Hadithi fupi: Mbeya yetu

ProMagufuli

JF-Expert Member
Apr 6, 2021
219
235
Sehemu ya 1.

𝗛𝗔𝗗𝗜𝗧𝗛𝗜 𝗙𝗨𝗣𝗜: 𝗠𝗯𝗲𝘆𝗮 - 𝟭

“MBEYA NI MJI wa ovyo sana.”

“Unasema?” Sajo aliuliza.

“Nasema hivi,” Oba alisema. “Mbeya ni mji wa ovyo sana. Kwanza hata ni aibu kuita jiji. Ilifaa tu kuitwa kijiji kikubwa.”

“Wacha we!” Sajo alisema. Akapiga funda la cappucino mbele yake. Akairuhusu kushuka huku akimtazama Oba. Akasema, “tatizo lako umekariri sana maisha.”

“Wala hajakariri,” Liza alidakia. Hakuruhusu mtu amjibu, akaendelea, “mimi sioni chochote cha maana kuhusu Mbeya.”

“Hivi,” Sajo alisema. “Hiyo Mbeya mnayosema hamuoni chochote cha maana mnaifahamu kweli ama mnaishia kuisoma Twitter?”

“Wachana na mambo ya Twitter,” Oba alisema.

“Hujajibu swali, Mwaisa,” Sajo alisema. “Unaijua vema Mbeya wewe?”

“Naijua vema. Sema kingine,” Oba alisema.

“Umefika mara ngapi?” Sajo aliuliza.

“Mara nne ama tano hivi,” Oba alijibu.

“Na wewe?” Sajo alimgeukia Liza.

“Mara mbili,” Liza alijibu.

“Mmefika wapi na wapi?” Sajo aliuliza huku mkono ukipeleka kikombe chake mdomoni.

“Nimefika Mwanjelwa pale, mjini, Soweto na ile njia yote ya kwenda Songwe Airport,” Liza alisema.

“Na wewe, mzee baba?” Sajo alimwuliza Oba.

“Nishakula sana bata pale City Pub na pale pengine sijui mnaita Mwailubi,” Oba alijibu.

“Sehemu nyingine?” Sajo aliuliza.

“Kuna sehemu nyingine tena ya wapi?” Sajo aliuliza.

Liza akadakia, “kaMbeya kenu si nd’o kameishia hapohapo!”

“Mnafeli sana,” Sajo alisema. “Na kwa sababu mmefeli sana mnapoteza muda kuwaaminisha watu kuwa Mbeya ni sehemu mbaya. Tena kama wewe Oba huwa naona tweets zako nyingi sana unavyoikandia Mbeya. Ni kwa sababu huijui Mbeya.”

“Aah, we bwana wewe,” Liza alisema. “Mbeya yenyewe yenye nyumba za matope?”

“Kosa jingine hilo,” Sajo alisema. “Kwa taarifa yako, zile nyumba unazoziona ukaziita za matope ni nyumba imara kuliko sehemu zingine. Katazame majengo ya pale mjini ama Sokomatola, yamejengwa miaka ya thelathini na arobaini huko, na bado ni imara hadi leo. Unafeli sana, Mwaisa.”

“Anafeli nini?” Oba aliuliza.

“Nakupa kazi uende ukaGoogle kuhusu pozzolana halafu uje tubishane hapa,” Sajo alisema huku akimpa ishara mhudumu amwongezee kikombe kingine cha cappuccino.

“Naona unavyoshobokea kahawa za watu,” Oba alisema. “Kwenu Mbeya hakuna vitu vizuri kama hivi.”

“Vitu vipi?” Sajo aliuliza. Akaongeza, “kahawa?”

“Ndiyo,” Liza alijibu.

“Nyie b’ana,” Sajo alisema. “Mnafaa kuonewa huruma. Tufanye kitu kimoja.”

“Kitu gani?” Oba na Liza waliuliza kwa pamoja.

Sajo akawajibu, “tufanyeni ziara ya wiki moja tu. Twendeni Mbeya. Suala la malazi na chakula tukiwa Mbeya niachieni mie. Jichangeni tu nauli.”

“Ili tukale mavumbi ya Nzovwe?” Liza aliuliza.

“Twendeni Mbeya,” Sajo alisema. “Tukimaliza ziara, tukutane tena hapahapa Grano Coffee, tutajidiliane.”

Ubishi wao uliendelea kwa muda mrefu. Wala haukuisha. Lakini siku chache baadaye, waliafikiana kuwa wangesafiri pamoja kwenda Mbeya.

Mwezi mmoja hivi baadaye, Oba na Liza waliambatana na Sajo kwa safari ya kwenda Mbeya. Sajo alipendekeza waondoke Dar kwa garimoshi. Na kwamba, wangerejea kwa ndege.

Siku ya Ijumaa, nyakati za alasiri, Sajo na wageni wake waadhimu Oba na Liza walianza safari ya garimoshi kuelekea Mbeya.

“Halafu, shem,” Liza alisema. “Ujue mimi sijawahi kupanda treni maishani mwangu.”

“Kaa kwa kutulia,” Sajo alisema. “Enjoy your trip.”

Ama hakika, walifurahia safari yao. Awali walikuwa wameketi chumbani kwao. Walikinunua chumba kizima cha daraja la kwanza ambacho ni cha abiria wanne. Wakawa wao watatu. Lakini, kadri garimoshi lilivyochapa mwendo wakaamua kwenda sehemu ya lounge ili waburudike na vinywaji. Kwa kuwa Oba na mpenziwe, Liza walipenda maji, basi walipiga masanga huku wakicheza karata pamoja na abiria wengine. Muziki kutoka kwenye runinga kubwa ukumbini humo uliwaburudisha vilivyo.

“Hapa tumeanza mbuga ya Selous,” Sajo aliwaelekeza wakiwa njiani. “Tutaona wanyama wengi sana.”

Jambo hilo liliwasisimua sana Oba na Liza.

Wakati wa machweo, jua lilitoa taswira ya kuvutia sana. Wote waliketi usawa wa dirisha wakihangaishana kupigana picha kupitia sikano zao.

Wakati wa usiku, walikwenda kwenye mgahawa wa ndani ya garimoshi kwa ajili ya chakula. Iliwashangaza pakubwa Oba na Liza kuona mgahawa wa kwenye garimoshi una chakula kitamu ilioje. Walisifia mno.

Huku garimoshi likichapa mwendo, wakaingia chumbani kwao kulala.

Uzuri wa sura ya nchi uliosheheni uoto wa kijani wenye kuvutia huku ukifunikwa na ukungu ulioje, viliwastaajabisha na kuwasisimua kulipopambazuka. Walishangaa kuona garimoshi lao likipita juu ya madaraja makubwa yenye hadi kona.

“Muda si mrefu tutawasili stesheni ya Makambako,” Sajo aliwaeleza.

Baada ya kutoka stesheni ya Makambako, walikwenda tena mgahawani kwa ajili ya stafutahi. Waliketi hukohuko walipomaliza huku wakishangaa garimoshi lilikata mbuga kwenye tambarare ndefu.

“Hili ni Bonde la Usangu,” Sajo alisema.

“Usangu?” Oba aliuliza.

“Ndiyo,” Sajo alijibu. “Bonde hili lipo ndani ya Bonde la Ufa la Afrika Mashariki. Bila shaka umelisoma sana kwenye Jografia. Kwenye hili bonde, kunalimwa mpunga kwa kiasi kikubwa sana. Ndilo eneo linaloongoza, nadhani kwa Afrika Mashariki yote kwa kilimo cha mpunga.”

“Wacha we!” Liza alisema.

“Utajiju!” Sajo alisema.

Wakaangua kicheko.

“Kule ni wapi?” Oba aliuliza akionesha mlima mkubwa upande wa kulia.

“Kule,” Sajo alisema. “Kunaitwa Chunya Escarpment. Ni ukingo wa hili bonde la ufa. Kule juu kabisa mnakokuona, kuna barabara.”

“Haiwezekani!” Liza alisema.

“Na kwa taarifa yenu, kule juu ndiko kwenye barabara iunganishayo miji iliyo juu zaidi Tanzania. Na hivi ilivyopigwa lami, inasemekana ni Afrika Mashariki na Kati yote.”

“Ushaanza kamba zako,” Oba alisema.

“Kwa sababu?”

Liza akadakia, “barabara ya juu zaidi lazima itakuwa kwenye Mlima Kilimanjaro.”

“Tatizo lako,” Sajo alisema. “You listen to reply and not to understand. Kaa kwa kutulia uelewe bi’ mdashi.”

“Mmh!” Oba akaguna.

“Hilo tuliache kwanza.”

Hadi wanawasili Mbeya nyakati za alasiri, walikuwa wameoneshwa na kushangazwa na vitu vingi.

“Jambo la kwanza kabla hatujapumzika, tutakwenda road trip ya kilometa thelathini,” Sajo alisema.

Akachukua gari alilokwishafanya mpango kwa simu liwe tayari. Akawaendesha wageni wake kutoka stesheni ya reli ya uhuru ya Iyunga. Wakapita barabara ya Mbalizi hadi walipofika Mafiat na kushika kushoto kuifuata barabara ya Lumumba. Walipofika Rift Valley waliingia kulia kuifuata barabara ya Chunya.

“Mbona kama tunakwenda Chunya?” Oba aliuliza.

“Endelea kutulia, Mwaisa,” Sajo alijibu.

Kwa takribani dakika ishirini, Oba na Liza walistaajabishwa na mandhari ya kuvutia wakipandisha milima. Uoto wa kijani na ukungu kwa mbali viliwashangaza sana. Upande wa kulia waliuona mji wote wa Mbeya. Walipokwenda mbele zaidi, mji wa Mbeya ukawa kushoto kwao, na wakati mwingine, nyuma yao. Sajo alicheka moyoni namna wageni wake walivyochachawa na uzuri wa safari hiyo.

Mara, akapaki gari kushoto.

“Tumefika?” Liza aliuliza.

“Shukeni kwanza kwenye gari,” Sajo alisema.

Waliposhuka tu, macho ya Oba yalitekwa nadhari na kibao cheupe juu mlimani upande wa pili wa barabara. Akakisoma kwa sauti. “Highest point of all trunk roads in the country. Altitude 2,961m. Latitude 08 35. Longitude 33 35.”

“Naomba nisimame kule unipige picha. Hakikisha kibao kinaonekana,” Liza alisema huku akivuka barabara.

Baada ya picha nyingi wakaendelea na safari.

Macho ya Oba na Liza yalitekwa na mwoneko wa kuvutia wa barabara. Kona kali huku bonde kubwa likionekana mbele yao viliwafanya kusisimka zaidi. Kila baada ya umbali mfupi, Sajo alisimamisha gari wapige picha.

“Ila Mbeya ni kuzuri sana jamani,” Liza alisema.

Sajo hakutia neno. Alitabasamu. Akakumbuka walivyopata kunena wahenga, usiwaambie, waoneshe.

“Viewing Area,” Liza alisoma kwa sauti kibao kilichokuwa mbele yao wakati Sajo akiingiza gari eneo la wazi upande wa kulia.

“Hapa ni wapi?” Oba aliuliza.

“Hapa ni eneo maalumu la kutazama bonde lote. Hapa ni upeo wa mwisho wa macho yako. Utaona tambarare mbali kabisa hadi macho yako yasiweze kuona tena.”

“So amazing,” Liza alisema akihangaika kujipiga picha kwa sikano yake.

“Ile barabara inakwenda hadi wapi?” Sajo aliuliza akionesha barabara ya lami mbali kidogo mlimani.

“Inakwenda Chunya, Singida, Tabora hadi Mwanza.”

“Aisee!”

“Nasikia Chunya kuna dhahabu sana,” Liza alisema.

“Ndiyo,” Sajo alijibu. “Kuna mkondo wa dhahabu unaoanzia kusini mwa ziwa Viktoria ukaambaaambaa kote kule Geita sijui Kahama na wapiwapi huko na kuja hadi kule mbele unakoanzia ule mlima unaouona. Unaitwa Mlima Loleza. Na huo mkondo wa dhahabu unaitwa Lupa Gold Field.”

“Noma sana,” Oba alisema.

“Na kitu ambacho mnaweza msikijue. Chunya ndiyo iliyozaa mji wa Mbeya. Neno Mbeya limetokana na ibheya, ambalo ni neno la Kisafwa likimaanisha chumvi.”

“Ka’ sielewi vile,” Liza alisema.

“Hapo kale,” Sajo alisema. “Maeneo ambayo leo ni Mbeya mjini yalikuwa na chumvi nyingi. Hivyo wenyeji wa eneo hilo ambao ni Wasafwa walikuwa wanasema wanakusanya ibheya kwa maana ya chumvi.”

“Sasa ikawaje tena hadi Mbeya?” Oba aliuliza.

“Katikati ya jiji la Mbeya, kuna barabara maarufu inaitwa Lupa Way, ama njia ya kwenda Lupa kwa Kiswahili. Lupa ni eneo lililopo Chunya ambako kulikuwa na dhababu nyingi. Na dhahabu yenyewe ilikuwa alluvial tu.”

“Ni nini alluvial?” Liza aliuliza.

Sajo akajibu, “inamaanisha ilikuwa juujuu tu. Sasa Wazungu waliokuwa njiani kwenda Lupa Tingatinga kuchukua dhahabu waliweka makambi yao hilo eneo ambalo leo linaitwa Lupa Way. Ndipo ilipo Posta na TRA. Wahindi wakaona kuna fursa za kibiashara. Wakaanza kujenga maduka. Ghafla mji ukaanza kuchibua. Miaka ya 1920 wakati wakoloni Waingereza wanaanza kuitawala Tanganyika wakaamua kuufanya mji rasmi. Hawakuweza kutamka ibheya, hivyo mji ukabatizwa rasmi kuwa Mbeya.”

“Upo deep sana, mzee baba,” Oba alisema.

“Napiga Unyakyusa mwingi sana, Mwaisa.”

Kicheko na gonga-viganja vikatamalaki.

“Tuingie kwenye gari twende pale mbele,” Sajo alisema.

Wakajitoma garini. Sajo aliendesha gari uelekeo wa Chunya. Alisimama baada ya kama kilometa nne hivi.

“Oooh honey, ona what a beautiful sunset,” Liza alimwambia Oba akistaajabishwa na uzuri wa machweo.

Oba hakusema neno. Akili yake ilikufa bumbuwazi akishangaa uzuri wa jua linapochwea. Mchanganyiko wa rangi na namna ulivyosanifu mwonekano wa anga, ni kitu ambacho hakuwahi kukiona hapo kabla. Alitazama huku akishusha pumzi kwa nguvu.

“Mahali hapa, kitongoji kinaitwa Igawilo, kipo ndani ya kijiji cha Lwanjilo. Hapa ni mahali unapofaidi sunrise na sunset katika rangi na uzuri ambao nina hakika huupati mahali pengine popote. It is the best sunset experience. Kama nikitaka kuazima Kinge cha bi’ mdashi wako.”

Walicheka.

“Ila nyie watu wa Mbeya mna roho mbaya sana,” Liza alisema. Kabla mtu hajajibu, akaendelea, “halafu mna siri kwa kiasi kikubwa. Mimi sijapenda kabisa.”

“Kwa nini?” Sajo aliuliza.

“Kumbe Mbeya ina vitu vizuri hivi na vya kipekee halafu wala hamringi, na wala hamtuambii ili muendelee kufaidi wenyewe. Mimi sijapenda kwa kweli.”

Sajo alimtazama Liza alivyojitiisha huruma huku akiendelea kushangaa machweo kadri yanavyofifia na wekundu-manjano-machungwa wake.

“Ila Mbeya imebarikiwa, aisee,” Oba alisema.

“Nadhani,” Sajo alisema. “Mnataka muanze kunikwaza.”

“Kwa lipi tena, shem?” Liza aliuliza.

“Nimewaleta kuwaonesha trailer tu, tayari mmepanic? Hii ngoma bado mbichi sana. Kesho tunakwenda kuona maporomoko ya Mpanga-Kipengere. Keshokutwa tunaamkia safari ya Ziwa Kisiba, halafu tunalala ufukwe wa Matema. Bado tunasafari ya kuvinjari maajabu na upekee wa Mto Kiwira. Kama nilivyoaambia mara nyingi hapo nyuma, kaeni kwa kutulia.”

“Daaah!” Liza alisema.

“Shida yenu, mnajifungia huko maDaslamu yenu, kutwa kucha huko maTwitter na mawapi sijui mnaipondea Mbeya, sijui findu fiki. Kaeni kwa kutulia niwapige Unyakyusa mwingi.”

“Hadi hapa, nimeshafall in love na Mbeya. Hivi huku, hatuwezi pata hata shamba kweli?” Liza aliuliza.

“Andaa chapaa ya kutosha maana kila mahali nitakapowapeleka utauliza hilo swali la kupata shamba. This is Mbeya na picha ndiyo kwanza linaanza.”

Baada ya giza kuingia, wakaondoka.

“Sasa,” Sajo alisema. “Nataka niwaoneshe kwa nini nimeamua turudi Mbeya baada ya giza.”

Si punde, Oba na Liza walielewa minajili ya Sajo. Walishangazwa na uzuri wa Mbeya inavyoonekana usiku kutoka mlimani kabisa. Waliona taa za mji wote. Namna walivyouona utadhani walikuwa angani kwenye ndege. Mji uliokana mbele kwa chini kabisa. Iliwasisimua vilivyo.

“Ninyi si huwa mnasema sisi Mbeya ni washamba?” Sajo alisema.

“Hatujasema hivyo,” Liza alisema kwa unyonge huku akishangaa taswira ya kipekee ya Mbeya wakati wa usiku.

“Nawapeleka Del Caffe kwanza mkanywe cappuccino kabambe kuliko zile mnaringia nazo Dar. Tena, tutakunywa huku tukicheza karata na dominoes.”

“Ndiyo nini hicho?” Oba aliuliza.

“Nilidhani nyie watu wa Dar mnajua kila kitu,” Sajo alisema akiendelea kuchoma mafuta.

“Leo tumepatikana,” Oba alisema.

“Mwenzangu!” Liza akadakia.

“Kahawa ya Mbeya na Songwe ni kahawa bora zaidi. Harufu yake inakuachia msisimko ambao hujaupata popote. Hapo sizungumzii ladha yake, mtaona nabrag sana.”

Oba na Liza wakaangua kicheko.

Sajo akaendelea, “tukishatoka kwenye kahawa, nataka niwapeleke sasa Lupa Way kwenyewe. Huko tutaingia zetu mahali panaitwa 501 Soul Food tukapate chakula. Kuna huyo bwana, hapa mjini wanamwita Babu ni bingwa wa kupika vyakula vitamu hamjawahi kula nakwambieni.”

“Mie mate yameshanijaa,” Liza alisema.

“Wewe tena!” Oba akadakia.

Liza akatabasamu.

𝐼𝑡𝑎𝑒𝑛𝑑𝑒𝑙𝑒𝑎.

Fadhy Mtanga, 2022.


[/b]Copy and Paste.[/b]
View attachment 2252741
 
Posta na TRA haziko Lupa Way, nijuavyo ziko Jacaranda, Jacaranda inaanzia njiapanda ya kanisa la Anglikana kushuka chini mpaka kanisa la Moraviani na Lupa Way inapandisha juu kuelekea Uzunguni.
 
Du aisee uzi mrefu huu mwenye summary anipe maelezo kidogo ya. Fani na maudhui ya huu uzi
 
Posta na TRA haziko Lupa Way, nijuavyo ziko Jacaranda, Jacaranda inaanzia njiapanda ya kanisa la Anglikana kushuka chini mpaka kanisa la Moraviani na Lupa Way inapandisha juu kuelekea Uzunguni.
Uh inawezekana uko sahihi mkuu.!
 
Du aisee uzi mrefu huu mwenye summary anipe maelezo kidogo ya. Fani na maudhui ya huu uzi
Ni kuhusiana na mkoa wa Mbeya, mandhari na uzuri wake. Kwa wale wasioujua vizuri inaweza kuwapatia mwanga.

Hata wale wanaoponda wanaweza kubadili fikra.
 
Back
Top Bottom