SoC02 Elimu yetu

Stories of Change - 2022 Competition

Nemboyao

New Member
Aug 13, 2022
1
1
Kwakuwa nna uzoefu mzuri na wa mda mrefu sasa na bado naendelea kusoma nitoe mtazamo wangu.

Mimi ni bint na nasoma kidato cha sita sasa katika elimu yangu nimesoma shule zote za serikali mpaka sasa nilipofikia. Kusoma kwangu kumekuwa na changamoto sana na baadhi niliziona tuu hazikunikuta lakini ni changamoto kweli kweli.

Jamii yetu katika sekta ya elimu inapitia vikwazo vingi. Nchi nyingi za Afrika mashariki hazina idadi kubwa ya wasomi kutokana na changamoto zifuatazo kwanza ni:-

Utayari wa mwanafunzi. wengi wetu husoma kwa msukumo tuu na sio kwa utayari wetu. Kwenye kila kitu lazima kuwe na nia kamili ili uweze kufanya unachotaka kwa ufasaha.

Jamii zetu asilimia kubwa kusoma ni hiyari na sio lazima lakini wanasahau vitabu vya dini vinalazimisha kusoma kwani elimu ina umuhimu wake dunia.

Katika elimu yangu nimeshuhudia mwanafunzi akipigana na mwalimu kwasababu mwalimu anamuadhibu kwa kufeli. Hii inakuwa ni changamoto kwa walimu katika kuinua ufaulu.

Utayari wa mwalimu Kwenye sekta ya elimu baadhi ya masomo wanafunzi hufaulu sana na mengine hufeli sana kwasababu wafundishaji wenyewe hawana utayari katika ufundishaji wao.

Utayari unamfanya mwalimu afundishe kwa moyo kwani anapenda kuona wanafunzi wanafaulu lakini baadhi ya walimu hawana utayari uo.

Katika elimu yangu mwalimu aliwahi kutamka darasani kuwa hata ukifeli au ufaulu mwisho wa mwezi naenda ATM. kwa maneno haya mwalimu huyu anaonyesha kuwa hana utayari hivyo hajali kuhusu kuinua ufaulu wa wanafunzi anajali maslahi yake binafsi jambo hili pia ni changamoto kwa wanafunzi.

Wazazi kwa kiasi kikubwa kuna wazazi ambao hawajali kuhusu elimu wala ufaulu wa watoto wao. Mfano mzazi amhamasishi mtoto kwenda shule kwaiyo hata wiki inapita hajaenda shule na mzazi wala hajali kuhusu ilo swala.

Pia katika vikao vya wazazi mzazi anakuwa mzito kuhudhuria kujua hali ya mwanae kitaaluma na hata kuangalia ripoti yake. Kwa watoto wasio na utayari na elimu wanachukulia hii kama fursa.

Makundi Ukiwa mwanafunzi unakuwa na makundi ya marafiki ambao ndio watu wako wa karibu. Lakini sio kila rafiki ni rafiki wengine ni maadui. Wanafunzi wengi wanapoteza muelekeo mashuleni kwasababu ya makundi yao hasa kushawishiana.

Mapenzi shuleni pia yanasababishwa na makundi. Katika elimu yangu wanafunzi wawili shuleni walipeana mimba wote wakiwa shule na sababu ilikuwa ni ushawishi wa marafiki zake kuhusu kufanya zinaa na hao marafiki walishindwa kumpa namna ya kuepuka mimba za utotoni.

Hivyo basi wote waliacha shule na yule wa kiume alihama nchi.

Mazingira ya kujifunzia nilivyokuwa shule ya msingi madarasa yalikuwa ni machache sana shuleni hivyo ilitupasa kuingia kwa awamu saa 1-6 na saa 7-12. Kwetu wanafunzi ilikuwa vigumu zaidi kwa awamu ya mchana wengi hupata uchovu wa kwenda shuleni na akili imeshachoka na hata akienda anasinzia darasani.

Pia awamu ya asubuhi ilikuwa ni ngumu kwani ukitoka shule hufanyi mazoezi ya mwalimu na kwenda kucheza na watoto wenzio hivyo kiujumla hali ilikuwa ngumu kwetu na kwa walimu pia kwasababu waliofundisha asubuhi watafundisha tena mchana kwahiyo walichoka sana na hata walimu wengine awamu ya mchana walikuwa hawafundishi kabisa.

 Umbali kutoka nyumbani hadi shuleni katika serikali ya awamu ya nne ndio shule za kata zilianzishwa lakini hata hivyo mpaka sasa sio nyingi.

Nilivyokuwa kidato cha kwanza nililazimika kutembea kilomita 3 ili kufika shuleni na kurudi nyumbani lakini kwasababu wanafunzi tulikuwa wengi basi hata nilikuwa sioni kama ni mbali kiasi hicho.

Lakini shida ilikuja kwenye njia ambazo zinaniwezesha kufika shule ni mapori kambi ya jeshi na misitu hakuna nyumba za watu ilikuwa mwaka 2017 lakini mpaka sasa hakuna kilichobadilika kwasababu papo vile vile hakuna shule iliyojengwa karibu lakini sehemu zenye mapori kwasasa umekuwa ni mji.

Kitendo cha kuwa mbali na shule kilinifanya nishindwe kujisomea mda wa ziada kutokana na uwoga kwasababu ni porini na mimi ni wakike pia vitendo vya uporaji na ubakaji vilishamiri sana kwasababu hiyo sikuwa na kiwango kikubwa cha ufaulu hivyo basi wazazi wangu walinihamisha shule kidato cha 3.

Vifaa Shule nyingi hazina vifaa vya kufundishia. Katika elimu yangu hii ya kidato cha sita shule ninayosoma kuna uhaba mkubwa wa vitabu tena haswa katika mchepuo wa sanaa. Maktaba ipo lakini haina vitabu.

Kwa wanafunzi wenye uwezo wananunuliwa na wazazi wao na wengine tunabaki kusikiliza tusichokiona hivyo uelewa wetu hauwi sawa na hata katika ufaulu wetu.

Pia uhaba wa madawati bado shule niliyomaliza kuna wanafunzi wanakalia kiti kimoja wawili na zaidi. Namna hii mwanafunzi hapati uhuru wa kuandika na hata hawi makini na mwalimu kuliko alivyomakini na alivyokaa ili asidondoke.

Mila potofu hadi leo siamini jamii yetu nini inaamini. Kuna binti katika mtaa nnaoishi amemaliza darasa la 7 na baba yake ameamua asiendelee na masomo hata hivyo amepangiwa shule na serikali na mwaka ndo unaisha sasa. Basi tena muelekeo wa huyu binti umepotea na hata watu wakimuhamasisha amuendeleze hataki na hata wao wamuendeleze yule baba amekataa. Suala hili linanihuzunisha mimi kama msichana.

Bajeti ya serikali kutokana na suala la elimu bure wanafunzi wameongezeka kwa kiasi kikubwa mashuleni. Japo nia ya serikali ni kufanya nchi iwe na wasomi wengi lakini inatakiwa iongeze bajeti yake katika sekta ya elimu.

Kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi suala hili linachosha mwalimu kwani anatakiwa atumie nguvu kubwa ili wote tuelewe lakini idadi ya wanafunzi tuu ndo imeongezeka ila idadi ya walimu ni ile ile hivyo kwa kuwa hamna uwiano basi upande mmoja utaelemea ambao ni wa walimu ambal ni wachache.

Kwa namna hii inakuwa ngumu kumuuliza mwalimu swali katika kipindi kwani hatoi nafasi hiyo kwasababu anaogopa atarudia kufundisha na atatumia sauti kubwa na nguvu nyingi pia hata ukinyoosha kidole anakusubirisha mpaka akimaliza kufundisha na akimaliza anaondoka.

 Rushwa kwa walimu na wanafunzi. Tukianza na walimu kipindi cha kufanya mitihani walimu hutoa upendeleo kwa wanafunzi wanaowajua na watu wao wakaribu hata kama wanauwezo wa chini wanapandishwa juu.

Suala hili linatuvunja moyo wanafunzi tusiojulikana kwa walimu wetu. Kwa upande wa wanafunzi ni pale ambapo mwalimu anataka mahusiano na mwanafunzi walimu wengi wa kiume ndo wanaongoza na kama ukikataa basi utateseka mpaka unapomaliza shule.

Hili limenikuta mwalimu alinitaka kimapenzi lakini nilikataa basi kutokana na jambo hilo nilianza kuteswa nilisurubiwa sana nikashindwa nikaenda kushtaki kwa mama bahati nzuri mama yangu hana jambo dogo mbele ya mwanae alifika shuleni na polisi kumkamata mwalimu kwasababj nilikuwa na ushahidi wa barua zake basi hakuweza kukataa.

Haikuishia hapo nguvu ya pesa iliongea basi akatoka polisi lakini mkuu wa shule alimhamisha kwasababu aliona anaichafua shule. Kwangu hilo halikuwa suluhisho kwani huko aendako bado ataendelea tu na tabia yake lakini kwangu ndo nikaponea hapo. Kwa wanafunzi jambo hili ni gumu sana katika elimu yetu.

Ofa ya kusoma nje ya nchi KWeli ni wenye uwezo wa kimaisha ndio hupelekwa kusoma nje za nchi na wazaz wao lakini kilichonishangaza ni kwamba wageni kutoka nje za nchi wanafaidika na wataalamu kutoka nchini kwetu.

Kwani watu wenye uwezo mkubwa kielimu hupewa nafasi ya kusoma nje ya nchi na wasio na uwezo hubaki nchini. Jambo hili linasababisha nchi isiendelee pia kwasababu wenye kuiendeleza kwa kiwango kikubwa hawapo wamebaki wenye kiwango kidogo tuu ndio maana tunasema nchi yetu haiendelei kumbe watu wetu wamechukuliwa.

Miradi shule zinanoongoza kwa kuwa na mazingira mazuri na kufaulisha ni zenye miradi. Haswa shule za mjini ndio zenye miradi mfano malazi ya magari na maduka ambayo shule inakusanya maoato na kufanyia ukarabati wa shule na kuajiri walimu binafsi ambao wanashika nafasi kuwafundisha wanafunzi ambao katika shule hiyo waalimu wa masomo yao hawajaajiriwa.

Kutokana na hivyo shule za mjini pekee ndio zinazoonekana kufaulisha na za kata huonekana ni shule za msingi tuu.

 Posho Kila litu kinahitaji amsha amsha ili kiende kwa kasi. Walimu wa shule za serikali hawapewi posho hivyo basi hata kufundisha kwao hawakutilii maanani wanafundisha kidogo na hata mitihani ikikaribia wanasema tujisomee wenyewe.

Jambo hili linatutatiza wanafunzi kwani huwa hatuwezi kufanya kila kitu kwa uwezo wetu tunahitaji uwezo wa walimu pia lakini walimu hawatoi ushirikiano. Mfano tukiwa tunawahitaji walimu kutufundisha baada ya mda wa vipindi hawakubali kwasababu hawalipwi hivyo wanaona ni kupoteza muda tuu. Na haswa katika kufaulu kunahusisha kufanya mitihani kwa kiasi kikubwa lakini walimu hawatungi mitihani na wakitunga hawasimamii kwani kwasiku kufanya mitihani miwili kunapita mda wa vipindi hivyo wanaondoka na kuona ni kupoteza mda tuu bora wakafanye biashara zao.

 Upangaji Kimadaraja na kupangiwa shule. Wanafunzi wenye uwezo wa juu yaani daraja A na B kwa darasa la 7 hupangiwa shule za vipaji na wengine hupangiwa shule za kata. Jambo hili linaleta matabaka kati yetu kwani wanaosoma shule za mjini hujiona ni bora zaidi kuliko wa chini.

Na hawa wa chini wakiachwa wenyewe nani atawashika mkono? Na hao wenye uwezo wote mwisho wao ni nini? Wengi wapo shule za kata na wachache shule za vipaji hivyo kwenye kufaulu shule za kata zipo chini na zinaendelea kuwa chini kwasababu ukiachana na ufundishaji wa mwalimu kuna kuelekezana wanafunzi kwa wanafunzi je kama wanafunzi wote hamjui?

Nani amuelekeze mwenzie hivyo basi inabidi tuchanganywe wenye uwezo na wasio na uwezo ili tushirikiane pamoja.

Ufanisi wa walimu Asilimia kubwa walimu sio wote wanapenda kusomea ualimu bali serikali huwapangia kusomea ualimu.

Jambo hili linasababisha walimu wasiwe wafanisi na kazi zao kwasababu hawapendi wanachokifanya. Mwalimu ndio kila kitu kwasababu yeye ndie kamfundisha raisi, waziri, mbunge, daktari, hakumu, mwandishi wa habari n.k lakini serikali inachukua watu wenye kiwango cha chini cha ufaulu na kuwapangia kusomea ualimu.

Kwaiyo kama hao walimu walikuwa na kiwango cha chini cha ufaulu je watatoa wanafunzi wenye kiwango cha juu cha ufaulu? Hili ni tatizo kubwa sana katika sekta ya elimu nchini.

Ajira Maelfu ya wasomi hawajaajiriwa je mimi ntaajiriwa? Hili swali linaulizwa na wanafunzi wengi sana hivi sasa lakini ukilifikiria sana na ukiangalia na hali ya nchi huwezi kuona umuhimu wa elimu hata theruthi. Hivyo basi wengi wao huachana na elimu na kuanza maisha ya mtaani.

Hili linaongeza Asilimia ya watu tegemezi tena haswa vijana. Kama nchini kwetu ajira ingekuwa ukimaliza elimu naamini kila mtu angesoma na angesoma kwa bidii sana ili apate ajira lakini watu wanaona haina maana ndio maana matukio mengi yasiyofaa yanaongezeka kama vile uhalifu (PANYA ROAD) Kutokana na ukosefu wa elimu na ajira pia.

Thamani ya Elimu imeshuka sana nchini hivyo ajira kwa vijana ziongezeke ili kuchochea ufaulu katika sekta ya elimu.

Masomo kwa Maisha baada ya shule Shule chache sana hufundisha masomo haya ambayo yanakuza vipaji na kumuandaa mwanafunzi kujikomboa na maisha baada ya shule mfano somo la upishi, ushonaji na uchoraji.

Masomo hayo yanamanufaa kwa wanafunzi baada ya shule lakini yanafundishwa kwa uchache na sio masomo ya lazima. Hili ndio tatizo zaidi masomo ya lazima mwanafunzi akirudi nyumbani baada ya kumaliza shule hata hayamsaidii mfano Jiografia na Historia mwanafunzi akirudi anajua historia na kuwahadithia nani na yeye pekee ndo aliesoma mtaani?

Na Jiografia anaitumia wapi na hakuna hata wa kumuelekeza akamuelewa? Lakini kwa shule zinazofundisha masomo ya ufundi stadi yanafanywa ya ziada mfano uhunzi kijana akirudi nyumbani anatafuta mtaji anajiendeleza lakini mfumo wetu wa elimu hautilii kipaumbele jambo hilo.

Elimu ya ziada wazai wengi wanaamini mtoto akisoma (TUTION) elimu ya ziada itamsaidia zaidi. Sawa ni kweli lakini walimu wa hizo shule za ziada wanasifa za kuwa waalimu? Au wamejipa tu ualimu? Hili ni la kuzingatia kwa wazazi.

Anachofundishwa shule ni sahihi lakini akifika kwenye shule ya ziada mwalimu wake anamwambia hapana basi mwanafunzi anamuamini wa shule ya ziada zaidi ya mwalimu wa shule. Akifika kwenye mtihani anaandika uongo wa shule hulia na kufeli hili linashusha ufaulu kwa wanafunzi wengi nchini.

Naamini ndani ya habari yangu hii mabadiliko yatatokea kwa jamii , wizara ya Elimu, wazazi , walimu na wanafunzi pia.
MWISHO.
 
Back
Top Bottom