Mrema 'ayeyuka' na hati ya wito wa Mahakama

Rutashubanyuma

JF-Expert Member
Sep 24, 2010
219,470
911,174
Mrema 'ayeyuka' na hati ya wito wa Mahakama
Send to a friend
Thursday, 07 July 2011 21:06


James Magai
MWENYEKITI wa Chama Cha Tanzania Labour (TLP), Augostine Mrema, anadaiwa kugoma kusaini hati ya Mahakama inayomtaka kuwasilisha maelezo ya maandishi ya utetezi wake dhidi ya kesi aliyofunguliwa na mwanachama wake, Mwahija Chogga. Mwahija ambaye ni Diwani wa Viti Maalumu, kupitia chama hicho na pia Katibu wa TLP, Wilaya ya Arusha Mjini, amemfungulia Mrema kesi katika Mahakama ya Wilaya ya Arusha akipinga, hatua ya Mrema kutangaza kumfukuza uanachama.

Mbali na Mrema walalamikiwa wengine katika kesi hiyo namba 14 ya mwaka huu 2011 ni Leonard Makanzo, Mwamvua Wahanza, Mohamed Maabad, Jacob Molel, Salma Jumanne na Deodatus Humaya, ambao pia ni wanachama na viongozi wa TLP. Kufuatia kesi hiyo jana Chogga ambaye amefungua kesi hiyo chini ya hati ya dharura kupitia Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Hamad Tao, akiwa ameambatana na askari polisi kutoka kituo cha Magomeni, alimfikishia Mrema hati hiyo ofisini kwake Magomeni saa 6.00 mchana.

Licha ya kupokea hati hiyo inayomtaka afike mahakamani Julai 13, mwaka huu, Mrema alikataa kuisaini akidai kuwa yeye ni mbunge hivyo hawezi kupokea samansi mitaani, badala yake alimtaka Tao aipitishe kwa Spika. Akizungumza na Mwananchi jana, Tao ambaye alifika kwenye ofisi za gazeti hili, Tabata jijini Dar es Salaam, akiongozana na mlalamikaji na mwanachama mwingine wa chama hicho James Haule, alisema licha ya Mrema kukataa kuisaini hati hiyo, alikataa kuirejesha kwa mlalamikaji. “Niliamua kumchukua askari kwa ajili ya usalama.

Baada ya kukataa kuisaini nilimwambia mbele ya askari kuwa airudishe lakini, alikataa kuwa mpaka mlalamikaji mwenyewe aende au karani wa mahakama kutoka Arusha ndio aifuate,” alisema Tao. Hati hiyo iliyotolewa na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Arusha June 24, mwaka huu inampa Mrema siku 21 kuwasilisha maelezo ya utetezi kwa maandishi na kwamba, kama atashindwa kufanya hivyo katika kipindi hicho, mahakama itatoa hukumu ya upande mmoja.
Jibu la Mrema

Mrema lipoulizwa jana na gazeti hili kuhusu tuhuma hizo, alikiri kupokea samansi hiyo lakini, akakanusha kugoma kuisaini wala kutoirejesha kwa mlalamikaji. Alisema baada ya kukabidhiwa samansi hiyo, alitaka ofisa wa mahakama ya Arusha aliyeileta ajitambulishe ndipo asaini na kuirejesha.

"Samansi ya Mahakama lazima ipelekwe kwa mhusika na ofisa wa mahakama,” alisema Mrema. “Mimi namtaka huyo Ofisa wa mahakama aliyeileta hiyo samansi aje hapa maana samansi ya Mahakama inatolewa na proper (maalum) afisa wa mahakama na si mtu yeyote tu from no-where (kutoka kusikojulikana)." Mrema alisisitiza: "Siwezi kukataa kusaini samansi ya mahakama maana mimi si mwendawazimu. Sikukataa bali nimeuliza huyo ofisa yuko wapi wakasema wanakwenda kumleta.

Mpaka sasa (saa 11:00 jioni jana) niko ofisini namngojea. Mimi sina ugomvi na mahakama ya Arusha,” alisema Mrema. Kuhusu suala la askari polisi kumsindikiza Tao kupeleka samansi hiyo ofisini kwake, Mrema alikanusha kuwa hakuna askari yeyote aliyekwenda na kusema habari alizozipata ni kwamba, askari hao walikaa kwa kuwa suala hilo linamhusu ofisa wa mahakama.

“Kwanza nina mashaka naye, kwani ni mshirika mkubwa katika kukiangamiza chama hiki (TLP),”alisema Mrema akimtuhumu Tao ambaye katika siku za hivi karibuni, wamekuwa katika msuguano mkubwa wa kisiasa kuhusu uendeshaji wa chama hicho. Pia Mrema alisema hawezi kutumia nafasi yake ya ubunge kama sababu ya kukataa amri ya mahakama, kwani hawezi kuogopa kesi hiyo wakati amewahi kuwa na kesi nyingi na nzito, ikiwamo kesi dhidi yake na Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamini Mkapa.

Mrema pia alisema anaisifu mahakama hiyo kwani haikuzuia mkutano wake utakaofanyika kesho katika Ukumbi wa Friends Corner, Manzese jijini Dar es Salaam na kutoa wito kwa watu kwenda kushuhudia alichokiita demokrasia ndani ya TLP. Katika kesi hiyo Chogga anaiomba mahakama itangaze kuwa barua zilizotolewa na walalamikiwa ambao ni Mrema na wenzake ni batili. Pia anaiomba mahakama iwazuie Mrema na wenzake, kutangaza kuwa mlalamikaji amefukuzwa uanachama wa TLP.

Mlalamikaji ameiomba pia mahakama iwaamuru Mrema na wenzake wamruhusu kutekeleza majukumu yake kama Katibu wa Wilaya wa chama hicho na kuwaamuru kulipa gharama zote za kesi hiyo na fidia nyingine ambazo mahakama itaona zinafaa.

Hati hiyo ya madai inabainisha kuwa Novemba 16 mwaka jana, washtakiwa hao kinyume cha sheria na katiba ya TLP, walitoa barua kwa lengo la kumfukuza uanachama mlalamikaji. Pia hati hiyo inadai kuwa Novemba 29 Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Hamad Tao, aliwaandikia barua walalamikiwa akiwataka wafute barua hiyo kwa kuwa ilikuwa kinyume cha katiba ya chama hicho, lakini Mrema na wenzake walikataa.

“Desemba 8 mwaka 2010, mshtakiwa wa saba (Mrema) alitoa barua nyingine kuwaunga mkono washtakiwa wa kwanza hadi wa sita,” inasema sehemu ya hati hiyo iliyobainisha kuwa walalamikiwa hao hawana mamlaka ya kumfukuza uanachama mlalamikaji.

Hata hivyo, mlalamikaji anasisitiza katika hati hiyo ya madai kuwa yeye bado ni mwanachama wa TLP, ni diwani wa Arusha na kwamba, barua hizo zilizotolewa na walalamikiwa zilimvunjia hadhi yake kama mwanachama wa TLP na diwani.

“Walalamikiwa wamekuwa wakirudia kutangaza katika magazeti kuwa mlalamikaji si mwanachama wa TLP jambo ambalo ni uongo. Tangazo hilo linamkwamisha mlalamikaji katika utekelezaji wa majukumu yake kama diwani na Katibu wa Wilaya wa chama hicho,” inasisitiza sehemu ya hati hiyo ya madai. Mwisho.




 
Back
Top Bottom