KWELI Ngozi ya kuku ina mafuta mengi, haishauriwi kuliwa na Watu wenye Changamoto za Moyo, kisukari na mafuta mengi mwilini

Taarifa hii imethibitika kuwa ya kweli baada ya kufanya tathmini ya kina
Nimekuwa nikisikia kuhusu madhara ya mafuta yatokanayo na wanyama (fat) kuwa huganda kwenye mishipa na kusababisha shinikizo la damu.

Kilichonishitua zaidi ni kuwa ngozi ya kuku kuwa ni hatari zaidi kwani huwa na mafuta mengi sana na husababisha cholesterol kwa kiasi kikubwa.

Hii imekaaje?

1710408212704.jpeg
 
Tunachokijua
Kuku ni miongoni mwa nyama ambayo hupendwa sana duniani. Ulaji wa nyama ya kuku ni maarufu kwa sababu ina mafuta kidogo na inakabiliwa na vikwazo vichache vya kitamaduni au kidini.

Aidha, ni nyama yenye protini nyingi na chanzo muhimu cha vitamini na madini. Na pia ina viwango muhimu vya mafuta yenye faida ambayo yanaweza kusaidia afya ya moyo na mishipa.

skilletchicken.jpg
Nyama ya kuku pia imezungukwa na mashaka na dhana tofauti kwani kuna madai kuwa ulaji wa ngozi ya kuku si salama kwani ina mafuta mengi ambayo husababisha madhara kwa mlaji. Hoja hii imekuwa na hisia tofauti miongoni mwa watu huku wapo wanaopinga na wapo wanakubaliana na hoja hiyo.

Baada ya mdau kuleta hoja hiyo, Jamii Check imepitia machapisho mbalimbali ambayo yamekiri kuwapo kwa kiwango kikubwa cha mafuta kwenye ngozi ya kuku.

Ngozi ya kuku ina asilimia 32 ya mafuta yaani, kwa kila gramu 100 za ngozi tunayokula, gramu 32 ni mafuta, María Dolores Fernández Pazos, mtaalamu wa lishe katika Kituo cha Taarifa za Lishe ya Nyama, aliambia BBC Mundo.

Kati ya mafuta haya yaliyomo kwenye ngozi ya kuku, anaelezea mtaalamu, theluthi mbili ni mafuta yasiyo na madhara, kile kinachoitwa "mafuta mazuri", ambayo husaidia kuboresha viwango vya damu. Na theluthi moja ya mafuta ndio ambayo huchangia kuongeza viwango vya mafuta "mbaya" katika mwili wa binadamu.

Hiki ni kiwango sawa cha mafuta kinachopatikana kwenye nyama ya kuku. Kwa hiyo, anasema mtaalam, ikiwa tunakula kuku na ngozi, tutaongeza ulaji kiwango cha kalori mwilini kwa takriban 50%.

Kwa hivyo, kwa mfano, ikiwa tutakula vipande sita vya nyama ya kuku isio na ngozi, tutakuwa tunatumia kalori 284 (kulingana na data ya lishe ya Idara ya Kilimo ya Marekani), huku 80% ya kalori ikitoka kwa protini na 20% kutoka kwa mafuta.

Lakini nambari hizo huongezeka sana ikiwa tunajumuisha ngozi: sehemu ya kifua cha kuku itakuwa na kalori 386, na 50% kutoka kwa protini na 50% ya mafuta.

Kwa hivyo, mtaalamu wa lishe Dolores Fernández anapendekeza, kuondoa (ngozi) kabla ya kula, ili kutoongeza kalori au mafuta zaidi kwenye sahani.

Kwa watu ambao hawana historia ya ugonjwa, na uzito wa kutosha kwa urefu wao, muundo wa mwili, tunaweza kupendekeza kuacha ngozi ya kuku wakati wa kupikia na kuiondoa kabla ya kula, kwa kuwa uwepo wa ngozi wakati wa kupikia utasaidia nyama kukauka kidogo na kuwa na ladha tamu zaidi. anasema mtaalam.

Pia, JamiiCheck imezungumza na Afisa Lishe Mtafiti kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Glory Benjamin ambaye ameeleza kuwa:-

Kuhusu ulaji wa ngozi ya kuku inategemea na mhusika mlaji, mfano ambaye hana masharti ya kiafya katika ulaji kama vile moyo upo vizuri, hana changamoto ya mafuta kuzidi mwilini, Kisukari na mengine kadhaa, anaweza kula kama kawaida.

Lakini mtu ambaye anaweza kuwa na changamoto ya masuala ya kiafya kama hayo na masharti anaweza kupunguza kula au kutokula kabisa, kwani Ngozi ya kuku huwa ina mafuta ambayo kama mtu anakula kwa wingi inamaanisha anajiongezea mafuta mwilini.

Mbali na hapo kuku wengi wa kisasa wanakuwa na mambo mengi yanayohusua dawa au tiba, mfano baadhi ya Kuku wamekuwa wakitibiwa kwa Antibiotic zinazotumika wakati wa makuzi ya kuku.

Hivyo, ulaji inategemea na Afya ya mtu lakini pia haishauriwi kula Ngozi ya kuku kila siku kwa kuwa ina mafuta na hata kama huna changamoto ya kiafya inaweza kusababisha ukajiongezea mafuta mwilini.


Hivyo basi JamiiCheck imejiridhisha kuwa ulaji wa ngozi ya kuku unategemea afya ya mtu iwapo hana changamoto ya moyo au uzito mkubwa anaweza kula ngozi ya kuku. Hata hivyo haishauriwi kula kila siku hata kama huna changamoto kwani itakuwa ni kujiongezea mafuta mengi mwilini.
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom