SoC03 Elimu ya Kidato cha Tano na Sita iondolewe

Stories of Change - 2023 Competition

Mkoba wa Mama

Senior Member
May 5, 2021
113
45
Kulingana na utaratibu uliopo hivi sasa, mwanafunzi anapo hitimu elimu ya sekondari (kidato cha nne) na kufikisha alama zinazohitajika anaweza kuchaguliwa kuendelea na elimu ya kidato cha tano na sita/kujiunga na vyuo vya kati (astashahada/stashahada)

1. Mwanafunzi atakayechaguliwa/kuchagua mwenyewe kujiunga na elimu ya kidato cha tano na sita, akihitimu kidato cha sita na kufikisha alama zinazohitajika, atajiunga na elimu ya chuo kikuu (shahada). Na ikitokea mwanafunzi amehitimu kidato cha sita na hajafikisha alama zinazohitajika ili ajiunge na elimu ya chuo kikuu, itambidi arudi nyuma atumie cheti cha elimu ya sekondari (kidato cha nne) ili aweze kutuma maombi ya kujiunga na elimu ya vyuo vya kati (astashahada/stashahada).
Kwa maana hiyo mwanafunzi huyo atakuwa amepoteza miaka miwili aliyosoma kidato cha tano na sita, lakini pia wazazi wanakuwa wameingia gharama pamoja na serikali kugharamia elimu kwa mda wa miaka miwili ambayo haina manufaa wala matokeo chanya kwa mwanafunzi mwenyewe, kwa wazazi na taifa kwa ujumla, kwa sababu mwanafunzi huyo anakuwa bado hana ujuzi katika fani yoyote ile utakao muwezesha yeye kuajiriwa ama kujiajiri.

2. Kwa mwanafunzi atakaye chaguliwa/kuchagua mwenyewe kujiunga na vyuo vya kati, atakapo hitimu anaweza kuchagua kuendelea na elimu ya chuo kikuu/kuajiriwa/kujiajiri mwenyewe kwa sababu tayari anakuwa na ujuzi na maarifa ya kutosha kulingana na fani aliyosoma.

Napendekeza kuondolewa kwa elimu ya kidato cha tano na sita kwa sababu, ni njia inayopoteza mda kwa wanafunzi na kuingiza gharama kubwa wazazi na serikali kugharamia elimu ambayo mwisho wa siku mwanafunzi itambidi arudi tena kutumia cheti cha elimu ya sekondari (kidato cha nne) ili kujiunga na vyuo vya kati.

Sasa kwa nini mwanafunzi huyu asitumie cheti cha elimu ya sekondari mara tu anapohitimu kidato cha nne na kujiunga moja kwa moja na elimu ya vyuo vya kati kulingana na masomo aliyofaulu au fani atakayo ichagua yeye.

Nitoe mfano mmoja hapa:
Unatakiwa kufika kituo D (elimu ya juu/maisha ya kujiajiri/ kuajiriwa) ukitokea kituo C (kidato cha nne), kuna njia mbili za kukuwezesha kufika kituo D, ambazo ni elimu ya kidato cha tano na sita (njia A) au vyuo vya kati (njia B).

Njia A ni fupi (miaka miwili ya kidato cha tano na sita) lakini inakatiza mtoni, na njia B ni ndefu (miaka mitatu ya stashahada) lakini haikatizi mtoni.

Endapo utaenda na njia A unakuwa hauna uhakika wa moja kwa moja wa kufika kituo D maana kuna uwezekano ukakuta mto umefurika maji na usiweze kuvuka, kwa hiyo itakulazimu urudi tena nyuma uanze safari upya kwa kutumia njia B ambayo haikatizi mtoni ili ikufikishe kituo D.

Ikitokea hivyo, unakua umetumia jumla ya miaka mitano kwa safari ambayo kama ungelichagua njia B tangu mwanzo ingelikugharimu mda wa miaka mitatu tu kufika kituo D.

Mfano huu namaanisha nini:
Elimu ya kidato cha tano na sita mwanafunzi anapohitimu na kushindwa kufikisha alama za kumuwezesha kujiunga na elimu ya chuo kikuu, itamlazimu arudi tena nyuma kutumia cheti cha elimu ya sekondari (kidato cha nne) ili aombe kujiunga na elimu ya vyuo vya kati (astashahada/stashahada).

Lakini mwanafunzi aliyehitimu elimu ya vyuo vya kati, tayari anakuwa na ujuzi wa kutosha kumuwezesha yeye kujiajiri/kuajiriwa mahali popote kulingana na fani aliyoisoma na anakuwa na uwezo wa kuendelea na elimu ya juu kama atahitaji kufanya hivyo.

Elimu ya vyuo vya kati inatolewa kwa kiasi kikubwa ikijikita katika ujuzi na kwa vitendo kwa sababu wanafunzi wanaenda kufanya mafunzo kwa vitendo na wakiwa huko wanasimamiwa na kukaguliwa ni tofauti na elimu ya kidato cha tano na sita ambapo wanafunzi wanatumia mda mwingi kukaa darasani kukariri masomo ya nadharia na hata wakiingia maabara, majaribio wanayoyafanya hayana uhalisia kwa asilimia 100 na maisha watakayo kutana nayo baada ya shule aidha ni katika kujiajiri/kuajiriwa.

Elimu ya kidato cha tano na sita kwa sasa haina umuhimu kwa nchi yetu, ni lazima tuchague njia moja iliyo bora zaidi, maana mtu anahitimu kidato cha sita akiwa hana ujuzi wowote ule tofauti na elimu ya vyuo vya kati, ni kwa nini serikali iendelee kuingia gharama kugharamia suala ambalo tunaweza kuachana nalo na kujikita katika njia moja na gharama hizo zote kuelekezwa katika kuboresha mazingira na miundombinu (hasa katika suala la teknolojia) ya kujifunzia na kufundishia katika vyuo vya kati ili viwe bora zaidi na vizalishe wataalamu mahili wenye ujuzi na ubora unaohitajika.

Ni maarifa gani/ujuzi gani wa ziada anaoupata mwanafunzi aliyepita elimu ya kidato cha tano na sita utakao msaidia yeye katika ulimwengu wa sasa. Ama ni kitu gani cha ziada chenye manufaa watakikosa wanafunzi iwapo elimu ya kidato cha tano na sita itaondolewa na kubakia na elimu ya vyuo vya kati tu.

Naomba wadau, wizara ya elimu na serikali kwa ujumla ilitazame suala hili, tusiendelee kuwa na mifumo ya elimu kwa sababu ilikuwepo tangu mwanzo, kwa sasa inatakiwa tutazame zaidi mabadiliko yaliyopo, ulimwengu umekuwa wa sayansi na teknolojia na unahitaji watu wenye ujuzi zaidi (ili kuwawezesha aidha kujiajiri ama kuwa na sifa za kuajiriwa na kuwa wabunifu zaidi katika nyanja mbalimbali) kitu ambacho elimu ya kidato cha tano na sita haiwezi kutupatia jibu la suala hilo, zaidi ya wanafunzi kukariri vitu ili waje wajibu mitihani wafaulu, tofauti na elimu ya vyuo vya kati, ambapo mwanafunzi anapata mda wa kutosha wa kufanya mafunzo kwa vitendo na tena katika uhalisia, hivyo kumuwezesha kuwa na maarifa, ujuzi wa kutosha, uwezo mkubwa wa ubunifu na utatuzi wa changamoto zinazoikabili dunia katika fani aliyoisomea.

Hivyo itumike elimu ya vyuo vya kati mara tu mwanafunzi anapohitimu kidato cha nne. Hii itasaidia vijana wengi kuwa na ujuzi mapema zaidi na kuwa wabunifu na wenye uwezo mkubwa wa kujiajiri na sio kutegemea kuajiriwa tu.

Serikali iweke utaratibu maalum mwanafunzi anapohitimu kidato cha nne aangaliwe ni masomo gani alikuwa akifanya vizuri zaidi tangu mwanzo na sio mtihani wa mwisho tu, ili aende kusomea fani inayoendana na masomo hayo, au mwanafunzi achague mwenyewe fani anayoona anaimudu na anauwezo wa kuisoma na baadae kuwa na ujuzi wa kutosha katika fani hiyo.

Ahsanteni.
 
maneno mengi ila hapo kwenye kituo d ndio nimeishia kusoma....mimi ni mufaika wa elimu pasipo kupitia form 5 and six...walikuja watu wanatoka five na six huko wameangukia pua pcb eka pcm wakaja kupiga certificate ya uhasibu au procure.... ila hawakuwa na maajabu yoyote full sup!? kwa hio ni kuchoshana akili tu kwenda five na six
 
Mimi huwa nawaza kama muhitimu wa chuo aliyekaa mtaani miaka nane (8 years) toa ile mitatu ya masomo na hajafanikiwa kupata kazi ya kutumia elimu aliyoisotea huwa anajisikiaje linapokuja suala la kumpeleka mwanae hadi elimu ya juu?

Elimu ya darasani sasa hivi hasa kwa mtoto wa maskini haina inachomsaidia uangaliwe utaratibu wa kuwapa mafunzo mbalimbali vijana ili angalao wakitoka hapo four au six wawe na wepesi kujichanganya mitaani tofauti na sasa kukaa kusubiri matokeo ili waende vyuo,point yangu hapa ni kwamba wakati anaposubiri matokeo awe na msukumo wa kwenda kujaribu yale maarifa aliyofundishwa akiona yana-apply kwenye maisha yake anakomaa humo humo siyo kama sasa wanaenda chuo wote wanamaliza na vyeti wote then wanamwagwa mitaani wote kugombania goal ambalo limeshajazwa na ndugu wa mabosi
 
Hivi ukitoa vyuo vya kati vya ufundi na mambo ya afya kuna kada gani nyingine mtu anaweza kusoma akitokea form four na akajiajiri?


Je asilimia ngapi ya Watanzania tumefikia kuwa na akili za kujiajiri kwa elimu tulizosomea?

Je elimu ya form four na vyuo vya kati inatosha kukidhi Tanzania tunayoenda nayo miaka 50 ijayo?

Mi nadhani Advance iwe option ila isiondolewe.
 
Hivi ukitoa vyuo vya kati vya ufundi na mambo ya afya kuna kada gani nyingine mtu anaweza kusoma akitokea form four na akajiajiri?


Je asilimia ngapi ya Watanzania tumefikia kuwa na akili za kujiajiri kwa elimu tulizosomea?

Je elimu ya form four na vyuo vya kati inatosha kukidhi Tanzania tunayoenda nayo miaka 50 ijayo?

Mi nadhani Advance iwe option ila isiondolewe.
Una akili sana ndugu yangu
 
Back
Top Bottom