Hofu ya bajeti kukwama yatanda

dosama

JF-Expert Member
Dec 25, 2010
912
957
KAMATI YA UONGOZI YA BUNGE YAKUTANA NA WAZIRI WA FEDHA

HOFU imetanda mjini Dodoma juu ya kuwapo kwa uwezekano wa kukwama kwa Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2012/13 inayotarajiwa kuwasilishwa Bungeni keshokutwa na Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa.

Dk Ngimwa atawasilisha bajeti ambayo alilazimika kuifumua upya baada ya kuteuliwa kuchukua nafasi hiyo baada ya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyofanywa mapema mwezi uliopita na Rais Jakaya Kikwete na kumweka nje ya aliyekuwa akiongoza wizara hiyo, Mustafa Mkulo.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda jana alinukuliwa akizungumza katika kikao cha kutoa mwongozo kwa wabunge wote (briefing) kwamba Dk Mgimwa aliomba ridhaa ya Rais kufumua bajeti hiyo upya ili iweze kwenda sawa na mtizamo wake kama kiongozi wa wizara, hali iliyosababisha kuchelewa kwa vitabu vya bajeti kwani baadhi viliandaliwa upya.

Pinda alikuwa akijibu hoja za wabunge wa Serengeti (CCM) Dk Steven Kebwe, Mbunge wa Nzega (CCM), Dk Hamis Kigwangallah na Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Pauline Gekul ambao kwa nyakati tofauti walihoji sababu ya kuchelewa kwa vitabu vya bajeti kinyume cha Kanuni za Bunge, hali iliyowanyima fursa ya kuijadili kwa kina.

Hata hivyo, jitihada hizo za Dk Mgimwa zinaonekana kutowaridhisha wabunge ambao katika vikao vya kamati waliyakataa mapendekezo ya bajeti nyingi kutokana na upungufu wa kutozingatiwa kwa vipaumbele.

"Kwamba bajeti itapata wakati mgumu hilo halina ubishi licha ya kwamba wabunge wa CCM tunabanwa na kanuni ya ‘three lines whip,' si unajua ukikataa kuunga mkono bajeti unaweza kupoteza ubunge wako? Lakini kwa ujumla hali ni ngumu sana," alisema mmoja wa wabunge wa CCM kutoka mikoa ya Kanda ya Magharibi.

Jana jioni Kamati ya Uongozi ya Bunge ikiongozwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda; Waziri Mkuu, Pinda; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi ilikuta na Mgimwa "kuweka mambo sawa" kabla ya bajeti kuwasilishwa Bungeni.

Habari kutoka ndani ya kikao hicho zinasema miongoni mwa ajenda kuu zilikuwa ni mjadala kuhusu bajeti zilizokataliwa na Kamati za Bunge ikiwamo Bajeti kuu ya Serikali ambayo ilikataliwa na Kamati ya Fedha na Uchumi kutokana na kutotengwa kwa fedha za kutosha kwa ajili ya shughuli za maendeleo.

Ratiba ya vikao vya Bunge la bajeti inaonyesha kuwa kamati za wabunge za vyama zinakutana leo baada ya kipiondi cha maswali na majibu. Masikio yote yataelekezwa ndani kamati ya CCM ambako kunatabiriwa kuwapo kwa mvutano kabla ya kuwa na msimamo wa pamoja wa kuunga mkono Bajeti.
Baadhi ya wabunge wakiwamo wa CCM nao wameonyesha msimamo wa kuikataa wakitilia shaka kama itakidhi mahitaji ya wananchi, hasa kupunguza makali ya maisha.

Walisema Bajeti hiyo ya Sh15 trilioni huenda isilete matumaini kutokana na ile ya mwaka 2011/12 kushindwa kuonyesha tija.

Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola alisema walitarajia bajeti ya mwaka huu itaongeza fedha katika kukabiliana na sekta za elimu, afya na kilimo lakini matokeo yake fedha zimeendelea kupunguzwa.

"Walimu bado wanadai mabilioni ya fedha, mikopo elimu ya juu bado ni tatizo, kilimo chetu hakikidhi na hivyo kukosekana uhakika wa chakula katika maeneo mengi sasa badala ya bajeti kuongezwa inapungua," alisema Lugola.

Mbunge wa Ludewa (CCM), Deo Filikunjombe alisema Watanzania wasitegemee jipya katika Bajeti ijayo. Alisema Bunge litatenga fedha katika kila sekta lakini, tatizo ni kufika zilikotengwa na kusaidia maendeleo ya Watanzania na kukuza uchumi wa nchi.

Mbunge wa Arumeru Mashariki(Chadema), Joshua Nassari alisema Watanzania wasitegemee jipya katika Bajeti ijayo kwani ni ya madeni… "Bajeti hii mimi naiita ni ya madeni, kwani katika wizara kama ujenzi, kiasi kikubwa fedha kimetengwa kulipia miradi ambayo tayari imeanza."

Kamati ya Bunge
Juzi, Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi, inayoongozwa na Andrew Chenge ilimtaka Dk Mgimwa kuongeza bajeti hiyo au asubiri ikataliwe itakapofikishwa Bungeni.

Hatua hiyo inakuja baada ya waziri huyo kuwasilisha Bajeti iliyoonyesha kuwa Bajeti ya Maendeleo ni Sh4.5 trilioni.

Mabadiliko ambayo kamati ilishauri ni Bajeti ya Maendeleo iwe asilimia 35 na matumizi ya kawaida yawe asilimia 65, tofauti na mgawo wa asilimia 30 kwa 70 kama ilivyokuwa.
Hata hivyo, Dk Mgimwa amegoma kuongeza Bajeti ya Maendeleo badala yake amekwenda kuieleza kamati hiyo sababu za kuweka viwango hivyo.

Alisema matumizi ya kawaida yamezingatia mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2011/2012, ambayo ni shughuli zisizoepukika, stahili mbalimbali za utumishi, Mfuko Mkuu wa Serikali ambao umeongezeka kutoka Sh2.102 trilioni hadi Sh2.745 trilioni, mwaka 2012/2013.
Alipoulizwa kuhusu kamati kukataa taarifa hiyo, Chenge alijibu: "Hapa bado tunaendelea na mjadala, utasemaje tumekataa taarifa?"

Waziri Kivuli wa Fedha, Zitto Kabwe alisema kutokana na wizara kushindwa kutekeleza ushauri wa kamati, watakwenda kuikwamisha Bungeni.

Wadau wengine
Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba alisema tatizo la Bajeti liko katika utekelezaji: "Tunaitaka Serikali kuhakikisha kuwa fedha zilizotengwa zinatumika kama ilivyokusudiwa ili kuondoa kero mbalimbali zilizopo."

Alisema mwaka jana, Serikali ilikuwa haina fedha jambo ambalo lilisababisha Bajeti yake ya mwaka 2011/12 ya Sh trilioni 13 kushindwa kutekelezeka kama ilivyokusudiwa.
Mukoba alisema kutokana na hali hiyo, Serikali inapaswa kuhakikisha kuwa vipaumbele vilivyotangazwa vinatekelezwa.

Mkurugenzi wa Utafiti wa Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI), Hussein Kamote alisema mwaka jana Serikali iliweka kipaumbele kwenye sekta ya nishati, lakini suala la umeme bado ni tatizo jambo ambalo limesababisha viwanda vingi kushindwa kufanya kazi.
Alisema kutokana na hali hiyo, Serikali inapaswa kuhakikisha kuwa changamoto zinazojitokeza kwenye sekta hiyo zinatekelezwa ipasavyo.

Ofisa wa Mipango ya Utafiti na Uchambuzi wa Sera wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Gloria Shechambo alisema mpango wa bajeti ya miaka mitano ulioanza kutumika mwaka jana ambao mwaka huu ni mwaka wake wa pili wa fedha, umewapa kipaumbele wakulima wakubwa huku ikiwasahau wadogo.
"Serikali iangalie wakulima wadogo wanaotumia nguvu nyingi, kwani kwa kipindi kirefu wanawaangalia wakulima wakubwa pekee jambo ambalo siyo la haki," alisema Shechambo.

Aliongeza kwamba, uchumi wa nchi hauwezi kuongezeka kama mahitaji ya msingi ya watu hayajafikiwa kwa sababu watu hawawezi kushiriki kukuza uchumi wa nchi kama hawapati mahitaji yao ya msingi.
Umoja wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Tanzania (Tahiliso), umesema moja ya changamoto ya kushughulikiwa katika bajeti ya mwaka huu ni kupungua kwa wanafunzi wanaopata mikopo kila mwaka.

Rais wa Tahiliso, Paul Makonda alisema wakati makadirio ya mwaka jana yalikuwa ni kuwapa mikopo wanafunzi 40,000 kila mwaka, hali imekuwa tofauti na idadi yao imekuwa ikipungua.
"Ilishuka kutoka wanafunzi 40,000 mpaka 28,000 mwaka juzi na sasa mwaka huu unaoisha imekuwa 23,000."

Rais wa Chama Cha Madaktari (MAT), Dk Namala Mkopi alisema bajeti inayokuja haitakuwa na kipya kutokana na Serikali kutokuwa na vipaumbele ambavyo inavitekeleza.
Dk Mkopi alisema sekta ya afya imekuwa ikiyumbayumba na Serikali haijaonyesha jitihada za makusudi kuhakikisha wananchi wanapata huduma iliyo bora.

"Kila mwaka tunatapatapa na bajeti na hakuna jipya katika sekta ya afya ambako kumekuwa na matatizo kibao, wahudumu wa afya bado hawathaminiwi kwa kusikilizwa kwa wakati."

Wiki iliyopita, Serikali iliwasilisha mwelekeo Bajeti ya mwaka 2012/13, ikionyesha vipaumbele saba ambavyo ni pamoja na miundombinu ambayo imegawanyika katika makundi hayo manne yakiwemo reli, umeme, majisafi na salama, usafirishaji na uchukuzi ambazo kwa ujumla zimetengewa kiasi cha Sh4.5 trilioni.

Vipaumbele vingine ni pamoja na kilimo, viwanda, rasilimali watu, huduma za jamii, utalii, biashara ndani na nje ya nchi pamoja na huduma za kifedha.

Source: Mwananchi

Concern: Na ikwame coz ni changa la macho hakuna hela
 
tusubiri tuone wazalendo ila kweli inaonekana haikidhi mahitaji ya kujikomboa, inatakiwa ikite kwenye maendeleo zaidi ya kilimo, elimu, afya, etc. hizi sector ni muhimu na ndizo zaweza kututoa tulipo na kutuweka pazuri au kutudidimiza zaidi tusipoziimalisha zaidi
 
Back
Top Bottom