Dunia haina usawa

SEHEMU YA 09

Godwin hakujibu kitu, akanyamaza, akakiinamisha kichwa chake chini, alipokiinua, macho yake yalikuwa mekundu na baada ya sekunde kadhaa machozi yakaanza kumtiririka mashavuni mwake kuonyesha kuchomwa na swali alilouliza Winfrida.

“What has happened to you?” (nini kimetokea?) aliuliza msichana huyo.
“I will tell you!” (nitakwambia)
“When?” (lini?)
Godwin hakujibu kitu, alichomwambia Winfrida ni kumuacha kwani alitakiwa kuendelea na kazi yake kama kawaida. Msichana huyo alikuwa na maswali mengi, akahisi kulikuwa na kitu kikubwa kilichotokea kwa mwanaume huyo.

Alitaka kufahamu, kila alipokutana naye swali lake lilikuwa lilelile kwamba ni kitu gani kilitokea mpaka kuishi maisha aliyokuwa akiishi. Godwin hakumjibu kitu, kila siku alimwambia kwamba angemwambia japokuwa hakumwambia siku ambayo angemueleza ukweli kuhusu maisha yake.

Baada ya kuwa karibu kwa miezi miwili huku kila siku msichana huyo akimuuliza swali hilohilo, hatimaye akamwambia kwamba alikuwa tayari kumuhadithia kila kitu ambacho kilitokea kwenye maisha yake.
Akamchukua na kumpeleka katika kibanda kimoja chakavu, akakaa naye mahali hapo. Winfrida alikuwa na kiu ya kutaka kusikia kile kilichokuwa kimetokea katika maisha ya mwanaume huyo.

“Godwin! Niambie ukweli! Nini kimetokea mpaka kuwa mpiga debe na masikini hivyo?” aliuliza Winfrida huku akimwangalia Godwin ambaye hapohapo akaanza kufungua vifungo vya shati lake na kisha kumuonyeshea maneno yaliyoandikwa kwa tattoo ya korosho, maneno yaliyosomeka ‘I WANT TO KNOW WHO KILLED MY DAD, MOM AND SISTER’ (ninataka kumjua aliyemuua baba, mama na dada yangu)

Winfrida alipoyasoma maneno hayo, akashtuka, akahisi kabisa kwamba kulikuwa na simulizi ndefu juu ya maisha ya mwanaume huyo. Akajiweka vizuri na kumuuliza kama alikuwa tayari kumwambia kuhusu kile kilichotokea katika maisha yake.

“Nitakwambia! Nitakuhadithia kila kitu,” alisema Godwin, akaingiza mkono mfukoni na kutoa kitambaa kichafu na kuanza kuyafuta machozi yake. Akajiweka sawa kwa lengo la kumuhadithia msichana huyo kila kitu kilichotokea, historia kali iliyomchoma moyo wake kila siku.
 
SEHEMU YA 10

25/10/1998, Dar Es Salaam
Hakukuwa na utulivu nchini Tanzania, kila mtu alikuwa kwenye presha kubwa juu ya uchaguzi mkuu ambao ulikuwa ukienda kufanyika mwaka huo.

Kila mtu mitaani alikuwa akizungumza lake, wapo waliokuwa wakikipenda chama tawala, Labour Party ambacho kilisimamisha mgombea wake mashuhuri, Ibrahim Bokasa lakini pia wapo waliokuwa wakikipenda chama cha upinzani, Tanzania National Party ambacho kilimsimamisha mwanaume mwenye nguvu, mvuto, aliyependwa kila kona, Melkizedek Mapoto.

Kwa mwaka huo, uchaguzi ulikuwa na nguvu kuliko miaka mingine ya nyuma, kila mtu alikuwa na uhakika kwamba huo ndiyo ungekuwa mwaka wa mwisho kwa chama tawala kuwa madarakani, kila mmoja aliamini kwamba Bwana Mapoto ndiye angekuwa rais mpya wa Tanzania kwani kila kona, jina lake lilikuwa likiimbwa huku watu wakipeperusha bendera ta chama chake.

Kila mtu aliyekuwa katika chama tawala aliogopa, waliuona mwisho wao, wananchi ambao kila siku walikuwa wakiwapigia kura kwa mwaka huo wakabadilika, hawakutaka kuongozwa na chama tawala tena, walihitaji kuwa na mabadiliko na hakukuwa na mtu ambaye alionekana kuwa na nguvu ya kuwaletea mabadiliko zaidi ya Bwana Mapoto.

Kila alipokwenda mikoani kwa ajili ya kampeni, alipokelewa vizuri, wakinamama walitandika kanga chini na kumtaka kukanyaga juu, wazee wa kimila hawakukubali, wao, walimchinjia ng’ombe na kumtabiria kwamba yeye ndiye angekuwa rais mpya wa nchi hiyo kwani watu walichoka kunyanyaswa na kwa kipindi hicho hakukuwa na kingine walichokihitaji zaidi ya mabadiliko tu.

Watu wengi wa Chama cha Labour wakajitoa kwenye chama chao na kujiunga na Chama cha Tanzania National Party ambapo waliamini kwamba kulikuwa na mabadiliko ya kweli ambayo yangewatoa katika maisha ya umasikini waliyokuwa wakiishi na kuwapeleka katika nchi ya maziwa na asali.
 
SEHEMU YA 11

Hali ilikuwa ni ya mvurugano ndani ya Chama cha Labour, hakukuwa na aliyeona dalili za ushindi mbele yao, Bwana Mapoto alitisha, alikuwa akitikisa kila sehemu na kwenye kila kona ya nchi ya Tanzania, jina lake liliimbwa kwa shangwe huku wengine wakisema kwamba hatimaye Mungu alisikia kilio chao na kumleta mtu aliyeahidi kuleta mabadiliko na kuipeleka Tanzania kuwa nchi yenye nguvu barani Afrika.

“Nimechanganyikiwa kwa furaha! Leo nimemgusa Mapoto,” alisema mwanaume mmoja, alikuwa amevalia kofia ya chama hicho, fulana, kwa jinsi alivyoonekana kuwa na uzalendo na chama hicho, alikuwa kama mtu aliyekunywa maji ya bendera.

“Natamani sana na mimi nikamguse. Huyu ndiye mgombea wa ukweli, ndiye rais wetu ambaye ataweza kututoa hapa tulipokuwa. Maisha yamekuwa magumu sana kisa Labour Party! Huu ndiyo mwisho wao, yaani nikifika kwenye chumba cha kupigia kura, lazima niwachinje,” alisema jamaa mwingine huku akionekana kuwa na kiu ya kuhitaji mabadiliko.

Chama tawala kikachanganyikiwa, hawakuamini kile kilichokuwa kikiendelea. Hawakuona mahali pa kutokea, walizoea kwenda vijijini ambapo waliamini kwamba huko wangechukua watu wengi, kwa mwaka huo kila mmoja aliwashtukia, na walipokanyaga mguu tu, walikuwa wakizomewa na wakati mwingine kupigwa mawe.

“Jamani! Hali imebadilika, hebu zungumza na rais mstaafu,” alisema mwenyekiti wa kampeni, Bwana Edward Mrope.
Simu ikapigwa kwa rais aliyemaliza muda wake, alipewa taarifa juu ya hali ilivyokuwa imebadilika.

Kule vijijini ambapo ndipo walikuwa wakipategemea, palibadilika na kila walipokanyaga, ni jina la Mapoto tu ndiyo lililokuwa likisikika.
“Unasemaje?” aliuliza rais mstaafu.
“Huku hali ni mbaya, kila kona Mapoto, Mapoto, Mapoto tu,” alisema mwenyekiti wa kampeni maneno yaliyomfanya rais huyo kushtuka.

“Haiwezekani!”
“Huo ndiyo ukweli mkuu! Tufanye nini?”
“Nipigie simu baada ya dakika tano,” alisema rais mstaafu na kukata simu.
 
SEHEMU YA 12

Alichanganyikiwa, hakuamini, hali ilikuwa imebadilika, moyo wake ulijuta kwani kwa mambo aliyokuwa ameyafanya, mambo ya ubabe, ya kujiona kwamba yeye ndiyo yeye ndiyo ambayo yalikuwa yakikigharimu chama hicho na kuona hawafai kabisa.

Hakutaka kukubali, hakutaka kuona chama kikimfia mikononi mwake, kwa haraka sana akachukua simu yake na kumpigia katibu wa chama hicho, Bwana Idrisa Awadh na kumwambia kwamba iwe isiwe ilikuwa ni lazima kuhakikisha kwamba chama chao kinapata ushindi kwa namna yoyote ile.

“Hakuna tatizo! Hilo suala niachie mimi! Wewe wala usiwe na hofu na wananchi, sisi ndiyo tunaishikilia nchi hii na kujua ni wapi pa kufanyia kazi,” alisema katibu huyo.
“Nakuamini!”
“Siwezi kukuangusha mkubwa. Kama ulivyoniamini mwaka 1993, unatakiwa kuniamini na sasa hivi,” alisikika katibu huyo.

Kidogo moyo wake ukapata ahueni, alimwamini katibu wake, alikuwa mtu machachari aliyeweza kucheza na masanduku ya kura, kwake, hiyo ilikuwa ni kazi ndogo na kama alivyofanya mwaka 1993 ndivyo ambavyo angefanya mwaka huo.

Chama cha Tanzania National Party kiliendelea kusonga mbele, kwa kipindi hicho walijizatiti vijijini, waliamini kwamba watu wote wa mjini walikuwa watu wao kwani kila kona kulitawala bendera zao na kila mtu aliyekuwa akiuliza, alionyesha ishara ya mabadiliko kwamba alihitaji ladha mpya ya chama na si ileile ya miaka yote.

Bwana Mapoto akaonekana kuwa mwiba mkali kwa chama tawala, kila alipopita, watu walipomuona, wengine walizimia, kwenye kila mkutano wa kampeni watu walijaa huku neno mabadiliko likisikika kila kona.

“Nu nene ndinghaya uyu ng’wenekele (na mimi namtaka huyuhuyu) alisema mwanamke aliyekadiriwa kuwa na miaka themanini, hata naye alihitaji mabadiliko.

“Nu nene mama nanoga na kikalile iki,” (hata mimi bibi! Nimechoka na maisha haya) alisema msichana mmoja huku wakimwangalia Mapoto aliyekuwa jukwaani katika Uwanja wa CCM Kirumba alipokuwa akihutubia.
 
SEHEMU YA 13

Kadiri siku zilivyozidi kwenda mbele, hali iliendelea kuwa ngumu kwa chama tawala, hata kabla siku ya kupiga kura haijafika, tayari walijiona kushindwa na ilitakiwa kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha kwamba wanaubakiza urais huo mikononi mwao.

“Nimekuja na sera moja tu ya kutaka mabadiliko. Mmekuwa hampati maisha mazuri kwa kipindi gani? Nchi yetu imekuwa ikichekwa kwa kipindi kirefu, tuna kila sababu ya kuwa na uchumi mkubwa, tuna madini ambayo hata sehemu nyingine hakuna, tuna vyanzo vingi sana vya mapato.

Mungu hakuwa mjinga kutupa mbuga za wanyama, madini na vitu vingine, alikuwa na maana ila kwa sababu ya watu wachache tu, nchi haikusonga mbele. Huu ni muda wenu kuchagua, kama mngependa kunywa chai bila sukari au kula asali,” alisema Bwana Mapoto kwa sauti kubwa.

“Tunataka asaliiiiiiiiiiiiiii…” uliitikia uwanja mzima.
“Basi msifanye makosa tarehe 19!” alisema Bwana Mapoto na kuibua makofi ya shangwe uwanjani hapo.

Je, nini kitaendelea?
 
SEHEMU YA 14

“Mke wangu, unaamini kwamba tunakwenda kukaa ikulu?” aliuliza Bwana Mapoto huku akimwangalia mke wake aliyekuwa akimwangalia muda wote.
“Naamini hilo! Ila sidhani kama hawa wa chama tawala watakubali,” alisema mkewe, mwanamke mrembo aliyeitwa kwa jina la Rosemary.

“Watakubali tu! Kwa kipindi hiki tutawazuia kwa kila hali kuhakikisha hakuna wizi wa kura, tutaziba njia zote ambazo zinaonekana kutoa mwanya mkubwa wa wizi wa kura.”
“Kama mtaziba njia zote, naamini kwamba tutaingia huko,” alisema Rosemary huku uso wake ukiwa kwenye tabasamu pana.

“Ninaumia sana nikiwaona Watanzania wanateseka, wanaishi katika maisha yenye maumivu makubwa. Mungu si mpumbavu kutuzawadia madini, mbuga za wanyama na mlima Kilimanjaro, naamini kwamba alitaka watu wanufaike na kujivunia maisha yao, lakini cha kushangaza, nchi hiyohiyo yenye kila kitu ndiyo nchi masikini. Nitapambana! Nitapambana mke wangu!” alisema Mapoto huku akionekana kuwa mtu mwenye maumivu makubwa moyoni mwake.

Alimaanisha alichokuwa akikizungumza, alihitaji kuibadilisha Tanzania, aliyaona maumivu ya Watanzania, jinsi walivyokuwa wakiteseka, hakutaka kuendelea kuangalia maumivu hayo, alitaka kupambana kwa hali na mali kuhakikisha kwamba kila kitu kinakuwa vizuri na Watanzania waanze kujivunia nchi yao.

Mbali na kuwafikiria Watanzania, aliwafikiria watoto wake wawili, Godwin na Irene waliokuwa na miaka saba. Alitaka kuwapa maisha bora, alijua kwamba kupitia wao angepata wajukuu ambao aliamini kwamba kama angeyatengeneza maisha yao basi hata hao wajukuu wangekuja kuishi vizuri.

Alikuwa katika mapambano makubwa, hakutaka kushindwa, hakutaka kurudi nyuma, mbele yake aliyaona mafanikio makubwa, aliona jinsi Watanzania walivyokuwa wakimuunga mkono, aliamini kwamba Watanzania wote hao wangempigia kura kwa sababu kila mtu kwa kipindi hicho alihitaji mabadiliko.
“Nitapambana kwa ajili ya Godwin na Irene,” alisema Mapoto.

Wakati akizungumza na mkewe, watoto wake walikuwa shuleni, walikuwa miongoni mwa watoto waliokuwa wakisoma katika shule ya watoto matajiri na viongozi serikalini, St. Marie iliyokuwa Masaki jijini Dar Es Salaam.
 
SEHEMU YA 15

Alitaka watoto wake wapate elimu bora kwa ajili ya maisha yao ya baadaye na kila siku dereva wao alikuwa na jukumu la kuwapeleka shule na kuwarudisha nyumbani.
Kila siku Mapoto alipata muda wa kukaa na watoto wake na kuzungumza nao.

Aliwapenda, alijitahidi sana kuwaweka karibu nao kwani aliamini kwa kufanya hivyo ingekuwa rahisi kugundua matatizo waliyokuwa wakikutana nayo kila wanapokuwa shuleni au sehemu nyingine.
Urafiki mkubwa ukatawala, watoto wake walikuwa kila kitu katika maisha yake. Alijiahidi kwamba ni lazima ailinde familia yake, hakutaka mtu yeyote yule aiingilie, aliithamini na kuipa nafasi ya kwanza maishani mwake.

Wakati Irene akiwa mzungumzaji sana, mtundu lakini ilikuwa tofauti kwa Godwin, alikuwa kijana mpole, mkimya ambaye hakuwa mzungumzaji kabisa. Kila wakati alionekana kama mtoto aliyekuwa na mambo mengi kichwani mwake, alipokuwa akionewa au hata kukasirishwa, hakuwa akikasirika, alipendwa na wazazi wake kwa sababu ya hali ya upole aliyokuwa nayo.

“Godwin! Unataka kuwa nani ukikua?” aliuliza baba yake.
“Nataka kuwa mchungaji!” alijibu.
“Kwa nini?”
“Nataka niombee watu wapone kama Reinhard Bonnke,” alijibu Godwin huku akitoa tabasamu pana.
Hicho ndicho alichokuwa akikitaka, kila siku walipokuwa nyumbani, baba yake aliwawekea televisheni ya Praise And Worship kwa ajili ya kuangalia mahubiri na kujifunza neno la Mungu.

Kila alipokuwa akimuona Mwinjilisti Reinhard Bonnke akihubiri, moyo wake ulisisimka, alifurahia huku naye akitamani sana kuwa kama mwinjilisti huyo ambaye alikuwa akivuma sana duniani miaka hiyo.

“Na wewe Irene?”
“Niongee jukwaani kama wewe!”
“Unamaanisha mwanasiasa?”
“Eeeh!”
“Wote mtafanikiwa. Mtakuwa kama mnavyotaka kuwa,” alisema Mapoto huku akiwaangalia watoto wake.

Kampeni hazikuisha mitaani, mara kwa mara alikuwa akizungumza na wananchi na kuwaomba kura zao kwani alikuwa na ndoto za kuingia ikulu na kuibadilisha Tanzania ambayo kadiri miaka ilivyozidi kwenda mbele ndivyo ilivyokuwa ikiharibika kutokana na viongozi wengi kutumia nafasi zao kupiga madili makubwa ya pesa.
 
SEHEMU YA 16

Viongozi wa Chama cha Labour Party hawakutaka kutulia, waliweka vikao vingi wakijadili namna ya kumzuia Mapoto ambaye alionekana kuwa mwiba wa kuotea mbali.

Kwenye kila kikao walichokuwa wakikaa na kupanga mipango, walishtukia kuiona mipango yao katika magazeti na masikioni mwa watu hali iliyowaonyeshea kwamba kulikuwa na watu ndani ya chama ambao walikuwa wakishirikiana na Chama cha Tanzania National Party ambao walitoa kila mipango waliyokuwa wakiipanga.

Rais mstaafu aliliona hilo hivyo alichokuwa akikifanya ni kumuita katibu wa chama na mwenyekiti wa kampeni na kuzungumza nao. Walipanga mipango lukuki lakini mpango mkubwa ambao ulitawala vichwani mwao ni namna ya kuiba kura kwani waliamini kwamba kama wasingefanya hivyo basi Mapoto angeweza kuingia ikulu.

“Kuna mchezo nitaucheza,” alisema Hawadh.
“Upi?”
“Sisi si ndiyo tutakaotoa fedha za kutengeneza karatasi za kupigia kura?”
“Ndiyo!”
“Basi tutacheza na karatasi hizo na matokeo utayaona,” alisema Awadh.
Huo ndiyo ulikuwa mpango uliotakiwa kufanywa, walijua dhahiri kwamba wasingeweza kushinda uchaguzi huo kutokana na Watanzania wengi kumkubali Mapoto hivyo walichokitaka ni kucheza na karatasi za kura tu.

Siku zikakatika mpaka siku ya mwisho ya uchaguzi ambapo watu wengi wakajitokeza katika vituo vya kupigia kura huku idadi kubwa wakiwa na dhamira ya kukiondoa chama tawala madarakani.
Kura zikapigwa, kwa sababu kila mtu aliogopa kura kuibwa, wapo waliokesha huku wakifuatilia kila kitu kilichokuwa kikiendelea, mpaka kura zilipopakizwa ndani ya magari na kuondolewa katika maeneo ya kupigia kura, kila mmoja alikuwa akifuatilia.

Siku hiyo, Mapoto na viongozi wengine wa Chama cha Tanzania National Party walikuwa makao makuu wakifuatilia kila kitu kilichokuwa kikiendelea. Waliwasambaza vijana wao sehemu mbalimbali na kila kura za vituo zilizokuwa zikitangazwa waliwatumia matokeo haraka sana.
 
SEHEMU YA 17

Kila mmoja akaona kwamba hiyo ndiyo nafasi waliyokuwa wakiisubiri kwani kwa maeneo ya mijini, hakukuwa na wasiwasi, waliamini kwamba walifanikiwa kwa asilimia mia moja, kazi kubwa ilikuwa ni kwa vijijini ambapo waliamini kwamba kama wasingekuwa makini, basi huko wangeweza kupigwa vibaya.

“Vipi huko?” aliuliza Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania National Party, Bwana Luzukumi.
“Huku poa. Mwanza nzima tumekimbiza! Tena taarifa zinasema Kanda ya Ziwa yote tumetoka kidedea,” aliongezea mtoa taarifa huyo.

“Safi sana!” alisema Luzukumi pasipo kufahamu kwamba upande wa pili, chama tawala walikuwa makini mno, walikuwa tayari kupoteza uchaguzi wowote ila si wa mwaka huo, hivyo walijipanga vilivyo. Wakati wao wakipigia mahesabu 12345 wenzao walihesabu ABCDE.

“Tumeuangangusha mbuyu,” alisikika katibu wa Chama cha Labour Party akimwambia rais mstaafu.
“Unasemaje?”
“Fungua televisheni uanze kufuatilia,” alisema Awadh huku uso wake ukiwa na tabasamu tele. Harakaharaka rais akafungua Global TV na kuanza kufuatilia.
 
SEHEMU YA 18

Hakukuwa na mtu wa Chama cha Labour Party ambaye alikuwa radhi kuona nchi ikienda upande wa wapinzani, walikuwa tayari kupoteza kila kitu, hata familia zao ziteketee lakini si kukubali kuona nchi ikichukuliwa na chama pinzani.

Wakati chama pinzani cha Tanzania National Party wakihangaika na wananchi kwamba wafanikiwe kuichukua nchi ya Tanzania wenzao walichokifanya ni kucheza na karatasi za kura.

Walijua kwamba serikali ndiyo ingesimamia mchakato mzima, kwao, chama chao ndicho kilikuwa serikali yenyewe hivyo walichokifanya ni kuamuru zitengenezwe karatasi ambazo zitazifanya kura za wapinzani wote ziende upande wa pili, zifanye hivyo baada ya dakika thelathini.

Hilo halikuwa tatizo, Wachina wakaingia mchezoni na kufanya kazi hiyo ambayo kwao haikuwa na ugumu wowote ile. Waliifanya ndani ya siku tatu, yale masanduku yaliyokuja na karatasi za kupiga kura yakachomwa moto na kuletwa mengine, hayo yote yalifanyika kisiri na hakukuwa na mtu aliyejua.

Siku ilipofika, watu wakaingia vyumbani, wakapiga kura kwa nguvu zote na kila walipotoka walionyesha alama ya kuchinja kama ishara ya kuwachinja Tanzania Labour ndani ya chumba kile pasipo kugundua mchezo mzima uliokuwa umechezwa.

“Nimemchinja! Sikuwa na huruma. Nilipofika, nikamwangalia Ibrahim Bokasa na kumwambia kwamba sasa hivi na wewe unatakiwa kuwa raia wa kawaida kama mimi, baada ya hapo, nikapiga tiki ya uhakika kwa Mapoto,” alisema jamaa mmoja, si yeye tu, kila mtu alisema kwamba ndani alimpa kura Mapoto kwani ndiye aliyeonekana kuwa mtu sahihi.

Mchakato wa kura ukafanikiwa na hatimaye baada ya siku mbili watu kujiandaa kupokea matokeo yao. Kila mmoja alikuwa na uhakika kwamba hiyo ilikuwa siku yao ya ukombozi kwani kila mtu alikuwa amechoka na kwa moyo mmoja alitaka kusikia Mapoto akitangazwa na kuwa rais wa nchi hiyo.
 
SEHEMU YA 19

Kila mmoja akawasha televisheni na kuanza kumwangalia mkurugenzi wa tume ya uchaguzi jinsi alivyokuwa akitangaza matokeo. Alizungumza kwa sauti ya upole, tabasamu pana lilikuwa usoni mwake hali iliyowapa matumaini wananchi kwamba siku hiyo ndiyo ilikuwa siku ya ukombozi ambayo ingekuwa historia kizazi mpaka kizazi.

Matokeo yalianza kutangazwa, kadiri muda ulivyozidi kwenda mbele, hali ya hewa ilizidi kubadilika, katika majimbo yote makubwa ambayo yalikuwa na watu wengi, Bokasa aliongoza kwa asilimia nyingi na kummwaga mpinzani wake kwa kura zisizokuwa na idadi.

Kila mmoja alikunja sura yake, wengine wakahisi labda matokeo yaliyokuwa yakitangazwa na mkurugenzi wa tume yalikuwa ya uongo lakini hawakujua chanzo kilikuwa nini, hawakujua kwamba mchezo huo ulichezwa hata kabla ya masanduku ya kura kumfikia mkurugenzi huyo.

“Haiwezekani! Haiwezekani kushindwa uchaguzi huu!” alisikika jamaa mmoja akipayuka, aliongea kwa sauti kama mtu aliyekuwa amechanganyikiwa na kile alichokuwa akikisikia.

Si yeye tu, kila mtu aliyekuwa mahali hapo alichanganyikiwa. Kwa jinsi matokeo yalivyotangazwa, kwa Dar es Salaam, Mwanza, Arusha na mikoa mingine mikubwa, ni Chama cha Labour Party ndicho kilichokuwa kimeongoza kwa kura nyingi.

Watu hawakukubali, hawakutaka kuona wakishindwa, hawakukubali kabisa kuona Chama cha Labour Party kikiendelea kuongoza nchi na wakati kila mtu hakuwa akikitaka, kila mmoja alitaka kuona kikiondoka madarakani kama vyama vingine katika nchi nyingine.

Vijana wakajipanga, walitaka kuingia mitaani kwa ajili ya kuandamana, hawakutaka kukubali, waliyataka mabadiliko kwa karatasi lakini ilishindikana na kitu pekee walichokitaka ni kuyaleta mabadiliko kwa kupitia silaha.

Polisi walipewa taarifa juu ya maandamano makubwa yaliyotaka kufanyika, japokuwa watu walitangaziwa kutokufanya hivyo lakini hawakutaka kukubali, wakajipanga vijana zaidi ya elfu mbili na kuingia mitaani.

Wote walikuwa na kaulimbiu ya kuitaka nchi yao. Hawakuogopa polisi, walisonga mbele kuelekea ikulu kwamba hata kama hawakupewa nchi yao basi ilikuwa ni bora kukosa wote, kama vipi wachome moto ikulu.
 
SEHEMU YA 20

“Watu wote mnatakiwa kurudi nyumbani, hamruhusiwi kusogea mbele zaidi,” ilisikika sauti kwenye kipaza sauti, aliyekuwa akizungumza alikuwa Kamanda Mkuu Kanda ya Dar es Salaam, Abou Ishimeri.

“Tunataka nchi yetu! Yaani msituzingue kabisa. Leo ndiyo mtakiona,” alisema mwanaume mmoja, mkononi mwake alikuwa na kidumu kilichokuwa na mafuta ya petroli.

Kila mmoja alikuwa na nia moja moyoni mwake, kwa kipindi hicho hakukuwa na aliyejali kama polisi waliokuwa mbele yao walikuwa na mabomu ya machozi na risasi za moto, kitu walichokiangalia ni kufanya maandamano ya kuelekea ikulu na kuichoma moto.

“Tufanye nini?” aliuliza polisi mmoja.
Simu ikapigwa mpaka kwa Kamanda Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Andrew Kizota na kumwambia kile kilichokuwa kikiendelea ambapo kamanda huyo akawaambia kwamba huo ulikuwa ni muda wa kutumia mabomu ya machozi, na kama kungekuwa na ulazima wa kutumia risasi za moto basi ziwe kupiga hewani na si kuwapiga raia.

Hilo ndilo lililofanya, zikapigwa risasi tatu hewani na kupigwa mabomu manne ya machozi kuelekea kwenye kundi lile la watu. Kila mtu aliogopa, milio ya risasi ikawachanganya na kwa jinsi moshi mkubwa ulivyokuwa ukitanda ndiyo ukawavuruga kabisa na kuanza kukimbia hovyo.

Hiyo ndiyo ilikuwa nafasi ya polisi kufanya kile walichotakiwa kufanya, wakawafuata raia na kuanza kuwapiga hali iliyoanzisha mtafaruku mkubwa mahali hapo.

Je, nini kitaendelea
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom