Ombi kwa Watanzania wote wenye Upendo - Msaada wa HARAKA unatakiwa

August

JF-Expert Member
Jun 18, 2007
8,399
4,063
Nairat: Ninaumwa ugonjwa wa ajabu, nisaidieni

  • NI MTOTO MDOGO AMBAYE AMEKATISHA MASOMO KUSAKA MATIBABU

Sunday, 26 August 2012

Salma Said NAIRAT Hamis Ali ni mtoto wa miaka saba aliyelazimika kukatisha masomo yake katika hatua ya elimu ya awali baada ya kupatwa na ugonjwa wa ajabu ambao hadi sasa wazazi wake hawajui chanzo chake.

Ugonjwa huo pia umemwathiri dada wa Nairat aitwaye Bisambe huku jitihada za kupata matibabu zikiwa ngumu kutokana na hali duni ya kipato cha wazazi wao. "Mama, shuleni watoto wananiuliza, mbona ngozi yangu ipo hivi?"

Ndivyo anavyoanza kueleza Nairat alipofika kwenye Ofisi za gazeti la Mwananchi, visiwani Zanzibar. Nairat, ambaye wazazi wake wanaishi Tumbe, Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba amelazimika kukatisha masomo yake ya Chekechea kutokana na ugonjwa huo ulioanza kumsumbua tangu alipokuwa na miaka miwili.

Nairat ambaye anaonekana mcheshi na mwenye sura iliyobeba matumaini makubwa, anasema kuwa bado ana imani kubwa kuwa atapona na kuendelea na shule. "Nataka kusoma, lakini ninaumwa. Nikitibiwa na kupona nitarudi shule.

Pia nilikuwa nasoma chuo, najua kusoma Quraan. Lakini sasa ndiyo nimekuja Unguja kutafuta dawa," anasema Nairat akiinamisha uso wake chini. Ngozi yake imekuwa nyeusi na kuwa na mabaka, vidonda vimezunguka mdomo wake na macho yameota vidonda na kuanza kupoteza nuru ya kuona.

Nairat anasema kuwa vidonda vilivyozunguka midomo yake vinamsababishia kushindwa kula kutokana na maumivu hivyo muda mwingi analazimika kukaa na njaa akihofia maumivu. Mama yake Nairat Mama mzazi wa Nairat, Khadija Mohammed (30) anasema kuwa mtoto wake mara nyingi huwa hapati usingizi usiku kwa kulia kutokana na maumivu anayoyapata.

"Wallahi mwanangu usiku analia tu kwa maumivu, awali nilikuwa nikimpa dawa zilizokuwa zikimsaidia kupata usingizi, lakini dawa zimeniishia kwa kuwa sina pesa," anasema Khadija kwa uchungu akiongeza:

"Kula hawezi kwani akitia chakula tu anaanza kulia akisema anaumia. Maji pekee ndiyo anaweza kunywa."

Kwa mujibu wa Khadija ambaye alifuatana na watoto wake wawili wote wakiwa ni wagonjwa, dawa za kupunguza maumivu zinauzwa Sh70,000 na kwamba yeye hana uwezo wa kumudu gharama hizo. Mbali ya Nairat mtoto mwengine ni Bisambe ambaye pia ana ugonjwa wa ngozi kama wa Nairat huku pia akiwa ameacha shule.

Watoto wengine wa Khadija ni Yussra (5) na Abdul (2) ambao wapo salama. "Hawa watoto wawili tangu wadogo wamepata ugonjwa huu, nimejaribu kutafuta tiba, lakini unajua tena ukiwa maskini huna pesa basi unashindwa.

Muda mrefu nilikuwa nataka kuja Unguja, lakini nilishindwa," anaeleza Khadija. Mama huyo anasema kuwa maradhi hayo yaliwaanza watoto wake polepole na kwamba aliwapeleka katika Hospitali za Pemba na baadaye alilazimika kwenda Unguja baada ya madaktari kumshauri. Anasema kuwa hata alipofika Unguja alitakiwa kwenda Dar es Salaam ambapo anasema ameshindwa kutokana na kukosa fedha.

Mama huyo anasema kuwa mbali na kuhangaika huko Pemba na kushauriwa kwenda Unguja kutafuta matibabu, alilazimika kumwachisha shule Basimbe ili waende wote Hospitali ya Mnazi Mmoja Unguja, ambapo alipatiwa dawa na kushauriwa waende katika Hospitali ya Kanisa Katoliki iliyopo Machui, ambapo alipata matibabu.

"Nilipelekwa Machui nikapata dawa, lakini sikuweza kuendeleza kwa kuwa zimenishinda kwani sikuwa na fedha za kutosha,"anasema Khadija huku akiwaangalia watoto wake machoni. Anafafanua kuwa baada ya madaktari wa Hospitali ya Mnazi Mmoja kushindwa kuwatibu, walimshauri kuwapeleka watoto wake Dar es Salaam na kumtaka atafute Sh2 millioni kwa ajili ya matibabu.

"Madaktari waliniambia nitafute shilingi millioni mbili lakini, hadi leo hii sijapata hata shilingi," anasema kwa masikitiko. Anasema amefanya juhudi mbalimbali za kutafuta fedha ikiwa ni pamoja na kwenda katika Ofisi ya Mufti wa Zanzibar na kupewa fomu za kuombea misaada kwa wafadhili na watu mbalimbali, lakini bahati mbaya licha ya kuhangaika mwezi mzima wa Ramadhani, hajafanikiwa kupata hata shilingi moja.

Anasema ana wasiwasi juu ya mustakabali wa maisha ya watoto wake kwani madaktari walimtahadharisha kuwa iwapo atachelewa kupata matibabu, hali inaweza kuwa mbaya na pengine ikashindikana kumaliza tatizo hilo. Khadija anawaomba watu wenye imani wamsaidie fedha kwa ajili ya matibabu ili kuweza kunusuru maisha yao, hasa Nairat ambaye kwa sasa yuko katika maumivu makali usiku na mchana.

"Tunahitaji kupata ushauri wa wataalamu wa afya na tunawaomba wenye uwezo wa kuwasaidia hawa watoto watuelekeze nini tufanye."
"Pia kwa wale wenye uwezo wa fedha nawaomba wanisaidie," anasema mama wa watoto hao.

Kwa mtu ambaye ataguswa na mateso ya watoto hao anaweza kuwasiliana na sisi kwa kupitia namba ya simu 0777 477 101 kwa ajili ya kuwasilisha msaada wake.
 
Pole zake.
Tatizo la mswahili kipaumbele ni msaada! Hahitaji dr wa ngozi ambae anaweza kujitolea kumtibu bure?
Alternatively, maombi ni bure kabisa. Lakini akishauriwa hivyo nahofia atakwazika.
MziziMkavu ngoja nikamlete, alikuwa anahesabiwa kwanza
 
Last edited by a moderator:
Poleni sana, ila napata tabu kidogo, je habari hii ina sura yoyote ya kisiasa? Au Tz siasa ni kila kitu na kila kitu ni siasa!
 
Poleni sana, ila napata tabu kidogo, je habari hii ina sura yoyote ya kisiasa? Au Tz siasa ni kila kitu na kila kitu ni siasa!


Hilo suali Hata Mimi nilitaka kuhoji bora umenisaidia ila tujiulize nani mwenye kosa aliyeleta hii mada hapa au ni moderator? Mod tunawekana Sawa tuu Mkuu asinipe BAN maana najua ukinipa ban basi hii itakuwa BAN FOR LIFE Tehe Tehe Tehe
 
Hilo suali Hata Mimi nilitaka kuhoji bora umenisaidia ila tujiulize nani mwenye kosa aliyeleta hii mada hapa au ni moderator? Mod tunawekana Sawa tuu Mkuu asinipe BAN maana najua ukinipa ban basi hii itakuwa BAN FOR LIFE Tehe Tehe Tehe

Maisha ya mwanasiasa ajaye! Hiyo ni siasa mkuu. Huyu lazima atakuwa mpiga au mpigiwa kura. Tumsaidie kwa moyo mmoja.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom