mwalimu ni mtu muhimu sana

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
Ndugu zangu,

UALIMU si tu kazi ya wito, ni kazi ya utu . Katika nchi yeyote ile yenye dhamira ya kweli ya kusonga mbele, mwalimu ni mtu muhimu sana.

Ni busara kwa Serikali yeyote iwayo, kufanya kila linalowezekana kuepuka kuingia kwenye mgogoro na walimu. Maana, ualimu una maana zaidi ya kazi ya kufundisha darasani. Mwalimu ni mlezi pia. Ni kiungo muhimu kati ya Serikali na jamii. Ni msaidizi muhimu katika kuzifanya kazi nyingine za Serikali.

Alhamisi ya juma la jana nilijionea mwenyewe athari za mgomo wa walimu. Ndio, nilibahatika kufanya ziara ya miguu kutembelea shule ya msingi Mbaruku iliyopo Bagamoyo Mjini.

Hapo niliwakuta walimu wakiwa ofisini huku wakifanya kazi za makaratasi. Wanafunzi walikuwa nje wakicheza. Wengine walikuwamo darasani bila walimu.

Wanafunzi wanasema; " Walimu wamegoma". Walimu nao wanasema: " Tuko kazini, si unatuona!". Lakini, mtu mzima unaelewa kinachoendelea.

Niliingia darasa la saba lisilo na mwalimu. Nikakaa kwenye dawati kushuhudia mwanafunzi akiwafundisha wenzake. Na mazungumzo yangu na wanafunzi hao yaliyofuatia yalinipa mapya ya kutafakari.

Kama mwalimu, na kama mzazi , nilisikitika sana kumwona mtoto aliyekuwa akihangaika kuwasaidia wanafunzi wenzake wa darasa la saba kukokotoa hesabu.

Nami nilikaa kwenye dawati kama wanafunzi wengine, nilijaribu kumwelewa mwanafunzi yule. Hapana, yumkini alikuwa hodari wa hesabu, lakini, kuwa hodari wa hesabu ni kitu kimoja, na kuwafundisha wengine wakuelewe ni kitu kingine kabisa. Hatuwezi kuendelea na hali hii.

Ni muhimu sasa kwa pande zote; walimu na Serikali, kutanguliza hekima na busara. Wakae chini na kuzungumza kumaliza kadhia hii, kwa kutanguliza wajibu wetu kwa watoto hawa. Kwa kutanguliza maslahi mapana ya taifa letu.

Kamwe Serikali haiwezi kudai kuwa imeshinda mgogoro na walimu kwa njia ya hukumu ya mahakama. Maana, busara zinatwambia, kama mwalimu ameshindwa mahakamani kwa kile anachodai kuwa ni haki yake atimiziwe na mwajiri wake, basi, atarudi darasani shingo upande. Hivyo, kama taifa, sote tutakuwa tumeshindwa.

Ni vema na ni busara, kwa mgogoro kati ya walimu na Serikali kama mwajiri ukamalizwa kwenye meza ya mazungumzo. Wenye kudai haki yao wanaweza wasitimiziwe kila wanachokidai, lakini, wanaweza kuondoka kwenye meza ya mazungumzo wakiwa na chochote, hata kama ni ahadi. Ni kuonyesha kutambua mchango wao, kuonyesha kuwa wanathaminiwa na kuheshimiwa.
Tukumbuke, kuwa nchi yetu ingali katika huzuni ya uwepo wa mgogoro kati ya madaktari wetu na Serikali yetu. Ni huzuni iliyochanganyika na hofu na mashaka. Suluhu ya kushikana mikono bado haijapatikana.

Inasikitisha, maana, hii ni nchi yetu, waliogoma huko nyuma ni madaktari wetu, na sasa ni walimu wetu, na inayogomewa ni Serikali yetu. Ni wananchi wa nchi hii wenye kutaabika kutokana na migomo hii.

Haya ni mambo ya kuhuzunisha sana. Ni mambo yenye kuitia doa nchi yetu. Huko nyuma kuna tuliosisitiza, na hapa narudia kusisitiza msimamo wangu kama Mtanzania ninayeipenda nchi yangu, kuwa hakuna njia nyingine ya kuimaliza migogoro hii bali ni kwa njia ya mazungumzo ya kindugu na kirafiki.
Wahusika wana lazima ya kukaa kwenye meza moja kama Watanzania na kuitafuta suluhu ya migogoro hii kwa manufaa ya nchi yetu na watu wake.

Maana, mgomo wowote ni jambo la hasara. Kila siku inayokwenda kukiwa na mgomo ina maana ya hasara kwa nchi na watu wake.
Naam, huu ni wakati wa kutanguliza busara na hekima. Tufanye yote, lakini, njia mujarabu ya kutanzua migogoro katika jamii yetu ni mazungumzo katika mazingira ya kuheshimiana, basi. Nahitimisha.
 
  • Thanks
Reactions: MI6
Back
Top Bottom