CHADEMA yatangaza maandamano kudai Umeme, Maji Dar

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,491
8,356
Kufuatia kuwapo kwa mgawo wa maji na umeme katika Jimbo la Kibamba jijini Dar es Salaam, Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeandaa maandamano ya amani kwenda ofisi hizo ili kujua kiini cha tatizo.

Maandamano hayo yaliyopangwa kufanyika Jumatatu Novemba 28, 2022 na Jumanne yanatarajia kuhusisha wananchi, kwenda kwenye ofisi za Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Mamlaka ya Majisafi na Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) Wilaya ya Ubungo.

Hivi karibuni Tanesco ilieleza inakabiliwa na upungufu wa umeme megawati 300-350 kwa siku hali inayosababisha taasisi hiyo kushindwa kuhudumia wateja wake wote kama ilivyokuwa hapo awali.

Kutokana na upungufu huo unaotarajiwa kudumu hadi Januari 2023, ili mifumo yake iendelee kuwa imara nakuleta ufanisi unaotakiwa inalazimika baadhi ya maeneo nchini kukosa huduma hiyo kwa mgao ambao utakuwa unadumu masaa manane hadi 12.

Leo Ijumaa, Novemba 25, 2022 Mwenyekiti wa Jimbo la Kibamba wa Chadema, Ernest Mgawe akizungumza na waandishi wa habari amesema changamoto ya umeme inaafanya maisha ya wananchi kuwa magumu.

"Watu wengi wanategemea umeme kuendesha maisha yao, wapo wanaouza vinywaji baridi na wengine wenye saluni kitendo cha kujatika umeme siku nzima kinawaathiri," amesema Mgawe.

Amesema wafanyabiashara wamekuwa wakiteseka kutokana na kutofanya biashara, mtu ana majukumu lakini anapoamka asubuhi kwenda kazini anakaa hadi jioni bila kufanya chochote wakati huo familia inategemea.

"Wapo wajasiriamali wanaoendesha maisha yao na familia zao kwa kuuzaa vinywaji baridi, kutokuwa na umeme tunarudishana nyuma kimaendeleo mamlaka zinapaswa kujitathimini," amesema.

Kuhusu suala la maji, Mgawe amependekeza mradi wa maji wa Kigamboni uliozinduliwa hivi karibuni na Rais Samia Suluhu Hassa, usambazwe kwenye maeneo yenye changamoto.

Alipotafutwa Mkurugenzi wa Mawasiliano na Jamii wa Dawasa, Nelly Msuya amesema Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla amefanya ziara kwenye vyanzo vya maji na kutoa maelekezo.

Katika ziara hiyo Makalla ametangaza kutokuwa na mgawo wa maji ndani ya mkoa huo na kuitaka Dawasa kuelekeza nguvu zake kuimarisha miundombinu na miradi mikubwa ikiwemo Mabwepande.

Oktoba 24 mwaka huu, Makalla alitangaza kuwepo kwa mgawo wa majibu baada ya kutembelea vyanzo vya kuzalisha maji vya Ruvu Chini na Ruvu Juu na kujionea upungufu katika uzalishaji wa maji kulikosababishwa na ukame.

MWANANCHI
 
Back
Top Bottom