Hadithi ya Ali Wawili: Ali Hassan Mwinyi na Ally Kleist Sykes

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,921
30,264
HADITHI YA ALI WAWILI: ALI HASSAN MWINYI NA ALLY KLEIST SYKES

Majina yao yamefanana mtu na somo yake ila kila mmoja analiandika jina lake vingine.

Mimi na Hamza Aziz tulikuwa na Majlis yetu nje ya nyumba
yake kwenye kibanda cha makuti pwani kikitazama Bahari ya Hindi.

Hapa palikuwa na upepo mwanana.

Lakini baada ya muda nilikuja kujua kuwa Hamza Aziz hakupenda kuzungumza na mimi ndani nyumbani kwake kwa kuogopa ‘’kusikilizwa.’’

Naamini msomaji ushanielewa.

Mzee Kitwana Kondo yeye alikuwa anasema ukitaka ‘’usisikilizwe’’ fanyeni mazungumzo yenu kwenye pikipiki huku inatembea.

Wazee wangu hawa wawili wote walikuwa katika jeshi la polisi wakati Waingereza wanatawala Tanganyika.

Miaka hiyo wao walikuwa vijana na harakati za kudai uhuru zilikuwa zimepamba moto.

Kitwana Kondo akiwachunguza viongozi wa TANU na hili kanieleza mwenyewe kwa ulimi wake na Hamza Aziz inasemekana yeye akiwapelekea TANU siri za Waingereza.

Hamza Aziz yeye hakupata kunieleza hili nami kwa staha yangu kwake sikuweza kumuuliza.

Siku moja tukiwa Majlis akanieleza siku alipomjulisha Rais Ali Hassan Mwinyi kwa Ally Sykes.

Ilikuwa kwenye futari Ikulu na Hamza Aziz na Ally Sykes walikuwa wamekaa karibu sana.
‘’Sheikh Ali huyu ni Ally Sykes yeye na kaka yake Abdul ndiyo waliompokea Mwalimu hapa Dar es Salaam na wamefanya mengi katika kupigania uhuru wa Tanganyika, Abbas Sykes mdogo wao unamfahamu…’’

Na maneno mengine mengi.

Ally Sykes akamwambia Rais Mwinyi kuwa anamkaribisha nyumbani kwake.

Ally Hassan Mwinyi akajibu kuwa atafurahi sana kufika kwake.

Haya kanieleza mwenyewe Ally Sykes.

Anasema alimpelekea mwaliko lakini hakupata jibu lolote.

Iko siku wakakutana mahali pengine na Ally Sykes akamwambia Rais Mwinyi kuwa kamletea mwaliko lakini hakupata jibu kutoka kwake.

Rais Mwinyi akasema hajapokea taarifa yoyote ya mwaliko kutoka kwake.

Ally Sykes akanieleza kuwa alikuwa tokea mwanzo akihisi kuwa Rais Mwinyi hakupelekewa mwaliko wake.

Siku moja Ally Sykes katika mazungumzo akaniambia, ‘’Mohamed nimerudishiwa nyumba yangu ya Mtaa wa Lindi na Rais Mwinyi.’’

Nina historia na nyumba hii.

Nakumbuka kama jana vile.

Ilikuwa mwaka wa 1963 mimi na baba yangu tumekwenda kumuona Ally Sykes ofisini kwake iliyokuwa kwenye nyumba hii.

Nilikuwa na miaka 11.

Wakati huo ikiwa sehemu ya ofisi ndogo ya Peter Colmore, ofisi kuu High Fidelity Productions ikiwa Delamere Avenue, Nairobi.

Kufupisha mambo.

Nyumba hii Peter Colmore aliinunua na mambo yalipokuwa magumu Azimio la Arusha na siasa ya ujamaa imepamba moto akamuuzia hii nyumba Ally Sykes aendelee na biashara kama ataweza.

Colmore akarejea Nairobi.

Ilikuwa katika ofisi hii kwa mara yangu ya kwanza kuona ‘’air condition,’’ ‘’reel to reel tape deck'' na ‘’wall to wall carpet.’’

Lakini kilichokamata akili yangu ya kitoto ulikuwa ule muziki mororo uliokuwa ndani ya ofisi ile na mengine mengi.

Nyumba hii ikataifishwa na serikali.

Nyumba hii Ally Sykes siku zote akiniambia kuwa ilitaifishwa kwa fitna kwani ilikuwa haijafikia thamani ya nyumba zilizotakiwa kutaifishwa.

Nyumba nyingi za Waafrika wengine katika TANU ukiondoa za Wahindi zilitaifishwa.

Wengi wa hawa baada ya kustaafu walipigwa na ufukara mkubwa.

Rais Mwinyi alipoelezwa habari za hawa wastaafu kwa kuwahurumia aliwarejeshea nyumba zao ziwasaidie katika siku zao za mwisho.

Mzee Kondo anahadithia anasema mtu fulani akijidai sana wakati wa Nyerere na akimwangaisha sana kwa kuwa alikuwa pembeni ya rais.

Huyu mtu fulani nyumba yake ikataifishwa na alipostaafu akawa hoi.

Akiwa kwao bara akapata taarifa kuwa Rais Mwinyi anarejesha nyumba zilizotaifishwa na Nyerere.

Basi akaja Dar es Salaam kwa haraka lakini hajui vipi atafikisha suala lake kwa Rais Mwinyi.

Jamaa wakamwambia aende kwa Kitwana Kondo.

Hili likamwia tabu kidogo kwa kuwa alimtesa sana Mzee Kondo enzi za Nyerere.

Akapiga moyo konde akaenda nyumbani kwa Kitwana Kondo kumweleza shida yake.

Bahati mbaya hakumkuta akamkuta mkewe.

Huyu mzee wangu akamwachia Mzee Kondo ujumbe huu kupitia kwa mkewe, ‘’Mwambie Kitwana kuwa fulani kaja hapa ana shida.

Mwambie fulani anakuambia, ‘’Mungu kibidu.’’

Ujumbe ulimfikia Kitwana Kondo na alicheka sana.

Araf Sykes baada ya kifo cha Rais Ali Hassan Mwinyi ameniletea picha ya baba yake yuko na Rais Mwinyi wameshikana mikono.

Nikamuuliza hiyo picha imepigwa wapi?

Araf akaniambia imepigwa Diamond Jubilee Hall siku ya harusi yake.

Ally Sykes alimwalika Rais Ali Hassan Mwinyi na alihudhuria walima wake.

Rais Mwinyi alimrejeshea nyumba zake Bibi Titi zilizotaifishwa.

Bibi Titi alirudi kukaa katika nyumba yake ya Upanga karibu na Makao Makuu ya JWTZ na alifanya maulid kumshukuru Allah kwa wema wake.

Nilihudhuria dua ile na katika watu waliokuwapo siku ile alikuwa Tewa Said Tewa na mkewe Bi. Zainab.

Kwa kuhitimisha.

Ripoti ya Tume ya Rushwa ya Jaji Joseph Sinde Warioba iliyochapwa katika gazeti la Mtanzania ilitaja nyumba ya Ally Sykes na ya Bibi Titi Mohamed kuwa moja ya nyumba zilizorejeshwa katika mazingira hayo.

Mchana ule ule nilifikisha makala yangu kwa Mhariri nikieleza historia ya nyumba ile ya Ally Sykes na kusema kuwa ofisi ile ilitoa hela nyingi kwa TANU wakati wa kupigania uhuru wa Tanganyika.

Siku ya pili makala yangu ilitokea gazetini.
Hii ilikuwa mwaka wa 1996.

Ally Sykes alifurahi sana aliposoma makala yangu.
Ilimkumbusha mbali.

1709791173614.png

1709791217534.png
 
Asante kwa historia nzuri.

Umenikumbusha Kitwana Kondo ,Mjukuu wake alikuwa anakuja na Benzi Shule 90's na alikuwa anapiga unyunyu wa elfu 80 na raba mtoni za maana ,gari yake ilikuwa anapakiza mademu tu wa jangwani au zanaki.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom