Hadithi: Usife Haraka Mpenzi Wangu

Mwachiluwi

JF-Expert Member
Mar 10, 2022
17,796
32,148
USIFE HARAKA MPENZI WANGU

HANA haraka anapotembea, ukimtazama anaonekana kujiamini sana. Tabasamu mwanana linaupamba uso wake, lakini mavazi yake yanaonesha asivyo mtu wa dhiki! Hata kama siyo sana, lakini uwezo wa kubadilisha mboga ulikuwa mikononi mwake!

Anatoka kwenye duka hili maalum kwa kuuza kadi na zawadi mbalimbali lililopo ghorofa ya saba, katika jengo moja la KPC Towers, katikati ya Jiji la Dar es Salaam. Anatembea taratibu kuifuata lifti iliyokuwa mita chache sana mbele yake. Anatabasamu! Ni kweli anatabasamu!

Tena basi alikuwa na kila sababu ya kutabasamu, maana zilibaki wiki tatu tu, kabla ya ndoa yake na mpenzi wake wa siku nyingi Cleopatra ifungwe. Mkononi mwake ana bahasha ya khaki ambayo ndani yake kuna zawadi kwa ajili ya Cleopatra wake. Alijua anachotakiwa kumfanyia Cleopatra!

Siku zote alikuwa akinunua apple tu, mambo yanakuwa sawa! Huo ulikuwa ugonjwa mkubwa zaidi kwa Cleopatra. Alipoifikia, akabonyeza kitufe fulani mlangoni, mlango ukafunguka. Akaingia na kusimama, punde mlango ukajifunga, akabonyeza kwenye herufi G akimaanisha kwamba anataka kushuka chini!

Ni kijana mtanashati sana, anayevutia kwa kila mwanamke aliyekamilika. Anaitwa Deogratius Mgana. Mfanyakazi wa shirika moja lisilo la kiserikali jijini Dar es Salaam. Ana furaha moyoni mwake, maana anakwenda kufunga ndoa na chaguo lake.

Kwanini asitabasamu!
Hakika ana haki ya kutabasamu!
“Ni kweli lazima nitabasamu, kwanza nusu ya ndoto zangu tayari zipo kwenye mstari. Lazima nijisikie vizuri,” akawaza mwenyewe akiwa kwenye lifti.

Akabaki ametulia kimya akiwa amesimama kwenye lifti ile, ikaanza kushuka taratibu kwenda chini. Ghorofa ya sita, ghorofa ya tano, ghorofa ya nne...alipofika ghorofa ya tatu, lifti ikasimama. Hapo akajua kuna mtu aliyekuwa akitaka kushuka chini. Mlango ulipofunguka, wakaingia wanaume watatu, wote wamevaa miwani za jua.
“Mambo bro?” Mmoja akasalimia.

“Poa,” akaitikia Deo.
Lifti ikaanza kushuka taratibu, walipofika ghorofa ya tatu, ikasimama. Mlango ulipofunguka tu, ghafla wale vijana watatu wakamsukuma hadi nje. Mara mlango ukafunga.

“Paaaaaa!” Mlio wa risasi ukasikika.
Deo akaanguka chini, akianza kuvuja damu!

* * *
Alisikia vizuri sana mlio wa simu yake, lakini aliamua kupuuzia! Si kwamba hakutaka kwenda kupokea, lakini alikuwa na kazi muhimu sana aliyokuwa akiifanya, zaidi ya kwenda kupokea simu!
Cleopatra alikuwa anapika!

Chakula kizuri ambacho mpenzi wake alikuwa anakipenda sana. Alikuwa anapika viazi vya kukausha, maarufu kama maparage, ambavyo Deo alikuwa akipenda sana. Siku hiyo Deo alipanga kwenda nyumbani kwa akina Cleopatra, Mikocheni.

Ilikuwa zimebaki wiki tatu tu ndoa yake na Deo ifungwe. Siku ambayo alikuwa akiitamani sana na kuomba ifike haraka. Mlio wa simu yake ukaisha ghafla. Akaendelea na mapishi yake jikoni, lakini baada ya muda mfupi sana, simu ikaita tena kwa mara nyingine...

“Nani huyo aaah!” Cleopatra akasema kwa hasira kidogo.
“Mi’ nampikia Deo wangu bwana alaaah!” Akasema tena, akifunika kile chakula jikoni na kufunga kanga vizuri.
Yap! Kama ungekuwepo, ungeamini kweli Cleopatra alikuwa mwanamke mrembo. Pamoja na kwamba alikuwa amevaa kanga, lakini umbo lake lenye namba nane liliweza kuonekana vyema kabisa. Cleopatra alijaaliwa umbo zuri sana la kuvutia.

Ona anavyotembea...
Kama anaionea huruma ardhi. Ana hips pana zinazozidisha uzuri wake, ana macho mazuri yenye uwezo wa kumchanganya mwananaume yeyote yule. Labda niseme kwamba, Cleopatra alikuwa mwanamke mrembo sana.

Alivyofika sebuleni, simu ikaacha kuita. Akachukia sana, lakini akiwa anainua ili aweze kujua aliyekuwa akimpigia ili aweze kumpigia tena, akashangaa simu yake ikianza kuita tena. Kwenye kioo cha simu yake likaonekana jina ‘My Deo’!
“Jamani, kumbe ni sweetie!” Akasema akibonyeza kifufe cha kijani ili kumsikiliza.

Ilikuwa ni namba ya Deo ikionekana kwenye kioo cha simu yake...
“Yes baby, najua hujasahau kuninunulia apple na napenda kukujulisha kwamba, maparage yako yanakaribia kuiva, ila sijui ungependa nikuandalie juice ya nini? Machungwa, maparachichi, maembe au mananasi? Maana kila kitu kipo kwenye friji!” Cleopatra akasema kwa sauti iliyojaa mahaba mazito sana.

“Samahani dada, mimi siyo mwenye simu!” Sauti hii ya kiume, tulivu yenye mikwaruzo kwa mbali ilisikika kwenye simu ya Cleopatra.
“Sasa kama wewe si mwenye simu, kwanini umepiga? Kwanini unakosa ustaarabu?” Cleopatra akamwuliza yule mtu akiwa na hasira sana.

“Samahani sana dada’ngu, lakini nadhani ni vyema ukawa mtulivu na kuuliza kilichotokea. Si kawaida mtu kupiga simu isiyo yake kwa watu ambao wamehifadhiwa kwenye simu hiyo. Hiyo ingetosha kabisa kukufanya ugundue kwamba kuna tatizo!” Mtu huyo akasema akizidi kuonesha kwamba anahitaji utulivu wa Cleopatra.

“Ndiyo...enhee kuna nini? Hebu niambie, maana tayari nahisi nimeanza kuchanganyikiwa!”
“Sina shaka wewe ndiye Cleopatra!”
“Ndiyo!”
“Ni nani wako?”

“Ni mchumba’ngu, kwani vipi?”
“Usijali, tuliza moyo dada yangu. Mimi ni Dk. Palangyo wa Hospitali ya Taifa Muhimbili. Huyu ndugu mwenye simu, ameletwa hapa na wasamaria wema, baada ya kupitishwa katika Kituo cha Polisi Oysterbay!”
“Anaumwa na nini dokta?” Cleopatra akauliza akianza kulia kwa huzuni.

“Amepigwa risasi na watu wasiojulikana katika Jengo la KPC Towers. Hata hivyo, hana hali mbaya sana, matibabu yanaendelea, lakini nimeona ni vyema kukujulisha ili uwafahamishe na ndugu wengine!”
“Asante dokta kwa taarifa, baada ya nusu saa nitakuwa hapo,” Cleopatra akajibu akizidisha kilio chake.

Akatoka mbio, hadi chumbani kwake. Hakukumbuka kwenda kuipua chakula jikoni. Akavaa haraka na kutoka hadi getini! Ghafla kumbukumbu zake zikarudi!
“Mama yangu, nimeacha chakula jikoni na jiko linawaka,” akawaza akirudi ndani mbio.

Ilikuwa ni hatari sana, maana alikuwa anapikia jiko la umeme. Mara moja akarudi ndani na kuzima jiko, akaipua kile chakula na kutoka kwa kasi sana.
“Wewe vipi mwenzetu, mbona hivyo?” Mama yake Cleopatra akamwuliza baada ya kumuona mwanaye anaonekana kuwa na haraka ambayo hakujua ni ya nini.

“Nitakupigia simu mama!”
“Unakwenda wapi?”
“Mama nitakupigia!”
“Patra, mwenzako si anakuja au haji tena?”

“Mama Deo amepigwa risasi, yupo hospitalini,” akasema Cleopatra akiwa tayari ameshaingia kwenye gari.
Akapiga honi kwa nguvu, mlinzi akafungua haraka. Cleopatra akaondoa gari kwa kasi sana. Alikuwa anakwenda Muhimbili, huku nyuma akiwa amemuacha mama yake akiwa mwenye mawazo.
 
Akiwa jikoni anaandaa chakula kwa ajili ya mpenzi wake, Cleopatra anapokea simu kutoka Muhimbili, akipewa taarifa kwamba Deo, mpenzi wake amepigwa risasi na amelazwa. Taarifa hizo zinamshtua sana. Anatoka na gari haraka kwenda hospitalini. Nini kitatokea? Endelea...

CLEOPATRA aliendesha gari kwa kasi sana, hakujali ajali barabarani, alikuwa tayari kwa lolote litakalotokea! Aliendesha kwa kasi ya ajabu sana. Kutokea nyumbani kwao Mikocheni hadi Muhimbili, alitumia dakika ishirini!

