Magazetini
JF-Expert Member
- Aug 16, 2014
- 588
- 1,698
Viwango vya makato ya kodi kwa sasa katika mishahara ya watumishi wa umma ni asilimia 12 na lengo ni kupunguza zaidi katika kipindi cha miaka mitatu ijayo ili kuwaondolea mzigo watumishi hao.
Akizungumza na watumishi mbalimbali wa umma mkoani Kilimanjaro, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue, alisema serikali inasikia maombi ya watumishi hao kwani lengo si kuwakomoa.
Hata hivyo, Balozi Sefue alisema pamoja na maombi ya muda mrefu ya watumishi hao lakini serikali imekuwa ikijitahidi kushusha makato hayo, kwani awali ilikuwa asilimia 16, ikashuka hadi asilimia 13 na sasa asilimia 12.
Aidha Katibu Mkuu Kiongozi aliwaonya watumishi wa umma kutojihusisha na siasa na kwamba wale watakaobainika kufanya hivyo watachukuliwa hatua za kinidhamu.
"Ukiwa mtumishi wa umma, unatakiwa uchague moja, kama unaingia katika siasa acha kazi ya utumishi wa umma, vinginevyo usichanganye haya majukumu," alisema.
Alisema taifa linaelekea katika Uchaguzi Mkuu wa madiwani, wabunge na Rais mwakani na kwamba ni mwiko kwa watumishi kujiingiza katika siasa, kwani kwa kufanya hivyo ni kuchanganya majukumu na moja wapo halitafanyika kikamilifu.
Balozi Sefue alitaka watumishi hao kuzingatia sheria, maadili, kanuni na taratibu za utumishi wao kwani watambue kuwa yote wanayofanya kwa mujibu wa sheria wanamwakilisha Rais Jakaya Kikwete kwani asingeweza kuwa katika kila wilaya.
Hata hivyo, alitaka mamlaka za nidhamu kuhakikisha zinawaadhibu baadhi ya watumishi ambao wanakwenda kinyume na sheria na taratibu zilizopo ili kujenga nidhamu ya utumishi.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Jumanne Sagini, alionya tabia ya baadhi ya halmashauri zote nchini kutumia fedha za miradi ya maendeleo badala ya kuzihamishia miaka inayofuata.
"Zipo halmashauri za wilaya zinapewa mabilioni ya fedha kwa miradi ya maendeleo, lakini cha ajabu ni kwamba wanakaa na fedha hizo na mwisho wa mwaka zinahamishiwa mwaka unaofuata hii haikubaliki," alisema.
Kwa upande wao baadhi ya watumishi waliomba serikali kulipa madeni ya watumishi ili kuwapa ari ya kufanya kazi kwa bidii zaidi kuliko hali ilivyo sasa.
CHANZO: Habari Leo