Mwanafunzi unayemfundisha: a child study project

Nov 23, 2018
49
87
Moja kati ya wajibu muhimu wa mwalimu wa shule ya msingi ni kuwafahamu wanafunzi wake ; kufahamu uwezo na udhaifu wao na kuwa na ufahamu fulani kuhusu historia ya makuzi yao ili kuweza kubuni mbinu mujarabu ya kuwasaidia kujifunza wawapo darasani. Kwa kweli hii si kazi rahisi hasa ukizingatia mafuriko ya wanafunzi kwenye baadhi ya shule, lakini ni muhimu sana. Vinginevyo mwalimu atakuwa mganga anayempa dawa mgonjwa bila kujua ugonjwa unaomsumbua.

Miongoni mwa mbinu zinazoshauriwa kutumiwa na mwalimu ili kuwajua vizuri wanafunzi wake ni kupitia 'Uchunguzi wa Macho'(observation). Mwalimu anapaswa kuwa na utaratibu endelevu wa kuchunguza tabia za wanafunzi au miitikio yao kwa baadhi ya mambo. Matendo ya uso(miayo, kununa,kusonya, kukodoa macho, kutabasamu ) humsaidia mwalimu kutambua mwitikio wa mwanafunzi kwenye kujifunza au kazi nyingine. Matendo ya mwili (utundu, kuchezesha vitu, kunong'ona na jirani yake, kukaa vizuri, macho kumfuata mwalimu) pia ni alama zitakazomsaidia mwalimu kujua mahitaji ya mwanafunzi. Tabia za kijamii za wanafunzi pia huchunguzwa. Hapa tunajiuliza ni namna gani mwanafunzi anaamiliana na wengine; pengine ana aibu mno au mkorofi akiwa kwenye kikundi chake.

Hata hivyo Uchunguzi wa Macho hautoshi. Mwalimu anaweza kufanya uchunguzi wiki hii kisha wiki ijayo akasahau yupi kati ya Somoe na Juma alionesha tabia fulani isiyoridhisha.Kwa hiyo mwalimu anahitaji rekodi ili kumsaidia kukumbuka.

Sehemu hii tutajikita kwenye mbinu mbili za kuweka rekodi za wanafunzi kutegemea 'uchunguzi wa macho'. Mbinu hizo ni 1.Mbinu Kaguzi (survey method) na 2.Uchunguzi Kifani (case study method)

Katika 'mbinu kaguzi' mwalimu huandaa orodha ndefu ya maswali anayotaka kuyajibu kuhusu mtoto fulani. Hamuulizi mtoto moja kwa moja bali atamchunguza mwanafunzi kwa kipindi fulani hadi atakapofanikiwa kukusanya taarifa za kutosha. (Si vema mwanafunzi akajua kuwa anachunguzwa kwani akijua ataacha kuwa katika hali yake ya kawaida. Jifanye huelewi chochote kuhusu mienendo yake ukiwa unamchunguza.) Kisha mwalimu atachambua taarifa zake kwa makini, akijaribu kupata picha halisi ya mwanafunzi wake ili kuweza kumsaidia katika ujifunzaji darasani.

Mbinu ya 'uchunguzi kifani' inatofautiana na 'mbinu kaguzi' sio katika aina ya rekodi bali kwenye mbinu ya 'uchunguzi wa macho'. Mwalimu anapotumia mbinu ya 'uchunguzi kifani', hurekodi matukio mahususi aliyoyachunguza kwa mwanafunzi. Atarekodi kwa makini kilichotokea na jinsi mwanafunzi alivyoitikia. Uchunguzi kifani utaposhamiri, mwalimu atatengeneza rekodi ya kuvutia kuhusu tabia ya mtoto katika hali tofauti. Hizi chunguzi kifani alizozofanya mwalimu zitachambuliwa ili hatimae ziweze kumsaidia mwalimu kuja na mkakati kabambe utakaomsaidia mtoto kujifunza vizuri.

Aidha mwalimu anaweza kutumia mbinu ya 'uchunguzi kifani' katika mchakato wa ufundishaji darasani. Wanafunzi wanapoonesha vitendo visivyo vya kawaida wakati wa uwasilishaji darasani, mwalimu atapaswa kuandika kilichotea na waliohusika. Hiyo itamsaidia mwalimu kwenye tathmini kuona ikiwa somo limeeleweka au bado atapaswa kurudia tena. Pia itamsaidia mwalimu kubaini sehemu alizopatia na kukosea katika ufundishaji ili kuona namna mbinu yake inavyofanya kazi au imeshindwa kufanya kazi.

Huu ni mfano wa 'uchunguzi kifani' ulioandaliwa na mwl Longino kuhusu eneo la Nidhamu.

UCHUNGUZI KIFANI
Uchunguzi huu unamhusu binti mdogo wa darasa la Awali hapa shule ya msingi Ngorongopa-Liwale-Lindi. Alikuwa mtoto makini darasani na kwakweli alifanya vizuri kwenye mahiri zote. Kama alikuwa na tabia isiyopendeza basi, ilikuwa ni kucheka kupita kiasi. Kwake kila kitu kilikuwa ni kiroja na alikuwa anaangusha kicheko wakati wowote anaopoamua hata kama katikati ya kipindi. Tabia hii ilikuwa inawasumbua watoto wengine kwani alikuwa anacheka kwa sauti kubwa. Baada ya kuwa naye kwa takribani miezi sita, niliona naweza kumsaidia kwa kumuangalia usoni kwa namna fulani. Hii mbinu nilijifunza kwenye moduli ya kwanza ya ya mafunzo kazini chini ya mradi wa EQUIPT.
Baada ya kumtazama usoni mara kwa mara aligundua alipokosea na akawa anapenda kunifuatilia wakati wote wa ujifunzaji darasani. Ni sawa na kusema ameweza kuusoma uso wangu, nikitabasamu anajua naridhishwa, nikikaza sura anajua sijaridhishwa na vicheko vyake. Hadi hivi leo nimefanikiwa kumdhibiti mtoto mwenye tabia ya kucheka kwa sauti darasani bila kutumia viboko.

Hata hivyo mwalimu hawezi kuwa na muda wa kutosha kutumia 'mbinu kaguzi' na 'uchunguzi kifani' kwa wanafunzi wote kila siku. Mwalimu atatumia mbinu hizi wakati atakapoamua kumfuatilia mwanafunzi mahususi anayeonesha tabia zisizo za kawaida ili kumsaidia katika ujifunzaji. Sanjari na hilo mwalimu hawezi kukwepa kuwa na rekodi ya namna fulani ya kila mwanafunzi. Rekodi zigawanywe sehemu mbili: (a) Rekodi za Wazi na (b)Rekodi za Siri

Rekodi za siri zitakuwa zile za uchunguzi wa mtoto mmoja mmoja na ambazo zinabeba taarifa za faragha. Rekodi hizi zitatunzwa kwenye faili sehemu ambayo hakuna mtoto atakayeweza kuigundua. Pia hata mwalimu asiyehusika na darasa hapaswi kujua rekodi za siri za mtoto kwa sababu faragha ni haki muhimu ya binadamu. Rekodi za wazi ni zile taarifa za jumla ambazo kama zitawekwa wazi hakutamfanya mtoto kujisikia vibaya. Rekodi hizi zibandikwe kwenye ubao wa matangazo wa darasa(class bulletin board) ili kuwarahisishia wazazi na wageni wengine wanaotembelea darasa kujua taarifa muhimu za watoto wao.

Rekodi za siri zinahusisha vipengele vifuatavyo:

1.Jina la mtoto
2.Umri- tarehe ya kuzaliwa
3.Jina la mzazi na kazi yake
4.Anuani na namba ya simu
5. Idadi ya kina kaka na dada kwenye familia yake
6.Lugha inayotumiwa nyumbani
7.Maoni kuhusu hali ya Afya na hali ya mwili
8.Maoni kuhusu mazingira ya nyumbani kwao
9.Dini
10.Marafiki anaoambatana nao
11.Nyumbani kuna Tv ? na programu anazofuatilia.
12.Rekodi ya maendeleo ya kitaaluma.
(a) Maksi za mtihani
(b) Vitabu alivyosoma
(c) Maoni juu ya uwezo wake wa kitaaluma.
10.Maoni kuhusu marekebisho ya tabia


Rekodi za wazi zinaweza kuwa :
1.Majina ya Wanafunzi
2.Idadi ya wanafunzi waliosajiliwa na wasiosajiliwa
3.Wanafunzi mahiri —itabadilika kila yanapotokea mabadiliko ili kuwahamasisha watoto kusoma kwa bidii.
3.Idadi ya wanafunzi wasiomudu mahiri za KKK n.k



UALIMU NI ZAIDI YA KUSHUSHA NONDO DARASANI.
NI MCHAKATO.
NI SAYANSI(Hufuata hatua maalumu).
NI SANAA(Huhitajia mapambo na nakshi mbalimbali)
NI MALEZI.
NI WITO.
NI TAALUMA .
IMG_20200826_174402_054.JPG
 
Je kama mnafundishwa kutumia hiyo " 'mbinu kaguzi' na 'uchunguzi kifani' kwa wanafunzi " kugundua watoto wenye Autism(Wigo wa Akili) ??
Au mnawa classify kama matahira(Mental disorder) ???

Kuna aina nyingi za Autism ambazo zingine zinapelekea watoto kuwa na akili kupita kiwango lakini matendo yao ya kushirikiana na wengine, na mwingiliano wa kijamii kuwa vigumu na huonekana ni tofauti.
 
Back
Top Bottom