SoC02 Malezi ya Msanii Diamond Platnumz katika kuibua mabilionea vijana kupitia vipaji vyao

Stories of Change - 2022 Competition
Jul 18, 2022
45
55
Diamond Platnumz alizaliwa katika hospitali ya Amana iliyopo jijini Dar es Saalam tarehe 02 Oktoba 1989. Jina halisi alilopewa na wazazi wake ni Naseeb Abdul Juma. Akiwa na umri mdogo wazazi wake walitengana na alibaki akilelewa na mama yake mzazi aitwaye Sanura Kassim maarufu kama “Sandra”.

Naseeb Abdul Juma maarufu kama Diamond Platnumz siyo jina geni masikioni mwa watu hasa mashabiki na wapenzi wa muziki wa kizazi kipya nchini Tanzania. Diamond amejizolea umaarufu kutokana na nyimbo zake kugusa hisia za mashabiki wa burudani ya muziki uliosheheni ubunifu na hisia.

Akiwa darasa la tano, Naseeb Abdul alionekana kuwa na kipaji cha uimbaji ambapo alikuwa akiimba nyimbo za wasanii wa ndani na nje ya nchi.

Mama yake alimnunulia albamu zenye nyimbo mbalimbali na kumuandikia baadhi ya maneno ya nyimbo hizo ili kumrahisishia katika uimbaji wake. Vilevile, mama yake alimpeleka Naseeb katika matamasha na matukio mbalimbali ili kumpa nafasi ya kuonyesha kipaji chake cha uimbaji akiwa na matumaini kuwa mwanaye atapata nafasi ya kuimba.

Naseeb Abdul alikuwa ni mchezaji hodari wa ngoma katika kikundi cha ngoma na kwaya akishirikiana na wanafunzi wenzake.

Kutokana na uhodari wake shule yake iliweza kushinda katika matamasha mbalimbali ya ngoma katika wilaya ya Kinondoni.

Diamond ameishi na kulelewa na mama yake mzazi “Sandra” ambaye amehangaika naye mpaka hapo alipofikia sasa.

Diamond amekuwa akijivunia sana mama yake mzazi kutokana na ukweli kuwa amekuwa bega kwa bega kumsaidia kutimiza ndoto zake katika maisha yake. Wakati wote mama yake amekuwa msaada mkubwa katika kufikia ndoto zake akiwa kama mshauri wake mkuu.

Siyo tu katika maisha ya nyumbani kama mtoto bali hata alipoanza safari yake ya muziki alikuwa akienda naye kwenye matamasha mbalimbali ya vipaji (Talent shows) ili mwanaye afikie ndoto zake katika muziki.

Mama Diamond alimpeleka Diamond na Romy Jons mtoto wa ndugu yake (ambaye kwa sasa ndiye DJ wa Diamond). Hii ni tofauti na wazazi wengine ambao wamekuwa wakiamini kuwa muziki ni uhuni na mtu yeyote anayejishughulisha na suala hili ni mhuni.

Imani hii ni tofauti na vile ambavyo mama Diamond aliamini na hivyo aliamua kuungana pamoja na mwanaye kuhakikisha ndoto zake zinatimia. Majirani na watu wengine walimcheka na kuona kama anamdekeza na kumfundisha uhuni mwanaye.

Licha ya maneno na kejeli alizokuwa akizipata kutoka kwa watu hao bado mama Diamond aliendelea kumfariji na kumtia moyo kijana wake ili aendelee kuwa imara hasa katika kipindi kigumu cha changamoto na matatizo.

Kwa lugha rahisi ni kwamba mama Diamond anatupata funzo kubwa katika kufanikisha ndoto za watoto wetu katika familia zetu. Kuna familia zingine zimekuwa zikiua vipaji vya watoto wao kutokana na kuwakatisha tamaa na kuwalazimisha kufanya vile wao watakavyo na siyo watoto wao watakavyo.

Kadhalika, kuna familia zingine ambazo zimekuwa zikiwatia moyo watoto wao katika kutimiza ndoto zao kama familia ya Diamond.

Muda mwingine tunakutana na vikwazo vingi katika kufanikisha ndoto zetu kwa kuwa familia zetu zinakuwa hazikubaliani na kile tunachokifanya.

Kwa mfano mtoto akienda kucheza mpira au kuimba wazazi wake wanampiga kuwa anachokifanya siyo kizuri badala ya kumuandaa kisaikolojia na kumtia moyo.

Neno usifanye au hapana limekuwa likichukua nafasi kubwa sana kuliko neno fanya au ndiyo katika familia nyingi kwa kile ambacho watoto wengi wamekuwa wakijaribu kufanya kama sehemu ya kutimiza ndoto zao.

Kwa kufanya hivyo tumekuwa tukichangia kuua vipaji vya watoto wetu ambao wangekuwa na mchango mkubwa katika jamii. Familia zingine zimekuwa zikiwaaminisha watoto wao kuwa ukisoma ndipo maisha yako yanakuwa mazuri.

Sina maana kwamba tusiwahimize watoto wetu wasisome isipokuwa dhana ya kusoma na kupata ajira imepitwa na wakati, jambo pekee ambalo linaweza kuwasaidia ni kutumia uwezo na vipaji vyao kujiajiri. Kwa sasa ajira zimekuwa chache na waombaji wamekuwa ni wengi sana ukilinganisha na siku za nyuma.

Familia zitusaidie kutuandalia vijana wenye kutumia vipaji vyao na kufanikisha ndoto zao kama ilivyo kwa familia ya Diamond. Familia ni taasisi muhimu ambayo tabia na mwenendo wa mtu hujengwa na ina nafasi kubwa ya kumuandaa mtu kufikia ndoto zake.

Kama familia ikiwa na utamaduni wa kukatishana tamaa ni dhahiri kuwa mhusika anaweza kufa moyo na kukata tamaa na hivyo kumfanya mtu asifikie malengo yake. Lakini vilevile kama familia itaunga mkono juhudi za mhusika na kumtia moyo ni dhahiri kuwa mtu huyo ataweza kufikia lengo au ndoto yake.

Hivyo basi familia ina wajibu mkubwa wa kuhakikisha kuwa mwanachama wake anapata mahitaji muhimu na kumuandaa kushinda changamoto ili aweze kufikia ndoto zake.

Katika hili mama Diamond anatupata funzo kubwa katika kufanikisha ndoto za watoto wetu katika familia zetu. Uchumi wetu unategemea sana mafanikio ya watu ambao watatoa fursa za ajira na kipato kwa watu wengine kama ilivyo kwa Diamond.
 
Back
Top Bottom