Hii ni CCM ya mwendo kasi

kalulukalunde

JF-Expert Member
May 27, 2016
1,056
1,083
KATIKA kile kilichodhihirisha kwamba Rais John Magufuli ni muwazi na hana tabia ya kuficha kile anachokiamini, Jumamosi alituma salamu kwa wana- CCM kuhusu namna CCM atakayoiongoza itakavyokuwa.

Baadhi ya maneno yalihitaji mtu asiye na uoga kuyatamka hadharani, mbele ya watu ambao muda mfupi tu wamekuchagua kuwa Mwenyekiti wao. Maneno hayo ni kama vile kusema baadhi ya vyeo, kama vile nafasi za makanda wa vijana ambao wengi wanaochaguliwa ni watu wenye fedha anafikiria hazina tija katika chama. Mwenyekiti mpya wa CCM ameahidi kusimamia kikamilifu miongozo aliyopewa hadharani na Mwenyekiti mstaafu wa CCM, Jakaya Kikwete.

Miongozo hiyo ni pamoja na Katiba ya CCM na Kanuni za uongozi za chama hicho. “Nitasimamia kanuni, maadili ya chama ukurasa kwa ukurasa, kifungu kwa kifungu, kipengele kwa kipengele ili kuhakikisha CCM inazidi kuaminiwa na Watanzania,” anasema. Pamoja na mafanikio mengi ambayo anasema CCM imepata huko nyuma, Magufuli anasema haipaswi kubweteka bali kujitahidi ili kuwaletea Watanzania maendeleo zaidi na zaidi.

Anawakumbusha wana-CCM wenzake moja ya azimio la mkutano mkuu wa Taifa ulioketi Januari 21, mwaka 1977 katika kuelekea kuunganisha Tanu na Afroshirazi akimaanisha kwamba litakuwa moja ya dira yake kubwa katika uongozi wake.

Azimio hilo linasema: “Chama tunachokiunda tunataka kiwe chombo madhubuti katika muundo wake na hasa katika fikra zake na vitendo vya kimapinduzi vya kutupilia mbali aina zote za unyonyaji, kupambana na jaribio lolote lile la mtu kumuonea mtu, au shirika au chombo cha nchi, kuonea na kudhalilisha wananchi, kudhoofisha uchumi au kuzorotesha maendeleo ya taifa.”

Mwenyekiti wa CCM anasema bado Tanzania ina changamoto za umasikini, ukosefu wa ajira na kwamba vitendo vya dhulma, ufisadi, rushwa, ubadhirifu wa mali za umma unaendelea nchini mwetu kinyume na azimio hilo la kuundwa kwa CCM. Ni kutokana na hali hiyo, Magufuli anasema huduma bora zaidi za kijamii ikiwemo elimu, afya, maji na umeme zimeendelea kukosekana.

Hivyo anasema CCM aliyoanza kuiongoza tangu Jumamosi haina budi kujipanga na kuhakikisha inatatua changamoto hizo. Anasema CCM ikishindwa kukubaliana na changamoto hizo itapoteza mvuto kwa wananchi kwani watashindwa kuendelea kuiamini. Magufuli anaamini kwamba, Tanzania imara na yenye mafanikio inawategemea wana-CCM ambao ndio waliopewa na wananchi jukumu la kuongoza nchi.

Anasema atashirikiana na viongozi, watendaji wa ngazi zote ili kuhakikisha chama kinakuwa imara zaidi, kikienda sambamba na hali ya sasa bila kuathiri misingi iliyowekwa na waasisi wa chama hicho, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Abeid Amaan Karume. Mambo mahususi atakayofanya La kwanza kabisa anasema ataimarisha utendaji kazi wa CCM ili kuhakikisha inakuwa na uwezo wa kusimamia vizuri serikali kwani kama alivyosema Mwalimu Nyerere, chama legelege, huzaa serikali legelege na yeye hataki kuona hilo linatokea katika uongozi wake.

“Ikiwezekana tutapitia upya katiba, taratibu na kanuni za CCM na kuzifanya ziendane na hali ya sasa ili kuweza kuwatumikia vyema wananchi,” anasema. Namna ya kuimarisha utendaji madhubuti wa CCM, Magufuli anasema atahakikisha CCM inakuwa na safu bora ya uongozi, kuanzia shina hadi taifa.

“Hivyo kuna haja ya kuangalia muundo wa uongozi wa ngazi mbalimbali na kuondoa vyeo visivyo na tija katika chama hasa wakati huu. Kwa mfano, ni kweli tunahitaji chipukizi katika uongozi wa CCM? “Je, bado kuna umuhimu wa makamanda wa vijana ambapo wengi wanaopewa nafasi hizo ni wale wenye pesa?.... Washauri ndani ya Jumuiya ya Wazazi bado wanahitajika?

Vyeo hivi vinawasaidiaje wananchi kutatua kero zao au ni vyanzo vya migogoro ndani ya chama na hasa chaguzi zinavyokaribia?” Anahoji na kusema hayo ni mawazo yake lakini yatabadilishwa na CCM ikiona yana uzito. Katika muktadha huo, Mwenyekiti huyo mpya wa CCM anapania kupunguza tabia ya mtu mmoja kurundikiwa vyeo, hali ambayo inawapunguzia wana-CCM wengine kushika vyeo na hivyo kuonekana vipaji vyao vya uongozi.

Kingine atakachomulika katika uongozi wake Magufuli anasema ni kuimarisha jumuiya za chama kwa maana ya Jumuiya ya Vijana, Wanawake na Wazazi. Hilo anaamini litafanikiwa kwa kuweka safu za watendaji wenye sifa zinazohitajika katika kipindi cha sasa. CCM ya Magufuli itaona maslahi ya watendaji wa chama hicho yakiboreshwa pia kwani mwenyekiti huyo anasema hatopenda kuona watendaji wanakuwa ombaomba.

Anasema kwa bahati nzuri CCM ina rasilimali nyingi hivyo atatahakikisha rasilimali hizo zinatumika kwa manufaa ya chama. “Kikosi kazi kitaundwa kuhakiki mali zote za chama ili kujua zinatumikaje na akina nani wanazitumia na mapato yanayoingia kwa chama. Hivyo mali zote za chama zitaorodheshwa,” anasema na kuongeza. “Tunataka CCM ya kuchapa kazi, isiyo ombaomba wala kutegemea wafadhili.”

Wakati Mwenyekiti wa CCM aliyestaafu punde, Jakaya Kikwete akikiri kwamba kuna tatizo la wana-CCM kulipa ada za uanachama, Magufuli anasema hilo litakuwa moja ya mikakati yake, yaani kuhakikisha kwamba wanachama wanahimizwa na kuona umuhimu wa kulipa ada zao za mwaka kwa ajili ya kusukuma maendeleo ya chama. Ili kurahisisha jambo hilo anasema uongozi wake utaanzisha ulipaji wa ada kwa njia za kielektroniki.

Mkakati mwingine katika uongozi wake Magufuli anasema ni kuongeza idadi ya wanachama, wapenzi na mashabiki kwani anaamini kuwa siasa ni mchezo wa idadi (namba). Kwa sasa CCM inakadiriwa kuwa na wanachama milioni 8.7. Namna nzuri ya kuvuta watu kujiunga na CCM, Magufuli anasema, ni wana-CCM kutekeleza ahadi zao kwa kuhakikisha wanakuwa mfano bora na wa kuigwa katika jamii kwa maneno na vitendo.

Kukomesha rushwa Lingine atakalolisimamia kwa nguvu zake zote Mwenyekiti huyo mpya anasema ni kuzidisha mapambano dhidi ya rushwa, ufisadi na kukosekana kwa maadili ya uongozi ndani ya CCM. Magufuli anasema Katiba ya Nchi Ibara ya 9 (h) na Ibara 132 (5) C vinakataza rushwa. Pia anasema ahadi ya 3 ya mwana-CCM inasema ‘sintopokea wala kutoa rushwa’.

Kadhalika anasema kifungu namba 18 (b) cha Katiba ya CCM kinasema kwamba ni mwiko kiongozi kupokea mapato ya kificho, kutoa au kupokea rushwa. “Cha kusikitisha ni kwamba CCM ni miongoni mwa taasisi ambazo zina tatizo la rushwa,” anasema na kuongeza kwamba alipogombea urais aliona rushwa waziwazi na pia anakiri kwamba kama CCM isingekuwa imara, yeye asingekuwa rais kwani yeye hakutoa rushwa ili kupitishwa lakini kuna waliotoa rushwa za waziwazi ili kuhakikisha wanakuwa wagombea urais wa chama hicho.

“Nilikwenda Iringa kutafuta wadhamini lakini wilaya yote walikuwa wameshanunuliwa, ikabidi nisafiri kwenda ndani kwenye kata kutafuta wadhamini!” Anasema. Magufuli anakiri kwamba rushwa imekuwa ikiathiri sana maendeleo ya CCM na hasa nyakati za uchaguzi, kwani mara nyingine fedha ndiyo imekuwa kigezo cha mtu kupata uongozi badala ya uwezo wake. Kwamba wale ambao wana uwezo wa uongozi lakini hawana uwezo wa kifedha hawapati nafasi au wakipata basi ni kwa shida sana.

Anasema wakati mwingine CCM imepoteza jimbo kwa sababu ya kulazimisha mwenye pesa agombee ubunge au udiwani badala ya mtu anayekubalika na wananchi kutokana na uadilifu na uwezo wake. “Hatuwezi (katika CCM) kuondoa rushwa kama sisi wenyewe tutakuwa tunaikumbatia,” anasema. Ndipo kiongozi huyo mpya wa CCM ananadi: “Nimedhamiria katika uongozi wangu ndani ya CCM kukomesha tatizo la rushwa.

Yeyote atakayetumia rushwa, ajue hatochaguliwa na wala hatopitishwa kugombea nafasi za uongozi. Lazima ukichaguliwa ukawe mtumishi wa watu na siyo mtumishi wa pesa zilizokupa madaraka. Na hapo ndipo tutajibu kero na hoja za Watanzania.” Katika muktadha huohuo, Magufuli anawataka wana-CCM wenzake katika uchaguzi wa viongozi mwaka kesho wakahakikishe wanajiepusha na vitendo vya rushwa ikiwemo kukusanya michango na zawadi, kununua kadi za wanachama, kuanza kampeni kabla ya muda, kutoa takrima na kadhalika.

“Atakayefanya hivyo, chini ya uongozi wangu, chama hakitamuonea aibu wala huruma,” anaweka wazi na kuongeza: Usaliti ndani ya chama Lingine analoahidi kulivalia njuga mwenyekiti huyo mpya wa CCM ni kuhakikisha anakomesha usaliti ndani ya chama. “Katika uongozi wangu, sitaruhusu mtu asubuhi yuko CCM jioni yuko Chaema au chama kingine cha upinzani. Wenye tabia hiyo watubu kuanzia sasa au watupishe. Heri kukaa na mchawi kuliko kukaa na msaliti. Hatutaki CCM maslahi wala ndumila kuwili,” anasema.

'NUKUU MUHIMU

NAWAOMBA sana ndugu wajumbe, mniombee nipate angalau nusu ya moyo wa uvumilivu alionao bwana Kikwete - JPM.

Maisha ni mzunguko, usimuudhi sana mwenzako, mtakuja kukutana sehemu ukamuonea aibu - JK.

Nitasimamia kanuni, maadili ya chama ukurasa kwa ukurasa, kifungu kwa kifungu, kipengele kwa kipengele ili kuhakikisha CCM inazidi kuaminiwa na Watanzania -JPM.

CCM inatoka mikononi mwa kada anayekataa ufisadi kiasi cha kumtosa rafiki yake Lowassa na kwenda kwa kada mwasisi wa mahakama ya mafisadi - Yusuph Makamba.

Viongozi wa CCM hawatoki kwenda kwa wananchi lakini watani zetu wanakwenda… Tusipokwenda kwa watu, wakati wa uchaguzi tunalazimika kutumia nguvu kubwa kupata ushindi - JK.

Siyo kinachowekwa benki ni fedha tu. Hata uongo unawekwa akiba lakini wapinzani wanamaliza uongo wote... Sasa nawambia wapinzani, Jakaya aliwabatiza kwa maji, Magufuli atawabatiza kwa moto - Yusufu Makamba.

Chama Cha Mapinduzi ni kigumu kuking’oa, huwezi ukakiondoa kwa kususia vikao vya Bunge. Siasa ambazo utaeleza kwa wananchi lazima ziwe za ukomavu - John Cheyo.

Ukitaka kuepuka nzi lazima utupe kibudu. CCM iliwaondoa wale waliokuwa wanaleta harufu mbaya kwenye CCM... Unapohitaji kumchinja kobe unahitaji ‘timing’ na CCM ilifanya ‘timing’. -Fredy Mpendazoe.

CCM ikishindwa kukubaliana na changamoto hizo (huduma na maisha bora kwa Watanzania) itapoteza mvuto kwa wananchi kwani watashindwa kuendelea kuiamini - JPM.

Kuna haja ya kuangalia muundo wa uongozi wa ngazi mbalimbali na kuondoa vyeo visivyo na tija katika chama hasa wakati huu. Kwa mfano, ni kweli tunahitaji chipukizi katika uongozi wa CCM - JPM.

Hatuwezi (katika CCM) kuondoa rushwa kama sisi wenyewe tutakuwa tunaikumbatia... Atakayefanya hivyo (kununua uongozi), chini ya uongozi wangu, chama hakitamuonea aibu wala huruma - JPM.

Katika uongozi wangu, sitaruhusu mtu asubuhi yuko CCM jioni yuko Chadema au chama kingine cha upinzani. Wenye tabia hiyo watubu kuanzia sasa au watupishe - JPM.
 
Back
Top Bottom