Mshitakiwa aomba kesi iahirishwe akidai akili yake haipo sawa

Suley2019

JF-Expert Member
Oct 7, 2019
1,820
4,572
Mahakama ya Wilaya ya Handeni imelazimika kuahirisha kuwasomea hukumu washtakiwa wawili wa kesi ya unyang'anyi kwa kutumia silaha, Waziri Mohamedi na mwenzake Mohamed Ndumi baada ya mmoja kueleza hajisikii vizuri kiafya, mwingine akidai kuwa akili haiko sawa.

Hukumu hiyo ilipangwa kusomwa leo Aprili 8, 2024 na Hakimu Mkazi, Veronica Siao, aliyesikiliza kesi hiyo, lakini washtakiwa hao wameiomba Mahakama wapangiwe siku nyingine kutokana na sababu hizo za kiafya.

Washtakiwa hao wametoa maelezo hayo baada ya kuulizwa na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Nzagalila Kikwelele iwapo walikuwa tayari kwa ajili ya kusikiliza hukumu yao, lakini kila mmoja kwa nyakati tofauti walieleza hawataweza kuisikiliza kwa kuwa wanajisikia vibaya kiafya.

Mshtakiwa wa kwanza, Waziri, alipoulizwa na wakili Kikwelele kama alikuwa tayari kusikiliza hukumu hiyo, akadai anajisikia vibaya baada ya kuhisi homa wakati kesi hiyo inaendelea mahakamani hapo na kwamba anahitaji dawa ameze, hivyo akaomba hukumu ipangiwa tarehe nyingine.

Kwa upande wake, mshtakiwa wa pili, Mohamed alisema hataweza kusikiliza hukumu hiyo kwa kuwa akili yake haiko sawa, hivyo naye akaomba apangiwe tarehe nyingine, ili kwanza akili yake ikae sawa.

Wakili Kikwelele aliunga mkono maombi yao, akisema kuwa wana haki ya kusikilizwa, hivyo naye akapendekeza hukumu ya kesi hiyo kusogezwa mbele mpaka Aprili 12, mwaka huu.

Hakimu Siao baada ya kusikiliza pande zote, naye aliridhia maombi ya ahirisho la hukumu hiyo na akaahirisha kusoma hukumu yake.

Washitakiwa hao walipandishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Mei 17, 2023, kusomewa mashtaka ya unyang'anyi wa kutumia silaha, wakidaiwa kupora pikipiki yenye thamani ya Sh2.1 milioni katika kijiji cha Kwankonje.
 
Back
Top Bottom