Madhara utakayopata kwa kujizuia kula

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,376
8,120
Si jambo la kustaajabisha kumkuta mtu yupo kwenye mfululizo wa kutokula muda mrefu kwa kile wengine wanakieleza wapo kwenye ‘diet’ ya kupunguza mwili.

Mfumo huu wa maisha unaendelea kushamiri kwenye maeneo mbalimbali, wengi wakitafuta kurudia maumbile yao ya awali, wakisahau kushinda na njaa kwa muda mrefu kunakaribisha matatizo mengine mwilini.

Hali ya kustaajabisha zaidi, kifungo hiki cha kutokula wanachokiingia watu hawa, hujinasua pale wanapoanza kula kwa kufakamia chakula kingi zaidi, hali ambayo huchangia kutumia kundi moja la chakula.

Kutumia kundi moja la chakula nako wataalamu wanasema ni kuufanya mwili kukosa baadhi ya virutubishi muhimu, jambo ambalo ni hatari zaidi.

Rose Francis, mkazi wa Mbagala anakiri kuwa utaratibu wa kujinyima kula kuna wakati anapungua uzito, lakini baada ya muda huwa na uzito mkubwa zaidi anapoamua kuacha utaratibu huo.

“Nilikuwa na kilo 76, sasa nipo kwenye diet nimepungua kilo mbili, nikiacha ‘diet’ wakati mwingine nafika hadi kilo 80. Kwa hiyo sili sana lakini bado sipungui, sijui hao wataalamu wanashauri vyakula gani maana najinyima sana.

“Wakati mwingine nasikia kizunguzungu kwa kutokula, lakini tayari nimepanga muda wa kula ni asubuhi na wakati wa kulala tu,” anasema.

Tatizo la vidonda vya tumbo

Ofisa Lishe kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili- Mloganzila, Johari Matiko anasema mtu kuacha kula kwa lengo la kupunguza mwili, huvutia tatizo la vidonda vya tumbo kutokana na utumbo kukaa muda mrefu bila chakula.

“Mtu akishazoea anakula muda fulani hata asipokula muda huo mwili unaendelea kufanya kazi, mazingira ya umeng’enyaji chakula huandaliwa, maandalizi hayo huwa ni tindikali ambayo humwagwa tumboni kwa ajili ya kuchakata chakula.

“Sasa tindikali ile inapokuwepo tumboni na chakula hakipo inaanza kukwangua ukuta wa tumbo na mtu kupata vidonda vya tumbo,” anaeleza.

Johari anasema ili mwili upate usawa ni muhimu mtu ale chakula, kwani virutubishi ambavyo mwili huupata ni kupitia chakula anachotumia.

Anabainisha mtu anapoacha kula kwa minajili ya kupunguza mwili, hukosa vyakula muhimu vyenye virutubishi vya kujenga mwili na madhara yake kinga ya mtu kushuka na kuingia kwenye urahisi wa kuambukizwa magonjwa.

“Kwa sababu kinga yake ya mwili huwa chini, unakuta mtu anaacha kula wiki au mwezi, hivyo ndani ya muda huo kinga ya mwili inakuwa chini na ndio huwa mlango wa kushambuliwa na magonjwa,” anasema.

Anasema virutubishi havipaswi kuzidi au kupungua mwilini, akitaja faida zake ni kusaidia kuuweka mwili sawa.

Mifupa kuvunjika

Kutokana na kutokula, Johari anasema madini ya kalishiamu yanapungua mwilini, hivyo mifupa ya mhusika huwa rahisi kuvunjika na kupata matatizo ya gauti.

Kuhusu madini ya chuma ambayo ni mahususi kwenye utengenezaji wa damu anasema, kama mtu hatakula mbogamboga, nyama nyeupe na nyekundu husababisha uzalishaji wa damu na chembechembe zake kuwa chini.

Mtaalamu huyo anabainisha kuwa upungufu wa madini chuma ni hali inayotokea kwenye mwili wa binadamu, kutokana na kuwa na kiwango kidogo cha madini hayo, ikilinganishwa na mahitaji ya mwili.

Miongoni mwa sababu za upungufu wa madini hayo ni ulaji duni wa vyakula vyenye madini chuma na vitamin kama vile vitamini C.

Pia ulaji wa vyakula au vinywaji vinavyoingilia ufyonzwaji wa madini chuma kutoka katika vyakula mfano chai, kahawa, na vinywaji (soda aina ya cola).

Upungufu wa madini chuma kulingana na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) ni tatizo kubwa katika nchi nyingi duniani, ikiwemo Tanzania pia huchangia kupungua kwa wekundu wa damu.

Athari ya upungufu wa madini chuma pia huonekana kwa wanawake kujifungua watoto wenye uzito pungufu (chini ya kilo 2.5), kuongezeka kwa vifo vya wanawake vinavyohusiana na ujauzito au kujifungua.

Unachopaswa kufanya

Kuacha kula kwa kipindi fulani si njia sahihi ya kupunguza mwili, anaonya Johari ambaye anashauri njia salama ni kufanya mazoezi na kupunguza kiwango cha wanga (mfano ugali, wali chapati), sukari na mafuta kwenye mlo wake wa kila siku.

“Hatusemi aache, bali ale kiwango kidogo, atumie mbogamboga za majani kula wanga na mafuta kwa wingi, ndio zinakwenda kututengenezea nishati kwenye mwili, kwa hiyo tunavyokula ugali mkubwa tunaweka sukari na mafuta mengi mwilini.

“Mwili ukipata kiasi cha nishati yake kinachotosheleza, kinachobaki hutunzwa kwenye maeneo laini kama moyo, mishipa ya damu lakini mtu akipunguza vyakula hivyo na akafanya mazoezi na kula matunda na mbogamboga kwa wingi ni njia sahihi ya kuufanya mwili uwe na afya bora,” anaeleza.

Anasema hata kwenye ulaji wa matunda, mtu hapaswi kula yenye sukari kwa wingi, akishauri yatumiwe zaidi yale yenye nyuzinyuzi.

“Shida hii ni kubwa na hata marafiki na ndugu zangu wanaacha kula wakisema wapo kwenye ‘diet’, lakini nishukuru watu wameanza kupata mwamko kwa nini wananenepa na nini wanakula.

“Tatizo watu hawana elimu nini wale, ili kuweka miili yao sawa, wanachukua elimu za mtaani, mitandaoni wanajikuta wanaacha kula. Ni muhimu mtu akitaka kupungua aonane na wataalamu wa lishe ili amuelekeze aina ya vyakula anavyopaswa kula,” anabainisha.

Ofisa Kilimo Mkuu na Mratibu wa Lishe kutoka Wizara ya Kilimo, Margaret Natai anaeleza watu wanapaswa kufahamu uzito usiofaa au unene kupitiliza huchangiwa na ulaji na kutokufanya mazoezi.

“Kama unafanya kazi za ofisini unapaswa ule kwa kiwango kidogo ukilinganisha na mtu anayefanya kazi ngumu, ukiwa na kitambi umekula zaidi ya mahitaji ya mwili, lakini ukifuata utaratibu wa kitaalamu utakula kwa kiasi.

“Unapogundua una uzito kupitiliza ili kuondokana na tatizo, si kuacha kula kwa sababu hapo unatengeneza tatizo lingine,” anasema.

Anasema mtu hapaswi kujiamulia kuacha kula, huku akionya kuwa ni hatari kusikiliza elimu za watu wa mitaani.

“Ni vizuri kufuata ushauri wa kitaalamu, unapomwambia mtu ale hiki au asile kile labda ana tatizo lake la afya, unapomwambia kula hiki au usile kile hujui ataathirika vipi.

“Utakavyomshauri mgonjwa wa kisukari na mwenye shinikizo la juu la damu si sawa na mtu asiye na tatizo lolote,” anaeleza.

Tatizo kwenye ubongo

Anaeleza kuwa mtu anapoacha kula hupata tatizo la vichocheo kushindwa kuwa sawa na kutengeneza tatizo kwenye ubongo.

“Ili ubongo ufanye kazi unahitaji ule chakula, hivyo ukikaa muda mrefu bila kula utakuta kichwa kinashindwa kufanya kazi,” anasema.

Margaret anaeleza kuwa vichocheo hivyo hutengenezwa mwilini na ili vitengenezwe, lazima kuwepo kwa chakula, akibainisha kuwa mtu anapoacha kula huanza kupata matatizo mbalimbali, ikiwemo kupata choo kigumu.

Anasema mtu anayeacha kula kwa muda mrefu atakapokula hupitia maumivu ya tumbo kutokana na kutokula kwa wakati.

Valentina Gonza, Mratibu wa Girl Guide Associaton anasema wamekuwa wakihamashisha ulaji wa mlo kamili kwenye jamii na wamekuwa wakieleza kiasi cha chakula kinachohitajika mwilini.

Anasema endapo mtu atazingatia ulaji sahihi kwa kiwango sahihi, ataepukana na matatizo ya unene au uzito kupitiliza, huku akionya matumizi ya njia ambazo hazijathibitishwa kitaalamu.
 
Back
Top Bottom