Nani anaruhusiwa kisheria kusimamia kesi, kuandaa, kusaini na kuwasilisha nyaraka (documents) Mahakamani?

Apr 26, 2022
64
100
Haya ni baadhi ya maswali ambayo utapata majibu yake kwa kusoma makala hii fupi.

1: Je, mtu ambaye sio Wakili anaruhusiwa kumuwakilisha (kumsimamia) au kumtetea mtu kwenye kesi Mahakamani?

2: Je, mtu ambaye sio Wakili anaweza kuandaa, kushuhudia na kusaini nyaraka (documents) za kisheria na kuziwasilisha Mahakamani?

3: Nini tofauti kati ya mwanasheria na Wakili?

Kutokana na hayo maswali matatu, nimetengeneza maswali haya madogo ya nyongeza:

(i) Je, unaruhusiwa kujiandalia mwenyewe documents kama unafahamu kuziandaa?

(ii) Je ni lazima kuweka Wakili kwenye kesi yako au hata wewe unaweza kujiwakilisha mwenyewe?

Makala hii imeandaliwa na kuletwa kwako nami Zakaria Maseke, Advocate / Wakili.
(0746575259 - WhatsApp).
zakariamaseke@gmail.com

Nianze kwa kuelezea tofauti kati ya mwanasheria (lawyer) na Wakili (Advocate). Maana kwa kufanya hivyo nitakua nimejibu swali la kwanza na la pili.

Mwanasheria ni nani?

Kwa kifupi, mwanasheria - “ni mtu yeyote aliyesoma na kufaulu sheria,” preferably au hasa hasa mwenye shahada (degree) ya sheria yaani bachelor of laws (LL.B) kutoka chuo kikuu kinachotambulika. Labda swali lingine ni je, mtu aliyesoma sheria ngazi ya cheti tu (certificate in law) au diploma ya sheria pekee, na yeye ni mwanasheria? Au mtu aliyesoma akafeli?

Sheria sio ujanja au uzoefu tu wa mtaani, huwezi kuwa mwanasheria au kuruhusiwa kufanya kazi za kisheria kwa experience (uzoefu) au ujuzi wa mtaani pekee, ni lazima usome na kufaulu na upewe cheti. Tofauti na hapo wewe utakuwa ni mwanasheria kishoka.

Maana ya Wakili (Advocate):

Wakili (Advocate) - Huyu ni mtu aliyesoma na kufaulu au kuhitimu masomo ya degree (shahada) ya sheria (bachelor of laws - LL.B) kutoka chuo kikuu kwa miaka mitatu au minne (inategemeana na chuo alichosoma), alafu amesoma tena na kufaulu masomo ya sheria kwa mwaka mwingine mmoja kwenye shule ya sheria kwa vitendo (law school). Pia ameapishwa kuwa Wakili na Jaji Mkuu na ana muhuri. Huyo ndiye Wakili Msomi au Learned Advocate kama wanavyoitana

Kwa lugha nyingine Mawakili wote ni wanasheria ila sio wanasheria wote ni mawakili.

Sifa za Wakili (Advocate):
•Ana degree ya sheria kutoka chuo kikuu (LLB).
•Ana diploma kutoka law school (shule ya sheria kwa vitendo).
•Ameapishwa na Jaji Mkuu.
•Ana muhuri.
•Anaruhusiwa kumuwakilisha au kumtetea mtu kwenye kesi Mahakamani.
•Anaruhusiwa kushuhudia viapo, mikataba kuandaa na kusaini nyaraka (documents) mbalimbali kwa jina na muhuri wake na kuziwasilisha Mahakamani.
•Anaweza kuwa hakimu au Jaji.

Sifa za mwanasheria ambaye hajapita law school (shule ya sheria kwa vitendo).
•Hana muhuri.
•Haruhusiwi kumuwakilisha au kumtetea mtu kwenye kesi Mahakamani (isipokua baadhi ya kesi ambazo hazihitaji uwe Wakili).
•Haruhusiwi kushuhudia viapo, mikataba au kuandaa na kusaini nyaraka (documents) mbalimbali kwa jina lake na kuziwasilisha Mahakamani.
•Hawezi kuwa hakimu au Jaji maisha yake yote.

Kwa ufupi, ukiulizwa mtu (mwanasheria) ambae amemaliza degree ya sheria ila hajaenda law school anaweza kufanya kazi gani? Ni bora tu umwambie haipo ila atakuwa amepoteza muda kusoma sheria (maana sasa hivi karibia kila ajira ya sheria wanataka Mawakili tu (watu waliopita na kufaulu shule ya sheria kwa vitendo - law school).

Sasa nirudi kwenye swali la pili, “Je, mtu ambaye sio Wakili anaruhusiwa kuandaa nyaraka (documents) za kisheria na kuziwasilisha Mahakamani?”

Jibu ni inategemeana, je anaziandaa na kukupelekea kwa jina lake au anakusaidia kuandaa tu alafu akupe uzipeleke mwenyewe kwa jina na sahihi yako?

Tuanze na kukuandalia kwa jina lake:

Kisheria, ili mtu aweze kukuwakilisha au kukusimamia kwenye kesi yako Mahakamani au kushuhudia na kusaini viapo, mikataba au kuandaa nyaraka (documents) mbalimbali na kuziwasilisha (ku file) Mahakamani kwa jina lake na sahihi yake (DRAWN AND FILED BY… ADVOCATE), lazima awe na sifa zifuatazo:

(i): Lazima awe Wakili (Advocate). Kwa maana ya sifa zote za kitaaluma. Rejea maana ya Advocate kama nilivyosema huko juu.

(ii): Pili, sio tu awe Wakili, ila ni lazima pia huo muda anaokuwakilisha au kusimamia kesi yako Mahakamani au kushuhudia na kusaini nyaraka (documents) zako na kuziwasilisha Mahakamani, lazima awe na “IN FORCE PRACTICING CERTIFICATE” (hati/kibali/cheti HAI (in force) cha kumruhusu kuendelea kufanya kazi kama Wakili) na awe na VALID BUSINESS LICENSE (leseni halali ya biashara).

Akiwa ni Wakili tu ila hajahuisha (haja renew) practicing certificate au leseni, basi Wakili huyo anaitwa “UNQUALIFIED PERSON (MTU ASIYE NA SIFA/VIGEZO),” hana sifa kisheria za kufanya kazi yoyote ya sheria inayofanywa na Wakili tena ni kosa la jinai.

Sheria ya Mawakili (Advocates Act, CAP 341), kifungu cha 39(1), inaeleza maana ya “unqualified person,” ambapo sheria imetoa sifa za mtu mwenye sifa za kufanya kazi ya Uwakili alafu ikasema mtu ambaye hana sifa hizo nilizotaja huko juu anaitwa “unqualified person.”

Nanukuu section 39(1) of the Advocates Act, it reads: -
“No person shall be qualified to act as an Advocate unless;

(a) his name is on the Roll,
(b) he has in force a practising
certificate and
(c) he has a valid business licence,
and a person who is not so qualified is in this part referred to as an “unqualified person”.

Labda swali lingine ni je, nini kitakukuta ukisimamiwa kwenye kesi au kuandaliwa na kusainiwa nyaraka (documents) na mtu ambaye muda huo sio Wakili au ni Wakili ila alikuwa hana leseni au haja renew practicing certificate?

Kama ikigundulika kwamba mtu anayesimamia kesi yako sio Wakili kabisa au ni Wakili lakini muda ambao alikua anasimamia kesi yako au anandaa na kusaini nyaraka (documents) zako na kuziwasilisha Mahakamani, alikuwa hajauisha au ku renew practicing certificate au leseni, basi kuna mawili:

1: Moja ni kwamba, kila alichofanya, maneno yote aliyoongea Mahakamani kwa niaba yako, nyaraka zote alizokuandalia na kusaini, zitaondolewa haraka sana (will be expunged) kutoka kwenye kumbukumbu (records) za Mahakama.

Wakili huyo atafukuzwa kwenye hiyo kesi na anaweza hata kuchukuliwa hatua za kinidhamu lakini pia ni kosa la jinai, alafu kesi yako itaanza upya na utaambiwa uandae na kuleta upya nyaraka (documents) zingine. Huu ndio msimamo wa Majaji na Mahakimu wengi.

Ingawa hakuna kifungu chochote cha sheria nchini Tanzania, kinachosema kwamba ukikuta nyaraka zimeandaliwa na Wakili ambaye hana sifa, basi nyaraka hizo zifutwe au kuondolewa kwenye record za Mahakama. Ila huo ndio uzoefu (practice) na kuna kesi za kutosha ambapo Mahakama imefanya hivyo.

Kumbuka hizo nyaraka zenyewe zinakuwa hazina shida, nyaraka ni zile zile zinazotakiwa, ziko sahihi kabisa ila kwa kuwa Wakili aliyeziandaa hakuwa na leseni au alichelewa ku renew practicing certificate, basi kazi yake yote, Mahakama inasema haina thamani, inazitupilia mbali.

Naomba uzingatie kinachoangaliwa ni muda, tarehe na siku Wakili alipokua anakuandalia hizo documents. Kwa hiyo hata kama wakati mpo Mahakamani atakuwa amesha renew leseni au practicing certificate, wao wataangalia siku husika wakati anaziandaa alikua na hadhi (status) gani, bado wataziondoa tu. Mahakama inakwambia hakuna utakaso wa makosa ya nyuma (utakaso doctrine).

Na hili ni moja wapo ya mapingamizi kabisa, mko Mahakamani kesi inaendelea, upande wa pili ananyoosha mkono anasema Mheshimiwa Jaji hizi nyaraka ni batili kwa sababu Wakili aliyeziandaa hakua ame renew kibali/practicing certificate au kulipia leseni n.k.

2: Pili, kuna Majaji wengine hawana shida, hawakubali kuziondoa kwenye record nyaraka zilizoandaliwa na kusainiwa na Wakili asiye na sifa.

Kweli Wakili huyo kufukuzwa atafukuzwa kwenye hiyo kesi kama atakua mpaka muda huo haja renew kibali au kulipia leseni, lakini kesi haitaanza upya, ila tu Jaji au Hakimu atakwambia nenda katafute Wakili mwingine alafu kesi itaendelea ilipoishia. Majaji hawa wanasema hawaoni maana ya kumuadhibu mteja kwa makosa yaliyofanywa na Wakili. Sasa Majaji kama hawa wako wachache mno. Wale wa kundi la kwanza ndio wengi.

Kwa hiyo kwa ufupi, “mtu ambaye sio Wakili HARUHUSIWI kuandaa nyaraka (documents) za kisheria na kuziwasilisha Mahakamani kwa jina, sahihi na muhuri wake, maana hana sifa.” Na hicho ndo kitakukuta ukisimamiwa kwenye kesi au kuandaliwa na kusainiwa nyaraka (documents) na mtu ambaye muda huo sio Wakili au ni Wakili ila hana leseni au amechelewa ku renew kibali chake (practicing certificate).

Kuna kesi nyingi saaana kuhusu hii mada lakini siwezi kuziweka hapa, kuhofia mada itakua ndefu (kuna article nimezichambua hizo cases ingia google andika “A Review of the Law and Practice relating To Advocates Misconduct in Tanzania: A Case Study of Unqualified Person,” by Zakaria Maseke).

Sasa, hiyo ni kama anakuandalia kwa jina lake, je kama anakusaidia kuzindaa tu alafu akupe uzipeleke mwenyewe kwa jina na sahihi yako? Kuna ubaya?

Wengine wamekua wakifanya hivyo, wakiona hawawezi kumlipa Wakili kusimamia kesi yote, wanatafuta mwanasheria au Wakili anayejua, wanamlipa au wanamuomba anawaandalia documents (nyaraka) wanapeleka Mahakamani. Ziko nyaraka (documents) nyingi Mahakamani zimesainiwa na wateja wenyewe lakini kwa kweli hawajaziandaa wenyewe. Wameandaliwa na Mawakili au ndugu au marafiki zao ambao ni wanasheria.

Swali lingine kama hilo ni je, kama mimi ni Wakili au ni mwanasheria au sio mwanasheria lakini nafahamu mwenyewe kuandaa nyaraka (documents) za kisheria, naweza kujiandalia au hadi nitafute Wakili mwingine?

Jibu hapa inategemeana, kwa sababu kuna nyaraka ambazo zinatakiwa kushuhudiwa au kuapa mbele ya Wakili, mfano AFFIDAVIT (KIAPO), hata kama ni Wakili, huwezi wewe mwenyewe kuanza kujishuhudia na kujiapisha mbele yako mwenyewe na kujigongea muhuri wako mwenyewe. Hapo lazima utafute Wakili mwingine (ni kama padiri anavyoungamisha wenzake, padiri huyo huyo akitenda dhambi hawezi kujiungamisha mwenyewe lazima atafute padiri mwingine au askofu).

Lakini kama ni document ambayo haihitaji muhuri wa wakili mwingine na unajua vizuri kuiandaa, ruksa jichoree tu, uweke majina yako, kama una muhuri wako utaweka pia, kama huna muhuri weka jina lako tu, alafu peleka Mahakamani au huko inakotakiwa. Itapokelewa vizuri kabisa.

Je, hizo nyaraka anazokuandalia ndugu yako au rafiki yako mwanasheria uhalali wake ukoje kisheria? Kwa kweli Mahakama haitajua nani amekuandalia, kwa sababu jina linaloonekana kwenye document ni lako “drawn and filled by…”. Lakini Hakimu au Jaji anajua kabisa kuwa wewe huwezi kuziandaa.

Kwa lugha nyingine sio lazima kuweka Wakili, pengine huna hela ya kumlipa Wakili au wewe wenyewe ni msomi wa sheria basi unaweza kujiandalia documents na unaruhusiwa kujiwakilisha au kujitetea Mahakamani hata kama hujui sheria. Lakini ni hatari sana kujiandalia documents au kujitetea mwenyewe bila Wakili (mwanasheria).

HATARI ZA KUJIANDALIA DOCUMENTS WAKATI SIO MWANASHERIA:

(i) Kwanza hujui unatakiwa kupeleka au kujibu kwa kutumia document gani na inafananaje. Shida sio kuandaa, swali ni unaijua hiyo document? Ukikosea itapelekea documents zako zifukuzwe (ziwe struck out).

(ii) Hujui document ipi inatakiwa iwekwe muhuri wa Wakili na ipi unaruhusiwa kujiandalia mtu yeyote. Mfano affidavit lazima isainiwe na Wakili (hata Wakili hawezi kujisainia affidavit na kujigongea muhuri wake mwenyewe).

(iii) Hujui lugha ya kisheria au ya Mahakama. Unaweza kuomba kitu ambacho hata hakipo Mahakama ikabaki inakushangaa. Au ukasahau maombi ya msingi au ukaomba kitu kingine ambacho sio sahihi, baadae unashangaa nyumba imevunjwa kwa sababu ulikosea kuomba.

(iv). Hujui vifungu vya sheria wala kesi. Unapoandaa baadhi ya documents au maelezo yako kwenye maandishi unatakiwa kuyaunga mkono (ku- support) na vifungu au kesi za Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani. Swali unazijua?

(v) Hujui uweke viambatanisho (annexures) gani. Ukipeleka documents unatakiwa kuambatanisha na nyaraka unazotarajia kutumia kama ushahidi, usipoziweka utashindwa kuthibitisha (ku prove) kesi au madai yako.

(vi) Huna account ya ku file hizo nyaraka mtandaoni (sasa hivi kesi zinafunguliwa mtandaoni / electronically), una upload kwanza online baadae unapeleka hard copy (makaratasi) Mahakamani.

(vii) Mwisho hujui technicalities au ufundi wa kisheria. Watakuwekea mapingamizi alafu maneno yako kwa kilatini (Res judicata, pre mature, n.k). huelewi ujibuje.

(viii) Ziko hatari nyingi lakini mwisho kabisa ni kushindwa kesi na kulipa gharama juu.

Njia nyingine kuliko kujaribu kujiandalia documents na kuandika vitu ambavyo havieleweki ni heri uombe msaada wa kisheria bure Mahakamani au kutoka kwenye taasisi zinazotoa hiyo huduma kama vile LHRC, TAWLA n.k.

Ila nikuonye tu kuwa sheria sio taaluma au kazi ya kusema utaifanya peke yako wakati hujasomea. Huwezi kushindana na Mawakili Mahakamani wakati wewe sio mwanasheria.

Tumalizie na swali la kwanza ambalo lilikua, “Je, mtu ambaye sio Wakili anaruhusiwa kumwakilisha (kumsimamia) au kumtetea mtu kwenye kesi Mahakamani?” Hili nimeshajibu huko juu - Generally, HARUHUSIWI (isipokuwa kwa baadhi ya kesi ambazo hazihitaji mtu awe Wakili au kama atakuwa amepewa nguvu kisheria (Power of Attorney).

Kwa hiyo, kuna baadhi ya Mahakama na mabaraza hapa nchini ambapo mtu yeyote anaweza kukuwakilisha au kukusimamia kwenye kesi yako hata kama sio Wakili (mwanasheria).

Pia, mtu ambaye siyo Wakili ataruhusiwa tu kukuwakilisha Mahakamani pale tu atakapo kuwa amepewa nguvu kisheria ya uwakilishi (Power of Attorney) ya kumruhusu yeye kumuwakilisha mhusika kwenye kesi au jambo husika.

Tofauti na hapo mtu ambaye sio Wakili hana locus standi au miguu ya kusimamia Mahakamani na ku i address Mahakama kwa niaba yako.

-----MWISHO----

Disclaimer: Lengo la hii makala ni kutoa elimu kwa jamii. Huu sio ushauri wa kisheria kwa mtu yeyote. Kama unahitaji ushauri wa kisheria wasiliana na Mawakili Wasomi.

Pia natoa angalizo, wale wazee wa kukopi machapisho ya watu na kuweka majina yenu. Ni kosa kisheria. Hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayejimilikisha andiko hili. Unaruhusiwa tu kusambaza lakini usibadili yaliyomo. Ni heri uanze kuandika ya kwako mpya

Mimi mwandishi wa makala hii naitwa Zakaria Maseke - Advocate / Wakili
(0746575259 - WhatsApp).
zakariamaseke@gmail.com
 
Back
Top Bottom