimechelewa sana yule dereva akamfikia na
kumchoma begani.
Kizaazaa!! Mjomba aliendelea kupambana huku mama
akijaribu kuachanisha ugomvi ule.
Mwisho wa hili tukio hili tulisukumwa nje ya gari kwa
sababu mjomba alikuwa amejeruhiwa tayari hivyo
hakuweza kupambana. Basi abiria wakatusukuma nje.
Nikiwa sina hata mkono mmoja nikaanguka na
kujipigiza kichwa chini katika barabara ya vumbi.
Kumbe wakati naanguka mama yangu alimuona
mwanamke ambaye alinisukuma, nilipogeuka nikakuta
vurumai ya hali ya juu sana.
Mama alikimbia na kumchomoa yule mwanamke kutoka
katika kundi la abiria wale na kuanza kumshushia
kipigo huku akizungumza maneno mengi.
“Unamjua huyu mtoto nimepitia naye uchungu gani we
mwanahizaya.. sasa leo utatambua nini maana ya
uchungu wa mwana aujuaye mzazi” alimgalagaza yule
mwanamke pale chini.
Yule mwanamke alipiga mayowe ya uchungu mama
akaendelea kumkaba huku akimpa kichapo cha uhakika.
Nikiwa pale chini nikazitazama mbingu na kumshukuru
Mungu kwa sababu alikuwa akinionyesha maana ya
pendo la mama.
Nilijisikia fadhaa sana kwa sababu sikuwa na mikono
ya kumsaidia. Laiti kama ningekuwa mzima nilikuwa
nakaribia kuingia chuoni na bila shaka baada ya hapo
ningekuja kumsaidia mama yangu, kumtoa katika
dimbwi la umasikini na shida zile zilizopitiliza.
Wakati nayawaza haya mara nilimuona mwanaume
mmoja akimwendea mama yangu na hapo akampiga
teke kali mgongoni.
Ndugu msikilizaji, mama alimwambia yule mwanamke
kuwa uchungu wa mwana aujuaye mzazi. Hii ikawa
zamu yangu kumwonyesha yule bwana kuwa licha ya
kwamba sina mikono lakini siwezi kuhimili kushuhudia
mama yangu akiumizwa vile.
Nilijikuta nipo wima na mbio mbio nilimfikia yule
mwanaume.
Ilikuwa kama nilivyomkabili yule mwanasiasa. Na huyu
nikamtia meno katika bega lake na hakuweza
kuchomoka kirahisi hadi nilipomwachia akaanguka chini
huku akilia kwa uchungu mkubwa!!
Wakati huo gari lilikuwa limetengemaa, wakambeba
yule mwanaume na kumpakia garini. Kisha tukatengwa
na kuachwa pale chini.
Mimi, mama na mjomba wangu ambaye lile jeraha
lilikuwa limemlegeza sana na mama yangu alikuwa
ameumizwa na lile teke alilopigwa na na yule bwana.
“Majaliwqa mwanangu, huwezi amini nina furaha
kubwa sana moyoni, ninafurahi kwa sababu nipo hapa
na wewe. Ukifa nitakufa mwanangu sitakuwa na
sababu yoyote ya kuishi bila wewe. (akasita kisha
akamgeukioa mjomba)… Emma asante sana mdogo
wangu, yaani umenipa sababu ya kutabasamu. Asante
kwa kumtetea mwanangu. Najisikia vibaya sana kwa
sababu hatujaweza kufika tunapotakiwa kufika lakini
hebu tuungane na kumuombha Mungu maana ni yeye
anayeruhusu haya yote yatokee.
Tazama tupo jangwani hapa sijui hata ni wapi hakuna
nyumba za kuishi wala maeneo yoyote ya biashara
lakini amini kuwa yeye anatuona na anajua kuwa kwa
akili zetu hapa hatuwezi kutoka. Amini kuwa
asipotutumia msaada basi atakuwa pia ametupangia
jambo ambalo ni jema kwake…” mama alizungumza
kwa sauti ya chini huku sasa akisimama na
kujikongoja huku akiwa ameinama, bila shaka alikuwa
akipitia maumivu makali ya mgongo baada ya
kukanyagwa na yule bwana.
Alinifikia na kunikumbatia kisha tukasogea hadi
alipokuwa ameketi mjomba.
“Naishiwa nguvu na ninahisi kizunguzungu… sijui
kama nitapona… najisikia vibaya sana…” mjomba
alilalamika huku akiwa analigandamiza bega lake.
Alikuwa amevuja damu sana hakika na kama
alivyosema ilikuwa ni nadra sana kupona hasahasa
eneo kama lile ambalo hatukuwa na msaada.
Mama shujaa hakuacha kauli ya mjomba iwe neno la
mwisho. Akaondoka na kunisihi nisisogee popote pale
nitulie na mjomba wangu.
Akaondoka kwenda kutafuta msaada wowote ambao
utapatikana.
Alitumia takribani dakika thelathini, nikaanza kupatwa
na mashaka juu ya baya lolote ambalo limemkuta mama
yangu. Tatizo aliniambia nisitoke pale kabisa
alipokuwa amejilaza mjomba.
Yale mashaka juu ya mama yakanifanya kwa muda
nisahamu kumtazama mjomba.
Na nikiwa bado pale mara nikaona gari ikitokea mahali
kuja upande wetu.
Nikamshtua mjomba ili aamke kuitazama gari ile
ndogo.
“Mjomba… mjomba…” nilimuita lakini hakunijibu na ile
gari ilizidi kukaribia eneo tyulilokuwepo.
Nilimtikisa mjomba wangu lakini hakusema neno
lolote.]
Hatimaye gari likafika tulipokuwa, mjomba hakuwa
ameamka na ndani ya gari akashuka mama
akiongozana na wazungu wawili.
Akawaonyeshea kwa kidolea lipokuwa mjomba.
Walau kidogo nikapata nafuu. Kwani nilikuwa
nimeingiwa na mashaka kuhusu mama yangu.
Nikatabasamu lakini tabasamu lile halikudumu kabisa
baada ya wazungu wale kuzungumza kwa lugha ya
kiingereza kuwqa mjomba wangu alikuwa amekufa
tayari.
Ndugu msikilizaji nililia sana hakika, nililia kupita
maelezo. Mama kiutu uzima alijikaza lakini macho yake
yalikuwa mekundu sana.
Wale wazungu wakajadiliana na kisha wakapiga simu.
Baada ya muda mrefu kiasi ikafika gari ya kubeba
wagonjwa na kuubeba mwili wa marehemu mjomba
wangu.
Mjomba aliyenipigania hadi dakika yake ya mwisho,
mjomba aliyekufa kwa sababu alikuwa akinipigania
mimi.
Niliumia na hadi ninaposimulia mkasa huu maumivu yale
hayajaisha katika moyo wangu.
Naam! Tukaondoka na gari ile ikawa ni safari ya
kuelekea Dodoma lakini mimi nilizungumza na wale
wazungu na kuwaeleza ni kiasi gani nitaishi maisha ya
mashaka nikirejea Dodoma. Wale watu walikuwa na
utu sana walilalamika sana juu ya imani hizo dhaifu na
baada ya pale wakakubaliana kuwa mmoja kati yao
atangulie na mimi jijini dare s salaam na mama
akashughurikie suala mla kumzika mjomba.
Mama hakuwa tayari kuniacha katika mikono ya mtu
yeyote yule na hakutaka kumuamini mwanadamu.
Akagoma katakata!!
Akasema ni heri aambatane nami kila kona!!
 
Duniani kuna watu wana roho mbaya na ni mashetani....wanaishi kama vile hakuna Mungu ama kama vile wataishi milele...wakati nasoma natamani hata isiwe hadithi ya ukweli...natamani iwe ya kutungwa maana haya maumivu hayabebeki...
 
Back
Top Bottom