Gavana sasa ataka EPA iondolewe BoT ;usiogope subiri matokeo ya uchunguzi kwanza,

Pdidy

JF-Expert Member
Nov 22, 2007
50,956
22,149
Gavana sasa ataka EPA iondolewe BoT





Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu ambaye ametaka kuondolewa kwa fedha za EPA kwenye benki hiyo

Na Ramadhan Semtawa

WAKATI uchunguzi wa Kampuni ya Lazard ya Ufaransa kuhusu hatima ya madai katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ukiendelea, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu, ametoa msimamo wake akisema BoT haitajihusisha tena na akaunti hiyo iliyokumbwa na ufisadi wa Sh133 bilioni.


Tayari BoT kwa kushirikiana na Benki ya Dunia (WB) iliipa kazi ya miezi tisa kampuni hiyo ya Lazard, kuangalia uwezekano wa kuendelea au kutoendelea kulipa madeni ya EPA, kubaini wadai halali na namna ya BoT kuachana na akaunti hiyo.


Hata hivyo, ikiwa sasa ni takribani miezi mitano tangu Lazard kuanza kazi, Profesa Ndulu aliliambia gazeti hili ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana kuwa, vyovyote itakavyokuwa BoT haitahusika tena na akaunti ya EPA.


"Uchunguzi wa Lazard unaendelea ni mkataba wa miezi tisa, lakini sisi tunasema vyovyote itakavyokuwa hatutahusika tena na akaunti ya EPA," alisema Profesa Ndulu na kuongeza:,


"Hata kama Lazard wakisema watu waendelee kulipwa madeni ya EPA sisi hatutahusika, huo ni msimamo wetu ambao uko wazi, watakaohusika ni wengine."


Profesa Ndulu ambaye amekuwa kwenye mchakato wa kujaribu kuisafisha BoT na tuhuma za ufisadi ambazo zimekuwa zikiitikisa taasisi hiyo tangu miaka ya 2000, alisema hata Rais amekwishaonyesha nia hiyo ya kuondoa akaunti ya EPA mikononi mwa taasisi hiyo.


"Hata mheshimiwa Rais ameonyesha nia hiyo ya kuondoa akaunti ya EPA BoT, kwa hiyo ni msimamo unaoeleweka ambao pia uko wazi tu," aliongeza Profesa Ndulu.


Alisisitiza kuwa BoT ingependa kubaki na majukumu yake makuu ya msingi na ya kisheria ambayo ni kusimamia na kuhakikisha uchumi tulivu, utulivu na ukuaji wa taasisi za fedha na usalama wa mabenki nchini.


"Tunachotaka ni kubaki na majukumu yetu ya msingi, sasa kama ni malipo ya EPA nafikiri itabidi uangaliwe utaratibu mwingine kama itakuwa upo umuhimu wa kulipa madeni," alisisitiza Profesa Ndulu.


Kauli ya gavana Ndulu imekuja kipindi ambacho kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma chini ya mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe, ikitaka hata uchunguzi wa kiasi cha Sh 42.6 bilioni zilizoibwa na makampuni tisa ya kigeni, ufanywe na Lazard badala ya Kikosi Kazi (Task Force) cha Rais.


Hoja ya mwenyekiti Zitto inatokana na kuangalia kwa undani taarifa na utaalamu wa kubaini nyaraka za malipo na uhalali wake kutokana na makampuni hayo mengi kuwa nje ya nchi.


Tayari msimamo huo umewasilishwa kwa Waziri wa Fedha na Uchumi, lakini katika majibu yake, alisema kikosi kazi hicho kiliundwa na Rais ambaye ndiye ana mamlaka ya kuamua namna nyingine ya uchunguzi.


Lakini, tayari Agosti mwaka jana Rais aliongeza muda kwa kikosi kazi hicho ambacho awali kilikuwa chini ya Mwanasheria Mkuu aliyestaafu Johnson Mwanyika na wajumbe wengine wawili; Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Said Mwema na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Dk Edward Hoseah.


Hata hivyo, IGP Mwema, alidhihirisha ugumu wa kazi hiyo juzi wakati akijibu swali kutoka gazeti hili baada ya kuweka bayana kwamba, kuna ugumu wa kupata taarifa za malipo hayo kwa makampuni ya nje licha ya kutumia Polisi wa Kimataifa (Interpol).


Kwa mujibu wa takwimu za serikali, deni la EPA hadi mwaka 1999 lilifikia dola 623 milioni za Marekani, ambazo kati ya hizo, 325 milioni zilikuwa ni deni la msingi na 298 riba na kuongezeka hadi kufikia 677 milioni.


Hata hivyo, kulikuwa na Mpango wa Kununua Madeni (Debt Buy Back Scheme) wa mwaka 1994, kati ya serikali na Benki ya Dunia (WB), ambao waliokuwa wakidai BoT, waliombwa wakubali kulipwa sehemu tu ya fedha wanazodai.


Katika mpango huo, wapo waliokubali na wengine kukataa. Hadi mwaka 2004, taarifa zinaonyesha dola 228milioni za Marekani, zililipwa chini ya mpango huo.


Utaratibu huo ndiyo ulileta matatizo ambayo yalibainika katika Ukaguzi wa Hesabu za BoT za mwaka 2005/06, ambao ulifanyika Agosti mwaka 2005 na kuonyesha matatizo katika ulipaji wa madeni kwa utaratibu huo wa idhini ya kulipwa wakala wa mdai katika akaunti ya EPA.


Baada ya hapo, kulitokea hali ya kutoelewana kati ya BoT na Mkaguzi Kampuni ya Deloitte & Touche ya Afrika Kusini', aliyegundua tatizo hilo, lakini serikali iliingilia kati na Desemba 4, 2006 ilimwagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kuhakikisha ukaguzi huo unafanyika kwa uhakika.


Ukaguzi huo, uliofanywa na Ernst&Young ulibaini ufisadi wa zaidi ya Sh133bilioni ambazo zililipwa kwa makampuni 22 kiholela.


Kufuatia ufisadi huo, Januari 9, mwaka jana Rais Jakaya Kikwete, aliutangazia umma kupitia Katibu Mkuu Kiongozi Philemon Luhanjo, kuhusu kutimuliwa kazi kwa aliyekuwa Gavana wa BoT, Daud Ballali (kwa sasa ni marehemu) na kuunda Timu Maalumu (Task Force) chini ya aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Johnson Mwanyika, kuchunguza, kukamata na kufungua mashtaka dhidi ya waliohusika na ufisadi huo.


EPA ni akaunti ya madeni ya nje ambayo ilitumika wakati wa Mfumo wa Ujamaa, awali ilikuwa katika iliyokuwa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), chini ya usimamizi wa BoT. Ilihamishiwa BoT mwaka 1985.
 
"Hata kama Lazard wakisema watu waendelee kulipwa madeni ya EPA sisi hatutahusika, huo ni msimamo wetu ambao uko wazi, watakaohusika ni wengine."



Huyu Gavana na yeye mzushi sasa kama wameshafanya uamuzi wa kutondelea na akaunti ya EPA wanafanya uchunguzi wa nini
 
Back
Top Bottom