SI KWELI Mafuriko ya maji yametokea leo Disemba 5, 2023 Mlima Kitonga, Iringa

Baada ya kuitathmini taarifa hii, tumebaini kuwa si ya kweli.
Salaam Wakuu,

Nimeona taarifa imepostiwa na Boniface Jacob kupitia ukurasa wake wa X ikiambatana na video inayoonesha maji mengi ya mvua yakitiririka katika barabara ya Mlima Kitonga. Video hii imepostiwa pia na Change Tanzania pamoja na MwanaHabari.

Je kuna ukweli wowote kwenye hili?

SI KWELI.jpg
 
Tunachokijua
Julai 23, 2023, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilitoa taarifa inayothibitisha uwepo wa hatari ya kukumbwa na El Nino ambayo huambatana na mvua kubwa kutokana na ongezeko la joto la bahari katika eneo la kati la Kitropiki katika Bahari ya Pasifiki. Hii haikuwa mara ya kwanza kwa TMA kutoa angalizo la uwezekano wa kutokea kwa mvua hizi mwaka 2023.

Kwenye Dokezo la Julai 23, Meneja utabiri wa Mamlaka hiyo, Dr. Mafuru Kantamla alisema baada ya kupitia mifumo ya hali ya hewa walijiridhisha na kuona kwamba El Nino tayari ilikuwa imeanza kujitengeneza na inavyoonekana ni kwamba kulikuwa na 90% ya El Nino hiyo kuendelea kuwepo hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2023.

Meneja huyo aliyataja maeneo ambayo yanaweza kuathirika na mvua hizo kuwa ni nyanda za juu Kaskazini Mashariki ikihusisha mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara pamoja na maeneo ya Pwani yanayojumuisha mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Lindi na Mtwara.

Athari za Mvua zaanza kuonekana
Disemba 3, 2023, Maafa yanayotokana na mvua hizi yalianza kuonekana huko Hanang, Manyara baada ya kutokea kwa maporomoko ya matope yaliyoleta athari kubwa, ambapo hadi kufikia Disemba 5, 2023, watu 65 walipoteza maisha, 116 wakijeruhiwa vibaya huku mamia ya watu wakibaki bila makazi.

Kupitia taarifa ya Msemaji Mkuu wa Serikali Mobhare Matinyi ya Disemba 5, 2023, chanzo cha maporomoko hayo ni kumeguka kwa sehemu ya Mlima Hanang ambao ulikuwa na miamba dhoofu iliyonyonya maji na kusababisha mporomoko na hivyo kutengeneza tope.

Matinyi alibainisha kwamba sehemu iliyonyonya maji ilizua mgandamizo na sehemu ya mlima kushindwa kuhimili na kusababisha kumeguka kwa sehemu hiyo ambayo ilitengeneza tope lililoanza kuporomoko na kuanza kuzoa mawe na miti na kwenda kushambulia makazi ya wananchi katika maeneo hayo.

Aidha, Serikali ilifuatilia taarifa za matetemeko kuanzia Septemba mwaka huu hadi siku ya tukio na kubaini kuwa hakukuwa na tetemeko lolote wala mlipuko wa volkano.

Video za mafuriko zaanza kusambaa Mtandaoni
Baada ya kutokea kwa maporomoko ya Hanang, video kadhaa zilianza kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii zikionesha athari kubwa ya mvua hizi kwenye maeneo tofauti nchini.

Mojawapo ya video hizo ni ile iliyochapishwa kwenye mtandao wa X na Boniface Jacob ikionesha mafuriko ya eneo la Kitonga.


View: https://www.youtube.com/watch?v=KHEGcplqus8
Video inayosambaa Mtandaoni ikionesha Mafuriko ya Mlima Kitonga, Disemba 5, 2023

Video hiyo ilichapishwa pia kwenye mtandao huohuo wa X na Change Tanzania. Kwa pamoja, wote walichapisha video hii Disemba 5, 2023.

Aidha, kwenye mtandao wa Instagram, Mwanahabari Digital waliiweka ikiwa na maelezo kuwa eneo la kitonga lilikuwa limepata mvua kubwa kiasi cha kupelekea mafuriko yaliyofanya madereva washindwe kuendelea na safari.

Ufuatiliaji wa JamiiCheck
Ufuatiliaji wa JamiiCheck kwa kutumia Google Image Search umebaini kuwa video hii ni halisi lakini sio ya sasa.

Ilipandishwa kwenye Mtandao wa YouTube Februari 6, 2020 na Aboud International ambapo Februari 7, 2023 ilichapishwa tena kwenye mtandao huohuo na Syik Entertainment.

Aidha, JamiiCheck imebaini kuwa mtumiaji wa Mtandao wa X anayetumia utambulisho wa King Fahad, Februari 7, 2020 alichapisha ujumbe wenye video hiyo akibainisha athari za mafuriko yaliyotokea eneo la Mlima Kitonga.

Maoni ya watu wengi waliokutana na video hii Disemba 5, 2023 yanayonesha pia kupingana na madai ya watu walioichapisha.

JamiiCheck kupitia wakazi wa maeneo hayo imejiridhisha kuwa barabara ya Mlima Kitonga inapitika na hakuna Mafuriko kama inavyodaiwa.

Similar Discussions

0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom