Ongezeko la nauli ya vivuko Dar liendane na huduma bora

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,318
33,125
KATUNI(602).jpg

Maoni ya katuni


Serikali imetangaza ongezeko la nauli za huduma za vivuko katika kivuko cha Magogoni-Kigamboni kwenye kivuko cha Feri, jijini Dar es Salaam.
Ongezeko hilo lilitangazwa juzi na Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, na kuibua mvutano mkubwa kati yake na na Mbunge wa Kigamboni (CCM), Dk. Faustine Ndugulile.

Waziri Magufuli alisema kuanzia juzi, wizara kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa), imeongeza viwango vya nauli katika vivuko vyote vya serikali nchini na kwamba, kutokana na mabadiliko hayo, nauli ya kivuko cha Magogoni-Kigamboni imeongezwa kutoka Sh. 100 iliyokuwa ikitozwa zamani hadi Sh. 200 kwa mtu mmoja.

Kwa mujibu wa uamuzi huo, mtoto asiyezidi umri wa miaka 14 atalipa Sh. 50 na atakayeruhusiwa kutumia huduma hiyo bure ni mwanafunzi tu atakayekuwa amevaa sare na kubeba kitambulisho cha shule.

Baiskeli itatozwa Sh. 300; pikipiki (Sh. 500); mzigo wa chini ya kilo 50 (Sh. 200); mzigo wa zaidi ya kilo 50 (Sh. 500); toroli (Sh. 1,500); guta (Sh. 1,800); Bajaj (Sh. 1,300); ng’ombe (Sh. 2,000); wanyama wengine, kama mbwa, mbuzi na kondoo (Sh. 1,000); gari ndogo (Sh. 1,500); Pick up ya chini ya tani 1.5 (Sh. 2,000); basi dogo la abiria 15 (Sh. 3,500); na trekta lisilo na tela (Sh. 7,500).

Waziri Magufuli alisema uamuzi huo umefikiwa na serikali baada ya kushauriwa na Bodi ya Temesa ili kuendana na gharama za uendeshaji wa vivuko.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Temesa, Profesa Idris Mshoro, alisema ongezeko la gharama za uendeshaji wa vivuko ndilo lililoifanya bodi yake kuishauri serikali kuongeza nauli hizo.

Uamuzi huoumepingwa vikali na Dk. Ndugulile, akidai kuwa utaratibu uliotumika kuongeza nauli za kivuko umewasikitisha umekuja ghafla bila kuwaarifu wananchi. Mbunge huyo alitumia lugha kali dhidi ya Waziri Magufuli akidai kuwa anawapotosha wananchi.
Jana wabunge wa mkoa wa dare s Salaam waliingilia kati kwa kutoa tamko la kumtaka Waziri Magufuli kuwaomba radhi wakazi wa

Jiji la Dar es Salaam kwa kauli zake ambazo walidai kuwa ni za kuwadhalilisha wakazi hao. Aidha, walitaka upandishaji wa nauli usitishwe kwanza hadi utakapowekwa utaratibu mpya.

Kwa kuwa serikali imeeleza kuwa lengo la kuongeza nauli ya vivuko ni kutokana na kupanda kwa gharama za kuvihudumia, ni vizuri kama pande zote zote yaani wizara, wabunge na wakazi wa maeneo husika kuacha malumbano na kutunishiana misuli, badala yake kutumia majadiliano.

Sio vizuri kutumia siasa katika kushughulikia changamoto kadha zinazojitokeza yanayojitokeza katika jamii. Itakuwa busara kama siasa itawekwa pembeni na changamoto zikashughulikiwa kwa kuzingatia hali halisi.
Ni ukweli kwamba hali ya maisha inapanda kila siku na kuwasababishia matatizo wananchi. Hata hivyo, ni vizuri kusikiliza hoja

zinazotolewa na upande mwingine kama walivyosema Waziri Magufuli na Temesa kuhusiana na kupanda kwa gharama ya kuendesha huduma za vivuko.

Bila shaka hakuna mwananchi ambaye hataki kupata kuduma ya kivuko, bali anachotaka ni huduma nzuri na ya uhakika. Haitakuwa busara kwa serikali kusitisha usafiri wa vivuko kwa sababu tu ya kuongezeka kwa gharama.

Huduma hiyo serikali ikijitoa na kuiacha kwa watu binafsi, wananchi wajue kuwa wataumia zaidi kwa kuwa watoa huduma binafsi wanajali faida zaidi.

Wananchi wanapaswa kuelewa kuwa kivuko ni mali yao hivyo wana wajibika kuchangia ili kitoe huduma kwa wakati wote ili kiweze kutoa huduma endelevu.

Wananchi wana haki ya kuhoji pale wanapoona kuna kasoro katika huduma zinazotolewa kwao, lakini wanapaswa kuwa makini ili kuepukana na kutumiwa na wanasiasa kwa maslahi yao binafsi.

Kwa upande wa serikali, inapaswa kuhakikisha kwamba huduma za kivuko zinaboreshwa ili ziendane na ongezeko la nauli iliyotangazwa.

Tunatarajia kuwa uongozi wa wizara, wabunge na wananchi wanaotumia huduma za kivuko hicho wanakutana ili kujadiliana kuhusu changamoto mbalimbali. Tunaamini kuwa kwa kufanya hivyo, mvutano uliopo utamalizika na shughuli kuendelea kama kawaida.



CHANZO: NIPASHE
 
Back
Top Bottom