Dk Slaa: Nyongeza ya mishahara kiini macho

Sokomoko

JF-Expert Member
Mar 29, 2008
1,915
127
Salim Said, Kwimba
MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chadema, Dk Willibrod Slaa, amesema kwamba nyongeza ya mishahara ya wafanyakazi iliyofanyika hivi karibuni ni kwa ajili ya kutafutia kura na hakitakuwapo kama CCM itarudi madarakani Oktoba mwaka huu.Alisema kiwango cha fedha zilizoingizwa katika mishahara ya wafanyakazi kuanzia mwezi uliopita, zitatoweka baada ya Uchaguzi Mkuu kwa sababu hazikupitia kwenye mfumo rasmi wa kuongeza mishahara.
“Nataka niwaambie wafanyakazi kuwa wameliwa kwani fedha hizo zimeingizwa hivi sasa na baada ya uchaguzi hamtaziona kwa sababu haziko katika mfumo wa mishahara,” alisema Dk Slaa.

Alisema fedha hizo ziko kinyume na sheria na ndio maana Msajili wa Vyama Vya Siasa, John Tendwa, alikataa pingamizi na malalamiko ya Chadema kuhusu Jakaya Kikwete na nyongeza ya mishahara.
“Kwa kuwa mishahara hiyo ni kinyume na sheria ndio maana Tendwa akatupilia mbali pingamizi letu dhidi ya Kikwete,” alisema Dk Slaa.
Alisema chama chake kinataka kukiong’oa madarakani Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa sababu kimeshindwa kutekeleza kile walichoahidi Watanzania.
Aidha, Dk Slaa, alisema iwapo atafanikiwa kuingia Ikulu katika Uchaguzi Mkuu wa 2010, jambo la kwanza serikali yake itafumua mishahara ya wabunge na kuweka kiwango cha uwiano baina yao na watumishi wa umma.

Akihutubia mamia ya wananchi katika Uwanja wa Ngudu, Kwimba, mkoani Mwanza, Dk Slaa, alisema Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, aliwang’oa Wazungu nchini kwasababu walishindwa kutekeleza ahadi yao kwa wananchi.
“Tunataka kuing’oa serikali ya CCM kwa sababu imeshindwa kutekeleza ahadi zake kwa Watanzania, Mwalimu Nyerere aliwang’oa Wazungu si kwa sababu ni wabaya bali walishindwa kutimiza ahadi yao kwa wananchi ya kuwapa maisha bora,” alisema Dk Slaa.

Alisema Watanzania wa leo sio wale wa miaka ya 1960 na kwamba wanajua kila kitu kinachosemwa na serikali kama ni kweli au uongo.
“Serikali ikisema imejenga barabara, shule, zahanati wanajua kama ni kweli au wanadanganywa na pia wanajua ni shilingi ngapi zimeibwa na vigogo wa serikali,” alisema Dk Slaa.
Dk Slaa aliongeza kuwa, “Hatuna namna lazima CCM tuiweke pembeni na kwa sababu imeshindwa kutekeleza kile ilichowaahidi wananchi wa Tanzania.”

Alisema idadi ya Watanzania masikini ambao wanashindwa kumudu hata mlo wao mmoja wa siku, imekuwa na kufikia 13 milioni kwa takwimu za serikali.
“Nyumba zao ni mbovu hazitamaniki, afya zao hazifikiriki na huduma za jamii hazitamaniki, kazi yetu tutashusha bei ya bati hadi chini ya Sh5000 na simenti ili watu wajenge nyumba bora,” alisema Dk Slaa.
Alisema serikali yake itafuta walimu wote wa cheti na stashahada katika shule za sekondari na badala yake wataanzia na walimu wa kuanzia ngazi ya shahada kwa lengo la kukuza elimu.

“Tutatoa elimu bure kuanzia shule ya awali hadi kidato cha sita na afya bure kuanzia kituo cha afya hadi hospitali ya rufaa,” alisema, Dk Slaa, mbele ya ofisi za CCM Wilaya ya Kwimba.
Alisema CCM imewauza Watanzania kwa thamani ya fulana, khanga, shati, vitambaa vya kichwani, supu, ubwabwa, pombe na rushwa ya Sh 2,000.

“Ndugu zangu supu na pombe itawaponza, hakuna atakayewatetea kwa rushwa, pombe, supu au ubwabwa,” alisema Dk Slaa.
Dk Slaa alisema wabunge na baadhi ya viongozi wa ngazi za juu serikalini ndio walisababisha umasikini wa kumpindukia kwa Watanzania pamoja na kuwadidimiza, kwa kujiwekea viwango vikubwa vya mishahara kuliko watumishi wengine.

“Hili ni bomu lilitongenezwa kwa kujenga matabaka katika viwango vya mishahara na hatupendi kuwa na bomu, hivyo ndio maana tunataka kuing’oa CCM,” alisema Dk Slaa.
Alisema wabunge wanakaa katika vikao angalau kwa miezi sita kwa mwaka, ambapo kwa siku kila mmoja hulipwa posho ya Sh180,000 na Sh2500 kwa lita moja ya mafuta.

“Hivi ni wapi Tanzania hii lita ya mafuta ni Sh2,500? Kwa posho hizi ukijumlisha na mshahara wa Sh7 milioni hujajenga magorofa tu, ndio maana mtu unamuona muda mchache baada ya kuwa mbunge ana magorofa,” alisema Dk Slaa.
Dk Slaa alisema, “Hivyo jambo la kwanza tukiingia serikalini tutafumua mfumo wa mishahara ya wabunge ili iweze kuwiana na watumishi wengine wa umma.”
Alisema ahadi yao pia kwa watumishi wa umma ipo palepale kwamba kiwango cha chini cha mishahara kitakuwa Sh315,000 kwa sababu wanahitaji kura za wafanyakazi 350,000.

Alisema mshahara wa Sh7 milioni na posho ya Sh180 kwa siku hautakuwapo katika serikali ya Chadema.
Alisema tabia ya kutenga Sh30 bilioni kwa ajili ya chai katika maofisi ya serikali itakoma katika serikali ya Chadema na fedha zote hizo zitaingizwa shuleni ili malaika wa Kitanzania asilipia hata shilingi kuanzia awali hadi kidato cha sita.

“Dawa ni kusimamia, kudhibiti na kuingiza katika sekta ya elimu asilimia kubwa ya fedha zinazokusanywa kwa Watanzania. Pia tutafumua mikataba yote ya madini na kuingiza fedha zake katika elimu, kama madini hayana faida nasi ni bora yakae chini kwani hayaozi,” alisema Dk Slaa.
Alimtambulisha mke wa mtoto wa Baba wa Taifa, Madaraka Nyerere, Leticia, kuwa ndiye mgombea wa ubunge wa Jimbo la Kwimba kupitia Chadema.
“Huyu ni mke wa Mdaraka Nyerere, ndoa yake imefungwa Ikulu, amelelewa Ikulu, lakini mke wake baada ya kuona hali mbaya ya Watanzania wenzake ameamua kuingia katika kinyang’anyiro ili kuwakomboa,” alisema Dk Slaa huku akishangiliwa.

Alisema Wilaya ya Kwimba yenye wananchi 600,000 ina shule za msingi 150 huku zikiwa na walimu wa daraja la IIIA, 109, huku kwa upande wa sekondari shule 35 na walimu wa diploma 37.

“Je kuna mafanikio au hamna?,” alihoji Dk Slaa na kujibiwa hamnaaa!.
Alisema katika mikutano yao hawatafuti Chadema, CCM wala CUF bali wanatafuta Watanzania kwa sababu, ndio wenye matatizo.

“Matatizo hayajali kuwa huyu ni CCM au CUF au Chadema, bali yanamvaa kila Mtanzania, ukienda dukani huendi na kadi ya chama chochote, kila mtu atanunua sukari au mchele kwa bei moja,” alisema Dk Slaa.
 
Hawa jamaa ni wajanja sana, nimeona hii habari niirudishe ili tuijadili. Mie pengine sipo kwenye dunia hii hivi hii mishahara iliongezwa kwa kiwango gani? na mbona maisha yanazidi kupanda? Umeme juu, kodi za nyumba zimeongezeka na maisha bora yamekuwa ndoto!
 
Jk alichofanya ni bonge moja la uhuni tena wa karne.ni sawa na mtoto kulia njaa halafu baba anampa pipi na ananyamaza kulia.
 
Hawa jamaa ni wajanja sana, nimeona hii habari niirudishe ili tuijadili. Mie pengine sipo kwenye dunia hii hivi hii mishahara iliongezwa kwa kiwango gani? na mbona maisha yanazidi kupanda? Umeme juu, kodi za nyumba zimeongezeka na maisha bora yamekuwa ndoto!

Sokomoko wakati watu walikuwa wanaongea mambo ya maana wewe na wenzio mlikuwa mnatetea ujinga, sasa subirir cha moto
 
Kwanza Sokomoko alikuwa ni mmoja wa watu waliomshangilia Kikwete.

Leo Kikwete kawa Rais, ndiyo anakuja KUTUCHEKA humu ndani walala hoi.

Ni kweli kabisa, Watanzania waliompa Kikwete Kura kwa kuamini maneno haya, HAMNAZO.

Mtu na akili zake huwezi amini maneno kama haya na sasa MOTO unawaka.

Mtu kama Sokomoko utakuta HAYA HAYAMHUSU (si ajabu ni CCM LONDON) au ndugu wa Mafisadi.
 
Yaani umenikumbusha mbali,afadhali umeleta kitu kwa muda muafaka maana akina zombi & co wanajifanya trumpet za mafisadi
 
Back
Top Bottom