Historia Zilizojificha Katika Karatasi za Barua

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
21,056
30,395
HISTORIA ZILIZOJIFICHA KATIKA KARATASI ZA BARUA

Picha ya kwanza hapo chini ni Mamboleo Rashid Makoko, picha ya pili ni Julius Nyerere na ya tatu ni Chief Michael Lukumbuzya wa Ukerewe.

Historia za watu hawa watatu zote zinaunganishwa na historia ya Tanganyika kama ilivyokuwa wakati ikielekea kwenye mabadiko makubwa ya siasa mwaka 1950.

Mamboleo Makoko ni mtoto wa Rashid Makoko mzalendo maarufu Tanga na mmoja wa wazee waliokuwa mstari wa mbele katika TANU mjini Tanga.

Rashid Makoko alifungwa Jela ya Maweni, Tanga mwaka wa 1958 kwa kosa la kuwaandikisha Waafrika wasio na sifa kupiga kura katika Uchaguzi wa Kura Tatu.

Kifungo hiki kiliharakisha kifo chake alipofunguliwa.

Jina lake limepewa barabara Ngamiani Tanga.

Kuna picha zimetundikwa Patwa Restaurant Tanga ambako yuko Julius Nyerere, Sadiki Patwa (Muasia tajiri aliyekuwa na mtambo wa soda), Rashid Makoko na mwanae Mamboleo, Makata Mwinyi Mtwana, (Mwafrika tajiri na amfanyabishara mkubwa wa kuuza khanga).

Kabla ya uhuru Mamboleo Makoko aliondoka Tanganyika kwenda masomoni Uingereza na hakurudi ila kuja kuzikwa kwao Tanga.

Ally Sykes amehifadhi barua alizokuwa akiandikiwa na Mamboleo toka miaka ya 1950 hadi unapatikana uhuru.

Nimejaaliwa kuzisoma barua hizi.

Natamani kama barua hizi siku moja zingechapwa watu waelewe jinsi wasomi wa wakati ule waliitazamaje Tanganyika na walikuwa na matumaini yapi na Tanganyika huru.

Mamboleo alikuwa bingwa wa lugha ya Kiingereza msomaji utapenda kumsoma na hutochoshwa na kalamu yake.

Mamboleo Makoko kaandika mengi sana kuhusu uongozi wa Rais wa TANU Julius Nyerere na hali ya baadae ya chama uhuru utakapopatikana.

Makoko alitabiri baadhi ya mambo na yakatokea sawia.

Chief Michael Lukumbuzya akirejea likizo kutoka Makerere alipanda meli moja na Abdul Sykes mwanzoni miaka ya 1950s.

Abdul Sykes alikuwa anakwenda Nansio kwa Hamza Mwapachu na Michael Lukumbuzya anarejea kwao likizo.

Wote wawili walipanda meli Mwanza.

Abdul Sykes alikuwa kafuatana na mkewe Bi. Mwamvua bint Mrisho, maarufu kwa jina la Mama Daisy.

Kilichomshangaza Lukumbuzya meli iliposhusha nanga Nansio ilikuwa kukuta ngoma za Kikerewe bandarini kumpokea Abdul Sykes kiongozi wa TAA.

Hii ilikuwa mipango ya Hamza Mwapachu ambayo hata Abdul Sykes mwenyewe alishangaa.

Abdul Sykes alikuwa amekwenda Nansio kwa Hamza Mwapachu kuomba ushauri nini kifanyike TAA HQ New Street baada ya viongozi wote wa juu kuondolewa Dar-es-Salaam na Gavana Edward Francis Twining na kupelekwa majimboni.

Chief Lukumbuzya baada ya haya aliyoshuhudia pale kwao bandarini Nansio akawa kila akija Dar es Salaam atakwenda nyumbani kwa Abdul Sykes kumsalimia kama walivyokuwa wakifanya machifu wote.

1714509302439.png

 
Sh Mohamed
Hakika historia nzuri,
Mwenyeezi Mungu awasamehe makosa yao waliotangulia pia Mwenyeezi Mungu akuzidishie elimu
Ahsante
 
Back
Top Bottom