Mkataba baina ya serikali na DP World kielelezo cha ombwe katika uongozi

gstar

JF-Expert Member
Jun 19, 2011
759
1,250
Hivi karibuni serikali ya Tanzania imesaini mkataba na serikali ya UAE kupitia kampuni ya DP World ili kuweza kuendesha bandari zote za Tanzania kupitia kampuni hiyo bobevu katika maswala ya uendeshaji wa bandari Duniani. Walakini kumeonekana kuwepo kwa mapungufu mengi kwenye mkataba huo aidha mkataba huo umeletwa kwa wananchi ukiwa umekwisha sainiwa hali inayo onesha kwamba maoni ya wananchi yamepuuzwa kabla ya kusaini mkataba huo.

Wananchi wa Tanzania tuliaminishwa kuwa maliasili zote ni mali za umma yaani wananchi wana mamlaka kamili katika kuzilinda na kuzisimamia maliasili hizo, mfano ardhi, madini na mbuga za wanyama. Hivyo basi viongozi wetu yawezakuwa walifanya makosa makubwa kusaini mkataba huo pasi na kuruhusu maoni ya wananchi kusikilizwa kwanza.

Katika hali ya kushangaza, kumeonekana kuwepo kwa vipengele vyenye ukakasi katika mkataba huo, vingi vikionekana kuwa ni vya kinyonyaji na kikandamizaji. Swali la kujiuliza ni kwamba je, serikali yetu tukufu kupitia kwa mamlaka inazo zisimamia na haswa wale waliohusika katika kusaini makataba huo hawakuviona vipengele hivyo kwamba havifai kuwemo kwenye mkataba huo na kwamba ni vya kikandamizaji?

Serikali ya Tanzania kusaini mkataba na kampuni ambayo inamilikiwa na nchi ya UAE ni hatari kwa sababu itakapo tokea mgogoro wowote wa kimkataba utaathiri zaidi nchi ya Tanzania kuliko nchi ya UAE. Hii ni kwa sababu serikali ya Tanzania imesaini mkataba na kampuni ya DP World inayo milikiwa na UAE na wala haikusaini mkataba wa moja kwa moja na nchi ya UAE.

Hivyo ikitokea kuvunjwa kwa mkataba isivyo halali basi mahakama ya kimataifa inaweza kuamuru kukamatwa kwa mali zetu na tunu zetu za Taifa ndege zetu ama viongozi wetu kuzuiwa kusafiri. Kuamriwa kulipa fidia kubwa itakayo athiri uchumi wa nchi. Upo ushahidi wa mambo hayo uliokwisha kutokea hapo nyuma ambapo ndege yetu ya Air Tanzania ilikamatwa nchini Afrika ya kusini, ilipaswa tujifunze kupitia jambo hilo.

Mkataba umekosa uhalali, kwa kuwa mkataba hauonyeshi muda halisi wa kikomo chake na pia hakuna vipengele vya moja kwa moja vinavyombana mwekezaji kuendeleza bandari kwa matakwa yetu, aidha serikali ya Tanzania haitaweza kumwajibisha mwekezaji huyo kwa namna yoyote ikiwemo kuvunja mkataba huo endapo tu ikionekana kwamba baadhi ya vipengele muhimu vya kimkataba vimekiukwa.

Kwa maoni yangu ni kwamba serikali yetu imeharakisha kuingia kwenye mkataba huo, yamkini ingejipa muda katika kuusoma na kuutathmini, na kwakuwa serikari imefanya haraka kusaini mkataba huo basi ni halali kusema kwamba Waliosaini walikuwa na malengo ovu ndani yao (malengo binafsi) ama walikosa maarifa na elimu ya kutosha kung'amua kwamba mkataba huo hauna nia njema na utatuingiza shimoni kama Taifa.

Utaratibu haukufuatwa. Mswada ulipaswa kuletwa bungeni ili kujadiliwa na kisha kukubaliwa na wengi basi ndio mkataba usainiwe. Bunge letu kukosa uhalali wa wananchi na kulifanya kuwa dhaifu kwa sababu wabunge wengi walipita bila kupingwa huko majimboni mwao na hivyo hawathamini sauti na machozi ya wananchi wanao wawakilisha. Wabunge wengi kuona kwamba wananchi hawana uelewa wala hawafikirii kisawasawa hivyo basi wamekosa uhalali wa kuwawakilisha kwasababu yale wanayoyasema bungeni si sauti ya wananchi wanao wawakilisha.

Mwisho naweza kusema kwamba sauti za wasiokuwa na sauti zisipuuzwe kwa maana ni wengi. Hata kama mkataba ule umesha sainiwa, ni bora tukakubali kama taifa kulipa fidia ya kuuvunja mkataba huo kuliko kuendelea nao kwa sababu ni dhahiri kwamba madhara yatakayoletwa na utekelezwaji wa mkataba huo yatakuwa makubwa zaidi kuliko gharama za kulipa fidia hiyo.

Serikali ising'ang'anie kubinafsisha bandari kwa kampuni ambayo baadaye itageuka kuwa mwiba kwetu. Wachambuzi na wataalamu wachambue madhara na faida zitakazo patikana kisha wapime kipi kitakuwa bora na baada ya hapo maamuzi sahihi yafanyike.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom