SoC02 Mapenzi ni Janga kubwa kuliko UKIMWI

Stories of Change - 2022 Competition

Tukuza hospitality

JF-Expert Member
Jul 30, 2022
242
615
Mapenzi ni mahusiano kati ya watu wawili wenye jinsia tofauti (yaani, mwanamke na mwanaume). Kwa mujibu wa chapisho la Blog ya Muungwana ya tarehe 17/01/2018, mapenzi ni ile hali ambayo watu wawili wanaingia katika mahusiano ambayo yanabeba mambo mengi yakiwemo uvumilivu, unyenyekevu, busara, upendo, uwazi, na heshima.

Uvumilivu katika mapenzi ni muhimu sana kwani mapenzi ni kama safari ambayo ina mambo mengi yakiwemo mateso na mabadiliko mbali mbali.
Unyenyekevu ni muhimu katika mapenzi ya kweli.
Busara ni muhimu sana wakati wa kufanya maamuzi katika mahusiano.
Upendo ni hali ya kutengeneza imani imara baina wawili hawa katika mahusiano.
Uwazi ni hali ya kusomana na kufahamiana kimoyo, kimwili na kifikra.
Heshima nayo pia ni njia kuu ya kutengeneza maelewano sawiya.
Nakubaliana na chapisho hili, kwamba ni vigezo sahihi vya mahusiano.

Mapenzi ni hitaji la kila binadamu! Mwandishi nguli wa nyimbo nchini Canada, Leonard Cohen alisema 'Mapenzi hayana tiba lakini ndiyo dawa pekee ya magonjwa yote'.
Pia mwanamuziki nguli wa Tanzania, Fresh Jumbe, katika wimbo wake alisema, “Penzi ni Kikohozi”, akimaanisha penzi halifichiki!

Picha .. Wapenzi Aug 2022.jpg

Chanzo: NI NINI MAANA YA MAPENZI

Kwa nini Mapenzi yanakuwa Janga na sii Furaha?
Watu wengi wanaingia kwenye mahusiano kwa kusukumwa na tamaa pamoja na maslahi yao binafsi. Kwa upande wa wanawake, wengi huingia kwenye mahusiano na wanaume ambao wana uwezo wa kifedha, yaani hufanya wanaume kama vyanzo vya mapato kwa ajili yao na familia zao; na wanaume wengi hupenda mahusiano na wanawake wenye sura na maumbile ya kuvutia kimahaba. Katika vigezo vya mahusiano sahihi, fedha au uzuri havimo! Lakini fedha na uzuri ndio vigezo vilivyoshikilia mapenzi ya watu wengi ulimwenguni, na pale vinapokosekana, ndipo migogoro na majanga hulipuka.

Kwa nini nasema Mapenzi ni Janga kubwa kuliko Ukimwi?
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), kufikia mwaka 2014 ugonjwa wa ukimwi umeua takriban watu milioni 39, wengi wao wakiishi barani Afrika, hasa kusini mwa Jangwa la Sahara. Kwa mwaka 2015 pekee, wamefariki watu milioni 1.2, wengi wao wakiwa watoto.

Ugonjwa wa VVU/UKIMWI (Virusi vya Ukimwi/ Upungufu wa Kinga Mwilini) umeingia Tanzania mwanzo mwa miaka ya 1980, ambapo watu waliupa majina mbalimbali, yakiwemo “Juliana”, “Slim”, “Ngoma”, “Miwaya”, “Umeme” nk. Ugonjwa huu kwa kiasi kubwa unaambukiza kwa njia ya kujamiana (ngono).

Raisi wa Tanzania, awamu ya pili, Alhaji Ali Hussein Mwinyi, katika kampeni zake dhidi ya ugonjwa waVVU/UKIMWI, aliwahi kunukuliwa akisema; “Ugonjwa huu umeingia mahali pale kila mtu apapenda”. Watu wengi wanapenda mapenzi kiasi cha kufanya ngono zembe bila kuchukuwa tahadhari yoyote dhidi ya magonjwa ya ngono, ikiwa ni pamoja na VVU/UKIMWI; ndio maana ugonjwa huu umeendelea kuwepo kwa zaidi ya miaka arobaini sasa.

Sasa, nadhani unanielewa kwamba kwa kiasi kikubwa, MAPENZI ni chanzo cha VVU/UKIMWI!

Mbali na ukweli kwamba mapenzi ni moja ya sababu zinazoeneza VVU/UKIMWI (ambao husababisha vifo), kuna mauji ya moja kwa moja yanayotokana na mapenzi. Takwimu za Jeshi la Polisi zilizotolewa Julai, 2021 zilionyesha katika kipindi cha miezi miwili tu, Mei mpaka Juni, 2021 mauaji yaliyotokana na wivu wa kimapenzi yalikuwa 21. Ninaamini matukio yanayoripotiwa katika vyombo vya dola ni machache, matukio mengi humalizwa kindugu, hasa katika maeneo ya vijijini.

Katika vyombo mbalimbali vya habari, mwaka huu wa 2022 (ambao haujaisha) kumeripotiwa matukio mengi ya mauaji yanaotokana na wivu wa kimapenzi. Ni mwezi huu (Agusti, 2022) kijana mmoja (mwanaume) kule Songea amejinyonga baada ya kuambiwa kuwa mpenzi wake ambaye amekuwa akimsomesha chuo kwa gharama zake, amevishwa pete ya uchumba na kijana mwingine. Jambo hili liliamsha kichaa chake, na hakujua cha kufanya zaidi ya kujitoa uhai kwa kujinyonga!

Majanga ya Mapenzi yamekuwepo tangu zamani
Miaka mingi kabla ya kuzaliwa Yesu Kristo, Mfalme Daudi akiwa katika paa la nyumba yake alimwona mwanamke mzuri sana akioga, jina lake ni Bathsheba, binti wa Eliamu na mke wa Uria Mhiti. Daudi aliwatuma watumishi wake wakamchukue, na akalala naye. Ili Uria (mwenye mke) asimsumbue, Mfalme Daudi aliamrisha apelekwe vitani mstari wa mbele, na hatimaye aliuwawa huko. Habari hii inapatikana katika kitabu cha Biblia: 2 Samweli 11: 2 – 4; 26 – 27; 12: 24.
Mapenzi yalimchanganya Mfalme Daudi, ambaye alikuwa mtumishi wa Mungu, na kusababisha mauaji, je watu wa kawaida watasalimika?

Cleopatra ni Malkia wa Misri, aliyezaliwa mwaka 69 kabla ya Kristo na kutawala kati ya mwaka 51 na 30 kabla ya Kristo. Alikuwa mwanamke mrembo kuwahi kutokea, hadi leo. Alikuwa na mahusiano na mtawala wa Dola la Kirumi “Julius Caeser” ambapo walizaa mtoto mmoja wa kiume. Baada ya Julius kuuwawa, Cleopatra alianzisha mahusiano na Mark Anthony (mrithi wa “Julius Caeser”), na kuzaa naye watoto watatu. Anthony alimpenda sana Cleopatra, ndio maana akiwa nchini Italia, aliposikia uvumi kuwa Cleoptra amefariki, alijiua kwa kujikata na upanga, kumbe hazikuwa habari za ukweli! Cleopatra aliposikia Anthony amefariki, alienda kumzika, na baadaye naye alijiua kwa kutumia nyoka mwenye sumu kali. Cleopatra alifariki akiwa na umri wa miaka 39 tu, akiwa ametawala Misri kwa miaka 22.

Unaweza kuona, viongozi wawili wakubwa wanakufa kutokana na mapenzi! Mbali na kusababisha uyatima kwa familia zao, mataifa yao yalibaki yamevurugika kwa namna nyingi na kwa miaka mingi.

Nini kifanyike kupunguza majanga yanayotokana na Mapenzi/Mahusiano?
Kuhakikisha kwamba hutoi moyo wako wote kwa yule unayempenda; hii ni kwa sababu hujui moyo wa mwenzio. Ndio maana mwanamuziki Ben Paul aliimba “Moyo, sukuma damu na sii vingine”.

Serikali ikishirikiana na wadau mbalimbali iingize somo hili la mahusiano katika mitaala ya elimu kuanzia shule za msingi hadi elimu ya juu.

Serikali, ikishirikiana na wadau mbalimbali ianzishe madawati maalumu na kuajiri wataalamu husika (hasa wa saikolojia) kuanzia ngazi ya mtaa, watakaoshughulikia matatizo ya mahusiano.

Watoto wa kike wafundishwe kuanzia nyumbani na mashuleni, kujitegemea katika kutafuta njia za kipato, badala ya kufikiria wavulana/wanaume kama vyanzo vya mapato yao. Jambo hili litapunguza, kama sii kutokomeza kabisa mimba za utotoni, ndoa za mapema, na/au mahusiano ya kukurupuka.

Hitimisho
Mapenzi ni asili ya mwanadamu, yana kanuni zake ambazo zikifuatwa kikamilifu, basi dunia hii itakuwa mahali pazuri na salama pa kuishi.

Rejea

Yusuph Mazimu, BBC Swahili (1, Juni 2022), Mauaji ya wivu wa kimapenzi Tanzania, yalianza kama kipele, sasa ni jipu la kutumbuliwa



 
Sasa nimepata picha kamili ya mapenzi kuwa janga kuliko ukimwi, kwa kweli ndugu zangu wana JF kwa watu wenye wivu ni bora tuungane tu na mwanamuziki ben pol "Moyo sukuma damu sii vingine". Mapenzi sii kitu cha kukurupukia ni vyema kuwa makini wakati wakuchagua mwenza wako.
 
Back
Top Bottom