UZUSHI Kupakata laptop au kuweka simu kwenye mfuko wa suruali hupelekea upungufu wa nguvu za kiume

Baada ya tathmini, tumebaini kuwa taarifa hii ni ya uzushi
Hivi ni kweli kuwa watumiaji wa kompyuta mpakato huku wameipakata mapajani, pamoja na sisi tunaotumbukiza simu zetu zikiwa on air kwenye mifuko yetu ya mbele ya suruali tupo kwenye hatari ya kupoteza nguvu za kiume?

IMG_6760.jpeg
 
Tunachokijua
Upungufu wa nguvu za kiume kwa kiswahili hutafsiriwa kwa namna nyingi, lakini maana sahihi ya hali hii ambayo kwa lugha ya Kitaalam huitwa Electile Dysfunction ni kukosekana au kupungua kwa uwezo wa mwanamme kwenye kusimamisha uume wake kiasi cha kutosha kuhimili ushiriki wa tendo la ndoa kikamilifu. Hii ni kwa mujibu wa NIH consensus Conference, 1993

Mwitikio wa kihisia unaochochea kusimama kwa uume hutegemea kwa kiasi kikubwa mfumo wa mzunguko wa damu mwilini hivyo magonjwa kama kisukari na Shinikizo kubwa la damu pamoja na hali zingine zinazoathiri mfumo wa damu na moyo hutajwa kama mojawapo ya sababu zinazopelekea kutokea kwa changamoto hii.

Uhusiano wa kupakata laptop au kuweka simu mfukoni na upungufu wa nguvu za kiume.
JamiiForums imepitia maelezo ya kitaalam na tafiti nyingi za afya zinazothibitisha kuwa kompyuta mpakato (laptop) inapowekwa kwenye mapaja huzalisha joto linaloweza kuathiri ufanisi wa makende (Korodani) katika kuzalisha mbegu za kiume.

Hii inaweza kusababisha tatizo la kushindwa kurutubisha yai la mwanamke (kutungisha ujauzito), yaani ugumba kwa wanaume.

Aidha, uhifadhi wa simu kwenye mifuko ya mbele ya suruali huhusishwa na kutengeneza mbegu za kiume zenye kasi ndogo na vinasaba dhaifu. Inaweza pia kuchangia kutokea kwa ugumba.

Pamoja na uwepo wa uthibitisho huu wa kuathiri uzalishwaji wa mbegu za kiume na kusababisha ugumba, JamiiForums imebaini kuwa hakuna maelezo ya kitaalm yanayofafanua uhusiano wa vifaa hivi na tatizo la upungufu wa nguvu za kiume.

Japokuwa kwa kiswahili upungufu wa nguvu za kiume ni nadharia pana inayotafsiriwa vibaya, kitaalam humaanisha hali ya kukosekana au kupungua kwa uwezo wa mwanamme kwenye kusimamisha uume wake kiasi cha kutosha kuhimili ushiriki wa tendo la ndoa kikamilifu ambayo hadi sasa haijaweza kuhusianishwa na matumizi ya kompyuta mpakato au uhifadhi wa simu kwenye mifuko ya suruali.

Hivyo, JamiiForums inatambua kuwa tabia hizi zinaweza kuleta ugumba kwa kuathiri uzalishwaji wa mbegu za kiume, lakini haziwezi kusababisha upungufu wa nguvu za kiume.

Katika nyakati fulani, Ugumba na nguvu za kiume ni mambo yanayoweza kwenda sambamba lakini hayana tafsiri na maana moja.
1 Reactions
Reply
Back
Top Bottom