Maoni ya Wadau Kwenye Miswada ya Sheria za Uchaguzi na Muswada wa Vyama vya Siasa - Sehemu 2

Bull Bucka

Member
Oct 5, 2023
34
46
JamiiForums, Jukwaa la Katiba (JUKATA), Tanganyika Law Society (TLS), Twaweza East Africa, Centre for Strategic Litigation (CSL) na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwa pamoja tunawasilisha maoni kwenye miswada minne: Muswada wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani; Muswada wa Sheria ya Vyama vya Siasa na Gharama za Uchaguzi; na Muswada wa Sheria ya Tume ya Uchaguzi.

Serikali iliwasilisha miswada hii Bungeni na ilisomwa kwa mara ya kwanza tarehe 10 November, 2023. Kisha Kamati ya Bunge ya Sheria na Katiba imealika wadau kutoa maoni kwenye miswada hiyo kuanzia Januari 6-10, 2024.

Hii ni fursa muhimu sana katika ujenzi wa demokrasia nchini kwetu na kulinda haki muhimu za raia. Tunatambua pia awamu hii miswada hii haikuwasilishwa Bungeni kwa hati ya dharura na hivyo imeongeza muda kwa wadau kuweza kuichambua na kuwasilisha maoni. Kamati ya Bunge imefanya vyema pia kupokea maoni kwa siku kadhaa na kwa njia mbalimbali ili kuwezesha wadau wengi zaidi kuwasilisha maoni yao.

Kwa kuitikia wito huu na katika kutekeleza wajibu wetu wa kikatiba, tunafarijika kuwasilisha maoni yetu ili kuchangia katika kuboresha muktadha wa kisheria utakaowezesha kuimarisha demokrasia nchini kwetu Tanzania. Tunaamini haki na demokrasia ni misingi muhimu sana ya kuwezesha ushiriki wa watanzania wote katika kufikia malengo ya maendeleo.

Katika kila muswada, tunawasilisha maoni ya jumla na maoni mahsusi kifungu kwa kifungu. Maoni ya jumla yanatoa muhtasari wa mambo ya msingi katika kila muswada na maoni mahsusi yanatoa ufafanuzi wa kina wa mapungufu na maboresho katika vifungu vingi.

Muswada wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani unafanya jambo zuri la kuunganisha sheria mbili za awali na kutengeneza sheria mama ya maswala ya uchaguzi. Hili ni jambo zuri ili kurahisisha rejea ya kisheria. Maoni yetu yamelenga kuboresha utaratibu mzima wa uchaguzi ili kuhakikisha chaguzi zetu ni huru, za haki na za uadilifu. Tunapokuwa na chaguzi huru na za haki inaepusha uvunjifu wa amani na hivyo kuimarisha demokrasia yetu.

Muswada wa Sheria ya Vyama vya Siasa unapendekeza mabadiliko kadhaa kwenye Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2019. Pamoja na mambo chanya kadhaa ikiwemo kutoa ufafanuzi wa kuboresha maswala ya ujumuishi wa makundi maalum ndani ya vyama, muswada huu hauna mabadiliko makubwa sana katika sheria iliyopo. Na baadhi ya vifungu pendekezwa vinahitaji maboresho kama ambavyo tumebainisha katika uchambuzi wetu ili kuviwezesha vyama vya siasa kutekeleza majukumu yao ya kisiasa bila kukiuka katiba ya nchi yetu na sheria nyinginezo. .

Muswada wa Sheria ya Gharama za Uchaguzi unalenga kuhamasisha uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika maswala ya fedha kwa wadau wote wa uchaguzi. Hili ni jambo zuri katika kujenga demokrasia imara yenye uwazi na uwajibikaji wa wadau wote.

Muswada wa Sheria ya Tume ya Uchaguzi unapendekeza kuanzishwa kwa sheria inayojitegemea kuhusu Tume ya Uchaguzi. Sheria hii itatoa ufafanuzi wa kina kuhusu Tume ya Uchaguzi tofauti na ilivyo sasa ambapo Tume imetajwa kikatiba lakinin maelezo yake yamekuwa sehemu tu ya Sheria za Uchaguzi. Maoni yetu yamekusudia kuboresha muundo wa Tume na kuifanya iwe tume huru isiyoingiliwa na mamlaka yoyote katika utekelezaji wa shughuli zake.

Muswada wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani
Muswada huu unaunganisha sheria mbili za uachaguzi. Muswada hauna tofauti sana kimaudhui na sheria zilizokuwepo awali isipokuwa baadhi ya mambo mapya yamependekezwa ikiwemo kuiwezesha Tume ya Uchaguzi kukataa jina la mgombea wa chama kwa nafasi tajwa kwa kutumia sababu ambazo zimebainishwa katika muswada huu (Vifungu 36-37).

Uchambuzi wetu umezingatia matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977, mapendekezo ya ripoti mbalimbali hasa ripoti za Tume ya Taifa ya Uchaguzi, maamuzi ya mahakama za ndani na za kikanda pamoja na uzoefu na mifano kutoka nchi nyingine.

Kiujumla, muswada huu unamambo mbalimbali mazuri ikiwemo kuunganisha sheria mbili ambazo ni Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, 1979 kuwa sheria moja.

Miswada inapendekezwa kunzingatia na kuheshimu utawala wa sheria na uhuru wa mahakama katika maamuzi mbali mbali yaliyofanyika juu ya sheria na mambo yote ya uchaguzi.

a) Kesi ya Jebra Kambole dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Maombi namba 018/2018
iliyoamuliwa na Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu kuhusu kupinga matokeo ya uchaguzi wa Rais mahakamani.

b) Kesi ya LHRC, TLS na Mchungaji Mtikila dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Maombi namba 011/2011 kuhusu Mgombea Binafsi, iliyoamuliwa na Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu.

c) Kesi ya LHRC na Bob Chacha Wangwe dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Maombi namba 011/2020
kuhusu kuondoa Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji kuwa wasimamizi wa uchaguzi. Kesi iliyoamuliwa na Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu. Kifungu cha 6 (1) nafasi ya wakurugenzi kusimamia uchaguzi PIA REJEA MAPENDEKEZO YA TUME YA UCHAGUZI TANGU 1995.

d)
Kesi ya Tito Elia Magoti na wengine watatu (3) dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Shauri Na. 3/2022 kuhusu haki za mahabusu na wafungwa kupiga kura. Kesi ya Julius Ndyanabo kuhusu gharama za uchaguzi, kesi iliyoamuliwa na Mahakama ya Rufaa ya Tanzania. Kifungu cha 3 (d) 10(c) 10(2)

e)
Kesi ya Julius Ndyanabo dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali [2004] T.L.R. 14 [CA] kuhusu gharama za uchaguzi, kesi iliyoamuliwa na Mahakama ya Rufaa ya Tanzania. Vifungu cha 140 (2), 144 (2), 147 na 150(2) Milango ya haki inapaswa kuwa wazi wakati wote hata kwa watu masikini nchini”- Jaji Mkuu Mstaafu Barnabas Samata”

f) Kesi ya Joaran Bashange dhidi Mwanasheria Mkuu wa Serikali Shauri Namba 11/2021 kuhusu mgombea kupita bila kupingwa. Vifungu cha 38, 54 kimezingatia

g)
Kesi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali dhidi ya Dkt. Aman Walid Kabourou ambayo ilitoa tafsiri ya Ibara ya 74 (12) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 kuhusu kushtakiwa kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Kifungu cha 53 (6) “….anaweza kukata rufaa kwa Tume, na uamuzi wa Tume utakuwa ni wa mwisho na hautahojiwa na mahakama yoyote, isipokuwa kwa njia ya mashauri ya uchaguzi yatakayowasilishwa

h) Kesi ya Godbless Jonathan Lemba dhidi Musa Hamisi na wengine rufaa namba 47/2012 katika Mahakama ya Rufani Arusha, iliyoainisha mtu mwenye haki ya kufungua shauri la kiuchaguzi.

i) Freeman Mbowe, Hashimu Rungwe, Salum Mwalimu and Legal and Human Rights Centre v. Attorney General of the United Republic of Tanzania consolidated reference No. 3 and 4 Mahakama ya Afrika Mashariki ilibatilisha vifungu 3, 4,5,9, 15 and 29 vya Political Parties Act ambavyo vilionekana viko kinyume na Ibara za 6(d), 7(2) na 8 (1) (c) za Mkataba Unaoanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki, 1999 na kuelekeza serkali ya Tanzania irekebishe sheria iendane na Mkataba huo.

Pia soma: Maoni ya Jumla ya Wadau Kwenye Miswada ya Sheria za Uchaguzi na Muswada wa Vyama vya Siasa - Sehemu 1
 
Back
Top Bottom