Chonde chonde mshikamano wa Wazanzibari: Tunataraji ACT Wazalendo Hawatasutwa na Dhamira yao katika Uchaguzi wa 2025

Jamhuri ya Zanzibar

Senior Member
Jul 17, 2012
126
195
Mapambano ya kupigania Uhuru wa Zanzibar yalisababisha Zanzibar kufuata mikondo ya siasa za kikabila ambayo ni ngoma iliyopigwa na kuimbwa vyema na wakoloni wa Kiingereza na kuwahemua Wazee wetu hadi wakaifahamu barabara kuicheza na kuiimba. Wenye asili ya Kiarabu waliunga mkono zaidi chama cha ZNP na wale waiokuwa na asili za Kishirazi na Kibantu waligawanyika katika mirengo yao ya kisiasa lakini wengi wao waliunga mkono ASP huku wengine wakiunga mkono ZNP.

Siasa zilizojitenga katika mipaka ya ukabila ziliwezekana zaidi katika kisiwa cha Unguja ambako jamii zilijigawa sana kwa misingi ya kikabila na rangi za ngozi. Kwa upande wa kisiwa cha Unguja, Mwarabu alikuwa pake, Mshirazi pake na Mwafrika pake. Waliishi kama ni jamii tofauti. Hata hivyo kwa upande wa Kisiwa cha Pemba mambo hayakuwa hivyo. Makabila hayakuathiri mjengeko wa kijamii. Mwarabu, Mshirazi na Mbantu waliishi pamoja, walioana na kuzaa machotara.

Hivi ndivo walivo Wapemba mpaka leo. Katika uso mmoja wa Mpemba, Uarabu upo, Ushirazi upo na Ubantu umejaa tele. Katika kisiwa cha Pemba tokea zamani hadi leo, koo zina michanganyiko ya makabila yote. Huwezi kuona ukoo unaojifagharisha kwa Uarabu kwani ukoo huo umejaa wingi wa Ushirazi na Uafrika. Hata katika hizo chaguzi za ASP na HIZBU za miaka ya 1950 na 60 kwa upande wa Pemba, matokeo ya chaguzi zile yalibainisha wazi kuwa ni vigumu kufanya siasa za kikabila Pemba.

Wakati katika kisiwa cha unguja, mgawanyiko wa majimbo ya uchaguzi na hata ushindi katika chaguzi ilitegemea jimbo hilo ni la Waararbu, Washirazi au Waafrika. Kwa upande wa Pemba hakukuwa na jimbo la Waarabu. Au Washirazi au Waafrika. Familia moja na ndugu wa mama na baba mmoja walitofautiana katika vyama wanavyoviunga mkono, sawa tu na ilivyo sasa. Wapemba tokea hapo zamani ukabila sio ngoma yao.

Kama unataka uwakosee Wapemba katika kilele cha hisia zao, basi gusa heshima yao, utu wao na nchi yao. Ndio maana hata wana ASP wa Pemba katika zama za kupigania Uhuru, hawakuvutiwa na chinja chinja ya Mapinduzi ya 1964 dhidi ya ndugu zao hata kama waliipenda sana ASP yao. Kwa Mpemba, kumchinja Mwarabu ilikuwa ni kumchinja baba, mama, ndugu, shangazi au mjomba.

Kila aliegusa maeneo hayo yenye kubeba heshima kwa Wapemba alikiona cha mtema kuni, kwani Wapemba hawakukubali. Walipambana hadi mwisho wa tone lao la damu. Ule msemo maarufu wa Pemba Peremba ukija na joho utarudi na kilemba unatuchorea taswira na wasifu huu wa Wapemba kwa ufasaha zaidi. Msemo huu unamaanisha Wapemba hawahitaji wala hawaghilibiki na utukufu wala cheo cha mtu bali wanahitaji kuheshimiwa na kuthaminiwa.

Ukienda kwa Wapemba siku zote uwe mnyenyekevu hata kama ni mfalme, ukifanya hivyo utarudi ukiwa na mataji mawili ya kifalme. Ukienda kwa Wapemba hata kama wewe ni mjuzi sana, basi ujifanye mjinga, utarudi ukiwa mwerevu zaidi ya ulivyokwenda. Kinyume chake, ukienda kwa Wapemba kuwaonesha utukufu wako, utarudi ukiwa mtumwa, usie na thamani yoyote. Halkadhalika, ukienda kwa Wapemba kuwaonesha ujuzi wako, utarudi ukiwa mjinga.

Wapemba walijitawala wenyewe katika kipindi cha Makamndume tu, miaka mingi sana kabla hata ya ujio wa Mreno. Baada ya Mkamandume na himaya za Washirazi kwa ujumla kuanguka kufuatia uvamizi wa Wareno, Wapemba hawakupata tena kujitawala wenyewe hadi leo. Halkadhalika hawakuwahi kutoa mtu wa jamii yao kuwa mtawala wao, ukiwacha wale vibaraka wachache kutoka Pemba, waliowahi kuwa watawala kwa maslahi ya mabwana zao.

Katika kipindi chote cha histroia ya Zanzibar na tawala zake zote, Pemba ilikuwa ikitawaliwa kwa isivyopendeza. Ilikuwa ikidhalilika na ikiwekwa nyuma sana katika kila jambo. Ilikuwa hivyo katika zama za Mremo, ilikuwa hivyo katika zama za Sultani, ilikuwa hivyo katika zama za Karume na Wanamapinduzi wenzake na ipo hivyo hadi leo katika zama za ushindani wa vyama vingi vya siasa. Katika kipindi chote hicho, Wapemba hawakupigania cheo na madaraka bali walipigania heshima yao na heshima ya Zanzibar kwa ujumla.

Marehemu Maalim Seif, alipoingia katika siasa aliungana na Wazanzibari kwa jumla kuondoa ubaguzi na udhalilishaji wa jamii moja dhidi ya nyengine ndani ya Zanzibar. Alipambana kuondoa mitazamo ya siasa za zamani na visasi vya kihistoria. Akiwa yumo katika siasa na uongozi katika miaka ya 1980, alichukiwa mno na Wanamapinduzi ya 1964 waliokuwa wakipendelea kuendeleza faasafa zao za kimapinduzi; kwamba kila jamii iliyokuwa haikushiriki vyema katika siasa za Mapinduzi ya 1964 na chinja chinja yake, ni adui kwa Zanzibar na haifai kuhusishwa na uongozi wa nchi. Itakumbukwa kuwa ASP ilishindwa na ZNP kisiwani Pemba kwa ushindi mwembamba sana kabla ya Mapinduzi ya 1964 na kwa msingi huo Wanamapinduzi wakaihesabu Pemba kuwa ni jamii ya Wapinga Mapinduzi wasiostahiki kupata heshima na thamani kama jamii nyengine za Zanzibar.

Hata hivyo kwa bahati mbaya sana Wanamapinduzi wenyewe wakalea Mussa mpinga fikra zao potofu. Mussa huyu ni Marehemu Maalim Seif. Walimtengeneza Mussa mpaka akawa tayari kushika hatamu za Urais wa Zanzibar ndani ya jekejeke la fikra za potofu za kimapinduzi. Ilipofika wakati huo, ilikuwa tayari Marais wanne kutoka Unguja wameshakaa madarakani tokea Mapinduzi ya 1964 (yaani Mzee Karume, Mzee Jumbe, Mzee Ali Hassan Mwinyi na IMzee dis Abdul-wakil).

Hivyo Wazanzibari walio wengi wakaamini sasa ni wakati wa jamii ya Wapemba kutoa Rais ili kukuza mshikamano wa visiwa viwili vya Unguja na Pemba. Hata hivyo Wanamapinduzi wakitegemea walilipinga hilo na hivyo Maalim Seif akafanyiwa hila na kunyimwa fursa ya kuwania Urais wa Zanzibar wakati huo akiwa CCM. Hata Mzee Kambarage aliemuamini sana Maalim Seif na ambae hakuzipenda fikra potofu za Wanamapinduzi wa Zanzibar hakuwa msaada wowote kwa Maalim Seif. Ili kummaliza kabisa asiweze kuendeea na azma yake ya kuwa Rais, Nyerere na CCM chini ya shinikizo la Wanamapinduzi, walimfukuza Maalim Seif katika Chama na Serikali na baadae kumuweka gerezani.

Maalim alikuja kuwa kiongozi Mkuu wa siasa za upinzani Zanzibar mpaka umauti ulipomfika. Jamii za Wazanzibari wasiopenda ubaguzi na unyanyasaji ziliungana na kumueka mbele Maalim Seif bila kujali upemba wake ili kuziongoza harakati hizo. Maalim aliziongoza harakati hizo kwa zaidi ya miaka 30 hadi umauti ulipomfika Februari, 2020. Hivyo jamii ya watu wa Unguja tunaweza kusema kuwaliwaamini ndugu zao wa Pemba katika kuwaongoza katika siasa na mapambano kwa miaka mingi.

Jambo linalotia moyo katika kulea mshikamano wa Waunguja na Wapemba katika siasa za upinzani Zanzibar ni kile kilichofanyika mara baada ya kifo cha Maalim Seif. Mtu alierithi uongozi wa Chama na siasa ametoka upande wa Unguja, Juma Duni Haji. Hili ni jambo la kupomgezwa sana. Hii ni sawa na kusema katika kambi ya upinzani, watu wa Unguja na Pemba wanaaminiana. Hawaahofiani wala hawabaguani. Waunguja waliwaweka mbele ndugu zao Wapemba katika uongozi wa siasa zao kwa miaka zaidi ya 30, sasa Chama kimeona ni wakati sahihi wa kutambua mchango wa watu wa Unguja katika mshikamano huo na hivyo kuona wakati umefika na watu wa Unguja kuongoza siasa zao.

Halkadhalika tokea kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa, kwa upande wa upinzani hapa Zanzibar, Wazanzibari kwa ujumla wao wamekuwa wakiwaamini na kuwaweka mbele Wapemba kuwawakilisha katika kinyang’anyiro hicho. Maalim Seif Sharif Hamad amekuwa mgombea wa Urais pekee kwa mara 6 wa kambi ya upinzani alieungwa mkono na jamii ya watu wa Unguja na Pemba kwa ujumla wao. Hii ni heshima kubwa waliopewa Wapemba na ndugu zao wa Unguja na Wazanzibari kwa jumla.

Kwa kuwa CCM imekuwa ikiiba chaguzi zote za Zanzibar, kambi ya upinzani imekuwa ikifanikiwa kutoa Makamo wa Kwanza wa Rais tokea kuundwa kwa serikali ya Umoja wa Kitaifa. Nafasi hiyo amekuwa akiishikilia Marehemu Maalim Seif kwa kuwa yeye ndie alikuwa mgombea wa Urais pekee kutoka chama kikuu cha upinzani Zanzibar. Baada ya kifo cha Maalim Seif, Februari, 2020, Awamu ya Tatu tokea kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, nafasi hiyo bado iliendelea kushikiiwa na mtu kutoka Pemba, Othman Massoud Othman, aliekuwa Mwansheria Mkuu wa Zanzibar. Hii bila shaka ilikuwa ni makubaliano na busara ndani ya Chama hicho.

Makala hii inatoa changamoto kwa ACT-Wazaendo katika siasa za kuelekea kinyang’anyiro cha Urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025. Wasijewakalipuuza hata kidogo suala nyeti la utenegemano wa Wapemba na Waunguja. Wazanizibari walio wengi kutoka katika kambi ya upinzani bila kujali ni kutoka Unaguja au Pemba, kwa sasa wanaamini wakati umefika kwa ACT-Wazalendo kuonesha uungwana, kuonesha mshikamano wa Unguja na Pemba kwa vitendo, kuitekeleza dhamira ya Maalim Seif ya kuwaunganisha Wazanzibari baada ya kugawiwa kwa muda mrefu.


Kiila mpenda umoja wa Wazanzibari kutoka kambi ya upinzani Zanzibar, kila asiesutwa na dhamira ya kupigania mshikamano wa Wapemba na Waunguja alioiishi Maalim Seif katika uhai wake wote anaamini hoja hii kwamba sasa ni wakati sahihi wa kumtanguliza mbele mgombea wa Urais kutoka upande wa Unguja. Ni wakati wa kuwaambia watu wa Unguja kuwa mlituamini sasa na sisi tunawaamini. Ni kweli wakati wa kuonesha kwa vitendo ile laana ambayo ASP na CCM ya kuwabagua wengine na kuwatukuza wengine katika siasa na kushika nyadhifa za uongozi wa Zanzibar haifanyi kazi katika ACT-Wazalendo.

mansoor.JPG

Mansoor Yussuf Himid na Juma Duni Haji
katika kikao cha Baraza la Wawakilishi Zanzibar​

Hatutarajii ACT-Wazalendo watarejea makosa ya ASP na CCM. Katika zile siasa za miaka ya 1950 na 60, ASP na CCM waliwalaghai Wazanzibari kuwa wanapigana vita dhidi ya ukabila, ubaguzi, ubwana na utwana. Matokeo yake wakaondoa ubwana wa Waarabu wakaweka ubwana wa Wafanya Mapinduzi na aila zao. Baada ya ubaguzi wa mwarabu dhidi ya mtu mweusi wakaweka ubaguzi wa mtu mweusi dhidi ya mwarabu na mtu mweusi dhidi ya mtu mweusi mwenzake. Itoshe kusema ASP na CCM waliwasaliti Wazanzibari na hadi leo wanasutwa na dhamira yao hio walioiitangaza kupidia Mapinduzi ya 1964. ACT-Wazalendo msije mkasutwa na dhamira yenu.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom