Magufuli anawatesa CCM, anaumiza Upinzani, analiaibisha Bunge!

Interest

JF-Expert Member
Apr 11, 2015
3,434
7,055
KAZIya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama yalivyo mabunge yoteya nchi za Jumuiya ya Madola (Commonwealth) ni kuisimamia serikali(scrutiny). Usimamizi huo una maana ya bunge kufuatilia kwa ukaribu shughuli za kila sikuza serikali na kutia changamoto za kiutendaji, kiuamuzi na kimahesabu(to check and challenge). Bunge ndilo linalotunga, kubadilisha na kurekebisha sheria (legislation),vilevile kufanya mijadala mbalimbali muhimu kuhusu nchi (debating).

Majipu yanayotumbuliwa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), hususan katika Bandari ya Dar es Salaam na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),yanafanya tujiulize Bunge la 10 lilikuwa wapi? Swali kama hilo linahusu Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali(NAOT) na uwajibikaji wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu zaSerikali (CAG).

Kama taasisi walikuwa wapi wakati madudu ya bandarini yanatokea? Ndiyo tuseme bunge lenyewe ni siasa tu? Au CAG na ofisi yake (NAOT) wao wanajua Tegeta Escrow tu? Huu wizi wa kila siku bandarini, makontena yanatoroshwa bila kulipiwa ushuru wa forodha na kodi mbona hatukuona moto ukiwaka bungeni? Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), chini ya Zitto Kabwe, ilikuwa ikizungumzia matatizo ya ukwepaji kodi kama hoja ya jumla (general)kuwa ni janga sugu kwa nchi yetu.

Haikuwahi kuzama na kuweka wazimakampuni yanayokwepa, vilevile watumishi wa umma wanaofanya mchezo wa kukwepesha. PAC haijawahi kuchambua ripoti ya CAG kuhusu utoroshwaji wa makontena bandarini bila kulipiwa kodi. Bila shaka hii ni kwa sababu hawajawahi kupewa ripoti. Ni kwa nini?

Kamatiya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, chini ya Peter Serukamba, iliyokuwa na dhima ya usimamizi wa wizara tatu, Ujenzi, Uchukuzi naMawasiliano, Sanyasi na Teknolojia, nayo ilikuwa inafanya kazi zake katika sura ipi mpaka wizi huu wa bandarini haukuonekana? Moses Machali ambaye alikuwa Waziri Kivuli wa Uchukuzi, nyakati za mwisho za uhai wa Bunge la 11, anaweza kujitetea kuwa alikamata usukani kipindi cha lala salama, lakini je, mtangulizi wake Mhonga Said Ruhwanya, hakuuona?

Kumekuwa na malalamiko kuwa wabunge wa upinzani, hususan mawaziri vivuli kutopewa ushirikiano wa kutosha wanapokuwa wakifanya ufuatiliaji waokwenye idara za serikali. Hii inafanya ushirikiano wa serikali(executive) na bunge (parliament) kuwa na doa. Hili la wapinzani kunyimwa ushirikiano kwa sababu wanaonekana viherehere vya kuiumbua serikali, linaweza kuwa mwavuli wa kuwakinga Zitto, Machali na Mhonga, vipi Serukamba na timu yake?

Serukambani CCM na alipambana mno kuhakikisha Edward Lowassa anakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi. Je, hakuona, hakuoneshwa au hakufanya kazi yake sawasawa?

Mawaziri wa Uchukuzi waliopishana, Omar Nundu, Dk Harrison Mwakyembe na Samuel Sitta, nao ni nini kiliwapata mpaka hawakuwahi kusema chochote kuhusu ufisadi huo? Uwajibikaji wao tunautambuaje katika mazingira ya namna hii ya kuonesha ukipofu dhidi ya wizi mkubwa bandarini? Waziri wa Fedha, Saada Mkuya na manaibu wake wawili, Mwigulu Nchemba na Adam Malima, walikamatwa na usingizi wa aina gani mpaka kuacha maofisa wa TRA, wakifanya wanavyotaka, wakicheza dili na wafanyabiashara wahuni kukwepa kodi bandarini?

Hili pia analo hata Waziri Mkuu aliyepita, Mizengo Pinda, naye alikuwa anafanya kazi gani? Alikuwa 'bize' kiasi gani? Yeye kama bosi wa mawaziri, dhima aliyochukua kuhakikisha wasaidizi wake wanafanya kazi ipasavyo na kubaini ukwepaji wa kodi kisha kuudhibiti ni ipi?

Leo hii, lipo kundi linamtazama Dk Jakaya Kikwete kuwa utawala wake haukushughulikia ufisadi wa bandarini kwa umakini wa kutosha. Bandarini eneo nyeti mno kwa nchi. Asilimia 60 ya mapato ya serikali hutoka Bandari ya Dar es Salaam. Kwa mantiki hiyo, huwezi kupuuza hata chembe shughuli za kila siku zinazofanywa na bandari.

Makosa yaliyofanywa mpaka kufikia tulipo sasa ni kielelezo cha ushiriki mpana wa wizi mkubwa wa watendaji wa juu serikalini au uzembe wa kiwango cha juu wa wanasiasa waliopata kushika dhamana husika. Saada na wasaidizi wake wawili walikuwa wanafanya kazi kwa nguvu na mtandao upi kama walishindwa kutambua fujo za maofisa wa TRA waliokuwa wanavuna fedha utadhani wapo kwenye ghala la mavuno ya bibi zao?

Tunaambiwa kuna kamishna TRA ana nyumba 75 ndani ya Dar es Salaam. Nchi hii kweli? Kamishna ana nyumba ndogo zisizopungua 20 na zote amezijengea nyumba! Kwamba yupo kamishna alikuwa anafanya kazi siku tatu tu kwa wiki, zilizosalia alisafiri kwenda Afrika Kusini au Dubai kula matunda ya wizi wake. Serikali ilikuwa likizo?

Nchi imepita kwenye jaribio lahaja! Tukae mstarini sasa; Nchi inasafishwa na mkuu wa kaya aliyepo, Dk John Magufuli. Ushirikiano na mfumo wa usalama katika nchi, unawezesha matokeo makubwa kuwahi kutokea. Ni ripoti, vitendo kisha matokeo!

Mfumo huu ambao Dk Magufuli anautumia ulikuwepo pia kabla. Lakini haukufanya kazi kwa sababu Rais Kikwete alifanya kazi na mwaziri ambao wengi wao ni wazembe, wavivu na waoga. Kukosekana kwa Baraza la Mawaziri hivi sasa, imekuwa sababu ya huu wepesi wa Dk Magufuli pamoja na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kupenya kwenye idara mbalimbali, kufanya vitendo na kuleta matokeo.

Kama mawaziri wangekuwepo, kisha rais na waziri mkuu wangeingia kweny eidara fulani, ingeonekana wanamuingilia waziri mwenye dhamana. Na uchafu uliopo bandarini, siyo wa kusubiri vikao vya ndani ya Baraza la Mawaziri, vyenye maneno sukari (sugar-coated).

Nyakati za sasa, hatuhitaji Siasa Soda (Soda Politics), zile zenye utamu mwingi na unaopumbaza kama ambavyo mwandishi mtaalam wa lishe na sosholojia, Profesa Marion Nestle wa Marekani, alivyoandika kwenye kitabu chake, Soda Politics.

Kwamba kama ambavyo soda ilivyo na nguvu na kushika mpaka uchumi wa mataifa mengi duniani ndivyo ambavyo na siasa ilivyo lakini ukweli ndani yake ni kuwepo kwa athari kubwa kiafya kwa watumiaji. Mantii ni kuwa siasa zikiendekezwa huwa zina athari kubwa mno kwa watu kuliko utamu unaoonekana. Na baadaye aliweza kutengeneza documentary ambayo aliita Sugar Coated. Ikizungumzia pia siasa mbovu, zilizopakwa asali na kubeba utamu wa juu lakini ndani kuna madhara makubwa.

Ndiyo hoja hapa kuwa Dk Magufuli lazima atumie ukweli mchungu ili kunyoosha nchi. Ni lazima ajitenge na uongo wenye asali. Hii ndiyo sababu watu tunaona bora hata Baraza la Mawaziri lichelewe ili nchi iwekwe sawa kwanza. Mtanzania wa leo ameanza kuakisi umuhimu wa kutokuwepo kwa Baraza la Mawaziri kwa sababu yanayofanywa sasa na vichwa vitatu vya juu, yanaleta matokeo makubwa.

Watanzania wamekuwa sasa washangiliaji wa matokeo. Ambayo hawakuwahi kuyaona kwa miaka mingi iliyopita. Mifumo iliyopita haikujikita katika kuwaonesha Watanzania matokeo. Yaliyotangazwa yaliachwa gizani. Watu wanaambiwa matokeo lakini wakiyatafuta kwa tochi hawayaoni. Wanaambiwa tu!

Nadharia iliyobebwa na wengi ni kuwa kilichokuwa kinafanyika kilikuwa kiini macho. Wakubwa walikuwepo kwa minajili ya kugawana keki ya taifa. Mtindo ambao Dk Magufuli amekuja nao ni wenye matokeo kuwa serikali ya sasa ipo kwa ajili ya wananchi. Na umaarufu wa serikali yoyote duniani hutokana na jinsi inavyojikita kutatua kero za kimsingi walizonazo wananchi wa kawaida.

Watanzania hawajawahi kuuchukia Utanzania wao. Wanalipenda taifa lao. Hawajawahi kuuchukia uongozi waliousimika, wamekuwa na chuki kubwa dhidi ya mfumo kandamizi. Wamekuwa wakichukia mfumo unaonyonya maslahi ya wengi. Ndiyo maana hawajawahi kuwa na kisasi dhidi ya wastaafu. Huchukizwa na watendaji waliopo mamlakani.

Ni kwa sababu Magufuli amekuja tofauti, leo amekuwa nyota wa nchi. Tutazame sasa anachokifanya. Wakati akipata umaarufu mkubwa kwa wananchi, upande wa pili anawaumiza wengi. Mawaziri wengi katika muhula uliopita hawana furaha. Wanauguswa, wanapata presha!

Zipo taarifa kuwa makontena yaliyotoroshwa kwa vimemo, kuna wakuu walikuwa wakiagiza yapitishwe bila kulipiwa kodi. Majina yameshakabidhiwa kwa waziri mkuu. Ni hapo ndipo unaweza kuona kuwa wakati Magufuli na serikali yake wakichanja mbuga inayowafanya Watanzania wengi wakenue, vigogo wengi ambao walikuwa wakitumia vibaya dhamana zao wapo kwenye wakati mgumu mno.

Hii ndiyo sababu ya kueleza kuwa Serikali ya Magufuli inawatesa baadhi ya vigogo wa CCM. Hawajiamini kama wanaweza kusalimika au yatawafika makubwa baada ya mapitio. Misimamo ya Magufuli inawatesa mno. Tatizo kwa vigogo na faida kwa wananchi wa kawaida ni kuwa Magufuli hana katikati. Akiamua kusimamia jambo, hulitenda kwa sura ambayo yeye mwenyewe itamridhisha, vilevile kuona matokeo yatakayodhihirika kwa kila mtu.

Katika wana CCM waliokuwa wakitumia madaraka vibaya, nani ambaye anaweza kupumua kipindi hiki? Inatajwa Bandari ya Dar es Salaam tu, badom aeneo mengine hayajapigwa jicho la uchunguzi. Upande wa pili wapinzani wanaumiza kichwa jinsi ya kutoka.

Kati ya mwaka 2005 mpaka 2015, uimara wa upinzani ulitegemea zaidi matukio na kasoro za kiutendaji zenye kufanywa na Serikali ya CCM. Baada ya Uchaguzi Mkuu 2015, wapinzani hususan Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), waling'ara na madai yao ya kuibiwa kura.

Naendelea kusisitiza, ile ilikuwa hoja dhaifu lakini ilipata mbeleko kutokana na kiu ya mabadiliko iliyokuwemo ndani ya wananchi. Ulifanyika uchaguzi mdogo na kusababisha mshikemshike. Nchi ikawa kwenye vipindi vigumu vya misuguano ya kisiasa.

Kimsingi, kati ya mwaka 2010 na 2015, kulikuwa na nyakati nyingi za malumbano, mitifuano na minyukano ya kisiasa kuliko utendaji wenye tija kwa nchi.

Mwaka 2015, mambo yamekuwa tofauti kabisa. Wapinzani wameshafanya majaribio mawili kama yale yaliyowapa mtaji mwaka 2010. Kwanza walifanya zaidi ya kile kilichotokea wakati wa ufunguzi wa Bunge la 10. Katika Bunge la 10, wabunge wa Chadema walinyanyuka na kutoka nje baada tu ya Rais Jakaya Kikwete kuingia bungeni.

Awamu hii, haikuwa Chadema peke yake, wabunge wote wa Ukawa, yaani Chadema, Cuf na NCCR-Mageuzi, walimzomea Magufuli alipoingia ndani ya ukumbi wa bunge. Zomeazomea hiyo ilitawala, mwisho Spika wa Bunge, Job Ndugai, aliwatimua nje ya ukumbi wabunge wote wa Ukawa.

Hilo lilikuwa jaribio la kwanza la kuupa changamoto uongozi wa Magufuli. Jaribio hilo lilikosa umaarufu kutokana na hotuba kali iliyosomwa na Magufuli. Zaidi wananchi waliona upinzani umekosa mabadiliko, kwani zile tamthiliya, maigizo kama siyo komedi zilizokuwepo Bunge la 10, hawakupenda kuona zikijirudia.

Baada ya kukosa mashiko, jaribio la pili likawa Mwanza. Pamoja na ukweli kuwa polisi walitaka kucheza faulo kuzuia aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Geita, Alphonse Mawazo kuagwa kwa heshima kama chama chake kilivyotaka, lakini lingeweza kuchukua msisimko mkubwa. Nguvu ya Mwanza na tukio la Mawazo, halikuweza kuchukua uzito ambao lilistahili kitaifa kwa sababu Magufuli na Majaliwa walikuwa wakifanya matukio makubwa, yenye kuhitajika zaidi na wananchi.

Watanzania wameonesha kuwa kwao siasa siyo muhimu. Wanachotaka ni kuona mambo ya nchi yao yanakwenda vizuri. Na hiyo ndiyo sababu ya Watanzania kugeuka mashabiki wa Magufuli.

Katika nyakati hizi ambazo Watanzania hawahitaji kusikiliza siasa kuliko vitendo, vyama vya upinzani vinakuwa kwenye hali tete. Wanaumia jinsi ya kuendelea kukamata nafasi kwenye mzunguko wa habari za nchi. Ilivyo sasa ni kwamba Watanzania wanategea kusikia nini ambacho Magufuli atakuwa ameamua au jipu litakalokuwa limetumbuliwa na Majaliwa. Hawataki habari za siasa kwa sasa.

Unaweza kujiuliza sasa hivi kuna maeneo yamefanya au yanaendelea na uchaguzi mdogo wa ubunge. Mathalan Arusha Mjini, lakini huko siko ambako kuna sikio la wananchi tena. Kumbuka uchaguzi mdogo wa Igunga na Arumeru Mashariki ulivyotikisa nchi mwaka 2011 na 2012. Rejea Kalenga kisha Chalinze, sasa ona ambavyo watuwa livyo 'bize' utadhani hakuna kinachoendelea. Hizi siyo nyakati za siasa!

Wapinzani wanahitaji umakini wa hali ya juu kumudu kasi ya Magufuli. Maana anatenda kile hasa ambacho wananchi wanataka. Kile ambacho hata William Hague wa Conservative, Uingereza, angefanya kubana matumizi. Wakati wa uongozi wa Tony Blair na chama chake cha Labour, Hague akiwa Kiongozi wa Upinzani, akiwa pia kiongozi wa Conservative, alipigania mno kubana matumizi ya serikali kwa kupunguza ukubwa wa Baraza la Mawaziri na ukubwa wa bunge.

Njia anazopita Magufuli, ndizo ambazo zilimfanya marehemu Lee Kuan Yew kuipaisha Singapore kutoka taifa maskini hadi kuwa tajiri kiuchumi na kimaendeleo. Mpaka leo, Yew ndiye anabaki kutambulika kama Baba waTaifa la Singapore.

Mwalimu Julius Nyerere ni Baba wa Taifa la Tanzania kwa sababu ya kupigania uhuru na kuiunganisha nchi kutoka mkusanyiko wa makabila na koo mpaka kuwa taifa moja. Pengine Magufuli akawa nembo ya pili ya taifa kwa kujenga uchumi wa kisasa, utakaoivusha Tanzania kutoka dunia ya tatu kuelekea ulimwengu wa kwanza. Hakuna kinachoshindikana.

Tanzania ina kila kitu, kinachotakiwa ni kudhibiti vizuri mapato ya nchi. Taifa lijengwe. Uharamia na ujangili vitoweke. Taifa lipige hatua kwa kasi. Tutafika.

Wakati tukitazama mbele kwa matumaini kuwa tutafika, vema kila upande ufanye marekebisho. Bunge, CAG na mawaziri watakaoteuliwa. Uwajibikaji ndiyo njia pekee la kuliokoa taifa letu.

Sasa tuweke hoja zote kwenye kapu moja; Utendaji wa Magufuli ni mshangao kwa CCM, hususan wale wapenda mazoea. Umefunika matarajio ya kile ambacho wengi waliamini upinzani ungefanya kama ungechukua nchi. Umegusa mtima wa mamilioni ya Watanzania.

By Luqman Maloto
 
Sijui hata huo uprofesa aliupataje mahana hanafanya yake tu hanavunja sheria za nchi.hawezi hata kuongea kizungu


swissme
 
Back
Top Bottom