'Marshall Plan' - Restoration and Recovery Plan for Tanzania

Sanctus Mtsimbe,
Mkuu samahani sana, nitakuomba uandike maelezo yako kwa lugha yetu ya Kiswahili ili wengi wasomaji wpate kukuelewa.
Binafsi sina pingamizi na matumizi ya kiingereza isipokuwa kutokana na experience yangu ni kwamba Watanzania wengi wana elimu ya darasa (Theory) na huwa shida sana kwao kuweza kujieleza kwa lugha yao wenyewe kwa sababu masomo yote waliyopitia huwa ni kwa lugha ya kigeni (kiingereza) na katika mazingira ya kigeni (Ulaya) hivyo huwa vigumu kwao kuweza kuandaa vitu vinavyolingana na mazingira yetu ambayo asilimia 80 ya wananchi hawazungumzi kiingereza. Na kibaya zaidi ni kwamba wananchi hawa walio wengi hawafahamu kitu hutoka watupu kama vile wanatazama sinema za kihindi ama za Kichina kina Mithun na Cheng Sing..Utaonekana Starring lakini kila ulosema hakuna waliliambulia...
Kwa hiyo mkuu nitashukuru sana kama utaweza kuyaweka maelezo yako ktk lugha inayoeleweka kwa wengi na huwezi jua utawaelimisha wengi na pengine kuweza kupima uzito wa mapendekezo yako kulingana na watu na mazingira yeke.

Rev. Kishoka,
Mkuu tunaomba muda zaidi unajua tena summer hii wengi ndio wakati wa laana hivyo muda wa kukaa nyumbani jua kali inakuwa ngumu..
Tunaipitia MP taratibu na bila shaka tupo pamoja.
 
Sanctus Mtsimbe,
Mkuu samahani sana, nitakuomba uandike maelezo yako kwa lugha yetu ya Kiswahili ili wengi wasomaji wpate kukuelewa.

Mkuu Mkandara, nitajitahidi kufanya hivyo. Unajua kilichotokea ni coincidence ya mawazo yangu na Plan ya Rev. Kishoka. Issue ya Elimu na Kilimo nimekuwa nikivifanyia kazi muda mrefu na nilikuwa nimeviandika kwa kiingereza katika kumbukumbu zangu kwa sababu za kiutendaji na hivyo ilikuwa rahisi kwa mimi kutoa mawazo yangu katika lugha hiyo.

Bila ya shaka nitajitahidi kuzingatia ushauri wako
 
Mkuu Mkandara, nitajitahidi kufanya hivyo. Unajua kilichotokea ni coincidence ya mawazo yangu na Plan ya Rev. Kishoka. Issue ya Elimu na Kilimo nimekuwa nikivifanyia kazi muda mrefu na nilikuwa nimeviandika kwa kiingereza katika kumbukumbu zangu kwa sababu za kiutendaji na hivyo ilikuwa rahisi kwa mimi kutoa mawazo yangu katika lugha hiyo.

Bila ya shaka nitajitahidi kuzingatia ushauri wako

Binafsi nimekuelewa Mtsimbe na kwa kweli plan yako pia ni safi sana...Halafu ni very applicable.
Pia kwenye kilimo ndio umemaliza kazi...Swali la muhimu ni hapo..Tutumie madini yetu na nishati pamoja na tourism kukiinua kilimo chetu na uone jinsi Tanzania itakavyoneemeka...Watu watakimbia mijini na kila mahali hadi vijijini kutakuwa ULAYA ULAYA!
Hakuna maendeleo ya kweli tutakayoyapata kama tusipoweka mkazo kwenye kilimo.
 
Sanctus, JMushi, Mkandara,

Nawashukuru kwa kurudisha uhai kwenye hii mada.

Sanctus, nashukuru sana kwa mchango wako na kunipa mawazo ya ziada na naomba kuibia kutoka kwako.

Kwa ujumla, Waraka huu una madhumuni ya kumfikia mwananchi wa kawaida kwa kutumia lugha rahisi na inayoeleweka pamoja na vitendea kazi na mifano halisi ambayo inaweza kumfanya ajielewe na kujua umuhimu wa kuchagua viongozi bora na hivyo kudai maendeleo kutoka kwa uongozi kwa kutumia vigezo hivyo.

Mfano wa mapato ya madini ni rahisi sana. Katika kila shilingi 1000 ya ratili moja ya dhahabu inayochimbwa Tanzania, Tanzania kama Taifa inapata shilingi 30 tuu kama pato na kodi, je hii ni sawa? sasa ukimwambia Mtanzania kuwa anahujumiwa kwa mfano hai kama huo, basi ni uamuzi wa Mtanzania huyu kusuka au kunyoa, kuendeleza libeneke la UOngozi mbovu ambao unalea dhuluma na kupunjwa au atataka uongozi mpya ambao utahakikisha kuwa maslahi ya nchi yanalindwa na maliasili zinatumika na kuwapa Watanzania manufaa!

Niliondokana na kuwa na lugha ya kifundi na kitaalamu sana kwa kuwa mlengwa halisi wa Waraka huu, si Mtaalamu au bingwa wa mambo ya Uchumi, Kilimo, Madini au mambo mengine ya uzalishaji mali, Elimu au afya. Waraka huu ni wa kumfumbua macho Mtanzania ajue ni vipi anaweza kuyataka maendeleo na kwa tafsiri kamili ya maendeleo.

Kujenga shule, zahanati ajira, mapato ni vitu vya kawaida, na ukimuonyesha Mtanzania kuwa maendeleo ya kweli yanawezekana kwa urahisi ikiwa yeye atashiriki katika ujenzi wa Taifa na kuchagua uongozi bora, basi mambo yatakuwa dole tupu na si magumu na visingizio vingi ambavyo tunapewa na viongozi wetu.

Leo Rais anatutamkia kuwa hali ya uchumi ni ngumu, lakini kila siku anasafiri nje ya nchi, je wananchi wanajiuliza hata mara moja, kuwa kama hakuna pesa za kununa madawa au kulipia waalimu, Raisi anapata wapi pesa za kutalii dunia nzima na msururu wa wapambe? Mawaziri wanapata wapi pesa za kutembea kila kona kwa ufahari huku Waalimu, Waganga na Wafanyakazi kwa ujumla wanaishi kwa dhiki huku tunaambiwa tufunge mikanda?

Serikali ya Tanzania inavyofanya mambo na kudai hali ngumu ya fedha kuwajibika ni sawa na Mzazi (Baba) ambaye anawaambiwa watoto na mkewe kuwa hana fedha za chakula, nguo au kununua vitabu, lakini kila jioni, mzazi huyu akitoka kazi au baada ya shughuli anakwenda kutumia pesa kwenye ulevi!
Tuendeleze mjadala.
 
Rev. Kishoka,
Mkuu mimi nimefurahi sana na mtazamo wako kwa Tanzania ya kesho kwa sababu kubwa moja.
Kama unakumbuka tulikuwa na mada moja iliyokuwa ikikusanya mawazo ya watu kuhusiana na Kile Tanzania inakihitaji ili Kuendelea...
Mawazo mengi yalichangiwa na nadhani binafsi nilianza kuandika kitu kuhusiana na mfumo wa Kiuchumi...Ulikuwa waraka mrefu ambao sikuweza kuumalizia kutokana na safari yangu Bongo.. lakini baada ya kurudi toka Bongo niligundua kwamba Tanzania ipo ktk melikebu inayoingiza maji au ni pakacha linalovuja... sio tu inahitaji Dira kutufikisha ktk hiyo promised land (maendeleo) lakini muhimu zadi Tanzania ilikuwa imegubikwa na kundi baya la MAFISADI ambao waliweka tobo ktk meli yetu ya usafiri..Nikasema kwamba bila tanzania kuondokana na UFISADI kamwe hatuwezi kwenda popote hata kama tutakuwa na rasilimali kubwa kama mafuta na kadhalika..

Sasa baada ya kushindwa kuondoa UFISADI kwa njia bora - SHERIA kutokana na sababu kwamba katika hao manahodha wetu tuliowategemea kutuongoza ndio wao washiriki wakubwa ktk UFIISADI, nilianza kukata tamaa...Nikakubaliana sana na msemo wa Nyani ngabu kuwa sisi NDIVYO TULIVYO na pengine viongozi wetu hawa ni reflection yetu sisi wenyewe (wengi kati yetu)... Nikaanza kuamini pengine hata mimi nikpewa nafasi ya Uongozi sintakuwa na tofauti na viongozi waliopo leo kwani hiyo ndiyo hali halisi ya Tanzania - Under any circumstances, No one can change it....Kwa hiyo maendeleo yatabakia kuwa ndoto ya mchana ambayo sana sana ni jinamizi wakati mataifa mengine ndio kwanza yamefungua macho yao na kuelewa umuhimu wa kutambua maslahi ya nchi yanatangulia kila kitu...

Ni hadi hapo niliposoma waraka huu wa Marshall Plan ndipo nilipopata wazo jipya, nikafikiria pengine Mapinduzi ya Kifikra kwa wananchi ndio dawa kubwa ya kuondokana na adha zote yaani ikiwa manahodha wetu ndio MAFISADI na hakuna uwekezekano wowote wa kuwaondoa MAFISADI kisheria kwani wao ndio WATAWALA waliokaa mbele ya sheria, basi pengine ni jukumu letu sisi wananchi wenyewe kuchukua nafasi hiyo ya kuwaodoa hawa viongozi MAFISADI ktk viti vyao. Na hakuna njia bora kama kuwaelemisha wananchi wapiga kura ambao wataweza kuyaona mazuri yaliyowezekana bila kuwa na Uongozi mbaya.
Nikapenda zaidi mtililiko na mpangilio wa Marshall Plan kwa sababu ulianza kumtazama na kumuuliza mwananchi mwenyewe MALENGO ya safari yake.. Ni kweli kabisa huwezi kuwa na nahodha mzuri na akasifiwa kwa kazi yake ikiwa hafahamu wasafiri wake wanataka kwenda wapi?..

Miaka yote ya nyuma tumekuwa tukipangiwa safari, ni mfumo uliotangulia chini ya Mwalimu ambaye alikuta usafiri wa wakati ule ulipitia njia mbili tu - KUSHOTO ama KULIA..
Ni katika mfumo huo inawezekana kabisa tulijenga watu ambao wanaitwa Untouchables - Wanasiasa ambao kwa wakati ule waliitwa waasisi wa chama cha TANU kina Rupia, na baadaye wakati wa Mwinyi tukawaona Ditopile na Kitwana Kondo (watoto wa mwalimu) wakiwa na nguvu kubwa serikalini kuliko hata Waziri mkuu..

Pamoja na mapinduzi ya kiuchumi likazaliwa Azimio la Zanzibar ambao kwa mfumo huo huo likazua Untouchable wengine - Wafanya biashara kina Rostam ambao leo hii wana nguvu kuliko Wanasiasa... Ni muhimu tukubali kwamba ktk dunia hii SIASA siku zote ni mchezo mchafu, hata nchi zilizoendelea kama Marekani zinaendeshwa na watu kama hawa Untouchables.. lakini wao huwatumia WASOMI zaidi watu kama Karl Rove au Law firms ambazo zinajihusisha moja kwa moja na siasa..

Kwa hiyo ni muhimu kwa wananchi hasa wana JF kuelewa kwamba sasa kinachofanyika hapa ni hatua kubwa moja inayotangulia YOTE baada ya kushindwa kuendelea kwa kutumia rasilimali zetu kutokana na MAFISADI. Kushindwa kuwaondoa Mafisadi kwa sababu ni kati ya hao VIONGOZI wetu watawala ambao hawataki kuona maendeleo kwa wananchi wote isipokuwa matumbo yao, na pengine yawezekana kabisa hata wale wazuri waliopo hawafahamu sisi wananchi WATANZANIA tunataka kwenda wapi!..Nini maendeleo kwetu na wataweza vipi kuelekeza sera na dira zao Kichama kuweza kufikia Malengo yetu...UONGOZI bora ni ule tu unamwezesha mwananchi kufikia malengo ya yaliyokusudiwa... na kwa pamoja ni muhimu sana tujipange kuweka malengo yetu wazi...

Kwa hiyo mkuu hongera sana na pengine ningekuomba tu ktk Utangulizi wako uneweka kifungu kinachozungumzia MALENGO...
Ni vizuri kwa wasomaji waelewe Malengo haya kwa sababu nimeona mara nyingi watu hutaka kuelewa Marshall Plan hii inamlenga nani na wapi inaelekeza mapambano yake kama ulivyomjibu KINTO ukurasa wa 7...

Tuendelee kukumbuka maneno ya MKAMAP aliposema haya:-
Tatizo mimi ninaloona ni kua sisi wengi wetu ni kujaribu fikiri matatizo yetu ni kutokana na muono mbovu ama ufupi wa uelewa wa viongozi wetu kuhusu matatizo ya nchi yetu na kujaribu kutumia nguvu nyingi kuwapa plan B na namna ambayo ingefaa kuchukuliwa.
Ukweli ni kwamba hawa viongozi wana uelewa mkuu juu namna mbinu na mikakati ya kututoa ktk umasikini. Sasa basi kwanini hawafanyi hivyo?
Ni jaribio hatari kwao na falme zao za kimwinyi kujaribu kumletea masikini maisha bora,kwao ktk hali hiyo ya umasikini ni Bora zaidi ya mara mia kuliko kuwaendeleza wananchi na hatimaye utawala wao kupeana vijiti kua ktk hali tete.
Yani kwao kumuendeleza masikini ni sawa na kumpa adui yako silaha makini na mbinu maridadi.
Wao wana endekeza mfumo huo ili wapokezane madaraka watoto wajukuu,vitukuu,vining'ina.
Na ukitaka kuangalia kwa makini na kuunganisha nukta ni kwa nini bodi ya mkopo pale wanataka lazimisha mtoto wa masikini lazima asome Engineering?? Maana akisoma masomo mengine ama asipate kabisa mkopo ama wampe 50% sasa hizo zingine atatoa wapi??.
Tatizo la TZ sio mipango wala sera ,tatizo ni patriotism tupiganieni patriotism kwanza..

Maneno mazito sana na ndio maana naipenda JF...
 
Mchungaji,
Napata shida sana kwani watu kama wewe wenye mitazamo mizuri hampati nafasi ktk utawala wa taifa letu, nchi yetu sasa inarithishwa kwa watoto waviongozi na si vinginevyo.

Mchungaji hapo nyuma ktk thread yangu( Mbowe jiuzulu ukinusulu chama) nimeshauri kuwa tupate kiongozi mwingine anayeweza kuendeleza kazi njema aliyoianzisha, la kushangaza wewe na vigogo wengine ktk forum hii mmekaa kimya, ama mmeiona ni mada hiyo ni tete au vipi.

Mchungaji
Mchango wako bado unaitajika ktk taifa letu

Mungu ibariki Tanzania

IsayaMwita,

Kuwa na uwezo wa kujieleza na kuchambua siasa hakuna maana kuwa basi naturally mtu anafaa kuwa kiongozi!

Kunatofauti sana kati ya Uanasiasa na Uongozi. Ni watu wachache sana wenye uwezo wa kuwa Wanasiasa wazuri na Viongozi bora.

Nitaendelea kupiga kelele, kwa kuwa nimejifunza kutoka kwa Kikwete. Kikwete alikwenda kama mwanasiasa akitegemea kuwa angeweza kufanya analotaka. Lakini ukweli ni kuwa kwa kuwa alirithi kundi la Wanasiasa na viongozi kwa takriban asilimia 80%, uwezo wake kiutawala kama kiongozi umeingia kigugumizi na mashaka na hivyo kuonekana kuwa ni kiongozi dhaifu. Mbaya zaidi ni mbinu alizotumia kuingia madarakani na ushirika alioujenga wakati akiingia madarakani na kuendelea nao mpaka leo.

Naamini kwa dhati sasa hivi Kikwete anajutia faulo na ushirika alioujenga tangu 1995 mpaka alipochaguliwa kuwa Kiongozi wa Taifa letu. Kabakia mtalii, hawezi kufoka wala kutoa amri.

Waraka huu si wa kubadilisha kichwa, ni kubadilisha mfumo mzima wa uongozi. ndio maana kama umenisoma mara nyingi hoja zangu kwa wapinzani, nimeuliza kuna faida gani kukimbilia Ikulu na Uraisi ikiwa Bunge na sehemu nyingine za Serikali bado ziko katika mfumo wa zamani na CCM?

Wazungu wanasema overhaul, tunahitaji overhaul ya mfumo mzima wa Uongozi anzia Serikali kuu, Mahakama, Bunge na sehemu nyingine kama tunataka kuona maendeleo na ufanisi ukiongezeka kulijenga Taifa na kuleta demokrasia.

Ndiyo maana waraka unaanza kwa kumhoji Mtanzania na kumsukuma ajihoji ni yapi aliyoyafanya ambayo yamezuia Taifa kuendelea.
 
Mkandara,

Nimekupata mkuu. Waraka huu unahitaji kusomwa kwa makini na ikiwezekana mtu aurudie tena ili aweze kuuelewa.

Alipokuwa Allien na kudai tuache kulalamika na tuanze kutoa mambo ya kujenga nchi, nilikuwa tayari nikilifikiria hili jambo la kuandika Marshall Plan. Katika miaka yangu yote ya Forums, iwe ni Nyenzi, BCS, TEF, Jambo na sasa Jamii, nimeelekeza nguvu na utashi wa kukosoa au kujenga kwa masikio mabovu, Viongozi na vyama vya kisiasa. Natamka rasmi masikio mabovu hata kama Mnyika, Zitto na Dr. Slaa watakasirika ni ukweli tumeshakata ishu (nikimuiga FMES) nyingi sana ambazo hasa watu wa Upinzani au Serikali wangeweza kujifunza na kuamua kuzifanyia kazi.

Nimebadili mlengwa safari hii na kuwa ni Mtanzania yule wa vijijini, mijini mpiga kura ili niweze kujua je, tukiwafikia wao na kuwaelimisha, watabadilisha mfumo ulioko na kupokea maoni na elimu hii ya bure? au wao kama Wanasiasa na Viongozi wataendeleza libeneke na kuboresha yaleyale tuliyoyaoea na hivyo kufanya na kutimilisha kauli ya Nyani Ngabu "ndivyo tulivyo"?

Nimechukua muda nikipanga mawazo yangu upya na nitarekebisha mambo kadhaa na kuanza kuuchapa waraka katika magazeti nyumbani ili watu waanze kuusoma na hata ikiwezekana waanze kuusambaza na majadiliano yaanze.

Si tunasikia KALOKIRO wameanzisha magazeti manne mapya na tayari wanaye rafikiye FMES kama Mtarajiwa 2015, jinsi Kikwete alivyofanywa mtarajiwa na ROLOKIMK 2005?

Kama wameshaanza kupangiana nani atarithi ili kulinda maslahi yao, basi tunahitaji kufanya kazi ya ziada kuwapindua kwenye vita vya itikadi na kuwafikia wananchi ili tusiendelee kupumbazwa na Ulabu, Ubwabwa, Kikoi na Gagulo.
 
inaendelea...


Viwanda, Mashirika, Huduma na Biashara

Makosa ya Azimio la Arusha ni sawa na yale mapinduzi ya viwanda ambayo yalifanywa na Stalin kule Urusi na hata Mao wa China na ile sera ya Great Leap Forward. Aidha makosa ya wakati wa kubinafsisha viwanda miaka ya 1990-2008 ili kuachana na kuendesha viwanda kutokana na ufanisi mdogo na kuingia hasara hayatarudiwa.

Tumejifunza kuwa tunataka kuwa na viwanda, lakini kilichotushinda hapo awali ni kukosekana utaalamu, motisha, ubunifu na tija katika kuendesha viwanda hivi. Viwanda kama Machine Tools, Mgololo, Ufi, Mwatex na vinginevyo havikustahili kufa.

Makosa ya kuzubaa na kuendelea kuvikamua na kutumia mapato ya viwanda hivi kwa kazi nyingine ambazo hazihusiani na shughuli za uzalishaji mali wa viwanda hivi kama kujijenga kisiasa na vyama vya siasa, ulisababisha kwa kiwango kikubwa kuanguka kwa viwanda vyetu. Makosa ya kubebesha Mashirika na Viwanda mzigo wa Public Welfare, haukuwa mzuri. Ni mfumo huo ambao ulisababisha mapato ya wafanyakazi kudumaa na hivyo kuchochea vitendo vichafu ambavyo viliua moyo wa uchapa kazi, uwajibikaji na uadilifu.

Mpango wa Mchungaji ni kurejesha viwanda vya kusindika mazao ya chakula na biashara, viwanda vya mchecheto (processing) mazao kama katani, pamba, viwanda vya bidhaa za matumizi ya nyumbani na viwanda na yote haya ni katika jitihada za kupunguza uagizaji wa bidhaa za matumizi kutoka nje. Motisha utatolewa kwa viwanda vya zana za kilimo na ujenzi.

Msukumo wa kujijenga kiviwanda utalenga kujenga na kuimarisha viwanda kutokana na rasilimali tulizonazo zikiwa ni pamoja na kilimo na chakula, mifugo, uvuvi, misitu, madini, ngozi, nguo, madawa, mbolea, na kama tutakuwa na uwezo, viwanda vya teknolojia kama vifaa vya umeme.

Kwa kuwa tutakuwa tumeweka nguvu katika nishati, kuwepo kwa umeme wa kutosha kutakuwa ni motisha kukaribisha viwanda vya wawekezaji wa kimataifa ambao hukimbia nchi zao kutokana na gharama kubwa za uzalishaji na kutafuta gharama rahisi za kuzalisha mali. Kukaribisha wawekezaji hawa, hakuna maana kuwa Tanzania itakubali wafanyakazi wake wanyonywe au kudhalilishwa kwa kuwa ni cheap labor. Serikali itahakikisha kuwa sheria za kazi za nchi na kimataifa zinafuatwa ikiwa ni pamoja na kanuni za usalama viwandani.

Mashirika kama SIDO na NDC, yatapewa msukumo wa kuchocha ukuaji wa viwanda na taaluma za ndani. Wahitimu kutoka vyuo vya VETA , watapewa miongozo na usimamizi na kusaidiwa shughuli zao kupitia SIDO. NDC itarudishwa kuwa nguvu iliyoleta maendeleo ya viwanda kabla ya zoezi ka kuuza mashirika.

Kama Taifa, tumejijenga kwa kuwa na biashara ndogo ndogo na si biashara kubwa. Tumejenga utamaduni wa kukimbila biashara za bidhaa dhaifu na zisizo na ubora na kutokana na mtazamo duni, tunashindwa kukabili ushindani wa kibiashara kutoka kwa wageni.

Elimu ya biashara, utunzaji mahesabu, bajeti, masoko na matangazo ya biashara, yatasaidia sana kuhakisha sekta hii ya biashara na viwanda inakuwa kwa ushindani na umahiri. Tukiangalia wenzetu Wakenyana hata Rwanda, mipango yao ya maendeleo ni shirikishi katika kuelimisha wafanyabiashara wao mbinu bora za kufanya biashara.

Bodi kama BET na BIT zinabidi ziungane na TCCIA kuwa na mikakati bora ya kuimarisha viwanda na biashara.

Pendekezo moja ambalo litasaidia jamii na wafanyakazi katika nyanja hii na hasa katika Viwanda na Mashirika ya Biashara na Huduma ya umma ni kuanza kuwashirikisha wafanyakazi katika umiliki wa vyombo hivi kwa kutoa hisa za mashirika haya kwa wafanyakazi wake, ili nao wanufaike na mgawanyo wa riba za mapato. Hii itakuwa ni motisha na kichocheo kikubwa cha kujenga Uwajibikaji, Uaminifu, Tija na Utii (loyalty).

Katika kila nyanja ya uzalishaji mali, huduma na kuwa na malengo bora ni kiini cha mafanikio. Waliosema kuwa mteja ni mfalme hawakukosea. Viwanda, Mashirika na Wafanyabiashara wetu wanabidi kujizatiti na kukabili ushindani kwa kuwa na huduma na bidhaa bora, kuwa watangazaji wa bidhaa za ndani ili kuongeza mapato ya ndani

itaendelea...
Nimefarijika kuona Rev. Kishoka umetumia muda wako na kushusha mipango, hata kama ina dosari hapa na pale lakini kuna starting point na ni mwanzo mzuri kwa mjadala mkubwa. Kila mmoja wetu akishusha kwa mtindo huu wa uwazi na mkamilifu, tunaweza tukagundua matatizo yetu yako wapi! Hongera sana Rev. Kishoka
 
Nimefarijika kuona Rev. Kishoka umetumia muda wako na kushusha mipango, hata kama ina dosari hapa na pale lakini kuna starting point na ni mwanzo mzuri kwa mjadala mkubwa. Kila mmoja wetu akishusha kwa mtindo huu wa uwazi na mkamilifu, tunaweza tukagundua matatizo yetu yako wapi! Hongera sana Rev. Kishoka

Dr. Slaa,

Nami nafarijika kuona kuwa umechukua muda kuusoma waraka huu. Kama utapenda, nitumie anuani pepe (email) ili nikutumie waraka mzima kwa ukamilifu na si vipande vipande.

Waraka bado haujakamilika, bado navuta muda kupokea maoni ya watu na baadaye kuhakiki na kuuchapa na kuusambaza kwa Taifa.

Tuliambiwa ili tuendelee tunahitaji Watu, Ardhi, Siasa safi na Uongozi Bora. Ardhi tunayo, Watu tunao ingawa tunaambiwa hatuna watu wa kutosha wenye uwezo wa kufikiri, kinacholegalea ni Siasa safi na Uongozi bora.

Tukiweza kuwapa watu nguvu na uwezo wa kujiamini, basi watatumia ardhi vizuri, watasahihisha siasa mbovu na kuondoa uongozi uliooza!
 
Kwa wale ambao walikuwa wanahitaji nakala ya Waraka wa mchungaji, mkibonyeza hichoo kitufe chenye kuonyesha attachment, mtaipata nakala kamili ikiwa katika word document format.
 
Kwa wale ambao walikuwa wanahitaji nakala ya Waraka wa mchungaji, mkibonyeza hichoo kitufe chenye kuonyesha attachment, mtaipata nakala kamili ikiwa katika word document format.
Rev Sijaona hiyo attachment!? au ni mimi tuu?
 
Inaendelea...

Uchumi utaanza kujengeka kwa kuanza kujenga misingi bora ya maarifa na hii ni kupitia sekta ya Elimu.

Elimu

Mfumo wa elimu wa Tanzania unabidi kubadilika na kuhakikisha kuwa tunajenga mfumo wa elimu ambao unachochea ubunifu, unarahisisha uzalishaji mali na unawiana na maendeleo yetu. Kuna haja ya kuachana na mfumo wa Elimu ya kufaulu na kuhakikisha kuwa kinachofundishwa kinaeleweka na kinaweza kutumika ipaswavyo na wanafunzi wote, kuanzia chekechea, shule ya msingi, sekondari, vyuo vya fani stadi na hata elimu ya juu.

Mpango wa Rev. Kishoka kuboresha Elimu ni kuhakikisha kuwa mitaala na silabasi za kufundishia zinalingana na mahitaji ya jamii. Kipaumbele kitakuwa si kuongeza shule ili kuongeza maarifa na taifa la walioelimika, bali ni kuwa na elimu ya kiwango cha juu, elimu ambayo itafundishika kwa urahisi na kuweza kutumika kwa vitendo kadri wanafunzi wanavyoendelea kujifunza.

Mkazo utakuwa ni kuwa na walimu wenye uwezo wa kufundisha na wenye mapenzi katika fani ya ualimu. Waalimu watapewa kila nyenzo zinazohitajika kuhakikisha kuwa kazi zao zinafanyika kwa ufanisi na mafanikio na matunda ya kazi zao yanaonwa na kupokewa na jamii nzima.

Katika mpango wangu, kila Wilaya itapaswa kuwa na Shule si chini ya mbili za Sekondari na chuo cha ufundi ambazo zitakuwa chini ya mamlaka za Tamisemi. Kila mkoa utapaswa kuwa na shule za sekondari ya elimu ya juu si chini ya 4, Vyuo vya ualimu, uuguzi na utabibu, kilimo, uvuvi na mifugo, , biashara na uhasibu, ufundi (mithili ya Dar Tec), sanaa utamaduni na michezo.

Katika elimu ya juu ya kiwango cha Chuo kikuu, msukumo utakuwa wa kuwa na chuo kikuu kwa kila mkoa ifikapo mwaka 2050. Katika hili, uchochezi wa kupanuka kwa sekta ya kilimo utajumuisha watu binafsi, taasisi za kidini na jumuiya za maendeleo za mikoa.

Jukumu la Serikali kuu litakuwa ni kuratibu mfumo wa elimu na si kuendesha kila kitu kuhusiana na Elimu. Chini ya mpango huu, Serikali Kuu itasaidia kwa kipindi cha miaka minne kwa shule na vyuo kujijenga na uendeshaji wake na baada ya hapo, jukumu litakuwa katika Serikali ya mitaa na jamii kuhakikisha kuwa wajibu wa kuziendesha shule na vyuo hivi havitegemei Serikali kuu pekee.
Serikali kuu itakuwa tayari kutoa msaada na ushauri. Serikali kuu itajenga mfuko na mfumo mpya wa mikopo ya Wanafunzi na kuachana na bodi ya mikopo ya Wanafunzi iliyoko sasa hivi ambayo ni kero kwa wananchi na wanafunzi.

Matarajio ya mpango huu wa elimu ni kuwa kwa kusogeza mchakato mzima wa elimu kwa mamlaka za mikoa, zitasaidia ile dhamira ya kusukuma madaraka mikoani, wananchi wa mikoa na wilaya watapata fursa sawa na wale walioko katika mikoa mingene ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikinufaika kwa kuwepo kwa kila aina ya shule na vyuo.

Msisitizo utakuwa katika elimu ambayo itazalisha watu ambao wako tayari kufanya kazi. Fani kama uhunzi, uashi, useremala, ufundi mchundo, bwana shamba, bwana maji, fundi umeme, magari, na ujenzi zitaongeza idadi ya watu wenye ujuzi si wa asili na kuvumbua binafsi, bali kwa kupata mafunzo na nyenzo za kuboresha vipaji asili katika fani hizo.

Tutakapoweza kuwa na msingi bora wa elimu ambayo utaongeza maarifa na kuchochea juhudi za kila mmoja wetu na kuhakikisha kuna ushiriki wa kila mmoja na kila mmoja ana nafasi ya kuwa bingwa katika fani yake, masuala kama ukosefu wa ajira au kukosekana kwa walio na utaalamu katika fani mbali mbali utapungua.

Lakini hatutaweza kufanikisha azma ya kuwa na mfumo na elimu bora ikiwa maslahi na vitendea kazi vya waalimu na shule zetu vitaendendelea kuwa duni na dhaifu, huku Serikali ikifumbia macho na kusukuma wajibu huo kwa Wananchi, Waalimu na uongozi wa shule na vyuo hivi. Suala la maslahi ya waalimu nitaliongelea kwa mapana na marefu katika kipengele cha Ujira, Mishaharana maslahi ya Wafanyakazi.

itaendelea...


Mch. Ningependa uongezee kipengele cha LUGHA katika sehemu ya ELIMU. Hii nikutokana na ukweli kwamba lugha ndio inatumika kuhifadhi au kubeba ufahamu (knowledge) kutoka sehemu moja kwenda nyingine. mfano kutoka kwa mwalimu kwenda kwa mwanafunzi na kinyume, kutoka kwenye vitabu kwenda kwa mwalimu au mwanfunzi. n.k

Kwa mantiki hiyo, lugha inabidi ipewe msisitizo MAALAMU katika sera ya elimu. Kwa maoni yangu, Tanzania ni Lazima tujifunze na kujua kwa ufasaha angalau lugha mbili, kiswahili na kingeereza. Hii itawawezesha waTanzania kuchota ufahamu mwingi ambao tayari upo katika lugha ya kiingereza bila kutegemea wakalimani nk na wakati huo huo kuendelea kuwa na identity yetu kupitia lugha ya Kiswahili.

kwa mtazamo wangu, tatizo la lugha Tanzania ni KUBWA na lenye mizizi mirefu ndani ya jamii, kuliko watuwengi wanavyo dhani, na suluhisho lake linahitajika haraka!


Asante.
Selemala.
 
Mch. Ningependa uongezee kipengele cha LUGHA katika sehemu ya ELIMU. Hii nikutokana na ukweli kwamba lugha ndio inatumika kuhifadhi au kubeba ufahamu (knowledge) kutoka sehemu moja kwenda nyingine. mfano kutoka kwa mwalimu kwenda kwa mwanafunzi na kinyume, kutoka kwenye vitabu kwenda kwa mwalimu au mwanfunzi. n.k

Kwa mantiki hiyo, lugha inabidi ipewe msisitizo MAALAMU katika sera ya elimu. Kwa maoni yangu, Tanzania ni Lazima tujifunze na kujua kwa ufasaha angalau lugha mbili, kiswahili na kingeereza. Hii itawawezesha waTanzania kuchota ufahamu mwingi ambao tayari upo katika lugha ya kiingereza bila kutegemea wakalimani nk na wakati huo huo kuendelea kuwa na identity yetu kupitia lugha ya Kiswahili.

kwa mtazamo wangu, tatizo la lugha Tanzania ni KUBWA na lenye mizizi mirefu ndani ya jamii, kuliko watuwengi wanavyo dhani, na suluhisho lake linahitajika haraka!


Asante.
Selemala.

Selemala,

Kirutubisho kikubwa ambacho tumekipuuza na sikukiweka kwa makusudi hapa n ihiki ulichokileta cha lugha.

Ubaya mmoja ambao unaleta mgawanyiko ni ile hisia kwa ili Tanzania iendelee na kufana katika nyanja za kimataifa, ni lazima kila kitu kifanywe na kufundishwa kwa lugha ya Kiingereza.

Najiuliza iweje Mchina, Mjapan, Msweden, Mrusi, Mjerumani, Mturuki, Muajemi wa Iran, Mkorea, Mgiriki, Muargentina na wenginewe, waendelee mbele kwa kujifunza mambo kwa kutumia lugha zao kuu za asili na si lugha ya pili?

Iweje sisi Watanzania na hata Waafrika wengine kwa ujumla, tuhenyee na kuhemea kwa kuongea Kiingereza, Kifaransa, Kiarabu na Kireno ambazo ni lugha za pili na si mama ili tuwe na mwamko wa kutoa elimu na mafunzo?

Kiingereza ni lugha ya pili ukiondoa Kiswahili ambacho tumekifanya kuwa ni lugha kuu na kila Mtanzania anakielewa na ana uwezo wa kusoma na kuandika.

Kwa nini hatufanyi mapinduzi ya nguvu ya kujivunia tulichonacho na kukimbilia kudai ni lazima tujue kukoroga yai na kuongea ung'eng'e na umombo ili tuonekane tuna uwezo katika nyanja za kimataifa?

Laiti Watanzania na viongozi wao wangejua kuwa tungemfundisha mwanafunzi wa Tanzania masomo ya sayansi, biashara, utawala, sanaa na mengineyo kwa kutumia Lugha aliyo na uwezo nao na mamlaka nayo, tungekuwa tumepiga hatua sana kuleta jamii inayojitegemea na bunifu.
 
Rev:

Maandiko yako ni mazuri sana lakini napingana nayo kwa sababu hakuna jipya zaidi ya kueleza vilivyoeleweka kwa muda wa miaka mingi kwa kutumia lugha nyingine.

Kwanza Tanzania haiitaji Marshall Plan. Marshall Plan ilitumika ku-restore uchumi wa nchi za Ulaya magharibi kutoka na vita vya pili vya dunia. Kwa upande mwingine Tanzania haina cha ku-restore. Maendeleo yote yanayokuja Tanzania ni mapya na sio kitu kinachofanyiwa ukarabati (restoration).

Mfano wa Tanzania ni sawa na mtu anayejenga nyumba mpya ya kisasa wakati hakuwahi kumiliko kitu chochote na hana technologia ya ujenzi wa nyumba. Restoretion and Recovery Plans zinatumika kwa mfano wa mtu ambaye alishamilika nyumba na anao ujuzi wa kujenga au kumiliki nyumba lakini kwa bahati mbaya vitu nyumba iliharibika kwa sababu ya mafuriko au kitu kingine.

Swali Rev. Kishoka na wachangiaji wengine, je Tanzania ilikuwa na vitu gani ambavyo tunataka ku-recover au ku-restore. Kama vitu hivyo havipo basi safari ya maendeleo ilianza na mguu mbaya.

Vilevile kuna wachangiaji hapa wanaoleta masuala ya kimikoa kuonyesha kuwa watu wa mikoa fulani wanafanya kazi sana kuliko wengine na ndio sababu tupo nyuma. Nadhani hoja zako ni za maendeleo ya kiuchumi. Katika maendeleo ya kiuchumi kufanya kazi sana SIO CHANZO CHA MAENDELEO.

Narudi tena kwa herufi kubwa KUFANYA KAZI SANA SIO CHANZO CHA MAENDELEO YA KIUCHUMI.

Wanaochanganya hoja ya KUFANYA KAZI SANA wanatuletea MYTH katika dhana nzima ya maendeleo.

Kwa mfano watu wa mikoa ya Mwanza na Shinyanga wanafanya kazi sana na zenye mitulinga lakini mazao wanayouza kama pamba yanategemea sana bei katika soko la kimataifa. Hivyo juhudi zao za kufanya kazi haziwaletii maendeleo.

Kwa upande mwingine watu wa mkoa wa Kagera, Rwanda au Burundi wanafanya kazi wanafanya kazi ya kutunza mashamba yalioachwa na mababu zao hivyo hawafanyi kazi za mitulinga. Lakini kutokana na thamani ya kile wanachotunza, faida wanayopata ni kubwa sana kuliko ndugu zangu wasukuma.

Vilevile mmasai mwenye ng'ombe 1,000 anafanya kazi kubwa sana kutunza ng'ombe wake lakini katika maendeleo ya kiuchumi hana chochote anachochangia zaidi ya kuleta uharibifu wa mazingira. Kwa upande mwingine, mfuga nguruwe pale Kimara anatumia juhudi ndogo lakini anachofanya kina maana katika maendeleo ya kiuchumi.

Kwa kumalizia naomba watanzania tuanze kutumia akili zaidi, tuondoe myths katika dhana za maendeleo ya kiuchumi na tupunguze siasa.
 
Selemala,

Kirutubisho kikubwa ambacho tumekipuuza na sikukiweka kwa makusudi hapa n ihiki ulichokileta cha lugha.

Ubaya mmoja ambao unaleta mgawanyiko ni ile hisia kwa ili Tanzania iendelee na kufana katika nyanja za kimataifa, ni lazima kila kitu kifanywe na kufundishwa kwa lugha ya Kiingereza.

Najiuliza iweje Mchina, Mjapan, Msweden, Mrusi, Mjerumani, Mturuki, Muajemi wa Iran, Mkorea, Mgiriki, Muargentina na wenginewe, waendelee mbele kwa kujifunza mambo kwa kutumia lugha zao kuu za asili na si lugha ya pili?

Iweje sisi Watanzania na hata Waafrika wengine kwa ujumla, tuhenyee na kuhemea kwa kuongea Kiingereza, Kifaransa, Kiarabu na Kireno ambazo ni lugha za pili na si mama ili tuwe na mwamko wa kutoa elimu na mafunzo?

Kiingereza ni lugha ya pili ukiondoa Kiswahili ambacho tumekifanya kuwa ni lugha kuu na kila Mtanzania anakielewa na ana uwezo wa kusoma na kuandika.

Kwa nini hatufanyi mapinduzi ya nguvu ya kujivunia tulichonacho na kukimbilia kudai ni lazima tujue kukoroga yai na kuongea ung'eng'e na umombo ili tuonekane tuna uwezo katika nyanja za kimataifa?

Laiti Watanzania na viongozi wao wangejua kuwa tungemfundisha mwanafunzi wa Tanzania masomo ya sayansi, biashara, utawala, sanaa na mengineyo kwa kutumia Lugha aliyo na uwezo nao na mamlaka nayo, tungekuwa tumepiga hatua sana kuleta jamii inayojitegemea na bunifu.



Mch. Kishoka,

Labda majibu yatakayotosheleza maswali yako yanahitaji uchambuzi wa undani wa maswala mbalimbali. Hata hivyo ningependa kugusia swala moja kuhusu ufahamu (formal knowledge).

- je ilituweze kutumia kiswahili kama lugha ya kufundishia, itabidi tutengenze/tuvumbue elimu yetu wenyewe?

- kama ndio, je itahitaji nini kifanyike ilitufanikiwe? je ni kitu gani hasa kitafanya tuone kufundisha elimu tuliyovumbua wenyewe ni bora kuliku kufundisha elimu ambayo ipo tayari?

-kama sio, na kama tutahitaji kufundisha elimu iliyopo tayari, tutahitaji wakalimani na ruhusa ya kutafsiri maelfu ya maelfu ya vitabu, majarida, video ambazo tayari zipo/yapo kwa kiingereza (labda na lugha nyingine) Na ambazo zinaendele kuongezeka kila siku. je tutafanya kazi hii ya kutafsiri kwa muda gani? je ni mpango gani itabidi utumike ili kuhakikisha tunaendelea kuwa na wakilimani wa kutosha? je ni wakalimani wangapi na wenye elimu ipi (zaidi ya lugha) watatosha?

Binafsi naona tumeshachelewa sana kimaendeleo kuanza kutumia muda zaidi katika kutafsiri, badala yake tuimarishe ufundisha wa lugha hizi mbili, Kiswahili na Kiingereza, lakini kwa ufasaha zaidi. Ufundishaji fasaha wa lugha hizi utaleta mabadiliko chanya makubwa Tanzania.

natumaini, aina hii ya kufikiria itaamsha hamu ya kuchambua zaidi juu ya suala la lugha ambalo ninaona nitatizo kubwa lakitaifa.


selemala.
 
Ikiwa ni mwaka mzima umepita tangu niandike Waraka wa Mchungaji, najiuliza ni lipi lililobadilika?

Je ni muafa kwa Waraka huu kuendelea kupitiwa na kurudiwa tukijiandaa na Chaguzi za Tamisemi mwaka huu na Uchaguzi Mkuu mwakani?
 
Tatizo la Tz ni vipaumbele ni sifuri,as hatuwezi deal la vitu vyote at a time.
Kishoka Plan imetulia gonna dig deep into it later
 
Back
Top Bottom