Kisheria hii imekaaje?

Jayfour_King

JF-Expert Member
Nov 15, 2009
1,135
128
Nikiwa Mbeya mwanzoni mwa mwezi wa sita Halmashauri ya jiji kupitia kwa mkurugenzi wake waliwataangazia wakazi wa Mbeya kwamba sehemu iliyokuwa inaitwa Stela farm (Iwambi) itagawiwa viwanja kwa wananchi kwa ajili ya makazi na biashara.

Hii ilikuwa habari njema kwa wapenda maendeleo na wananchi wote wa mkoa wa Mbeya kwa ujumla wake, siku ya siku ilifika watu wakajitokeza kwa wingi kuitikia wito huo. Siku ya tarehe 7/6/10 kuna watu walishakuwa kwenye mistari ya kusubiri huduma tangu saa kumi na moja alfajiri.

Ofisi zilifunguliwa na huduma zikaanza kutolewa, watu walikuwa wengi sana na mpangilio wa usimamizi wa mistari ya kwenda kupokelea huduma haikuwa na waelekezi hivyo watu walijipanga kadiri walivyoona inafaa.

Ilipofika saa saba mchana ikiwa hata robo moja ya watu waliofika pale wakiwa hawajahudumiwa tulitangaziwa kwamba form zimekwisha, na kuaminishwa kwamba kikweli kilichokwisha sio form bali ni idadi ya viwanja vilivyotolewa ililingana na idadi ya form hivyo kwa maneno mengine ni kwamba viwanja vimekwisha!

Watu tuliondoka pale kila mmoja na staili yake, wengi hawakuridhika na waliona kama kuna agenda iliyojificha katika mchakato mzima wa shughuli husika. Na ikatangazwa kwamba form zilizotolewa ni lazima ziwe zimejazwa na kurudishwa katika kipindi kisicho zidi siku saba. Watu walitekeleza hilo kwa wale waliobahatika kupata hizo form.
Baada ya form hizo kuwa zimerudishwa ikachukuwa kiasi cha wiki tatu hivi majina yakatolewa kwamba hawa ndio "waliofanikiwa" kupata viwanja eneo la iwambi, majina mengi miongoni mwa watu waliokuwa na form hayakutokea kwenye orodha iliyotolewa na jiji.

Sisi tuliokosa baada ya kwenda kuulizia tukaambiwa kwamba tumewekwa kwenye reserve kwamba kuna watu hawajafanyiwa fidia ili kupisha eneo na pia kwa watakao shindwa kulipa katika kipindi cha mwezi mmoja tangu siku lilipotolewa tangazo husika. Japo maelezo yalikuwa na utata tulilazimika kuamini kwani eneo husika lilikuwa la serikali sasa sijui fidia wanalipwa kwatu kwa kuvamia au ni vipi hatukujali sana tukaendelea kusubiri.

Tumesubiri na tunaendelea kusubiri lakini katika mazingira ya rushwa yanayoendelea pale hatutegemei chochote cha maana kutokea, ikiwa ni miezi mitatu sasa tangu mwanzo wa zoezi hili kuanzishwa.

Ushauri wa kisheria ninaouomba ni huu:

1. Je hizi halmashari zetu miji/manispaa na majiji zinaruhusiwa kuwadanganya wananchi na kuchukua pesa zao pasipo kutekeleza kile walichoahidi kutoa kama huduma? Kama jibu ni sio sisi wananchi waathirika tunatakiwa kufanya nini kisheria?

2. Kwa kuona kwamba haki haikutendeka tunaweza kuweka pingamizi kisheria mahakama kuu kitengo cha ardhi kusitisha uendelezaji wa eneo husika ili uchunguzi ufanyike na haki itendeke? Kama jibu ni ndio tunatakiwa tuwe watu wangapi na hatua za kufuata ni zipi?

3. Kwa kuwa shida yetu sisi haikuwa hizi form walizotuuzia bali viwanja, yoote ya hapo juu yakishindikana tunaweza kurudishiwa pesa zetu na kulipwa fidia ya usumbufu na kupewa matumaini yasiyokuwepo?

Wanasheria ndani ya jamii forums naomba msaada ili nijue sehemu sahihi ya kuanzia katika suala hili nikiamini kwama suala hili sio la kufumbia macho na kuacha watu wachache wakifaidi visivyo vyao na wengine kubaki tukiangalia tu mambo mabaya yanavyokwenda katika jamii yetu.

Nawasilisha kwa ushauri wakuu.
Natanguliza shukurani
 
Back
Top Bottom