Maneno ya Mwigamba

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,789
288,020
Anaandika SAMSON MWIGAMBA
June 19, 2019

Zitto ajiandae kupambana na Maalim Seif, hana hadhi ya kupambana na JPM

QURAN Tukufu inasema alama za mnafiki ni tatu. Kwanza, akisema hasemi ukweli. Pili, akiaminiwa haaminiki. Na tatu, akiweka ahadi hatekelezi!

Nimekaa na kufanya kazi na wanasiasa wengi tokea niingie rasmi kwenye siasa. Katika wanasiasa wote niliofanya nao kazi mpaka leo, sijawahi kuona mwanasiasa mnafiki kama Zitto Zuberi Kabwe!

Hakuna mwanasiasa aliyewahi kumwamini Zitto Kabwe akaaminika. Kuanzia kwa Freeman Mbowe mpaka CCM ya Kikwete.

Aliaminiwa na Chacha Zakayo Wangwe hakuaminika. Siku anashirikiana na Mbowe kumshughulikia Chacha Wangwe pale Dodoma, Wangwe alimwambia Zitto Kabwe kwamba mkuki aliokuwa. anautumia kumchoma ndio huo huo utakaomchoma Zitto Kabwe mwenyewe.

Wakati anashikishwa adabu na akina Mbowe wale wale, Msafiri Mtemelwa alimkumbusha Zitto maneno ya Wangwe, akalia machozi.

Mwaka 2009 alipochukua fomu kwa mara ya kwanza ya kugombea uenyekiti wa taifa wa CHADEMA, ilikuwa ni wiki moja tu tokea apange namna ya kugawana nafasi za juu za chama na wakurugenzi wa makao makuu ya CHADEMA.

Zitto Kabwe alikaa na akina Benson Kigaila na wakurugenzi wengine makao makuu ya CHADEMA wakapanga kwamba kwa kuwa Dkt. Willibrod Slaa alikuwa ametangaza kustaafu ukatibu mkuu, basi yeye Zitto awe Katibu Mkuu, mwenyekiti taifa aendelee kuwa Freeman Mbowe. Anthony Komu awe Naibu Katibu Mkuu, nk.

Wiki moja tu, akina Kigaila wakasikia Zitto amechukua fomu ya kugombea uenyekiti wa taifa. Wengi wao wakamgeuka na kukataa huo mradi wake mpya alioshauriwa na akina Msafiri Mtemelwa. Akaanza kupanga safu nyingine tena.

Makamu mwenyekiti bara awe Mzee Philemon Ndesamburo, Katibu Mkuu awe Mzee Sylivester Masinde, Naibu Katibu Mkuu Bara awe Anthony Komu. Lakini tena wiki chache baadaye Zitto akajitoa kwenye kinyang’anyiro hicho na kumwachia Mbowe!

Kuanzisha ACT na kuondoka CHADEMA nako kulikuwa na rangi nyingi sana za Zitto Kabwe. Mwanzo kabisa aliweka msimamo kwamba CHADEMA wakimfukuza uanachama hawezi kuwa mbunge wa mahakama. Atakubali kufukuzwa waende kwenye uchaguzi mdogo.

Agombee kupitia chama kipya halafu yeye aiombe CCM (ya wakati huo) imsaidie kwa kuweka mgombea dhaifu na kuacha kumsaidia ili Zitto ashinde. Akadai kwamba akiwashinda wagombea wa CHADEMA na CCM, atakuwa amerejesha nguvu yake (renewing mandate).

Tuliposikia kikao cha kutujadili na kutufukuza uanachama kimekaribia, Zitto akasema sisi wawili tukubali kufutwa ila yeye anakwenda mahakamani kupinga kufukuzwa ili kulinda ubunge wake. Akageuka!

Alifanya hivyo kwenye kuhamia rasmi ACT, aligeuka mara tatu. Alifanya hivyo kwenye chama kusimamisha mgombea 2015. Mwanzo alitaka tuwe na mgombea, lakini tusishirikiane na Lowassa kwa namna yoyote ile. Baadaye akasema tukimpata Lowassa kuwa mgombea wetu itakuwa safi sana.

Tulipokaribia kabisa uchaguzi baada ya Dkt. Magufuli kupitishwa kuwa mgombea wa CCM akasema tusimamishe mgombea atakayeshindana na Lowassa halafu Magufuli ashinde. Na akawa anatushawishi tumteue Kitila Mkumbo awe mgombea wetu.

Alipoitwa na upande wa Lowassa akaahidiwa uwaziri mkuu, akageuka tena. Kwenye kikao cha kamati kuu akaungana na maswahiba wake kukataa mgombea wa ACT.

Baada ya Kitila kukataa kugombea, rafiki yake waliyepanga naye mwanzo kwamba wamshawishi Kitila agombee, akamfuata.
Baada ya kushawishiwa na huyo tena, akageuka kwa mara nyingine.

Akataka Kitila akubali kugombea, Kitila akakataa. Ni Zitto aliyetoa shilingi milioni 5 zilizokusanya watu mitaani Mbagala wasio wanachama wa ACT wakaja Makao Makuu ya ACT na kujifanya wana ACT wanaotaka Kitila agombee urais kupitia ACT.

Baadhi yao walipoulizwa mnayetaka agombee urais kupitia ACT anaitwa nani, walisema “Tunataka Prof. Mtikila agombee urais”. Walikuwa hawajui hata jina la Kitila.

Baada ya mpango huo kushindikana, akarudi tena kwenye mpango wa Lowassa. Alitumia nguvu kubwa sana kukishawishi chama kutosimamisha mgombea urais. Lakini Kamati Kuu na Halmashauri Kuu zikamgomea na baada ya kampeni zake dhidi yangu, hatimaye akapitishwa Mama Anna Mghwira kugombea.

Nikamwambia shida yangu ilikuwa chama kiwe na mgombea urais na siyo mimi kugombea. Niliombwa baada ya kukosekana mgombea, kwa kuwa Mama Mghwira amekubali, safi!Tuliotaka mgombea urais tukafurahi, yeye akanuna.

Akafanya mpango wa kuhujumu fomu za wadhamini wa mgombea urais mkoa wa Dar es salaam, pia akashindwa. Mwisho akaamua kususia kabisa kampeni za mgombea urais. Zitto Kabwe huyo!

Lakini ni Zitto Kabwe huyu huyu aliyegombana na akina Mbowe na Lissu walipokuwa wanampinga Magufuli baada ya kuchaguliwa. Alibaki bungeni akina mbowe waliposusia kikao cha Bunge cha Rais Magufuli kulizindua bunge, akamsifia sana Magufuli kwamba hotuba yake imetoka kwenye ilani ya ACT kwa asilimia 60.

Hata mara kadhaa alionekana kumsifia sana Magufuli wakati mwingine akimponda, na pale aliposhindwa kabisa kupata kile alichokitaka kwa Magufuli, ndipo akaamua kujiunga tena na akina Mbowe na Lissu kumpinga Magufuli hadi leo.

Huyo ni Zitto Kabwe aliyekuwa upande wa Lipumba wakati mgogoro wa ndani ya CUF umeanza. Alimsaidia Lipumba kwa kumpa vijana wa kufanya fitna. Lakini pia alimpa Lipumba wanasheria wa kumtetea kwenye kesi aliyofunguliwa na upande wa Maalim Seif.

Kabla kesi haijaisha akahamia upande wa Maalim Seif na leo Maalim Seif ni mwanachama namba moja wa ACT.

Sasa ameamua kuongeza dozi ya kumpinga Rais Magufuli. Na kwa vile sasa yuko na hasimu wa Dkt. Shein, ameanza kuwachanganya Rais Magufuli na Dkt. Shein. Ili awapendeze wagombea wake wote.

Anampinga Magufuli kwa ajili ya kumfurahisha yule mwana CCM aliyemwahidi pesa za kujengea chama anayefadhili harakati zake zote za hivi sasa na ambaye ameahidi kugombea urais wa Muungano kupitia ACT uchaguzi ujao. Wakati huo anampinga Rais Shein ili kumfurahisha Maalim Seif aliyejipanga kugombea urais wa Zanzibar kupitia ACT 2020.

Hiyo ndiyo mantiki ya mazungumzo yake na vyombo vya habari Jumanne ya wiki iliyopita. Aliponda serikali ya muungano na ile ya Zanzibar kwa pamoja. Alisema uchumi wa nchi yetu unaporomoka na akasema anatumia takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BOT) hususan tathmini za uchumi za kila mwezi.

Leo nataka niwaonyeshe uongo wake. Nimechukua ‘Tathmini ya uchumi ya kila mwezi kwa mwezi Aprili 2019’. Hebu tuipitie tuone anachokizungumza anayejiita mchumi Zitto Kabwe na kilichoelezwa na Benki Kuu ya Tanzania.

Tuanze na Wastani wa Pato la Taifa kwa mtu mmoja (GDP per capita). Wakati Rais Magufuli anaingia madarakani mwaka 2015, GDP per Capita ilikuwa dola za kimarekani 991.7. Mwaka 2016 ikapanda kuwa dola 1,006.5 na mwaka 2017 ikafikia dola 1,045.1.

Amezungumzia urari wa biashara (trade balance) katika nchi yetu. Kwa kawaida urari wa biashara unapatikana kwa kuchukua mauzo yetu ya nje na kutoa manunuzi yetu ya nje. Ili taifa lionekane linafanya vizuri kiuchumi, inatakiwa mauzo ya nje yawe makubwa kuliko manunuzi kutoka nje.

Manunuzi kutoka nje yakiwa madogo kuliko mauzo yetu nje, urari wa biashara unakuwa chanya (positive) na kadri hiyo tarakimu chanya inavyokuwa kubwa, ndivyo uchumi unavyozidi kuwa mzuri.

Mauzo ya nje yakiwa madogo kuliko manunuzi yetu toka nje, urari unakuwa hasi (negative) na kadri tarakimu hasi inavyozidi kuongezeka, ndivyo uchumi wetu unavyozidi kuonekana taaban. Twende kwenye takwimu sasa.

Tathmini ya uchumi ya Benki Kuu kwa mwezi Aprili mwaka huu inaonyesha kwamba urari wa biashara ulikuwa kama ifuatavyo: Mwaka 2013 dola -5,771.1; mwaka 2014 dola -5,723.7; mwaka 2015 dola 4,526.3; mwaka 2016 dola -3,513.9 na mwaka 2017 dola -3,027.8.

Nilijaribu pia kuangalia uwiano wa matumizi ya miradi ya maendeleo ikilinganishwa na pato la taifa (Development Expenditure to GDP ratio). Nao ulikuwa kama ifuatavyo:

Mwaka wa fedha 2013/14 – 5.0%; mwaka 2014/15 – 4.2%; mwaka 2015/16 – 4.3%; mwaka 2016/17 – 6.4%; na mwaka 2017/18 – 6.1%. Uwiano wa matumizi ya kawaida dhidi ya pato la taifa ni kama ifuatavyo:

Mwaka wa fedha 2013/14 – 12.9%; mwaka 2014/15 – 12.3%; mwaka 2015/16 – 13.2%; mwaka 2016/17 – 10.2%; na mwaka 2017/18 – 10.4%. Tumeongeza matumizi ya maendeleo wakati matumizi ya kawaida yanapungua.

Hiki kilikuwa kilio cha wapinzani enzi hizo. Tulitaka taifa litumie fedha nyingi kwenye matumizi ya maendeleo. Tulitaka hata taifa linapokopa litumie mikopo kwa matumizi ya maendeleo na si matumizi ya kawaida. Hili ndilo linalofanyika hivi sasa.

Takwimu hizi zote Zitto anadai uchumi unaporomoka. Hivi ni uchumi wa Tanzania ndio unaporomoka au ni uchumi wa Zitto ndio unaporomoka?

Mimi namfahamu Zitto kuliko watanzania wengi sana. Akiniambia uchumi wake umeporomoka, nitakubaliana naye mara moja. Sihitaji kujiuliza hata mara moja. Najua pesa alizokuwa anaziingiza kwenye ACT wakati huo achilia mbali za kwake binafsi.

Zitto Kabwe ni mbunge pekee aliyekuwa na watumishi binafsi 12. Jijini Dar es salaam alikuwa na madereva wawili, mhasibu (wa fedha zake binafsi) mmoja, mshauri wa uchumi mmoja, msaidizi maalum mmoja na katibu wake kama kiongozi wa chama mmoja.

Mjini Kigoma alikuwa na Katibu wa Mbunge mmoja, Afisa wa utawala ofisi ya Mbunge mmoja, afisa maendeleo ya jamii ofisi ya mbunge mmoja, dereva mmoja na wasaidizi maalum wa mbunge wawili. Kwa sasa kinachoendelea, Mungu ndiye anajua.

Wako waliompeleka idara ya kazi kudai mishahara yao, wapo walioamua kuacha kimya kimya bila kumwaibisha kiongozi wao, wapo wanaotaka kuondoka ila anawaahidi kila kukicha na wapo wanaovumilia.

Sasa anaponda hata hatua ya Rais kuwaita wafanyabiashara ili apate kutoka kwenye mizizi taarifa za uhakika za nini kinachoendelea kwa upande wao. Amekutana na wadau wa madini, amekuwa akikutana na wajumbe wa Baraza la Biashara Taifa, lakini wakati huu akasema akutane na wafanyabiashara wa kutoka kwenye kila wilaya ili apate taarifa muhimu.

Mkutano ule umempa picha pana na amechukua hatua muhimu za kinidhamu dhidi ya wasaidizi wake. Lakini hatua za kubadili kanuni au hata sheria zitafuata ili kuongeza ufanisi katika ukusanyaji kodi na kukuza biashara. Hilo nalo anaponda!

Hizi nguvu anazotumia kupambana na ‘jabali’ JPM anazipoteza bure na atazijutia. Magufuli anazidi kuchanja mbuga. Treni yake ya kuelekea uchumi wa kati imeshika kasi na kama Zitto anadhani anaweza kuizuia kwa tamaa yake ya madaraka, asimame relini kujaribu kuizuia ‘treni’ hii aone itakavyompasua vipande vipande!

Nguvu anazotumia kupambana na Magufuli, azitunze aje azitumie kupambana na Maalim Seif. Kwenye kila chama anachokuwemo Maalim Seif, kila mpemba aliyemo kwenye chama hicho anakuwa kiongozi na thamani zaidi ya kiongozi yeyote wa bara. Mpemba huyo anaweza kuelekeza jambo lolote.

Msimamo na malengo ya chama ni lazima yajikite Zanzibar kibajeti. Lazima kutakuwa na kikao cha wazanzibari walioko kwenye uongozi wa chama hicho nje ya vikao vya chama vya kikatiba kabla na baada ya vikao hivyo. Kila mtanganyika ni adui wa Zanzibar hata kama ni mwanachama wa chama alichomo Maalim Seif.

Maalim Seif ni Sultani wa pili wa Zanzibar baada ya yule wa kwanza kuondolewa kwa mapanga kwenye mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964. Sultani wa pili anawekwa mbali na ikulu kwa sanduku la kura!

Sultani huyu ana wapambe wake akina Ismail Jussa Ladhu, Salim Bimani, Nassor Mazrui na Issah Kheri. Kwenye chama chochote alichomo Maalim Seif, yeye na hawa wapambe wake ndio watakuwa na maamuzi. Hivi tunavyozungumza karibu wote hawa na wengine wengi wa upande wa Maalim Seif wameshaingizwa kwenye kamati kuu.

Baada ya uchaguzi wa ndani ya chama, watazidi kuingia wengine. Tayari mikakati ya ‘kuwapiga chini’ baadhi ya viongozi wa zamani ndani ya ACT imeshaanza.

Hata uchaguzi uliosimamiwa na viongozi wa zamani kwenye majimbo na mikoa nusura ufutwe na kamati kuu ili uanze upya. Baada ya uchaguzi mkuu wa 2020 ACT itakapokuwa na wabunge wote kutoka Pemba, ndipo tutakaposhuhudia mtanange wa maana kati ya Zitto na Maalim Seif. Mmoja mnafiki, mmoja Sultani.

Badala atunze nguvu zake za kupambana aje apambane na Maalim Seif, yeye anazimalizia kupambana na ngome asizokuwa na uwezo hata robo ya robo wa kupambana nazo!
 
Makala hii iliandikwa na Samson Mwigamba tar 9/12/2009
NAKUHURUMIA ZITTO KABWE
MHESHIMIWA Zitto Zuberi Kabwe, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, Katibu wa Kamati ya Wabunge wa CHADEMA katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, salaam.

Awali ya yote naomba kama nianze kwa kutangaza mgongano wa kimaslahi kama ilivyo kawaida kwa wabunge kufuatana na Kanuni za Kudumu za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Toleo la Mwaka 2007.
Mgongano wa kimaslahi ni kwamba ninakuandikia waraka huu nikitaka kujadili machache juu ya mwenendo wa mambo ndani ya CHADEMA, mambo ambayo yanakugusa kila wakati nikitaka kujaribu, kwa faida ya wasomaji, kuangalia kulikoni na wakati huohuo nikijua kwamba wewe ni rafiki yangu wa muda mrefu na ambaye tumekuwa pamoja tukikubaliana kwa mambo karibu yote, wakati wote.

Mheshimiwa unajua urafiki wetu ni wa muda mrefu na kwa kweli nilikupenda kabla wewe hujanifahamu; nikakuhesabu kama rafiki kabla hujanifahamu na kwa bahati nzuri sana uliponifahamu ukakubali kuwa rafiki yangu. Nimekuunga mkono katika matukio, maamuzi na hata mitazamo yako mingi kwa muda mrefu.
Nilikuwa upande wako katika kupiga vita ufisadi na hata uliposimamishwa ubunge wakati wa hoja ya Buzwagi nilikuwa upande wako.

Nilikuwa upande wako ulipotoka nje ya ukumbi wa Bunge kupinga utaratibu wa kuwachagua wabunge wa Afrika Mashariki na hata katika kile ulichokiita ‘bifu’ kati yako na Spika wa Bunge, lililotokana na hatua yako ya kutoka nje ya ukumbi wa bunge na maneno uliyoyatoa nje ya ukumbi huo kuhusu uwezo wa spika kusimamia kanuni za Bunge.
Nilikuwa pia upande wako uliposimama kumtetea Spika kuhusu hoja iliyotolewa na mwandishi mmoja akipinga uwepo wa Kamati ya Bunge ya Kutunga Sheria katika kanuni mpya za Bunge.

Nilikuwa upande wako pale ulipounga mkono maelezo ya kitaalam ya TANESCO kununua mitambo ya Dowans na hili unalifahamu zaidi maana tulikuwa tukiwasiliana sana na huenda mimi na Absalom Kibanda ni miongoni mwa waandishi wachache sana tuliodiriki kusema waziwazi kupitia kalamu zetu kwamba tunaunga mkono msimamo wako wa kununua mitambo ya Dowans.

Utakumbuka pia siku moja tulipishana mtazamo tulipokuwa tukichangia kwenye mtandao mmoja wa intaneti hoja ya utafiti wa taasisi moja iliyoonyesha kwamba bado Kikwete na CCM ni maarufu kuliko vyama vya upinzani kwa mbali sana.
Unakumbuka kwamba mimi nilitofautiana na wewe kwa hoja za kitaalam zinazohusu utafiti. Lakini baada ya kutoa hoja zako na mimi nikatoa hoja zangu na wewe ukazijibu nilikubaliana na wewe na hatimaye nikawa upande wako.
Lakini katika siku za karibuni nimejikuta nikiwa katika mfululizo wa matukio, mitazamo na maamuzi ya mimi kutokubaliana na wewe. Utakumbuka nilianza kutokubaliana na wewe kuhusu uamuzi wako wa kuchukua fomu ya kugombea uenyekiti wa taifa wa CHADEMA.

Nilikutumia barua pepe ndefu sana nikipinga uamuzi huo na kukuomba kwamba ujitoe kwa hoja nyingi ambazo najua unazikumbuka vema.
Kwa bahati mbaya hukujibu ile barua pepe, lakini sikukata tamaa, nikaambiwa nipitie kwa msaidizi wako David Kafulila. Nikafanya hivyo na Kafulila akanihakikishia kwamba kila tunachoongea anakufikishia na kwamba unampa majibu ya kunipatia.

Lakini mheshimiwa unakumbuka kwamba mwishoni kabisa majibu yako yalikuwa ni kwamba hoja zangu zote ulikuwa unazikubali lakini ulishazizingatia kabla hujaamua kujitosa kwenye kugombea uenyekiti na hivyo usingejitoa. Nashukuru kwamba baadaye uliamua kujitoa japo ulikuwa umechelewa.
Mheshimiwa Zitto, nilitofautiana na wewe pia kwa kauli zako ulizokuwa unazitumia kutaka kuwa mwenyekiti wa CHADEMA kabla ya kujiondoa.

Katika moja ya taarifa za habari ulinukuliwa ukisema unatofautiana na Mbowe kwa sababu wewe ni mjamaa wakati yeye ni bepari. Nikawaza na kukumbuka kwamba Agosti 13, 2006 wakati chama chenu kinazinduliwa upya ulikuwepo na ninaamini ulishiriki kikamilifu katika kufanya utafiti, kuchambua na hatimaye kuja na katiba mpya iliyowasilishwa kwenye mkutano mkuu siku hiyo na kupitishwa kuwa katiba mpya ya chama hicho.

Na kwamba maneno haya yanayosomeka kwenye utangulizi wa katiba hiyo mpya ya CHADEMA yakiwa
yametamkwa kwa kunyanyua mikono na wajumbe wa mkutano huo mkuu, basi yalikuwa ni yako pia: “Sisi wajumbe wa Mkutano Mkuu uliofanyika Agosti 13, 2006, mjini Dar es Salaam, tumeamua kuifanyia mabadiliko Katiba ya 2004 ya Chama chetu cha siasa kitanachoitwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ili kuipa sura inayoendana na mtazamo na msukumo mpya wa falsafa yetu ya Nguvu na Mamlaka ya Umma na Dira na Dhamira ya chama kuanzia 2006 na kuendelea.

“Kuanzia sasa CHADEMA, kitaendeshwa kwa mujibu wa katiba hii sambamba na kanuni, taratibu na maadili ya Chama vitavyotungwa kwa mujibu wa Katiba ili kuimarisha kutetea, kudumisha, na kuendeleza Demokrasia ya kweli na hatimaye kuweza kuleta maendeleo ya kweli ya kisiasa, kiuchumi na kijamii kwa jamii nzima ya taifa la Tanzania.”

Kama na wewe ni miongoni mwa wana CHADEMA waliotamka maneno hayo siku hiyo kwamba: “Kuanzia sasa CHADEMA kitaendeshwa kwa mujibu wa katiba hii sambamba na kanuni, taratibu na maadili ya Chama vitakavyotungwa kwa mujibu wa Katiba hii” nilitegemea uwe umeisoma katiba yenyewe na kuona kwamba ibara ya 3 ya katiba hiyo, ibara ndogo ya 3.B. kifungu cha 3.1.1 kinasema “CHADEMA ni chama cha itikadi ya Mrengo wa kati (center party)”.

Hata kwa elimu ndogo tu maelezo haya yanatosha kuonyesha kwamba chama hiki kinaongozwa kwa itikadi iliyoandikwa ndani ya katiba ambayo ni Mrengo wa Kati na wala si itikadi binafsi ya Mbowe ya ubepari ama ya Zitto.
Kwa imani niliyokuwa nayo kwako na nikizingatia elimu kubwa uliyokuwa nayo, nafsi yangu ikanituma kufikiria kwamba labda ‘wamekunukuu vibaya’. Nilihudhuria mkutano wenu na waandishi wa habari uliokusudia kuzika tofauti zenu na Mbowe na kusonga mbele kama chama.

Pale ulipoulizwa swali na mwandishi mmoja kwamba utawezaje kufanya kazi na Mbowe wakati wewe ni mjamaa na yeye ni bepari; ukajibu kwa namna ambayo haikukata kiu yangu ndipo nikaamini kwamba kumbe hukunukuliwa vibaya bali ni kweli ulisema maneno hayo.
Nilipingana na wewe pia pale ulipoamua kupinga uamuzi wa kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa Baraza la Vijana CHADEMA (BAVICHA).

Unakumbuka kwamba nilialikwa katika uchaguzi huo miongoni mwa wageni wachache wanafunzi, wanahabari, wanaharakati na watu wa kada mbalimbali walioalikwa kushuhudia uchaguzi ule.
Wakati wa uchaguzi wenyewe utakumbuka mimi na wewe tulikaa meza moja na tulitenganishwa na mtu mmoja tu (Mkurugenzi wa Uenezi Taifa wa CHADEMA, Erasto Tumbo).

Nilitegemea mambo yasiyoendana na sera na kauli mbiu za chama chenu ambazo zinatangazwa hata katika jina la chama (DEMOKRASIA na MAENDELEO) ambayo yalifanyika pale ukumbini uliyaona.
Najua jioni wakati wa kutangaza matokeo hukuwepo lakini nategemea ulipata taarifa za kauli za vijana mbalimbali walizotoa pale wakitaja waziwazi majina ya watu walioharibu uchaguzi ule.

Sikutarajia kama Naibu Katibu Mkuu wa chama upinge hatua ile iliyochukuliwa na msimamizi wa uchaguzi pamoja na kikao kingine chochote cha juu ya msimamizi wa uchaguzi eti kwa sababu tu rafiki yako Kafulila alikuwa anaongoza.
Hilo lilinipa taabu kubwa na naomba uniwie radhi rafiki yangu lakini nasema ukweli wa nafsi yangu kwamba nilifikia kujiuliza mara mbilimbili kama ungechaguliwa wewe kuwa mwenyekiti wa chama hicho taifa, hali ingekuwaje?

Na mwisho nilipingana na wewe pale ulipopinga kwenye vyombo vya habari kuvuliwa wadhifa kwa David Kafulila. Kwanza ulionekana umeweka ubaguzi kwa sababu katika maneno yote uliyonukuliwa ulisisitiza juu ya Kafulila peke yake na hukumgusia kabisa Danda Juju wakati wote walivuliwa kwa sababu
zinazofanana.

Lakini kwa sababu Kafulila ni rafiki yako sana, umemwandaa kuwa mbunge na unamuunga mkono katika harakati zake, na ni mbunge mtarajiwa kwa kuwa anakubalika sana jimboni basi ukamtetea na kumsahau ‘mhanga’ mwenzake. Hilo tu linafanya tutofautiane na zaidi sana tunatofautiana kwa kupinga maamuzi ya Katibu Mkuu wako nje ya vikao, maamuzi aliyoyachukua kwa mujibu wa mamlaka aliyonayo.

Najua yote haya umeamua kuwa kimya hujayatolea kauli yako ikiwa ni pamoja na yale ya kumfadhili Kafulila kwenda Kigoma kuichafua vizuri CHADEMA. Lakini kama ni kweli, napingana na wewe na kama unaendelea kukaa kimya nitaamini kwamba ni kweli.
Sasa limeibuka la kusema kwamba unatembea na barua ya kujiuzulu nyadhifa zako zote ndani ya CHADEMA ikiwa ni pamoja na ubunge. Bado pia sijapata kauli yako, narudia kusema kwa kuendelea kunyamaza unanifanya niamini kuwa ni kweli.

Na kama ni kweli, nakuhurumia sana Zitto Kabwe. Sasa naona kile nilichokuambia wakati nikikushauri ujitoe kugombea uenyekiti kinatimia. Nilikuambia ujitoe haraka tena kimyakimya kwa kumweleza tu Katibu Mkuu aweke fomu yako pembeni lakini hukutaka kunisikia.

Lakini utakumbuka moja ya sentesi zangu ilikuonya kwamba ukingang’ania kugombea iwe umeshinda
uenyekiti ama umeshindwa utapata shida kubwa. Nilikueleza kwamba hutaaminika tena na Watanzania na kila kitu utakachofanya utaonekana kama ulikuwa ni mamluki ndani ya chama.
Ni kwa bahati kwamba umetokea kuwa na viongozi wenye busara sana kina Freeman Mbowe na kina Dk. Wilbrod Slaa wakisaidiwa na hekima na kamati ya wazee.

Hawa wakaamua kukurejesha kwenye unaibu katibu mkuu. Nilishuhudia siku ile wajumbe wa Baraza Kuu la CHADEMA walivyoshangilia uteuzi wako na wa Dk. Slaa na Hamad Yusuph kama wakuu wa Sekretarieti ya chama.
Nilidhani sasa ungetulia na kufanya kazi ya kujenga chama chenu na kusonga mbele lakini haikuwa hivyo.
Baada ya kushauriana sana wakati ule ulipotaka kugombea uenyekiti niliamua kutafuta habari za kiuchunguzi ndani ya CHADEMA. Nimeongea na viongozi mbalimbali na maofisa wa CHADEMA makao makuu, nimeongea sana na David Kafulila na hata niliwahi kumsikiliza mama yako mzazi akiongea na watu ambao sikuwafahamu.

Nimegundua kitu kimoja tu: kwamba kama mambo haya huyafanyi kwa makusudi na kwa malengo maalumu, basi watu uliowaamini sana ndani ya CHADEMA hata kama walikuwa na nyadhifa ndogo, walikubali kutumiwa ili wakutumie wewe kuimaliza CHADEMA na wewe ukaingia mkenge.
Ukakubali kugombanishwa na viongozi wenzako wa ngazi za juu hasa Mwenyekiti Freeman Mbowe ili malengo ya watu hao yatimie. Sasa nakuonea huruma.

Nakuonea huruma kwa sababu kama ni malengo ya hao watu kukutumia kukimaliza chama hawatafanikiwa na badala yake watakumaliza wewe bure na utakuja
kushtuka ukiwa umekwisha kisiasa.

Kama ni malengo yako kwa utashi wako umeamua kutumika kukimaliza chama, nakuhurumia kwa sababu utajimaliza wewe na CHADEMA itaendelea kuimarika bila wewe wala Kafulila.
Ukitaka kujua ninachokisema, tuulize sisi waandishi tunaopata mawazo ya Watanzania moja kwa moja.
Kwa kuanzia muulize tu Edward Kinabo kwamba Jumatano iliyopita alipoandika makala ya “Simwelewi Zitto Kabwe” aliungwa mkono na wasomaji wangapi na walikuwa na mawazo gani juu yako. Hapo ndipo utakapoelewa kile ninachokisema.

Namalizia kwa ujumbe wa msomaji wangu mmoja tu kati ya wengi. Huyu aliniambia anaitwa Meshack na yuko Korogwe. Aliniambia, “Sisi tulishajua kwamba Zitto anaondoka CHADEMA na kwamba anachosubiri tu ni pensheni yake ya ubunge ambayo huwa inatolewa baada ya Bunge kuvunjwa.

Naomba Mwigamba kwa sababu unaweza kuongea na viongozi wakuu wa CHADEMA, waambie kwamba
wasije wakafanya kosa la kumvua Zitto uongozi wala kumvua uanachama.
Sisi hatutaki apate kisingizio cha kuondoka CHADEMA. Waambie wamuache tu mpaka atakapoondoka mwenyewe ili Watanzania wazidi kumfahamu,” mwisho wa kunukuu.


Tafakari mwenyewe ulikofika, uamue cha kufanya. Kumbuka uamuzi wa mwisho ni wako wengine tunakueleza tu maana tumejiapiza kuzungumza ukweli hata katikati ya ugomvi.

Kama utaamua kuondoka CHADEMA ama kujivua tu nyadhifa zako. katika yote nakutakia kila heri!
 
Je kwa muktadha huu,ZZK hawezi kuwa anatumiwa na au ni mwanakitengo?
Na project yake ni kuyumbisha kambi ya Upinzani?
 
  • Nzuri
Reactions: BAK
"Katika ujinga mwingi kuna moja linaweza kuwa la busara"-Abdulrahman Kinana.
 
Siku hizi huyo msaliti hatii mguu humu Mkuu mara ya mwisho kuingia kwa kulog in Ilikuwa miezi mitano iliyopita June 19, 2021. Kule Twitter kila anayeandika kuhusu UNAFIKI na USALITI wake huishia kupigwa tofali.
😂😂😂😂

Mheshimiwa Zitto, natambua fika huwezi kuacha kabisa huo unafiki unao tuhumiwa! Maana tayari upo kwenye damu yako.

Ila unaweza tu kujitahidi kuupunguza, ili uwe kama binadamu wengine ambao wana kiwango cha kawaida sana cha unafiki.
 
Sidhani kama ni mwanakitengo ila wameshamjua ni mtu mwenye tamaa ya pesa na wadhifa hivyo wanamtumia kudhoofisha upinzani au tunaweza kusema kuidhoofisha Chadema.

Je kwa muktadha huu,ZZK hawezi kuwa anatumiwa na au ni mwanakitengo?
Na project yake ni kuyumbisha kambi ya Upinzani?
 
Sidhani kama ni mwanakitengo hivyo wanamtumia kudhoofisha upinzani au tunaweza kusema kuidhoofisha Chadema.
Kumbe Chadema ni very strong political party na kinatisha hadi kitengo wamtumie mtu kukidhoofisha!.
Kwa maoni yangu Chadema kiko dholfu bin taaban, kiukweli kiko hoi hadi kushindwa kuitisha kikao cha Baraza Kuu kuumaliza ule mzizi wa futna wa Covid 19!.
P
 
Endelea kuonyesha ujuha wako hadharani huku ukihaha kutafuta teuzi. Maneno ya Msekwa kuhusu katiba na hao Wabunge wa Spika ZUZU Ndugai umeyasikia lakini bado unajitoa ufahamu. Chama dhoofu hakiwezi kuwa kinaongeza wanachama wapya kwa maelfu nchi nzima. Muziki wa Chadema unaujua na uliuona kwa macho yako. Chadema iko mioyoni mwa Watanzania hivyo utasubiri sana kudhoofika kwa Chadema.

Kumbe Chadema ni very strong political party na kinatisha hadi kitengo wamtumie mtu kukidhoofisha!.
Kwa maoni yangu Chadema kiko dholfu bin taaban, kiukweli kiko hoi hadi kushindwa kuitisha kikao cha Baraza Kuu kuumaliza ule mzizi wa futna wa Covid 19!.
P
 
Hapana Mkuu nimeitoa FB. Hii hapa chini ndiyo ya kutoka maktaba. Nilikuwa naitafuta siku nyingi hatimaye leo nimeipata.
Kuna sentensi imenifurahisha, ati tunataka mgombea awe Prof Mtikila badala ya Prof Kitila !!
 
  • Kicheko
Reactions: BAK
Back
Top Bottom