Mbunge aswekwa rumande kwa kushambulia mfanyakazi wa mamlaka ya maji

GM7

JF-Expert Member
Jun 26, 2009
492
24
Samuel Msuya na Lilian Lucas Morogoro

JESHI la Polisi Mkoani Morogoro linamshikilia mbunge wa jimbo la Morogoro Kusini-Mashariki, Samir Lotto kwa tuhuma za kumshambulia na kumpora vifaa vya kazi mfanyakazi mmoja wa Mamlaka ya Maji safi na Majitaka Manispaa ya Morogoro (Moruwasa).

Mbunge huyo alikamatwa jana saa 6:00 mchana katika eneo la nyumba yake ya ghorofa anayojenga kando ya barabara ya zamani ya Dar es salaam.

Mbunge huyo alikamatwa baada ya kudaiwa kukaidi wito wa polisi wa kufika Kituo Kikuu cha Polisi kutoa maelezo dhidi ya shtaka la shambulio lililofunguliwa Agosti 20 na mfanyakazi huyo wa Moruwasa, Michael Mapunda katika jalada namba MO/RB/8186/09.

Kamanda wa polisi mkoani Morogoro,Thobias Andengenye aliliambia gazeti hili jana kuwa mbunge huyo atafikishwa mahakamani wakati wowote baada ya upelelezi wa tuhuma zinazomkabili, kukamilika.

"Kweli tunamshikilia Mheshimiwa Lotto na sasa maelezo yake yanachukuliwa na kama ambavyo mnajua tumekuwa tukimtafuta pasipo mafanikio; askari wameshakwenda kwake mara nyingi na kumkosa na mara nyingi huelezwa kuwa amesafiri nje ya nchi. Pamoja na kwamba mbunge hana kinga juu ya hilo, tunachokifanya sisi ni kusimamia sheria za nchi," alisema Andengenye.

Inadaiwa kuwa Agosti 20 majira ya saa 6:00 mchana, mbunge huyo alimzaba vibao mfanyakazi huyo na kumkaba koo na baadaye kumnyang'anya vifaa vya kazi na Sh150,000 zilizokuwa kwenye makabrasha.

Habari zimesema kuwa mbunge huyo alifanya kitendo hicho wakati mfanyakazi huyo, ambaye ni mkazi wa Kihonda Mbuyuni, akiwa ameenda kukata maji katika mita ya nyumba ya mbunge huyo.

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya kituo cha polisi, Mapunda alisema alienda kukata maji katika mita hiyo baada ya kubaini kuwa kuna deni la Sh7,700.

Alisema muda mfupi baada ya kukata maji na kwenda kukagua katika jengo la msikiti wa Watanzania wenye asili ya kihindi jirani kabisa na ghorofa la mheshimiwa huyo, Lotto alitokea na kumtaka arejeshe maji.

"Baada ya kukataa alinikaba shingoni na kunichapa vibao na baadaye isha kuondoka na mfuko wangu uliokuwa nimehidhia nyaraka mbalimbali za Moruwasa," alisema.

Mfanyakazi huyo alisema, mbali na nyaraka hizo, mfuko huo pia ulikuwa na Sh150,000 alizokuwa amelipwa na mdeni wake muda mfupi kabla ya tukio hilo ndipo alipoenda kutoa taarifa polisi na kufungua jalada la shambalio hilo.

Source: Gazeti la Mwanachi
 
Back
Top Bottom