Mhadhiri afumua madudu vyuo vikuu |
Tuesday, 04 September 2012 07:08 |
Florence Majani WAKATI Serikali na wadau wa elimu nchini wakifanya jitihada ya kuongeza idadi ya wahitimu wa shahada huku kampuni zikitoa vipaumbele kwa wenye sifa hizo, imebainika kuwa asilimia 80 ya shahada hizo si halali. W alakini wa shahada hizo, umebainika kupitia utafiti uliofanywa na Dk Eliamani Sedoyeka wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) cha jijini Dar es Salaam. Katika utafiti huo, mhadhiri huyo, amebaini kuwa wahitimu wengi ama wameiba au wamenakili tafiti zao za mwisho kutoka katika tafiti za watu wengine au kwenye mitandao. Mtaalamu huyo wa Kitengo cha Hesabu na Mfumo wa Mawasiliano, alisema tatizo hilo ni kubwa na linaendelea kukua siku hadi siku. Kwa mujibu wa Dk Sedoyeka, baadhi ya wahitimu wanafanyiwa tatizo hizo na kampuni na wahadhiri wa vyuo. Alisema wengine wamekuwa wakipata alama za juu kwa kuibia kwenye mitihani yao. Dk Sedoyeka ambaye amefanya utafiti kuhusu sababu za wanafunzi kunakili shahada na kuibia katika mitihani yao, alisema asilimia 80 ya shahada hasa za kwanza pili na shahada za juu zina walakini mkubwa. Alisema tatizo hilo limechangiwa na kukosekana kwa uwiano kati ya idadi kubwa ya wasomi na maendeleo ya nchi. Mhadhiri huyo alisema Serikali inawekeza katika kuzalisha wasomi wengi kwa kutoa mikopo ya elimu ya juu, bila kuangalia ubora na matokeo ya wasomi hao katika maendeleo. Serikali inatakiwa iliangalie suala hili kwa upana kwa sababu tutaendelea kuzalisha wasomi wengi wasiokuwa na tija kwa maendeleo ya taifa, alisema Dk Sedoyeka. Sababu za wanafunzi kununua au kunakili shahada? Dk Sedoyeka alisema sababu zinazochochea tatizo hili ni wanafunzi kutojituma, matatizo ya kisaikolojia na upungufu wa wahadhiri. Alisema wahadhiri wachache wanaokuwepo vyuoni, wanasongwa na kazi nyingi na hivyo kushindwa kuwasimamia vyema wanafunzi. Mwanafunzi anapofanya research yake tunategemea atumie ujuzi wake aliojifunza kwa miaka mitatu au minne. Research anayoifanya itatuonyesha kama yuko tayari kufanya kazi au la, alisema Dk Sedoyeka. Anasema mwanafunzi anaponunua research au kufanyiwa au kuiba ya mtu hawezi kuwa nguvu kazi yenye tija, alisisitiza. Alisema kingine kinachochangia kuwapo kwa shahada mbovu i ni wahadhiri wenyewe. Dk Sedoyeka alisema wingi wa vyuo umesababisha kuajiriwa kwa wahadhiri ambao baadhi yao hawana ujuzi wa kina katika kuwasimamia wanafunzi kwenye tafiti zao. Huwezi kumsimamia mwanafunzi katika dissertation wakati wewe mwenyewe hukuifanya vyema na hufanyi tafiti yeyote katika maisha yako, alisema Anasema kinachosababisha shahada nyingi kuwa feki ni kitendo cha kununua au kuiga kugeuka utamaduni wa watanzania. Aghalabu mwanafunzi anasema, kama wengine wanaiba, wananunua na wanaiga, kwa nini na mimi nisifanye hivyo, Kwa kifupi mfumo umeoza, alisema. Anasema hata kama chuo kinahitaji wanafunzi wengi wafaulu, lakini taaluma inabaki kuwa taaluma na wanachuo wanatakiwa wafaulu kwa uhakika na si kuwalipua kisha kuwatupa duniani wakiwa hawawezi kufanya lolote. Jambo lingine linaongeza kasi ya shahada feki, ni mabadiliko ya siku za karibuni ambapo shahada za juu zinakuwa kigezo cha kupata ajira. Dk Sedoyeka ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Usimamizi wa Takwimu, Data na Mipango alisema kinachosababisha tatizo hili kukua kwa kasi ni ari ya vijana kupata elimu kunakoambatana na sheria dhaifu. Katika nchi zilizoendelea, hata kama ni mbunge, waziri au mwenye cheo kikubwa akibainika kuwa matokeo yake ya kitaaluma yana walakini anaachia ngazi, alisema. Anasema tafiti za mwisho za mwanafunzi zina umuhimu mkubwa kwani anapofanya tafiti hizo anajengwa katika kuibua tatizo, kulidhibiti na kulitafutia ufumbuzi. . Mhadhiri huyo anasema aliufanya utafiti wake kuanzia Juni 2011 katika Mkoa wa Dar es Salaam pekee na kukamilisha sehemu ya kwanza. Sasa yupo katika hatua ya pili itakayoangalia tatizo hilo kisaikolojia na kitabia. Mhadhiri Msaidizi katika Chuo Kikuu cha Tumaini Dare s Salaam, Godwin Gondwe alisema anakubaliana na utafiti wa Dk Sedoyeka na kwamba hiyo ni moja ya changamoto katika sekta ya elimu nchini. Gondwe ambaye ni Mtaalamu wa Habari na Mawasiliano ya Umma alisema chanzo kikuu ni mfumo mbovu wa elimu tangu awali ambapo wanafunzi wengi wanasumbuliwa na lugha ya kiingereza. Alisema sababu nyingine ni wahadhiri kuwasimamia wanafunzi wengi katika tafiti zao, jambo ambalo wakati mwingine linachangia wanafunzi kufanya vibaya. Mhadhiri huyo alisema Tanzania haina budi kuwa sera ya elimu itakayosimamia ubora na mwelekeo wa elimu nchini, ikiwa ni pamoja na kutumia teknolojia katika kuzipima tafiti za wanafunzi. Tutunge sera ambazo zitasimamia sekta ya elimu kuanzia ngazi ya chini kabisa, ili wahitimu wawe na tija, alisema Gondwe. Hata hivyo Gondwe alisema pamoja na utafiti huo kuonyesha asilimia kubwa ya shahada zina walakini, bado Tanzania ina wasomi ambao ni lulu katika nchi za jirani, kama Kenya, Rwanda na Burundi. Aliitaka serikali kuwekeza katika elimu ikiwemo kuweka fungu la kutosha kwa ajili ya kufanya tafiti. Dk Nandera Mhando, Mhadhiri msaidizi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kitengo cha Sosholojia alisema amekutana na changamoto za wanafunzi kunakili tafiti zao mara kwa mara. Alitoa mfano kuwa mwaka jana aliwapa sifuri wanafunzi karibu kumi ambao walinakili tafiti zao. Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Dk Shukuru Kawambwa, alipotafutwa kwa njia ya simu hakuweza kupokea simu yake huku Naibu wake, Philip Mulugo akisema kuwa yupo mkutanoni na kuwa hawezi kuzungumza kwa wakati huo. Utafiti uliofanywa na mwandishi ulibaini uwepo wa watu ambao hujipatia riziki kwa njia ya kuwafanyia wanavyuo tafiti. Mwandishi alizungumza na Kijana mmoja (jina linahifadhiwa),ambaye kazi yake ni kuwafanyia wanavyuo tafiti na aliahidi kuifanya tafiti hiyo kwa malipo ya shilingi laki tano kwa tafiti ya shahada ya uzamili. Kijana huyo alianza kwa kuuliza ni aina gani ya kozi, kiwango kipi yaani shahada ya kwanza au ya pili na alinitaka nimpe mada zisizopungua tatu ambazo ningependelea kuzifanyia utafiti. Baada ya kumtumia mada aliniuliza ni lini ninahitaji tafiti hiyo. Aidha alinisisitiza kuwa baada ya kumaliza kazi hiyo ni lazima niikariri kwa ajili ya kuitetea kwa wahadhiri kama ada ya tafiti zote zinavyofanyika vyuoni. |