Mbowe hakamatiki

baraka boki

Senior Member
Sep 20, 2010
181
80
Na Muhibu Said
4th June 2011






Watangaza mgogoro wa kuingilia uhuru wa Bunge
Polisi wadaiwa kuendesha upendeleo wa dhahiri
Hoja ya mvutano wa Bunge na Mahakama yaibuka

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, akiwaonyesha waandishi wa habari barua ya Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mwanza inayokwenda kwa Katibu wa Bunge kumuombea kibali cha Spika ili akamatwe Titus Mlegeni Kamani ambaye ni Mbunge wa Busega.

Siku moja baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kutoa amri ya kukamatwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu, amesema amri hiyo inaingilia uhuru wa Bunge na inahatarisha demokrasia nchini.

Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari katika Ofisi ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, iliyoko katika Ofisi Ndogo ya Bunge, jijini Dar es Salaam.

Alisema Kambi ya Upinzani Bungeni, imepokea kwa mshtuko, masikitiko na mshangao mkubwa taarifa za mahakama hiyo kutoa amri ya kumkamata Mbowe, ambaye ni Kiongozi wa Kambi hiyo.

Amri hiyo ilitolewa na Hakimu Mkazi, Charles Magessa, Mei 27, mwaka huu na kurudiwa tena juzi.

Mbowe, ambaye pia ni Mbunge wa Hai (Chadema) pamoja na wabunge, viongozi na wanachama kadhaa wa Chadema, wanakabiliwa na mashtaka kadhaa yanayotokana na maandamano yaliyofanyika Januari 5, mwaka huu katika Jiji la Arusha, yaliyosababisha askari polisi kuua watu watatu na wengine kujeruhiwa.

Lissu alisema Mbowe hakuhudhuria mahakamani katika tarehe zote mbili kwa vile amekuwa akihudhuria vikao vya kamati mbalimbali za Bunge vilivyoanza Mei 23, kwa ajili ya maandalizi ya Mkutano wa Nne wa Bunge unaotarajiwa kuanza Jumanne wiki ijayo hadi Septemba 7, mwaka huu.

“Kama Mbunge na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mheshimiwa Mbowe ni mjumbe wa Kamati mbalimbali za Bunge kama vile Kamati ya Uongozi. Aidha, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ni mjumbe katika Tume ya Utumishi wa Bunge na ndiye msemaji mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni,” alisema Lissu.

Kutokana na hayo, alisema Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeshtushwa na amri ya kumkamata Mbowe kwa vile inakiuka moja kwa moja sheria, mila na desturi za miaka mingi zinazohusu kinga, haki na madaraka na mamlaka ya Bunge, ambazo ndio msingi mkuu wa demokrasia ya Watanzania kibunge.

Alisema Ibara ya 100 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inatambua na kulinda uhuru wa mawazo, majadiliano na utaratibu katika Bunge na uhuru huo hautavunjwa wala kuhojiwa na chombo chochote katika Jamhuri ya Muungano, au katika Mahakama au mahali penginepo nje ya Bunge.

Lissu alisema uhuru huo wa kikatiba umetiliwa mkazo katika vifungu vya 5, 6 na 11 vya Sheria ya Kinga, Mamlaka na Haki za Bunge ya mwaka 1988 vinavyokataza mbunge kukamatwa au kupewa amri ya kuhudhuria mahakamani wakati akiwa ndani ya eneo la Bunge au wakati Bunge limekutana bila kuwapo kwa kibali cha Spika.

Alisema maneno ‘eneo la Bunge’ yametafsiriwa na kifungu cha 2 cha sheria hiyo kumaanisha “ukumbi ambao hutumiwa kwa vikao vya Bunge, pamoja na ofisi, vyumba, viambaza (lobbies), maeneno ya wageni (galleries), courtyards, bustani na maeneo mengine yaliyowekwa kwa ajili ya matumizi au malazi ya wajumbe, maafisa au wageni wa Bunge pamoja na njia zinazounganisha maeneo hayo na maeneo mengine yanayoweza kutangazwa na Spika kuwa ndani ya maeneo ya Bunge”.

“Kwa maana hiyo, mbunge anapokuwa anahudhuria vikao vya Bunge au kamati zake au anapokuwa mahali pengine popote kwa kuitikia wito wa kuhudhuria vikao hivyo vya Bunge hawezi akakamatwa ili kutekeleza amri ya mahakama au chombo kingine chochote nje ya Bunge,” alisema Lissu.

Alisema kufuatana na mila na desturi za kibunge za Jumuiya ya Madola, ambazo Tanzania imezikubali na inatakiwa kuzifuata, kinga ya wabunge dhidi ya kukamatwa inakuwa na nguvu wakati wa mkutano wa Bunge pamoja na muda mwafaka na wa kutosha kabla na baada ya mkutano wa Bunge.

“Kwa mujibu wa Erskine May, mwandishi maarufu wa mila na desturi za mabunge ya Jumuiya ya Madola, ‘muda mwafaka na wa kutosha umechukuliwa kwa ujumla kuwa ni siku arobaini kabla na baada ya mkutano wa Bunge’,” alisema Lissu.

Kwa mantiki hiyo, alisema wakati Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha inatoa amri dhidi yake, Mbowe alikuwa analindwa na kinga hiyo kwa kipindi chote cha Mkutano wa Nne wa Bunge pamoja na muda mwafaka na wa kutosha kama unavyotambuliwa katika mila na desturi za mabunge ya Jumuiya ya Madola utakapokwisha baada ya mkutano huo.

Alisema pia Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeshangazwa na kile alichokiita “unafiki na ubaguzi” wa wazi unaoonyeshwa na Jeshi la Polisi juu ya wabunge wa vyama vya upinzani.

“Hii ni kwa sababu Jeshi la Polisi limekuwa likiwakamata wabunge wa upinzani bila kuomba kibali chochote cha Spika kama inavyotakiwa na Sheria ya Kinga, Mamlaka na Haki za Bunge.

Aliwataja wabunge waliokamatwa bila kibali cha Spika kuwa ni Mbowe, Godbless Lema (Arusha Mjini), Philemon Ndesamburo (Moshi Mjini), Joseph Selasini (Rombo), Meshack Opulukwa (Meatu), Tundu Lissu (Singida Mashariki), Esther Matiko (Viti Maalum-Chadema) na Magdalena Sakaya (Viti Maalum-CUF),” alisema Lissu.

Hata hivyo, alisema wabunge wa CCM, ambao wanakabiliwa na tuhuma za makosa makubwa zaidi, wamekuwa wanaombewa kibali cha Spika kabla ya kukamatwa.

“Kwa hili tunao ushahidi wa barua ya Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Mwanza SP B.M Wakulyamba kwa Katibu wa Bunge ya kumwomba Mheshimiwa Titus Mlengeya Kamani (Busega-CCM) ili akahojiwe na Jeshi la Polisi kuhusu kuhusika kwake na njama za kutaka kumwua aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Busega, Dk. Rapahel Masunga Chegeni,” alisema Lissu.

Alisema barua hiyo ya Mei 31, mwaka huu, ilinakiliwa kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Makao Makuu ya Polisi, Kamishna Robert Manumba.

”Hakuna mbunge hata mmoja wa Chadema au chama kingine cha upinzani, ambaye kwa taarifa zetu amewahi kuombewa kibali cha kukamatwa na polisi kama inavyoonekana kwa wabunge wa CCM. Hii inadhihirisha upendeleo wa wazi wa Jeshi la Polisi kwa wabunge wa CCM,” alisema Lissu.

Alisema kwa sababu hizo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, haitarajii na itapinga kwa nguvu zake zote kitendo chochote cha kumtishia au kumkamata Mbowe kwa kipindi chote, ambacho ana kinga ya Bunge kama inavyotambuliwa na Katiba na sheria za nchi pamoja na mila na desturi za kibunge, ambazo Tanzania imechagua kuzifuata kwa hiari yake yenyewe.

Pia alisema wanatarajia mahakama pamoja na vyombo vingine vyote vilivyoanzishwa na vinavyofanya kazi zake kwa mujibu wa sheria za nchi vitatumia busara ili kuepusha nchi na fedheha ya kuonekana inakamata wabunge wake wakati wakiwa wanatekeleza wajibu wao wa kibunge.

Akijibu swali la mmoja wa waandishi kwanini ufafanuzi kuhusu sheria ya kinga ya wabunge wasizipeleke mahakamani badala ya kuzitoa kwa waandishi, Lissu alisema kanuni inasema mahakama inahesabika kuwa inajua sheria inazozisimamia, sikukuu za kitaifa, vyeo vya kitaifa, tarehe za kamati za Bunge, wabunge wanatakiwa lini bungeni na Bunge linaanza lini. “Sasa inawezaje kutoa taarifa ya mbunge kukamatwa wakati inajua hiki ni kipindi cha bajeti?,” alihoji Lissu na kuahidi kwamba, ufafanuzi huo utatolewa mahakamani.

Spika wa Bunge, Anna Makinda, alipotakiwa na NIPASHE jana kueleza iwapo anatambua kuwapo kwa kinga kwa wabunge, alikataa kuzungumzia suala hilo akisema hawezi kuzungumzia jambo, ambalo liko mahakamani.

“Kesi yao iko mahakamani na mimi kanuni za Bunge zinanikataza,” alisema Spika Makinda.

Awali, Mbowe alisema kauli ya mahakama hiyo imemsikitisha kwani yeye hawezi kuidharau mahakama, pia chama na kambi ya upinzani anayoiongoza hawana utaratibu wa kuidharau mahakama.

“Kila Mtanzania anajua hiki ni kipindi taifa linajiandaa na bajeti,” alisema Mbowe na kusisitiza kuwa ufafanuzi uliotolewa na Lissu ndio msimamo wao.

Alisema mara ya mwisho walipokwenda mahakamani, waliieleza mahakama kuwa watakabiliwa na majukumu ya kibunge, hivyo hawataweza kuhudhuria mahakama na kwamba, walielewana kwa jambo hilo.

Mbowe alisema anaamini kuna mkakati wa makusudi wa kutaka kuwatoa kwenye kujadili hoja za msingi, ambazo taifa linategemea watatekeleza kipindi hiki cha kuelekea kwenye bajeti na kuwaingiza kwenye malumbano na Jeshi la Polisi na Mahakama. Alisema hawaipuuzi amri ya kukamatwa kwake, kwani mawakili wao walioko Arusha wanaendelea na mchakato wa kutafuta suluhu na mahakama kuhusiana na amri hiyo ya mahakama dhidi yake.

Hata hivyo, alisema iwapo atakamatwa kama ilivyoamriwa na mahakama, jambo hilo litakuwa limewapendeza polisi, lakini akasema hawataacha kusimamia haki zao kwa gharama yoyote kwa vile hatua hiyo itakuwa ni ya uonevu na kwamba, wataipinga kwa nguvu zao zote.

Lissu alisema iwapo itatokea Mbowe kukamatwa, kitendo hicho kitakuwa ni uthibitisho wa dhahiri kwamba, Polisi si jeshi la kulinda raia na mali zao, bali ni la wahalifu na la kuonea raia.

Katibu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, John Mnyika, akijibu swali kama walishawahi kuwasiliana na Bunge kuhusu utekelezaji wa kinga ya wabunge, alisema waliwahi kuiandikia Ofisi ya Katibu wa Bunge dokezo, lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa.

“Tutaandika barua rasmi ya malalamiko,” alisema Mnyika, ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo (Chadema) na Katibu wa wabunge wa chama hicho.
 
Back
Top Bottom