'Marshall Plan' - Restoration and Recovery Plan for Tanzania

Bado nina imani kubwa sana kwa nilichoandika kuwa chachu na kuchangia mabadiliko yanayopaswa kutokea Tanzania.
 
Nimeamka asubuhi hii nikiota kuhusu huu waraka na hasa sehemu ya uongozi. Nanukuu tena hapa.


Uongozi; Serikali, Utawala, Dola
Tanzania (Tanganyika na Zanzibar) zimebahatika kuwa na awamu si chini ya nne za uongozi wa Serikali kuu, ingawa kwenye Bunge na Mahakama, watumishi wake wameendela kuwa ni wale wale kwa muda mrefu.
Tatizo kubwa tulilonalo kama Taifa ni ufinyu wa viongozi bora na utashi binafsi wa wachache walio katika nyanja za uongozi kwa kukosa sifa muhimu kwa viongozi. Mzee Mwinyi amesema majuzi kuwa Tanzania ina viongozi wasomi wasioelimika. Kauli hii ni ya kweli na ni ya msingi kutambua kuwa uongozi si lelemama, ni kipaji na ni kazi ngumu.
Uongozi ni kujitolea na kuweka matwakwa na maslahi ya wengine kuwa mstari wa mbele na si matakwa binafsi na kujinufaisha. Marehemu John Kennedy rais wa Marekani alitoa kauli moja maarufu iliyosema kuwa “kiongozi ajiulize ni vipi atalitumikia Taifa na si Taifa kumtumikia yeye Kiongozi” Umashuhuri na uzuri wa Kiongozi unatokana na hekima, busara, uchapakazi, ufanisi, ufuatiliaji, uimara, uungwana, uwajibikaji na unyenyekevu wake. Ama fikra endelevu na upeo wa kuongoza ni muhimu na si kauli tamu au uzuri wa sura.
Uwezo wa Tanzania kuwa na maendeleo ya kweli utaanza na Uongozi bora.
Uongozi bora ni ule;
· wenye mapenzi ya kweli na dhati na kujivunia Utaifa wake
· wenye kujali na kulinda maslahi ya Taifa lake na watu wake
· wenye uwezo wa kupanda mbegu imara ya Uzalendo kwa kila mwananchi bila kujali itikadi, rangi, kabila, dini, elimu, umri au jinsia
· wenye uwezo wa kuhamasisha na kuchochea juhudi za maendeleo ya jamii, umma na Taifa
· wenye nidhamu, watiifu, kuwajibika, tija, ufanisi, kujituma na ufuatiliaji wa hali ya juu
· wenye usikivu, uungwana na unyenyekevu kukiri makosa, kukubali kukosolewa na kupokea na kufanyia kazi maoni ya wengine
· wenye uwezo wa kufanya kazi, kufikiri, kuwa na upeo na wepesi wa kukabili na kufanya maamuzi magumu
· usiolea uzembe, ubaguzi, unyanyasaji, uhujumu, ubadhirifu, rushwa, kudharau, kudhalilisha, kujuana au kulinda maslahi ya wachache au kikundi Fulani
Wajibu wetu kama Taifa na haki yetu kama wapiga kura kuchagua viongozi kutuongoza unabidi uachane na mfumo duni tulioujenga wa kuangalia sura na chama na tuangalie wagombea wetu wa uongozi kwa vigezo hivyohapo juu ili kuunda tabaka jipya la viongozi ambao ni wachapakazi na watakuwa manahodha wazuri kutuongoza katika safari yetu ya kulijenga Taifa.
Tukilegalega katika hili na kupuuzia wajibu juu mkubwa na kuendelea kuchagua viongozi na wawakilishi wabovu, tutakuwa hatuna sababu yeyote kulia na kulalamika kuwa tu masikini au wanyonge kwa kuwa ni Ujinga na Upumbavu wetu kutumia akili na busara zetu tulizopewa Mungu tumekimbilia kurudia makosa ya kuwapa dhamana ya uongozi watu ambao hawafai kutuongoza.
Tuchague viongozi si kwa kuangalia vyama au sura, bali tuangalie uwezo wao wa kuongoza, kuhamasisha na kufanya kazi. Tupime kauli zao na matokeo ya kazi zao kama wanavyojinadi.
Serikali ni watu, inaundwa na watu tuliowachagua na tunawapa watu hawa na Serikali mamlaka makubwa ya kutuongoza, kupanga na kulinda Taifa na Katiba yetu. Dhamana hii imefanywa kwa kuaminiana kuwa Serikali itafanya kazi kwa manufaa ya Wananchi wake na kwa matakwa na utashi wa Wananchi wake.
Inapotokea kuwa Serikali inafanya kazi tofauti na dhamana iliyopewa, ni wajibu na haki ya kila Mwananchi kudai na kuhoji mapungufu yanayoonekana au kuzungumzwa. Ni wajibu wa Serikali na Uongozi kujibu na kuwajibika kwa Wananchi waliowapa dhamana ya kuongoza Taifa.
Ikiwa Serikali na watendaji wake na Viongozi wanashindwa kufanya kazi zao kama wanavyotegemewa kuzifanya na kushindwa kutimiza matarajio ya Wananchi na Taifa, ni wazi kuna umuhimu wa kupima uwezo wa viongozi na kuhoji Uzalendo wao na kama bado wanastahili kulitumikia Taifa.
Kuanzia Rais, Mawaziri, Majaji, Mahakimu, Wabunge, Wakuu wa Taasisi na Mashirika, Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Polisi, Magereza,Jeshi na watendaji wengine wa Serikali, tumaini la Watanzania na Taifa ni kuwa watu hawa wamepewa nafasi hizo kwa kuwa wanauwezo wa kitaaluma na kiutendaji kuwa viongozi na walinzi wa nguzo za Taifa letu kupitia Katiba na Sheria zake.
Hivyo basi pamoja na kuwa ni jukumu la sisi kama Raia na Taifa kudai uwajibikaji, lakini uzito wa kuhakikisha ufanisi wa Uongozi na uwajibikaji wake utaanzia na Mkuu wa Nchi ambaye ni Rais na Amiri Jeshi Mkuu.
Wasifu wa Uongozi bora nilioutaja hapo juu, si wa Rais pekee, ni wa kila mtu aliye kiongozi na ni shurti kila Mtanzania aishi kwa kuviangalia na kuvitumikia vipengele hivyo bila kujali yeye ni Kiongozi au la.
Serikali yetu ni kubwa sana na ina watendaji wengi ambao sitaficha kusema kuwa asilimia 55% hawastahili kuwa viongozi kutokana na kushindwa kuwa na sifa nilizozitaja hapo juu.
Hii ni hatari sana kwa Maendeleo na Usalama wa Taifa letu. Hatuwezi kuendelea kujiongoza kiholela huku zaidi ya nusu ya viongozi wetu hawana Uzalendo au uchungu na nchi yao. Swali kwako Mtanzania ni kwa nini basi ukubali kuendelea kujichagulia viongozi wabovu wasiofaa na kuwapa dhamana kubwa sawa na kumpa Simba jukumu la kulinda Mbuzi wako?
Kinachikosekana kutoka Uongozi Mkuu hasa Urais na hata Mawaziri ni uwezo wa kudai kwa nguvu uwajibikaji na uadilifu. Hadithi na tuhuma za ufisadi zilizotawala Taifa letu kwa kipindi cha zaidi ya miaka 10 ni kutokana na kuwa na Uongozi dhaifu, usiojali maslahi ya Taifa, uongozi uliojaa woga na kulindana na kushindwa kusimama kidete kulinda rasilimali za Taifa letu.
Viongozi wakuu wa jamii kuanzia wakuu wa vijiji, kata, tarafa, wilaya, mikoa hata Taifa, wameendelea kufanya kazi bila kupimwa na waajiri wao wawe Wananchi au Serikali kuu kuhusiana na ufanisi na uwezo wao katika safari ya kulijenga Taifa na kuleta maendeleo.
Mapendekezo yangu ambayo yataanzia na wewe Mtanzania ni kuwapima viongozi wako kwa kutumia vipimo vyepesi sana. Vipimo hivi ni kama ifuatavyo;
· kupitia ripoti za kila mwezi, robo, nusu na mwaka mzima za maendeleo na kupima mafanikio na matatizo ya shughuli za maendeleo
· kuhoji na kuhakiki viwango vya kuongezeka vita dhidi ya ujinga katika wilaya au mikoa kupitia shule za msingi, sekondari, vyuo na elimu ya watu wazima
· kuhoji maendeleo ya afya kupiga vita maradhi, kuangalia takwimu za kupungua vifo vya Uzazi, vifo vya watoto, kupungua kwa uadimu wa lishe na magunjwa kama Kwashiakor, Utapiamlo, kupungua kwa magonjwa na vifo vya Malaria na Ukimwi
· ongezeko la nyumba bora, maji safi, barabara nzuri, shule, hospitali na zahanati, vyanzo vya ajira, viwanda na shughuli za kilimo
· hifadhi za chakula kukabiliana na njaa, mauzo ya mazao ya biashara na chakula
· matumizi bora ya fedha za bajeti ikiwa pamoja na kubana matumizi yasiyo ya muhimu, kudhibiti matumizi na mahesabu ya fedha za bajeti za matumizi na maendeleo
· kukagua na kuhakiki shughuli za maendeleo kuwa ni endelevu na kuhakikisha hazizoroti
Kwa kifupi ni kuhoji na kutathmini, ni shule ngapi tulizonazo, ni ngapi zimeongezeka, ni wanafunzi wangapi wamehitimu shule, ni hospitali ngapi tulizonazo zina uwezo gani, msisitizo wa kinga ni mkubwa kiasi gani kulingana na tiba, kuongezeka kwa shughuli za uzalishaji mali na hifadhi za mazao, kubana matumizi na matumizi mazuri ya fedha.
Nimeweka wajibu huu kwako wewe mwananchi kwanza na si ile kasumba ya kusubiri Kiongozi Mkuu-Rais au Waziri Mkuu ndio wawe wenye jukumu na uhalali wa kuhoji haya.
Vipimo hivi haviishii kwa Mbunge, Mkuu wa Wilaya au Mkoa ni mpaka kwenye Serikali kuu na hata vigezo hivi vinaweza tumika katika mashirika na taasisi za umma na zile binafsi.
Kama vigezo hivi vya uongozi bora na kupima uwajibikaji vingekuwa vikifuatwa kwa makini, tungeweza kuona uwiano wa maendeleo wa Taifa letu. Lakini ni mpaka pale tutakaboshinikiza na kudai kwa nguvu Utawala na uongozi bora, ndipo tutakapoona mafanikio na hivyo kuanza kupata tumaini la maendeleo ya Taifa zima.
Uongozi na Utawala bora huendana sambamba na dola. Katika Utawala bora, Serikali na Viongozi ni wabunifu wa mipango mizuri ya maendeleo, ni wapimaji wa kasi ya maendeleo na hufuata kanuni na sheria katika kufanya kazi zao.
Panapokuwa na Uongozi na Utawala mzuri, kero za wananchi hupungua na hata matumizi ya dola na vyombo vyake huheshimika na huwa ni kwa ajili ya manufaa ya Taifa.
Hali halisi ya Tanzania imejenga mfumo wa utawala unaolinda utashi na maslahi ya chama tawala au kikundi chenye nguvu za madaraka nja mali. Hali hii imefikia hatua ya kikundi hiki cha watawala kutumia nguvu za dola kutawala kwa mabavu, kukiuka sheria na kanuni alimradi wanatumia kinga ya uongozi.
Utawala wa namna hii si mzuri na hauna manufaa hata kidogo kwa nchi yetu au Taifa lolote. Tunapaswa kukemea na kuondokana na mfumo huu mbovu wa Utawala ambao unatumia dola na kuweka wajibu wa kwanza wa Uongozi ni kulinda matakwa ya Chama au kikundi maalum.
Aidha matumizi mabovu ya dola na vyombo vyake, Bunge, Mahakama, Polisi, Jeshi na Usalama wa Taifa yamesababisha kwa kiwango kikubwa kuzorota kwa Uongozi, kuweko kwa utawala mbovu ambao umeishia kuangamiza uchumi na juhudi za maendeleo ya Taifa.
Wajibu wa vyombo kama Bunge na Mahakama ni kuwa mihimili mingine ya Serikali. Bunge likitunga Sheria, Mahakama ikitoa tafsiri za sheria na Serikali kuu kufanyia kazi sheria. Badala ya vyombo hivi kuwa huru na hata kuhakiksha vyombo visaidizi kama Polisi, Jeshi, Mahakama, Magereza, Usalama wa Taifa na ofisi ya Mwanasheria Mkuu vinabakia kuwa vyombu huru ndani ya mfumo wa kisiasa, vyombo hivi vimegeuzwa na kutumika kama silaha ya kulinda chama kinachotawala kwa kutoa vitisho kwa wananchi na vyama visivyo na madaraka.
Suluhisho la haya yote ni kuundwa kwa Katiba mpya na Sheria mpya ambazo zitalenga;
· kutoa haki sawa kwa kila mwananchi bila upendeleo
· kutofungamana na chama au kikundi cha siasa au watawala,
· kuwajibisha Watanzania wote bila kujali nafasi zao katika jamii na Taifa,
· kulinda maslahi, haki , uhuru na mali za Watanzania wote bila kujali itikadi, dini, elimu, jinsia, umri au kabila
· kutoa tafsiri na maelezo ya kisheria na kanuni ambayo hayana utata au kukosa nguvu kufanyiwa kazi na kufuatiliwa
· kumpa kila Mtanzania fursa na haki sawa katika kuchangia kwake ujenzi wa Taifa na hata kuongoza bila kuwa na vipingamizi vya kibaguzi ambavyo vimewekwa maksudi katika katiba ya sasa na Sheria kuzuia ushindani au kuwepo kwa uhuru kamili wa kujieleza na kufanya mambo ya siasa na uongozi
· kujenga miiko mikali na maadili kwa viongozi, utawala na wanachi kwa ujumla
· kuweka mfumo bora wa uteuzi au uchaguzi wa viongozi na wawakilishi
Penye nia pana njia, kama wote tutakaa mstari mmoja na kukubaliana kwa pamoja kuwa haya ndiyo tunayoyataka kutoka kwa viongozi wetu, mfumo wetu wa utawala na dola, nafasi ya kupata viongozi wazuri, kuwa na mipango mizuri itafanikiwa na hivyo kuruhusu wananchi na viongozi kuwajibika kwa dhati na kujituma ili kuhakikisha kuwa shughuli za Ujenzi wa Taifa kiuchumi unafanikiwa kukiwa na Amani, Mshikamano, Sheria na Uongozi Bora.
 
Waraka wa Mchungaji kwa Watanzania

Ndugu Mtanzania,

Naomba kuwasilisha kwako waraka huu ukiwa ni mwamsho na na hamasa kwetu kama Wananchi na Taifa ili kulikwamua taifa letu kutoka katika hali mbaya ya kiuchumi tuliyonayo inayoenda sambamba na kuzorota kwa Uongozi na Utawala bora.

Matatizo ya Tanzania yamegawanyika katika makundi makubwa mawili ambayo ukiangalia kwa kina, yanaoana na kila moja kinategemea mwenziwe. Matatizo haya ni Uchumi (Umasikini, Ujinga na Maradhi) na Uongozi (Utawala holela, Uzembe, Rushwa, Uvivu, uwajibikaji).

Naomba upokee waraka huu kupima nafsi yako na wale watakao kuja kwako kuomba kura yako wakati wa uchaguzi, uwe ni wa Serikali ya Mitaa, Wabunge au Urais. Nakusihi utumie mwamko na hamasisho hili kujihoji nafsi kuwa wewe binafsi una nafasi gani na nguvu zako zina nafasi gani ili kuleta msukumo utakaoleta maendeleo ya kweli na kulikwamua Taifa kutoka kwenye shida zinazotuzingira na kutudumaza. Kutumia waraka huu, jiulize kwa makini ni nini maana ya Maendeleo na ni maendeleo ya namna gani Watanzania wanayataka na yatawasaidia vipi wao na vitukuu vyao.


Miaka 9 iliyopita niliandika haya yafuatayo hapa chini kama ningekuwa mgombea Uchagusi Mkuu 2000. Nayarudia tena kwa kuwa ni katika haya kumi (10) ndivyo Mipango ya Maendeleo kwa mujibu wa mawazo na maoni ya Mchungaji (pamoja na kuwa si mtaaluma katika Uchumi na Uongozi )yanaweza kutumika kama nyenzo na dira kutukwamua kama Wananchi binafsi, jamii na hata Taifa.
  • Kurudisha na kuimarisha Heshima, Utu na Uadhi ya Mwananchi na Taifa la Tanzania
  • Kurudisha na kuimarisha Heshima, Wajibu na Hadhi ya kazi na kufanya kazi kwa Watanzania wote, vijijini na mijini
  • Kuelimisha Wananchi haki zao kama raia, wajibu wao na sehemu yao katika Taifa na Serikali yao kupitia Katiba, Serikali Kuu, Bunge na Mahakama
  • Kuimarisha Ufanisi na Ustawi wa Jamii katika kupiga vita Ujinga, Umasikini, Njaa na Maradhi
  • Kuhakikisha kuwa Katiba, Sheria na Kanuni zilizowekwa zinatekelezeka kutokana na nyakati zilizopo, zinafuatwa ipaswavyo na vyombo vyote husika; Serikali, Bunge, Mahakama na Wananchi wenyewe. Aidha kuweka maamuzi na mipango ya Serikali wazi kwa wananchi wote ili kuhakikisha uadilifu na uwajibikaji wa Serikali haufanyiki kwa siri na na kuwapa wananchi wote haki kwa kuwa wao ndio waliotoa dhamana ya kuwepo kwa Serikali na kuruhusu Uongozi uliopo uongoze nchi
  • Kubuni mbinu za kiuchumi ili kumpunguzia mzigo mwananchi wa kawaida hasa wale wa kipato cha chini na wakulima ili kujenga nguvu kubwa ya taifa kuwa katika Tabaka la kati (middle class)
  • Kuhakikisha kuwa njia kuu za Uchumi na uzalishaji mali zinaboreshwa na kutumika kwa manufaa ya kila Mtanzania na taifa la Tanzania linanufaika kwanza
  • Kuhamasisha na kuhakakisha kuwa Uzalishaji mali (kilimo, viwanda, uvuvi, ufugaji, biashara, madini , utalii, biashara, sanaa, michezo, huduma na maofisini) unafanyika kwa dhatgi, kisayansi, kiushindani, kiuwajibikaji, kiufanisi na kwa ubora wa hali ya juu kwa kutumia tija, kuongezeka kwa juhudi na maarifa ya uzalishaji mali huu
  • Kuhakikisha kuwa huduma za msingi zinaboreshwa na kupewa kipaumbele na kufikishwa kwa wananchi ili kujenga maendeleo ya kweli kwa jamii na Taifa;- Afya, Elimu, Maji safi, Chakula, Uchukuzi na Nishati
  • Kuhakikisha kuwa vita dhidi ya Rushwa, Ubadhirifu, Udini, Ukabila, Uzembe, Ufisadi, Uhujumu, Uvivu, Uzururaji na Kutowajibika au kutokujituma kwa watendaji wa Serikali na taasisi zake (wakuteuliwa au kuchaguliwa), waajiriwa , wafanyakazi na wakulima ni vita vya Taifa zima na linahitaji ushiriki na kushirikisha Wananchi wote. Wananchi wote bila kujali kabila, rangi, jinsia, umri, elimu au mwelekeo wa kisiasa ni wajibu wao kushiriki katika vita hii
Vipengele hivi kumi (10) si vigumu sana kutuumiza kichwa. Ni mambo ya kawaida ambayo tumekuwa nayo lakini kwa miaka karibu 20, tumeondokana nayo na kuishia kuzunguka kama punguani. Tumeshindwa kuwa makini katika Uongozi kitu ambacho kimezalisha uzorotaji na kudumaa kwa uchumi pamoja na takwimu zote zinazosema kuwa uchumi wetu unakua.
Uchumi wa Tanzania utakuwa pale ambapo Mtanzania ataacha kutafuta makombo ili aweze kumaliza siku moja anayoamka akiwa hajui kesho ikoje.

Kutokana na udhoofu wa Uchumi na kuzorota kwa Uongozi, hadhi yetu na kujivunia kwetu kuwa Watanzania kama tulivyozoea kujivuna na kuimba "Tazama ramani utaona nchi nzuri... Nasema kwa kinywa na kufikiri nchi hiyo nzuri ni Tanzania" imeshuka na hatujiamini tena. tumekuwa wanyonge na kukubali kuburuzwa na viongozi wetu na hata wafadhili.

Tunahitaji kujirudishia Uzalendo na hadhi yetu kama Taifa. Tukubali makosa tuliyofanya kwa kukusudia au bila kudhamiria. Hiyo itakuwa hatua ya kwanza ya kutafuta suluhisho la matatizo yetu na kujirudishia hadhi yetu na ya Taifa letu.

Msahafu na maandiko yanasema, "asiyefanya kazi na asile". Watanzania tumesahau nidhamu na wajibu wa kufanya kazi. Tumeendekeza malalamiko na manung'uniko, huku tukipunguza tija na juhudi kulilia motisha. Kama tutageuza nguvu zetu hasi kuhusu uchapaji kazi na kuzifanya chanya kuongeza uzalishaji mali na kuachana na kutegemea misaada, basi nafasi yetu ya kuwa na maendeleo ya kudumu yanayoendelea yatakuwa makubwa na hata viongozi wetu ambao wamekosa dira na mwamko wa kutuongoza wataona aibu tutakapoamka kudai haki zetu kutokana na jasho letu.

Ni wajibu wa kila mmoja wetu kuangalia Kazi kwa mtazamo wa kimaendeleo na chanya. Bila kufanya kazi, kwa ufanisi, juhudi na uhodari, hatutaweza achana na umasikini na unyonge. Iwe ni mijini kwenye maofisi, biashara, viwandani, mashambani au migodini. iwe kazi za kuajiriwa au kujiajiri, ni lazima tuheshimu kazi na kazi ziwe ni zile halali za kutupa mapato.

Hadhi na utu wa Uzalendo na Utaifa na Taifa letu, vitakuwa havina maana kama Mtanzania hatajua wajibu na haki zake Kikatiba, hatajua na kutumia Sheria na kanuni za nchi kujilinda na kujiongoza. Viapo vyetu vya utii visiishie kuwa ni viapo hewa kwa ajili ya kuapa. Tunapoapa kulitumikia Taifa na kuimba wimbo wetu wa Taifa "Mungu Ibariki.." ni lazima tuwe wakweli na wenye Uzalendo wa kweli ndani ya moyo. Kuelewa haki yetu Kikatiba kutaongeza ufanisi wetu na hasa wajibu wetu kama Raia katika kuweka Sheria za kuilinda nchi yetu na kuwa makini kuchagua viongozi wa kutuongoza kama Taifa.

Wajibu wetu mwingine ni kuhakikisha kuwa kazi yetu haishii katika kulinda katiba na kujua haki zetu kama Watanzania, bali ni kufuata sheria hizo na kuzithamini. Tuwe mstari wa mbele kufuata sheria na kanuni tulizonazo na tuwakosoe na kuwafikisha kwenye sheria wale wote ambao kwa makusudi au bila kukusudia wamekiuka sheria au kanuni. Tusiwaonee haya wale wanaopindisha sheria au kuvunja sheria biola kujali sehemu yao katika jamii. Kama Waziri anapinda Sheria ni wajibu wetu kama jamii kumwajibisha. Kama mbunge anavunja Sheria, ni wajibu kumfikisha mbele ya vyombo vya dola ili haki na hukumu kwa kuvunja Sheria ifanyike.

Sheria na kanuni hazikuwekwa zifuatwe na wananchi pekee. Watawala na Viongozi hawana kinga ya aina yeyote ya kuwaepusha kufuata kanuni,sheria au katiba. Sheria na katiba ziliundwa ili zifuatwe na kila raia na mkazi wa Tanzania.

Wakati wa Azimio la Arusha tulitamka kuwa ili tuendelee tunahitaji Watu, Ardhi, Siasa safi na Uongozi Bora. Tukatamka kuwa tunataka kujenga Taifa huru la Kijamaa na lenye Kujitegemea. Tukasisitiza kuwa vita dhidi ya Ujinga, Umasikini, Njaa na Maradhi vitashinda kama tutatumia Juhudi na Maarifa katika kazi zetu na maisha yetu.

Kazi tuliyonayo sasa si tofauti na ile ya mwaka 1967, ni ile ile na sana sana ni kulenga Nyenzo kuu za maendeleo yetu kama Taifa na kibinafsi kwa kupitia milango miwili. Ili tujikwamue kutoka hali hii mbaya tuliyonayo kama Taifa, ni wajibu wa kila mmoja wetu kuwajibika na kuwa na nia ya kweli kuyafanya yafuatayo;
  1. Kujenga Uchumi imara na madhubuti. Hili litatusaidia katika vita dhidi ya Umasikini, Ujinga, Maradhi na Njaa
  2. Kuwa na Uongozi mahiri na fanisi. Utawala na uongozi wa nchi unahitaji na unategemea Uongozi mahiri kutekeleza sera na mipango, wenye ufanisi kuhamasisha uzalishaji mali na uwajibikaji na wenye kuwa wanyenyekevu na kuheshimu dhamana walizopewa
Uchumi wetu hauwezi kujengeka kwa kutegemea misaada au wawekezaji kutoka nje kuja na kusukuma gurudumu la uzalishaji mali ili kutuongezea kipato. Aidha uchumi wetu hautajengeka kuwa madhubuti kwa kuanzisha mipango mipya au kufanya makosa yaleyale ya kale yaliyofanyika wakati wa Azimio la Arusha, Mipango ya kufufua uchumi 1985-2000 au mipango ya kuchochea Uwekezaji na kuvutia wageni washike hatamu za Uchumi ya 1992-2010.


Uchumi utakaoleta matunda ya kweli na ya maana ni uchumi utakaotokana na juhudi za wananchi katika shughuli zote za uzalishaji mali. Tunahitaji tuwe na mipango inayoeleweka na rahisi kufanikisha safari hii ya kujenga uchumi kwa kutumia mazingira yetu, rasilimali zetu na kwa faida yetu.

Moja ya njia zitakazotumika kuimarisha uchumi ni kubadilisha mfumo wa mapato ya Serikali na kudhibiti matumizi.

Kwa kuanzia, Serikali itabidi kupitia mikataba yote na kuongeza viwango vya kodi na ushuru (taxes, duty and royalties) zinazopatikana kutokana na wazalishaji mali wawekezaji. Kiwango cha asilimia 3% tunachotoza kwa shughuli za uchimbaji madini, gesi, makaa na hata huko mbeleni madini ni kidogo sana. Serikali ifuatilie kwa makini mapato halisi ya makampuni yote yanayojishughulisha na shughuli za uzalishaji mali na kuhakikisha kuwa Serikali inapata malipo ya kweli na yanayowiana na uzalishaji na mapato ya makampuni haya.

Serikali ipitie majedwali na ripoti za mapato ya kifedha (financial statements and bapance sheets) ya makampuni haya katika nchi zilikoandikishwa. Mfano pamoja na kuwa kampuni ya Barrick inatozwa asilimia 3% kama kodi kwa Serikali ya Tanzania, ni ukweli usiofichika kuwa Serikali na taifa la Tanzania linapunjwa. Mpango wangu utahamasisha kuchangua vitabu vya kampuni hii katika soko la mtaji la kimataifa kama NYSE, na kuangalia ni mapato kiasi gani ambayo wameyaorodhesha.

Mapendekezo ya kubadilisha viwango hivi vya mapato ya Serikali yanayotokana na uzalishaji mali wa makampuni mageni na hata enyeji, utahakikisha kuwa misamaha yote ya kodi na ushuru ambayo imetumika kama chambo cha kuvutia uwekezaji na kufanya biashara inafutwa au itapewa kipindi kifupi mno ili kupunguza hujuma na dhuluma. Mapendekezo ya kuongeza mapato yatakuwa ni kuongeza viwango vya kodi za mapato kwa makampuni haya kutoka 3% hadi kufikia 20% katika kipindi cha miaka mitano tangu sheria ianze kutumika.

Umiliki wa sekta za madini, uvuvi, utalii uhakikishe kuwa Watanzania kwa kupitia mashirika ya ndani yanakuwa naUshirika yanakuwa na 40% ya umiliki ili kuhakikisha kuwa Taifa haliendelei kunyonywa. Matarajio ya mpango huu ni kuwa Wawekezaji wenye utu watakubaliana na kufanya kazi na Serikali na Taifa kwa manufaa ya pande zote mbili.

Mapato haya ya kutokana na ongezeko la kodi, ushuru na umiliki yataliongezea Taifa pesa za kuweza kuondokana na misaada na mikopo ambayo imetulemaza na kutufanya kuwa tegemezi na masikini. Kuongezeka kwa mapato kutokana na kodi na ushuru kutapunguza ule mzigo wa Serikali kutegemea mazao ya chakula na biashara katika kupata fedha za uendeshaji. Mapato haya yatakuwa moja ya nyenzo kuu za kujenga uchumi kwa kutumika katika kuboresha sekta za Elimu, Afya, Miundombinu na Nishati.

Itaendelea...
Mwaka 2008 Ulisema utarudi Tanzania na kuanzisha chama chenye mtazo huo na mimi nilikuahidi kuwa mwanachama wako! Je kipi kilikushinda au ujio wa Dr.Slaa ulikupa matumaini kama sisi wengine?
 
Mwaka 2008 Ulisema utarudi Tanzania na kuanzisha chama chenye mtazo huo na mimi nilikuahidi kuwa mwanachama wako! Je kipi kilikushinda au ujio wa Dr.Slaa ulikupa matumaini kama sisi wengine?
Usiwe na shaka kaka, sikusema lini... ila iko siku...Si Dr. Slaa au CCJ changed my mind...
 
Back
Top Bottom