Hakukubali kukaa foleni, aliendesha kama daladala, kwani alipenyeza pembeni, sehemu zilizokuwa na foleni kubwa. Alipofika hospitalini, akaegesha gari lake kisha akapiga zile namba na kuzungumza na yule daktari.

“Nimeshafika dokta!”
“Ok! Uko wapi?”
“Kwenye maegesho!”
“Tukutane MOI!”

“Sawa dokta.”
Bila kupoteza muda, Cleopatra akachanganya miguu hadi ilipo wodi ya Taasisi ya Mifupa (MOI). Akiwa kwenye lango kuu la kuingilia, akamwona mwanaume mmoja mrefu aliyevaa koti jeupe na miwani, akahisi angekuwa ndiye daktari aliyekuwa akimfuata.

“Sorry, ni dk. Pallangyo?” Cleopatra akauliza akimkazia macho.
“Yes, karibu!”
“Ahsante!”
“Nifuate!”

Dk. Pallangyo akatangulia na Cleopatra akimfuata nyuma. Safari yao ikaishia ofisini kwa daktari yule.
“Karibu sana dada yangu!”
“Ahsante!” Cleopatra akajibu na kuketi kwenye kiti, kwa mtindo wa kutazamana na daktari.

“Ulisema mgonjwa ni nani wako?”
“Mchumba wangu!”

“Oh! pole sana...kilichotokea ni kwamba, mwenzio amepigwa risasi ya begani, lakini inaonekana kutokana na mshtuko alioupata, umesababisha apoteze fahamu. Tunashukuru kwamba risasi haijatokeza upande wa pili, kwahiyo tumefanikiwa kuitoa, lakini bado hajazinduka!”

“Mungu wangu, atapona kweli?”
“Uwezekano huo ni mkubwa sana, lakini tuombe Mungu, naamini atakuwa sawa.”

“Naweza kwenda kumuona tafadhali?”
“Bila shaka!” Dokta akamjibu na kusimama.

Akaonesha ishara kwamba Cleopatra amfuate. Akasimama na kumfuata nyuma yake.

* * *
Deogratias alikuwa amelala kimya kitandani, Cleopatra akiwangalia kwa jicho la huruma, simanzi tele ikiwa imemjaa moyoni mwake. Moyo wake unashindwa kuvumilia, macho yake yanazingirwa na unyevunyevu. Chozi linadondoka!

Chozi la huzuni!
Deo ametulia kitandani, mwili wake ukiwa umefunikwa kwa shuka jeupe, isipokuwa kuanizia kifuani, bandeji inaonekana mkononi mwake. Mapigo ya moyo wake yanakwenda taratibu kabisa!

“Deo wangu...Deo...Deo jamani...amka mpenzi wangu. Naomba usife kwanza mpenzi wangu jamani. Hebu amka baby, tufunge ndoa...bado nakupenda...” akasema Cleopatra akilia kwa uchungu.

Deo hakusikia kitu, alikuwa katika usingizi mzito akiwa hajui chochote kinachoendelea. Alikuwa amepoteza fahamu na hakuwa na uwezo wa kusikia chochote.

Wasiwasi wa Cleopatra ulikuwa mmoja tu; Kwamba Deo akifa asingeweza tena kufunga naye ndoa, tendo ambalo alikuwa akilisubiria kwa muda mrefu sana. Cleopatra akazidi kulia. Alitamani sana kuliona tabasamu la Deo.

Alitaka kuona akiongea, akimbusu, akimkumbatia na kumwambia maneno matamu ambayo amekuwa akimwambia mara nyingi sana.
Hilo tu!

Lakini Deo hakuweza kufanya chochote kati ya hivyo. Alikuwa amelala kitandani kama mzigo, hana taarifa kama mpenzi wake Cleopatra alikuwa kitandani kwake akilia.

“Basi dada yangu, mwache apumzike, usijali, huna sababu ya kulia. Atapona tu!”

“Lakini inaniuma dokta, bado wiki tatu tufung ndoa. Tayari ndoa imeshatangazwa mara ya kwanza kanisani, bado mara tatu ili nifunge ndoa na Deo wangu, sasa itawezekanaje tena? Si ndiyo nimeshamnpoteza? Si tayari nimeshapoteza ndoa?” Cleopatra akasema akionekana kuwa na uchungu sana.

“Hapana, hana hali mbaya, wiki tatu ni nyingi sana, kabla ya muda huo atakuwa amesharejea katika hali yake ya kawaida, bila shaka atapanda madhabahuni kufunga ndoa na wewe!”

Maneno ya Dk. Pallangyo kidogo yalimpa moyo Cleoptara, lakini ndani ya moyo wake, aliendelea kuwa na uchungu mwingi sana, kwani Deo alikuwa kila kitu katika maisha yake.

Yeye ndiye aliyekuwa wa kutimiza ndoto zake za kuingia kwenye ndoa, lakini sasa zinakaribia kuzimika!
Lazima aumie!
Lazima ateseke!...
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom