Rutashubanyuma
JF-Expert Member
- Sep 24, 2010
- 219,468
- 911,174
Mwenyekiti wa CCM,Rais Jakaya Mrisho Kikwete.
Mwandishi Wetu
KAMATI Kuu (CC) ya CCM leo inakutana jijini Dar es Salaam, huku chama hicho tawala kikikabiliwa na mtihani wa kutanzua baadhi ya migogoro ya chinichini inayowahusisha baadhi ya makada wake pamoja na matukio makuu ya kisiasa yaliyojitokeza nchini.
CCM katika kikao muhimu cha ambacho ni cha tatu tangu kufanyika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka jana, inatarajiwa pamoja na mambo mengine kujadili hali ya kisiasa nchini.
Kwa mujibu wa Idara ya Itikadi na Uenezi, chama hicho kitakutana chini ya uenyekiti wa Rais Jakaya Kikwete.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ajenda kuu za mkutano huo, ni pamoja na kujadili hali ya kisiasa nchini, maandalizi ya Sherehe za Miaka 37 ya CCM na kupokea taarifa mkutano wa Makatibu Wakuu wa Vyama vya Ukombozi Kusini mwa Afrika.
Mkutano huo ambao CCM iliwakilishwa ulifanyika mjini Luanda, Angola kuanzia Desemba 7 hadi 10 mwaka jana.
Hata hivyo, CCM pamoja na kuweka bayana ajenda hizo, habari za kidadisi za kisiasa ndani ya chama hicho zimeweka bayana mambo mengine yanayoweza kujitokeza katika mjadala wa hali ya kisiasa, ajenda inayopewa umuhimu mkubwa katika kikao hicho CC.
Kwa mujibu wa duru hizo za kidadisi za siasa ndani ya CCM, mambo hayo ni pamoja na kusudio la mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Shinyanga, Hamis Mgeja, kutaka kuwasilisha hoja akimshitaki Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, kutokana na kile alichokiita ni "kukirarua chama nje ya vikao".
Mgeja alitangaza kusudio hilo baada ya Sitta ambaye alikuwa spika wa Bunge la Tisa, kuweka bayana msimamo wake akipinga malipo ya Sh94 bilioni kwa Kampuni ya Dowans.
Sitta ambaye amefungua pazia kwa mawaziri kupinga hadharani mipango inayotiliwa shaka na umma, tofauti na utaratibu wa kawaida wa kulindana serikalini, anatarajiwa kukabiliana na wakati mgumu kutoka kwa makada wenye kuamini katika maslahi ya chama kushika hatamu ya dola.
Duru hizo ziliongeza kwamba, jambo la pili linaloweza kutikisaa chama hicho kwa leo ni pamoja na mvutano wa umeya katika jiji la Arusha.
Katika mvutano huo, CCM mbali ya kuvutana na chama cha upinzani na maaskofu, bado pia makada wake akiwemo Waziri Mkuu aliyejiuzulu Edward Lowassa, alitaka chama hicho tawala kifanye mazungumzo na Chadema.
Ingawa Lowassa si mjumbe wa CC kwa sasa, ajenda hiyo inatarajiwa kuingizwa katika mjadala wa ajenda kuu ya hali ya kisiasa.
Kauli ya Lowassa kutaka suluhu kati ya Chadema na CCM akitahadharisha Arusha kugeuka Ivory Coast, ilipingwa na Katibu Mkuu wake, Yusuph Makamba aliyetaka wapinzani hao waende mahakamani huku kada maarufu, Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais mstaafu mzee Cleopa Msuya, akiunga mkono akisema hakuna haja ya mazungumzo kwani hiyo ni sheria inapaswa kutafsiriwa mahakamani.
Duru hizo ziliongeza kwamba, katika ajenda hiyo ya Arusha CCM inatarajiwa kuangalia athari za udini zilizoanza kujitokeza baada ya baadhi ya mashekhe na maaskofu kupingana, huku chama hicho tawala kikiingia kwenye malumbano na baadhi ya maaskofu.
Katika ajenda hiyo, wadadisi wanaangalia kikao hicho kama muhimu kuangalia vurugu zilizotokea Arusha, hali halisi baada ya vurugu, njia ya kutatua tatizo hilo na nguvu zilizotumiwa kati ya polisi na Chadema.
Wadadisi hao wa siasa ndani ya CCM, wanataja jambo jingine ni pamoja na chama kujitathimini baada ya kupigwa kwenye ngome muhimu za majimbo ikiwemo Nyamagana, Ilemela Mwanza, Maswa Magharibi Shinyanga, Arusha Mjini, Hai, Moshi Mjini, Singida Kusini, Mbeya Mjini, Kawe na Ubungo jijini Dar es Salaam.
Mapema wiki iliyopita akizungumza na gazeti hili, Mzee Msuya alisema chama hivi karibuni kingekaa na kujitathmini namna kilivyotikiswa kwenye ngome zake muhimu za kisiasa.
CCM tangu kuingia madarakani kwa Serikali ya awamu ya nne, kimejikuta kikipigwa na mawimbi mazito yanayotokana na mpasuko kati ya genge la watuhumiwa wa ufisadi na wapambanaji wa ufisadi, ambao wameasi kutoka kundi moja la mtandao baada ya kupingana kimsimamo.