Maisha kama tuyafikiriavyo na kuyachukulia

Ayenda M

Member
Jan 4, 2018
97
132
#MASTORISTORIYAMWALIMUNAMZEEABDALLAH

Mwanangu tambua maisha yako ya leo yaweza yasiwe kama ya kesho! Ishikilie leo, ifurahie leo maana nani aijuaye kesho itakuja na nini?

Juzi tu nilikuwa nacheza bao na Mzee Athumani ila leo hayupo. Sio kuwa hajafika hapa kijiweni kwetu tu, hapana, hayupo na hatuwezi kuwa naye tena katika maisha haya ya damu na nyama.

Mwanangu Ishi! Jifunze na fanya kila lililo jema uwezalo. Ujifunze kila iitwayo leo wala usichoke.

Mwanangu jana tulikuwa nayo, tukaifurahia. Leo imekuja, imetupa kila sababu ya kuikumbuka jana kwa sababu yaweza jana ilikuwa bora kuliko leo.

Tunaikumbuka jana kwa sababu ilikuwa mbaya kuliko leo. Tunakosea, usiitumie jana kuiendeleza leo, itumie jana kukupa hamasa chanya ya kuijenga leo njema

Mwanangu, si unamuona binti yangu Mwajabu, jana aliachwa na mme wake tena kwa talaka tatu. Leo kaamka na uchungu wa jana.

Mwanangu, mimi ni baba! Nina moyo pia, kiukweli nimemuonea huruma ila nikamuuliza, "Nje ya kuachana na mmeo, nini kingine amebeba maishani mwako?, Urembo wako? Umri wako? Utu wako? Haiba yako? Akili zako? Cha muhimu kikubwa kabeba muda wako tu.

Mwanangu Ayenda, nimemsihi dadako Mwajabu aangalie anguko lake la jana kama kioo cha kuwa na leo njema. Leo yake ameishikilia mkononi. Kesho yake itajengwa na leo yake na sio jana yake.

Mwanangu, usiiweke kichwani sana jana. Jana imebaki katika historia. Izike tu mwanangu. Unayo leo, leo iliyojaa fursa kibao. Leo hii unayoweza kusahihisha mengi uliyokosea jana. Tafakari.

Mwanangu, yachukue maneno yangu haya. Andika kwenye diary yako. Chukua pen na karatasi hesabu makosa yako ya jana. Hesabu kila kosa ulilojitendea wewe. Jisamehe kwa kila ulipojikosea mwanangu.

Mwanangu, kisha anza kuhesabu wangapi umewaumiza katika jana yako. Wangapi wana vidonda vyako mwanangu? Wangapi wamelia jana kisa wewe? Waombe msamaha, wanakusikia, watapokea samahani yako na watakusamehe. Usiogope, waombe wote msamaha, walio hai na waliotangulia mbele za haki. Utasamehewa. Wasamehe waliokukosea, hao usitake hata kuwakumbuka.

Andika kila mtu alokusaidia jana mpaka ukaiona leo. Washukuru hata kama hawapo duniani. Washukuru walio hai hata kama huwezi kuongea nao, ulimwengu utafikisha shukrani zako. Waambie wote Ahsante kila upatapo nafasi ya kufanya hivyo. Washukuru kila dakika, kila lisaa. Shukrani zako wanazipokea, wanaziona, na wanakubaliki.

Mwanangu, jana yetu imejaa mengi. Usihesabu mazuri uliyotenda. Pambana kurekebisha wewe mwenyewe kila kosa ulilotenda. Fanya hiyo kazi mwenyewe, fanya kimya kimya.

Mwanangu, wakati unafanya yote hayo usisahau kumshirikisha MUNGU wako. Muite, aliijua jana yako, kakupa leo uliyonayo, kesho yako anaijua yeye. Mshirikishe yeye tu.

Mwanangu, fanya hayo... hautabaki hivyo ulivyo. Sasa hivi dadako MWAJABU kaolewa na ana watoto wawili. Mme wake katoka kumpa zawadi ya Gari kama zawadi yake ya mwaka mpya. Usiache kuishi leo kisa jana mwanangu. Kesho nzuri inakuja.

#BusaraZaMzeeAbdallah

#mastoristoriyamwalimunamzeedullah #ayendadaily
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom