SoC01 Jinsi ya kuanza kujiajiri kwa kutumia internet na mitandao ya kijamii

Stories of Change - 2021 Competition
Jul 14, 2021
10
19
Internet ni mfumo wa dunia wa kielektroniki unaounganisha kompyuta na vifaa vyengine vya kielektroniki vinavyokubali mfumo huo.

Mitandao ya kijamii ni teknolojia inayohusisha kompyuta ambayo hurahisisha kugawana na kusambaza mawazo na taarifa mbalimbali katika kujenga mtandao na jamii halisi.

Internet na mitandao ya kijamii kwa ujumla inaweza kutumika kukuingizia/kukuongezea kipato katika nyanja tofauti tofauti ila nitaongelea kwenye njia ya biashara sana.

Kupitia internet dunia imefanywa kuwa Kijiji hivyo basi ni rahisi kujua soko la nchi na dunia nzima linaendaje kwa mfano ni bidhaa gani inayoongoza kwa kununuliwa sana hapa nchini Tanzania, ni bidhaa gani inayouzwa kwa bei ya chini sana duniani, wapi duniani(nchi) unapoweza kupata bidhaa kwa bei nafuu, jinsi ya kuagiza bidhaa pamoja na kupata utaratibu na kujua makato ya ushuru. Mfano mzuri wa sehemu ambapo watu huagiza bidhaa kwa bei nafuu ni AliExpress ambapo bidhaa nyingi huuzwa kwa bei nafuu ya rejareja na hutumwa kwa njia ya Posta.

Baada ya kujua hayo yote kazi inayofuata ni kutafuta soko kwa ajili ya kuuza bidhaa zako pindi zitakapowasili mikononi mwako. Hapa hatuzungumzii kutafuta fremu za maduka na kuweka bidhaa zako, bali tunazumzia kutafuta majukwaa ya kibiashara mitandaoni pamoja na mitandao mingi ya kijamii. Shukrani kwa utandawazi, majukwaa ya kibiashara mitandaoni hapa nchini Tanzania yamekuwa mengi sana kama vile programu za Kupatana Tanzania, Jiji.co.tz, Zoom Tanzania, Bongodili, na nyengine nyingi. Hivyo hivyo mitandaao ya kijamii pia husaidia kutangaza na kufikia wateja mbalimbali kama makundi ya kibiashara ya Facebook, WhatsApp, akaunti za Instagram na mitandao ya kijamii mengine mingi.

Vitu muhimu vinavyohitajika:

Simu au kifaa chochote cha kielektroniki chenye uwezo wa internet: Hii ni kwa ajili ya kuweza kutengeneza akaunti na kujisajili sehemu ambapo utanunulia(utaagiza) bidhaa nje ya nchi ambapo kwa ushauri wangu ni vyema mtu kama ndio anaanza akatumia AliExpress. Pia simu za kisasa(smartphones) hutumika sana katika kutangaza bidhaa pindi unapohitaji. Mfano bidhaa inabidi zipigwe picha vizuri, zifanyiwe maboresho kama kuongeza mwanga na rangi kwa kutumia programu tofauti tofauti ambazo zitakuwa rahisi ili kuleta mvuto zaidi (mfano wa program hizo ni Collage Maker kwa picha na Filmingo kwa video). Picha na video za bidhaa zinapokuwa teyari inabidi ziwekwe kwenye majukwaa tofauti tofauti ya kibiashara mitandaoni ili uweze kuwafikia wateja wengi zaidi.

Kadi inayoweza kufanya manunuzi ya mitandaoni (Visa/Master Cards): Kadi hizi zinahitajika kwa sababu manunuzi mengi ya mitandaoni ya nje ya nchi huwa yapo katika hela za dola za kimarekani. Hivyo basi kadi hizi huweza kubadili thamani ya fedha za kitanzania (shilingi za kitanzania) kuwa dola za kimarekani. Benki nyingi hapa Tanzania hutoa hizi kadi nakukuwezesha kupata huduma hii. Kwa siku za karibuni hata mitandao ya simu kama Vodacom hutoa huduma hii ya kutengeneza kadi za manunuzi ya mitandaoni (Master Card), japokuwa makato yake huwa juu kidogo ukilinganisha na kadi za benki tofauti tofauti kama Equity Bank (Visa card), NMB Bank (Visa/Master card), CRDB Bank (Visa/Master card), na benki nyengine nyingi.

Sanduku la Posta: moja ya vitu vinavyohitajika ili AliExpress waweze kukutumia bidhaa uliyoinunua ni sanduku la posta ambalo lipo hai mfano P.O. Box 20199 – Dar es Salam. Hii ni kuweza kukurahisishia bidhaa yako iweze kusafirishwa kiurahisi kwenda kwenye ofisi ya Posta ya mahala ulipo.

Kitambulisho cha taifa/kura au pasipoti ya kusafiria: Pindi bidhaa uliyoiagiza inapowasili katika ofisi ya Posta ya mahali ulipo, ofisi ya Posta ya mahali husika hutuma ujumbe katika simu ili uweze kufika ukiwa na kitu kimojawapo tajwa hapo juu kuthibitisha utambulisho wako na uweza kuchukua bidhaa(mzigo) yako.
Kama ilivyo kawaida kila kitu huwa na faida, hasara(changamoto) na njia za kupambana/kutatua changamoto zinazojitokeza.

Faida

1.
Mtaji ndogo wa biashara: Kwa kuwa biashaara hii hujikita kwenye mtandao, hakuna haja ya kuwa na sehemu(fremu) ya biashara ambayo huongeza gharama nyingi kama vile kodi ya pango, kodi nyengine ya TRA ambayo ingeweza kulipwa mara moja tu pindi mzigo ulipochukuliwa Posta, bili za matumizi (utility bills), n.k. Juu ya hapo bidhaa nyingi nje ya nchi hasa bidhaa za kielektroniki huuzwa kwa bei nafuu ambapo hua ghali hapa nchini mfano spika za masikio zisizotumia waya (wireless earbuds/earphones) hugharimu takribani shilingi elfu kumi za kitanzania (10,000/=) ukijumuisha gharama zote ikiwemo TRA na Posta ila hapa nchini huuzwa shilingi elfu thelathini hadi hamsini (30,000/= - 50,000/=) za kitanzania ambapo faida hua nzuri.

2. Urahisi wa uangalizi na usimamizi wa biashara: Kwa kua biashara hii ni ya kielekroniki zaidi haichukui muda mwingi wa mtu kwa kuwa inahitaji tu kuagiza bidhaa nje ya nchi, kwenda kuzichukua ofisi za posta zinapofika na kutangaza katika mitandao ya kijamii au program za kibiashara kupata wateja. Ukiangalia kimakini biashara hii haihitaji kuchukua masaa zaidi ya 12 kwa siku na huweza kuendesha biashara hii bila kuharibu ratiba ya shughuli nyengine kama vile masomo(kwa wanavyuo) au kazini(kwa waajiriwa) kwani bishara nzima huendeshwa sehemu na wakati wowote kutegemea na ratiba ya mtu husika.

3. Muendano wa biashara na hali ya sasa ya utandawazi: Hii ni karne ya 21, hivyo basi watu wengi sasa huama kutoka kwenye mfumo wa kianalogia kwenda kidigitali ambapo vifaa vya kielektroniki vipo kwa wingi. Hivyo basi, manunuzi mengi ya bidhaa tofauti tofauti hufanywa mitandaoni na sio lazima mtu kwenda sehemu husika kutafuta bidhaa anazohitaji. Hii hufanya biashara za mitandaoni kukua sikua hadi siku na kwa kasi kubwa.

4. Kuwafikia watu wenye hadhi zote: Si rahisi kwa watu wenye hadhi kubwa kwenda madukani hasa ya kawaida, hivyo basi kwa kutumia mitandao ya kijamii na program za kibiashara huweza kuwafikia watu wa hadhi zote kama watu wa maofisini mbalimbali, watu wa nje ya nchi, wafanyakazi wakubwa wa serekalini na wengine wengi ili kuweza kuuza bidhaa zako.

Changamoto

1.
Ili kuweza kusimamia vizuri biashara hii ya mitandaoni unapaswa kuwa na simu ya mkononi ya kisasa au kifaa chochote cha kielektroniki chenye kukubali internet pamoja na kuwa na huduma ya internent kwani inakupasa kununua bidhaa mitandaoni na kutangaza matangazo ya biashara/bidhaa yako kwenye mitandao tofauti tofauti ya kijamii ili matangazo ya bidhaa zako yawafikie hadhara na walengwa.

2. Utapeli: Kadri siku zinavyoenda biashara za mitandaoni hukua na kujulikana na watu tofauti tofauti, hivyo basi hata matapeli hutumia njia hii kuwatapeli wafanyabiashara wa mitandaoni kwa mfano kutuma message ya muhamala hewa, wizi wa nguvu au akili zaidi na njia nyengine nyingi matapeli hao wanazozijua na kuzitumia.

3. Ushindani mkubwa wa kibiashara: Jinsi biashara za mitandaoni zinavyokuwa na kujulikana kwa watu ndivyo hivyo hivyo ushindani unavyokuwa mkubwa katika bidhaa tofauti tofauti. Mfano ndani ya mtandao mmoja wa kijamii au programu/majukwaa ya kibiashara mitandaoni unaweza ukakuta bidhaa zaidi ya 10 za aina moja.

4. Bidhaa kutokufika kwa wakati au kutokufika kabisa: Hii hutokana na aina/njia ya kusafirisha mzigo ambayo muuzaji aliyekuuzia bidhaa ametumia. Kama muuzaji atatutumia njia ya mizigo iliyosajiliwa (registered parcels) inakuwa ni rahisi na haraka kidogo kwani hutumia siku 14 hadi 21 mzigo kufika nchini na inakua rahisi kuufatilia mtandaoni mzigo wako umefikia sehemu gani katika kusafirishwa. Endapo muuzaji atatumia njia nyenyine ya mizigo isiyosajiliwa (unregistered parcels) basi huwa ni vigumu kwani wakati mwengine huchukua muda mrefiu kuwasili nchini na huwezi kuifuatilia (tracking) mitandaoni na mara nyingine isiweze kuwasili kabisa nchini.

5. Bidhaa zenye kasoro/dosari: Wakati mwengine bidhaa zinazowasili huwa zina mapungufu kama vile ubovu, upungufu wa ubora, idadi pungufu na iliyoagizwa, bidhaa tofauti na iliyoagizwa, n.k. Hii ni kwa sababu manunuzi ya bidhaa za mitandaoni sana sana nje ya nchi hakuna nafasi ya kuchunguza bidhaa kabla ya kununua.

Njia za kutatua changamoto

1. Ushindani mkubwa wa kibiashara:
Kabla ya kuagiza bidhaa husika, pitia mitandaoni kuona wafanyabiashara wa bidhaa kama hiyo husika wanatumia mbinu gani kwa mfano picha zao za bidhaa wanazotangazia zipoje, huduma zao wanatoaje, bidhaa zao wanaziuzaje n.k. Hii husaidia kuona mapungufu yao na kuyafanyia kazi ili kuwa faida kwako katika biashara na kuwa hatua kadhaa mbele yao.

2. Utapeli: Kwenye uagizaji wa bidhaa, manunuzi na malipo ya bidhaa yasifanywe nje ya jukwaa/programu husika ya manunuzi kwa mfano, kwenye AliExpress lipia ndani ya AliExpress, Alibaba lipia kwa Alibaba payment na Ebay lipia ndani ya Ebay. Kwa kuuza, usikubali kutuma mzigo kwanza halafu malipo baadae, kwa wateja wa mara ya kwanza usikubali malipo yoyote ya kimtandao(electronic money transfer), usikubali biashara kufanyika mida ya usiku na mwisho wa yote ni vizuri kufanya biashara uso kwa uso na si vingine.

3. Bidhaa kutokufika kwa wakati au kutokufika kabisa: Kabla ya kununua bidhaa ni vyema kufanya uchunguzi juu ya bidhaa hiyo kutafuta wauzaji tofauti toauti wanaouza bidhaa hiyo hiyo ili kuweza kuchagu ni muuzaji yupi mwenye bidhaa bei nafuu na mwenye mawasiliano mazuri ili akueleze anatumia njia gani ya kusafirisha mizigo na itatumia muda gani paka mzigo kuwasili. Hata hivyo ni vyema kuwa una fuatilia mzigo wa bidhaa yako ilipofika(tracking) ili kuweza kujua mahala ulipofika. Hii itasaidia kama mzigo usipowasili ndani ya mda ule uliokadiriwa kuweza kufungua mashtaka ili kuweza kurudishiwa hela yako.

4. Bidhaa zenye kasoro/dosari: Ni vyema kwa kila mzigo wa bidhaa unapowasili kuweza kukagua kila bidhaa ili kuweza kujua kama bidhaa zimefika kwa idadi sawa na hakuna dosari yoyote katika ubora wa kila aina ya bidhaa zilizoagizwa ila kama kukiwa na mapungufu uweze kufungua mashtaka ili uweze kurudishiwa hela yako.

Hitimisho
Kama ilivyo kawaida siku zote jitihada hazizidi kudra, mtangulize kwanza mwenyezi Mungu katika kila kitu unachokifanya na fanya kazi kwa bidii, matokeo mazuri yenye manufaa yataonekana kwenye kila kazi utakayofanya.
ASANTENI

Screenshot_20210723-180538.jpg


Screenshot_20210723-180913.jpg


Screenshot_20210723-181143.jpg


Screenshot_20210723-181157.jpg


Screenshot_20210723-181212.jpg
 
Back
Top Bottom