Prof. Pembe: Utoaji mimba usio salama unaweza kuchangia kizazi kupasuka

BigTall

JF-Expert Member
Mar 9, 2022
422
1,049
Jamii imetakiwa kuwa makini na matumizi ya vidonge na njia mbalimbali zinazotumiwa kwa lengo la kutoa mimba kuwa zinaweza kuwa na madhara makubwa kiafya na hata kusababisha kifo.

Baadhi ya dawa ambazo zimekuwa zikitumiwa na watu wengi kwa matumizi ya utoaji mimba ni Misoprostol ambapo imeelezwa kuwa kuna Wanawake wengi wanatumia ndivyo sivyo licha ya umuhimu mkubwa wa dawa hizo kwa matumizi ya afya.

Hayo yamebainishwa wakati wa warsha ya maswala ya Afya ya Uzazi lililoandaliwa na Chama cha Wanasheria Wanawake (TAWLA) na wadau wake mbalimbali, lengo la warsha likiwa ni kuhakikisha maswala ya afya ya uzazi na changamoto zake zinapatiwa ufumbuzi.

Wakiwa na kauli mbiu ya Kutoka kwa Uhamasishaji Hadi Kuchukua Hatua: Kuboresha Mazingira ya Kisheria kwa Afya ya Uzazi, wamekutana na kujadiliana mambo mbalimbali katika Warsha ya Kuendeleza Afya na Haki za Ujinsia na Uzazi kwa Wanawake wenye Umri wa Uzazi Tanzania.

Prof. Andrea Barnabas Pembe ambaye ni Profesa wa Magonjwa ya Kina mama na Uzazi kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) ni mmoja wa waliochangia mada katika warsha hiyo kuhusu utoaji mimba usio salama na madhara yake, huyu hapa anaelezea:
Prof. Andrea Barnabas Pembe.jpg

Prof. Andrea Barnabas Pembe

Utoaji mimba usio salama
Mimba ambazo zimetolewa katika nja zisizo salama ni zile ambazo hazizingatii afya na utaalam wa mchakato wa zoezi hilo.

Katika Taifa la Tanzania suala la utoaji mimba lipo juu kama ilivyo katika nchi nyingine za ukanda huu, takwimu zinaonesha kuna wakinamama 36 wanaotoa mimba kati ya 1,000.

Madhara ya utoaji mimba usio salama
Utoaji mimba unaweza kukusababishia hali mbaya kiafya kama vile kiwewe (trauma), kuwa mgumba, kuharibu Shingo ya Kizazi, Msongo wa Mawazo na hata kifo.

Pamoja na hivyo utoaji mimba kuna wakati unaweza kuwa na athari kulingana na historia ambayo inaweza kuendana na mila na imani ya watu au jamii husika.

Msongo wa mawazo hasa kwa wanawake huwa una athiri Wanawake wengi baada ya kutoa mimba.

Mwanamke anaweza kupoteza damu nyingi, kupata maambukizi makali ya bakteria yanayoweza kuathiri mwili ukashindwa kufanya kazi na hata kupoteza uhai wake.

Madhara mengine ni uwezekano wa kushindwa kupata mtoto kabisa kwa kuathiri mirija ya mfuko wa kizazi kuziba, pia aina ya utoaji mimba inaweza kuchangia ukuta wa mbele na nyuma wa mfuko wa kizazi kugandamana pamoja.
Misoprostol.jpeg
Elimu ya uzazi itolewe mapema
Nashauri Elimu ianze kutolewa mapema zaidi kwa kuwa tunajua vijana wengi wanafanya vitendo vya kujamiiana wakiwa na umri mdogo, hata mabinti wanaovunja ungo zamani ilikuwa wanatokewa na hali hiyo wanapokuwa na umri wa miaka 15 na kuendelea lakini kwa sasa hadi miaka 11 hadi 12.

Wanatakiwa kupata elimu hiyo mapema ili kuwaanda kujua ambacho wanaweza kukutana nacho, kwa kuwa wanavunja ungo mapema wanatakiwa kufundishwa namna ya kudhibiti mihemko yao.
Prof. Pembe.jpg
Utoaji mimba mitaani
Mwanzoni mwa miaka ya 1990 tuliona waliokuwa wakijaribu kutoa mimba kwa kutumia spoku za baiskeli, vijiti vya miti, vipande vya mizizi n.k kwa kuingiza vifaa hivyo kwenye nyumba za mimba wakiamini itatoka, walipata madhara mengi.

Wengine walienda kwa wahudumu wa afya ambao hawakuwa na utaalam wa kutoa mimba wakaishia kupata madhara makubwa. Wengine walitumia chai yenye majani mengi, kemikali kama vile Jiki, dawa kama kolokwini.

Zamani pia kuna walioamini mjamzito akifanya mazoezi makali au kazi ngumu au kukimbia basi mimba itatoka na wapo ambao waliamini kupigwa sehemu ya tumbo basi mimba itatoka, hiyo ilikuwa ni kutokana na uelewa mdogo waliokuwa nao.

Matumizi ya vidonge vya Misoprostol kutoa mimba
Misoprostol ni dawa muhimu lakini inaweza kuwa dawa hatari kutokana na matumizi husika, inafanya kazi kwa kuufanya mfuko wa kizazi kujikunyata na kukakamaa, hivyo kilichopo ndani kinaweza kutoka nje.

Ikitumika ndivyo sivyo kwa Mwanamke mwenye ujauzito mkubwa mfano ulio katika hatua ya tatu ya umri wa mimba, inaweza kusababisha msuguano mkali na kupasua kizazi na ikiwezekana mhusika kufariki kwa kupoteza damu nyingi.

Misoprostol ni dawa za nini?
Inapotumika inaweza kutoa ujauzito ambao upo katika hatua ya kwanza, uwezo wakewa kutoa mimba ni kati ya 73% hadi 96%.

Misoprostol iligunduliwa ili kutibu vidonda vya tumbo lakini matumizi yalipoendelea watu wakabaini inasababisha mfuko wa kizazi kusinyaa, walipobaini hivyo madaktari wakaanza kugeuza matumizi kutumiwa na Wanawake zaidi badala ya wagonjwa wa vidonda vya tumbo.

Moja ya matumizi mengine ya Misoprostol ni wakati kiumbe kimefia tumboni na inabidi kitolewe, unaweza kuitumika dawa hiyo kwa kulainisha shingo ya kizazi ili kufanikiwa kutoa.

Mwanamke anapokuwa na presha kubwa wakati wa kujifungua, Misoprostol inaweza kutumika kuanzisha uchungu hadi pale mama anapojifungua salama, hivyo ina faida nyingi kiafya lakini tatizo ni matumizi yanapokuwa si sahihi.

Matumizi mengine ni wakati mama aliyejifungua na kuanza kutoka damu nyingi kutokana na mfuko wa uzazi kutosinyaa, hivyo Misoprostol inaweza kutumika kwa kunywa, kuweka chini ya ulimi, mashavu au njia ya pull, dawa hiyo inasababisha mfuko kuanza kukakamaa na kuzia damu kuendelea kutoka.

Ujauzito wa ndugu unaweza kuambukiza magonjwa
Jamii inatakiwa kutambua kuwa maadili hayaruhusu ndugu wa kujamii, hilo ndilo la msingi tunalotakiwa kulizingatia.

Upande mwingine kitaalam kuna magonjwa yanayoendana na koo, mfano kama Selimundu (Sickle Cell) au Ualibino (albinism), hivyo ndugu wa aina moja wanapozaa uwezekano wa kupatikana au kutokea magonjwa ya koo ni rahisi.
Sehemu za huduma ni changamoto
Kuhusu huduma za afya bado hatuna wahudumu wa kutosha Nchini, pia vituo vyetu vingi vya afya zipo mijini kuliko vijijini.

Vijijini kuna vituo vya afya na zahanati na hakuna wataalam wengi kama ilivyo Mjini ambapo kuna hospitali kubwa.

Mada ya umri wa ndoa
Akizungumzia kuhusu mada ya umri sahihi wa ndoa, Wakili Fulgence Massawe anasema: Sheria inasema ukimuingilia mtoto chini ya miaka 18 inasema umembaka Sheria ya Ndoa inayoruhusu ndoa kuanzia umri wa miaka 15.

Mazingira hayo yanafanya mgogoro wa umri wa ndoa hauwezi kuisha leo wala kesho kwa kuwa ikifika hatua ya Serikali kufanya maamuzi kuhusu suala la umri inaogopa kutekeleza.
 
Nachukia sanaa wanaotoa mimba, ikiwezekana watumie tu hiyo ili vizazi vipasuke wasiwe na uwezo wa kuzaa kwa kuwa hawana haja na watoto
 
Back
Top Bottom