Lita moja ya mafuta imefika 2,200, serikali ipo wapi?

serikali ya ccm iko hoi na sikia wameomba mikopo kwenye mabenki kiasi cha bil 540
 
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimefichua kuwa serikali inakabiliwa na hali mbaya ya fedha kiasi cha kushindwa kulipa mishahara ya watumishi wake na ile ya wabunge hadi sasa.
Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe, akihutubia wakazi wa Wilaya ya Mbozi Mashariki katika viwanja vya ofisi ya Ofisa Mtendaji Vwawa mjini, alisema hadi kufikia jana Mei 7 watumishi wa serikali pamoja na wabunge walikuwa bado hawajalipwa mishahara yao ya mwezi wa Aprili.
Zitto ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni, alibainisha kuwa hata sehemu ya posho za wabunge za mkutano uliopita ikiwamo posho ya kugharamia mafuta ya safari za wabunge majimboni, bado hadi jana zilikuwa hazijalipwa kwa sababu serikali haina fedha.
Alisema serikali imefilisika kwa sababu ya kushindwa kukusanya kodi vizuri huku sehemu kubwa ya kodi hiyo inayokusanywa ikiwa haitumiki vizuri kwa sababu za ufisadi.
"Serikali imeshindwa kukusanya kodi inavyotakiwa, serikali imeshindwa kusimamia vizuri kodi yenu, matokeo yake sasa imefilisika.
Imekwenda kwenye mabenki ya ndani kukopa bilioni 540 ili watu wasijue kwamba serikali imefilisika. Haikopi ili ijenge bandari, haikopi ili ijenge viwanda, haikopi ili igharamie miradi ya maendeleo, bali inakopa ili ilipe mishahara ya wafanyakazi", alisema Zitto.
Alionya kuwa iwapo serikali ya Rais Jakaya Kikwete isipoheshimu ushauri wa CHADEMA, mkuu huyo wa nchi atamaliza kipindi chake cha utawala na kuacha zaidi ya Watanzania milioni 20 wakiwa maskini.
"Wakati Kikwete anaingia madarakani, maskini walikuwa milioni 10, leo kuna maskini milioni 12 , akimaliza muda wake maskini wanaweza kufikia milioni 20.
CCM imechoka kuongoza nchi hii, hawana mawazo mapya, hawana maono mapya…watuachie CHADEMA, sisi tunaweza kulikomboa taifa hili", alisema Zitto.
Alisema kama serikali ya CCM ingeingia mikataba mizuri na wawekezaji leo nchi ingekuwa na uwezo mzuri wa kifedha wa kugharamia miradi ya maendeleo.
Akitoa mfano, alisema mauzo ya dhahabu kwa kipindi kilichopita yalifikia sh trilioni 1.7, lakini fedha nyingi zimekwenda kwa wawekezaji kwa sababu ya mikataba mibovu iliyoingiwa na serikali ya CCM.
Akizungumzia hali ngumu ya maisha, alisema gharama kubwa za maisha zinazowakabili Watanzania hivi sasa zimesababishwa zaidi na mfumuko wa bei za vyakula na ule wa bei za nishati ya umeme, mafuta na gesi.
Kwa hiyo, aliwaahidi wakazi wa kata za Isansa, Mlowo, Vwawa na Watanzania wote kwa ujumla, kwamba katika kikao kijacho cha Bunge CHADEMA itapeleka pendekezo la kuitaka serikali ipunguze kodi inayotozwa kwenye mafuta ya petroli kwa asilimia 50 ili bei ya lita moja ishuke kutoka sh 2,050 ya sasa hadi kufikia sh 1,665.
" Katika kila lita moja ya mafuta ya petroli unayonunua, serikali inachukua hapo kodi ya asilimia 50. Kama kodi hiyo itaondolewa, lita moja ya petroli inayouzwa kwa takriban sh 2,050, itaweza kuuzwa kwa sh 1,665.
"Bei ya petroli ikishuka, nauli za mabasi na daladala nazo zitashuka, gharama za usafrishaji wa vyakula zitashuka na kwa hiyo bei ya sukari na vyakula nazo zitapungua, kwa hiyo gharama za maisha zitapungua.
"Tutaitaka serikali ifute misamaha ya kodi kwa asilimia 50 ili kufidia kodi ya asilimia 50 tunayotaka iondolewe kwenye mafuta. Tutaitaka serikali iuze hisa zake zilizoko kwenye Benki ya NBC na Kampuni ya simu ya Zain, kwani zitaipatia fedha ya kutosha ya kuweza kufidia kodi tunayotaka ipunguzwe kwa asilimia 50 katika mafuta. Hiyo ndiyo moja ya ajenda ambayo CHADEMA tunakwenda nayo bungeni Juni 7", alisema Zitto.
Alisisitiza kuwa kazi kuu ya CHADEMA baada ya uchaguzi kumalizika ni kusimamia jinsi kodi za wananchi zinavyotumiwa na serikali ili kuhakikisha hazitafunwi au kutumiwa vibaya na kukwamisha maendeleo ya wananchi.
"Sisi ni sawa na mbwa wa tajiri, jukumu letu ni kunusa na kubweka. Pale tunapoona kodi yenu imeliwa sisi tunakuja kuwaeleza, ili mchukue hatua za kuwawajibisha viongozi wenu na hatimaye mtupe ridhaa ya kuwaongoza …maana wenzetu wameshindwa kazi", alisema Zitto.
Katika hatua nyingine, alisema chama chake kitafuatilia na kuhakikisha wafanyakazi waliokuwa kiwanda cha nguzo chini ya Shirika la Uzalishaji na Ugavi wa Umeme nchini (TANESCO), wanalipwa mafao yote yanayofikia sh milioni 848.2 kwa mahesabu ya sasa.
Zitto alitoa msimamo huo ikiwa ni saa chache tangu akabidhiwe nyaraka zote za madai ya waastaafu hao wa jijini Mbeya ikiwamo nakala ya maamuzi ya kesi waliyoshinda katika mahakama ya kazi ambayo iliamuru walipwe fedha hizo.
"CCM wamechoka kuongoza nchi hii. Vijana hawana ajira kwa sababu hakuna shughuli za uchumi za kuwaajiri. Viwanda vimeuzwa. Leo mzee mmoja ameniletea nyaraka zote zinazoonyesha jinsi kiwanda cha nguzo cha hapa Mbeya kilichokuwa chini ya TANESCO kilivyouzwa. Mzee huyo pamoja na wafanyakazi wenzake wapatao 53, hawajalipwa mafao yao ya jumla ya sh milioni 848.2. Mahakama ya Kazi ilishaamua walipwe mafao yao . Tangu mwaka 1998 hadi leo hawajalipwa.
Alisema akiwa kama Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Masharika ya Umma, tayari ameliagiza shirika hodhi la mashirika ya umma (Consolidated holdings) limpe taarifa yote rasmi ya kwanini mpaka leo waastaafu hao hawajalipwa pesa zao, kama ilivyoamriwa na Mahakama ya Kazi.
"Kiwanda chenyewe walikiuza kwa bei ya kutupa, sasa natangaza kwamba CHADEMA tutalifuatilia suala hili mpaka wastaafu waliokuwa kwenye kiwanda kile walipwe haki zao", alisema Zitto.
Zitto aliwashukuru pia wakazi wa mkoa wa Mbeya kwa kuipigia CHADEMA kura nyingi za urais na ubunge huku akibainisha kuwa zile za urais zilichakachuliwa, kwani aliyeshinda ni Dk. Willibrod Slaa.
Awali Mbunge wa Viti Maalumu kutoka Mkoa wa Arusha, Joyce Mukya, akihutubia wakazi wa kata ya Insansa, Mlowo aliwataka wakazi wa kata hizo kuiunga mkono CHADEMA na kutumia haki zao za kisheria kuwaondoa viongozi wa vijiji wanaofanya ufisadi wa vocha za mbolea.
Akinukuu ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali, Mukya alisema vocha za mbolea za jumla ya sh milioni 130 ziliibwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, chini ya viongozi wa CCM.
"Jamani tuachane na viongozi wezi, tuendelee kuimarisha chama chetu cha wanyonge CHADEMA, tuikomboe Mbozi yetu", alisema Mukya.
Naye Raya Ibrahim Khamis, Mbunge wa Viti Maalumu (CHADEMA) kutoka Zanzibar , akihutubia katika mikutano hiyo, alisema yeye na wabunge wenzake wa viti maalumu kutoka chama hicho watafanya kazi ya kuchukua kero na matatizo yote yaliyopo kwenye majimbo yanayoongozwa na wabunge wa CCM, ili wapiganie haki zao bungeni.
"Mbunge wenu Zambi amewasahau, mmesema ujenzi wa zahanati unasuasua, vocha za mbolea wamekula, sasa nawaambia yote mliyotueleza kwenye risala yenu tutayakomalia bungeni. Kuanzia sasa sisi wabunge wa viti maalumu wa CHADEMA ndio tutakuwa wabunge wenu kwa kuwa Zambi ameshindwa kuwasemea.
Katika mikutano hiyo iliyofanyika jana kwenye Wilaya ya Mbozi pekee, wanachama kadhaa wa CCM walirudisha kadi za chama hicho na kupokea zile za CHADEMA kutoka kwa Zitto.
Nao viongozi wengine wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe waliendelea kufanya mikutano ya hadhara katika maeneo tofauti.
Akihutubia katika maeneo tofauti tofauti katika Jimbo la Rungwe Magharibi, Mbowe alisema Mbunge wa jimbo hilo, Profesa, David Mwakyusa, ameshindwa kuwatatulia wananchi matatizo yao kwa kuwa si mpambanaji.
Alisema kuwa mbunge wa CHADEMA mmoja ni sawasawa na wabunge wa CCM ishirini, hivyo Mwakyusa hana ubavu wa kushughulikia matatizo ya wananchi waliomchagua.
Alisema matatizo yanayowakabili wana Rungwe Magharibi yametokana na viongozi walioko madarakani, kwa kuwa ufisadi ndiyo tabia yao.
Alisema kuwa Tanzania bila CCM inawezekana kwa kuwa kitu chochote kikikaa muda mrefu kinakuwa hakina mvuto, hivyo ni wakati wa wananchi kujipanga kuhakikisha chama hicho kinaondoka madarakani uchaguzi ujao.
Alisema kwa mujibu wa Idara ya Kimataifa ya Maendeleo ya Uingereza, utafiti uliofanywa nao katika matumizi ya fedha za maendeleo katika bajeti ya Tanzania, asilimia 35 hadi 40 zinatumika katika kuwanufaisha viongozi badala ya kuwaletea wananchi maendeleo.
Grace Kiwelu alisema kuwa kutokana na matatizo ya wananchi yalivyo mengi na wabunge wa CHADEMA kwa uchache wao bungeni, watapambana bungeni kwa uchache wao huo hadi kieleweke.
Naye Dk. Slaa akiwa Chunya aliishangaa Serikali kwa kuwafilisi watu wake na kuwakimbiza nchini badala ya kuwasaidia wailetee maendeleo nchi.
Alisema serikali imeendela kumkumbatia Naibu Kamishna Mkuu wa TRA, Luoga, ambaye ameitia serikali hasara kubwa katika kumfilisi mmliki wa Tango Transport ya Arusha.
 
Back
Top Bottom