Kesi ya Chenge yazua manung`uniko

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,318
33,125
headline_bullet.jpg
Wakili alalamika imezidi kwa kalenda
headline_bullet.jpg
Asema nenda rudi yafikia mara tano



Chenge1%288%29.jpg

Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge



Wakili anayemtetea Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge (61), anayekabiliwa na kesi ya kuendesha gari kwa uzembe na kusababisha vifo vya watu wawili, Simon Mponda, ameilalamikia mahakama kwa kuahirisha mara kwa mara kesi hiyo.
Wakili Mponda aliiambia Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam jana kuwa uahirishaji wa kesi hiyo unasababisha usikilizaji wake uchelewe kuanza.
Wakili huyo alitoa malalamiko hayo mbele ya hakimu Kwey Rusema, mara baada ya Mwendesha Mashitaka, Inspekta wa Polisi David Mafwimbo, kuiomba mahakama iahirishe kesi hiyo kutokana na Wakili wa Serikali, Richard Rweyongeza, kushindwa kufika mahakamani.
Licha ya Rweyongeza kuchelewa kufika mahakamani, mahakama haijakamilisha maelezo ya awali, ambayo Chenge anapaswa kusomewa kabla kesi dhidi yake kuanza kusikilizwa.
“Mheshimiwa Hakimu, sina pingamizi la kuahirishwa kwa kesi hii, ila nilikuwa naiomba mahakama iharakishe kuandaa hayo maelezo ya awali ili kesi hii iweze kusikilizwa, kwa sababu kila mara tunapokuja hapa mahakamani kesi inaahirishwa tu, na sasa hii ni mara ya tano inaahirishwa, sijui ni kwa nini,” alihoji wakili Mponda.
Baada ya wakili Mponda kutoa malalamiko hayo, Hakimu Rusema alimweleza wakili huyo kuwa kesi hiyo iliahirishwa jana kutokana na wakili wa serikali kuwa na kesi nyingine katika Mahakama ya Rufaa.
Baada ya kutoa maelezo hayo, Hakimu Rusema aliiahirisha kesi hiyo hadi Aprili 9, mwaka huu, ambapo Chenge atasomewa maelezo ya awali kabla usikilizwaji wa kesi hiyo kuanza.
Chenge ambaye anadaiwa kugonga bajaj na kusababisha vifo vya watu wawili, yupo nje kwa dhamana ya Sh. milioni moja.
Chenge alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya Kinondoni mwaka jana, akikabiliwa na mashtaka manne ya kuendesha gari kwa uzembe bila kuwa na bima na kusababisha ajali iliyoua watu hao baada ya kuigonga bajaj. Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, katika ajali hiyo Chenge alikuwa anaendesha gari aina ya Toyota Pick up Hilux namba T 512 ACE iliyogonga bajaj yenye namba T 736 AXC na kusababisha vifo vya wanawake wawili, Beatrice Costantine na Vick George jijini Dar es Salaam.
Ajali hiyo ilitokea Machi 26 mwaka jana, saa 10:30 usiku katika Mtaa wa Haille Selassie, Masaki.



CHANZO: NIPASHE
 
Back
Top Bottom