CHADEMA nyuki wa asali au mbu wa malaria?

Bhbm

JF-Expert Member
Oct 31, 2009
714
208
NYUKI na Mbu ni wadudu wenye kung’ata na kusababisha maumivu. Kuumwa (kung’atwa) na wadudu hawa kunakera na kuhatarisha maisha.
Katika mchakato wa maisha yao, hatimaye mbu husababisha malaria au magonjwa mengine na nyuki huzalisha asali, inayonufaisha wafanyabiashara, wanunuzi na uchumi wa nchi.
Umuhimu huu wa nyuki unafanana na uamuzi wa CHADEMA kususia hotuba ya Rais Jakaya Kikwete bungeni. Ingawa wamemuumiza Rais Kikwete (mwanademokrasia) kuna siku nchi itafurahia asali.
Baada ya tukio hilo, tumeona maoni ya kuilaani CHADEMA na upotoshaji. Imejitokeza nguvu ya kukidhoofisha CHADEMA kutoka miongoni mwa wana-CHADEMA.
Ndani ya vikao, wachache walioshindwa walitaka ‘kupigana’ ili kuwashinda wenzao hao mbele ya umma. Wamefanya juhudi haramu zinazowaondolea imani ya kitaasisi.
Wengi wanapinga uamuzi wa CHADEMA wakiamini ni mng’ato wa mbu si nyuki. Yaani si tukio lenye manufaa kwa nchi zaidi ya kumdhalilisha Rais.
Tutafakari; kama tukio la CHADEMA halijavunja Katiba wala sheria na kinyume chake imekidhi matakwa Katiba na sheria hizo; je, aliyemdhalilisha Rais Kikwete ni nani?
Mosi; ni Katiba na sheria za nchi zilizotungwa na Bunge lenye wabunge wengi wa CCM (kama si wote) au CHADEMA iliyotumia fursa ya kikatiba na sheria hizo?
Pili; nani wa kulaaniwa? Ni wabunge wa CCM waliowahi kutunga Katiba na sheria zenye fursa inayoweza kumdhalilisha rais au wabunge wa CHADEMA waliotumia mitego iliyowekwa na wenzao hao?
Tatu; je, wanaolaani uamuzi wa CHADEMA kwamba ungefanyika kwa mazungumzo wamejitosheleza kwa busara? Nahoji busara zao kwa sababu kama zingejitosheleza; wangetaka marekebisho ya Katiba inayoruhusu ‘udhalilishaji’ huo.
Nne; Rais Kikwete ameonekana kupevuka zaidi ya wanaolaani tukio la CHADEMA kwa kusema bado ni rais wa wote. Nitafafanua baadaye.
Kabla ya kuendelea, tuwape nafasi magwiji wa falsafa. Magwiji hawa ‘wamejiumba’ katika maisha ya kuimarisha afya za akili zao kwa kudadisi mantiki badala ya ushabiki.
Kwa mfano, katika mkusanyiko wa mamia au makumi ya watu; wanafalsafa huhoji nafsi zao; kama kweli tupo hapa kusaidia wenye uhitaji; wengine wanafanya nini hapa? (“If it's true that we are here to help others, what are the others doing here?”)
Wamekuwa wakijiuliza; kwa nini mhandisi ahofie ujenzi wa ghorofa 13 wakati mchapishaji wa vitabu asihofie kuchapisha kura 11 au zaidi.
Sasa tuondoke kwenye madarasa ya wanafalsafa na akili iliyochangamka. Turejee katika mjadala wa wabunge wa CHADEMA kwa vipengele vifuatavyo.
Ni mng’ato wa nyuki au mbu?
Mapenzi ya wanadamu kwa nyuki ni asali, si maumivu. Nyuki anayeuma kama sharti la kutoa asali husababisha taharuki. Hata hivyo, licha ya kusababisha taharuki kuna matarajio chanya (asali), tofauti kama mtu akiumwa mbu.
Kwa uamuzi huu wa kikatiba na kisheria, CHADEMA imesababisha maumivu ya kiushabiki kwa baadhi, si maumivu ya mustakabali wa nchi. Hivyo imeuma mithili ya nyuki, sio mbu.
Hata hivyo, hoja halisi ya CHADEMA imekuwa ngumu kueleweka miongoni mwa wabunge wake wachache, baadhi ya wanachama, viongozi na sehemu fulani ya wananchi wakiwamo wasomi.
Baadhi ya wabunge wa upinzani (wasio CHADEMA) wako mstari wa mbele kuhakikisha hawaelewi hoja ya CHADEMA. Hawa ni pamoja na NCCR-Mageuzi na CUF ambao sasa wanaelekea kuwa wapinzani wa hoja za CHADEMA (hata zenye mantiki). Kuna dalili; bungeni mpinzani wao ni CHADEMA si CCM.
Ni kama vile CCM imekasimu sehemu ya madaraka kwa baadhi ya wabunge wa NCCR-Mageuzi na CUF. Angalau CUF inaweza kuwa na sababu za msingi hasa baada ya kugawana madaraka Zanzibar.
Hoja halisi ya CHADEMA ni kutoyatambua matokeo ya urais yaliyompa ushindi Kikwete wa CCM. Hoja ya CHADEMA si kutotambua urais wa Rais Kikwete.
Hapa ndipo propaganda inapojengwa kutokana na wengi kushindwa kutofautisha kati ya kutotambua matokeo ya urais wa Kikwete na kutambua urais wa Kikwete.
Kwa mazingira ya nchi kisheria (Kikatiba) ni rahisi zaidi kutofautisha matokeo ya urais na majukumu au wajibu wa urais.
Itakumbukwa, kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita kulikuwa na wagombea zaidi ya watatu; Kikwete (CCM), Dk. Willibrod Slaa (CHADEMA), Profesa Ibrahim Lipumba (CUF), Hashim Rungwe (NCCR-Mageuzi), Peter Mziray (APPT-Maendeleo) na wengine.
Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania na sheria za uchaguzi, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ndiyo yenye mamlaka ya kumtangaza mshindi wa uchaguzi mfano, urais.
Baada ya kutangaza matokeo hayo hayawezi kuhojiwa popote. Kwa mfano; NEC kwa makosa ya kihisabati au kosa lolote, ingemtangaza Peter Mziray wa APPT-Maendeleo, ndiye angekuwa rais halali kikatiba na kisheria.
Ingeweza kutokea mvutano wa kisiasa lakini kikatiba na kisheria huyo angekuwa rais halali na akaunda serikali.
Sio CCM, CHADEMA, CUF au chama kingine chochote kingeweza kuhoji au kupinga kisheria. Kati ya fursa zinazoweza kutumiwa na vyama vingine ni pamoja na ile iliyotumiwa na CHADEMA. Fursa hiyo ni kuibua vuguvugu jingine la kisiasa.
Katika vuguvugu hilo, zinaweza kupenyezwa ajenda za mabadiliko ya Katiba au sheria kadhaa ili hatimaye kurekebisha mfumo mzima unaoweza kumtangaza yeyote kuwa rais na isihojiwe.
Katika mazingira ya mfano huu mambo mawili yanaibuka. Mosi, vyama vya CCM, CHADEMA na CUF kutoridhika na matokeo au mchakato wa kumtangaza mgombea wa APPT-Maendeleo ni Rais wa Tanzania.
Uhalisia huu wa kutoridhika na matokeo au mchakato huo unabaki mioyoni mwao, ofisini kwao na miongoni mwa wanachama na wananchi wengine.
Pili; ni ukweli wanaopaswa kutambua kuwa hata wakilia machozi ya damu Mziray atabaki rais kikatiba na kisheria. Kwa hiyo, kikatiba na kisheria watamtambua ingawa matokeo ya mchakato wa kumtangaza hawaukubali.
Kwa hiyo, katika harakati zao za kisiasa (si kisheria) wanaweza kuonyesha hisia za kupinga matokeo au mchakato wa kumtangaza mshindi lakini bado wakamtambua mshindi huyo kwa mujibu wa sheria za kisheria.
Katika mfano huu; kwa ujumla kuna mambo mawili ya msingi. Kwanza, vyama havikubaliani na matokeo au mchakato wa kumtangaza mshindi.
Pili; licha ya kutokukubali matokeo au mchakato wa kumpata mshindi, wanalazimika kumkubali aliyetangazwa (kwa mujibu wa katiba si vurugu).
Katika mazingira haya, wabunge wa vyama hivi ni lazima washiriki shughuli za Bunge na majukumu mengine ya mbunge kisheria.
Lakini unapotokea mwanya wa kuonyesha hisia zao bila kuathiri Katiba au sheria zinazomtambua Rais aliyetangazwa; watazidi kumkumbusha ‘rais’ huyo mchakato wa kumtangaza haukuwa wa haki.
Kwamba mchakato haukuwa wa haki na hivyo, ili jambo hilo lisirudiwe ni wakati muafaka wa kurekebisha mfumo mzima wa mchakato husika.
Je, CHADEMA wamefanikiwa?
CHADEMA wamefanikiwa katika mambo manne kwa tukio lile. Mosi; wamefanikiwa kufifisha mjadala wa hotuba ya Rais.
Kisiasa; haya ni mafanikio kutokana na ukweli kuwa, hotuba ya Rais ndiyo dira yake ya kiutendaji na kisiasa kwa miaka mitano ijayo.
Kwa hiyo, kama hotuba hiyo ingepata nafasi kubwa ya kujadiliwa na umma maana yake, Rais angepata kipimo muafaka kuhusu mambo aliyodhani ni sahihi kwa wananchi kwa miaka mitano, hasa vipaumbele vyake 13.
Badala yake, CHADEMA wamepora nafasi ya mjadala wa hotuba ya rais. Wamegawana nusu kwa nusu fursa ya kujadiliwa na umma.
Kinachojitokeza hapa ni jinsi gani CHADEMA wanaweza kusimamia au kuendesha mjadala huu katika kuwajenga badala ya kuwabomoa mbele ya jamii.
Kwa mfano, tayari CCM wamesikika wakitaka maandamano kuwalaani, sijui CHADEMA wataanza operesheni Sangara.
Pili; wamefanikiwa kujipatia fursa ya kupima nguvu yao ya ushawishi kwa umma muda mfupi baada ya kura za Uchaguzi Mkuu. Ni fursa murua ya kujitathmini.
Fursa hii ya kuzua tukio linaloibua mjadala kitaifa, ni fursa adhimu kwa chama cha siasa na wanasiasa. Kama nilivyoeleza awali, mafanikio yatategemea zaidi hatua zijazo za CHADEMA.
Tatu; CHADEMA kimefanikiwa kujiweka katika nafasi ya kutambua kuwa je, uungwaji wake mkono kwa umma ni ule wa kufa au kupona yaani uungwaji wa kiitikadi na si upepo wa kisiasa, kama NCCR-Mageuzi mwaka 1995.
Nne; nafasi nzuri ya kujitathmini kwa kujipima na vyama vingine mbele ya macho ya Watanzania. Na hii izingatiwe kuwa CHADEMA ni chama kikuu cha upinzani, kilichotwaa nafasi hiyo kutoka kwa CUF kwa nguvu ya kura za Watanzania.
Ushauri kwa wanasiasa wengine
Ushauri wangu utaegemea mitazamo ya watu wengine waliopata kuwa mashuhuri duniani, hasa kitaaluma.
Kati ya watu hao ni mtabibu bingwa wa magonjwa ya mifupa (Orthopedics), raia wa Marekani, Dk. Mary O’Connor.
Ni mwanamama mwenye rekodi za kidaktari zilizowahi kushikiliwa kwa mara ya kwanza na mwanamke. Huyu alipata kusema; It's not so much how busy you are, but why you are busy. The bee is praised. The mosquito is swatted.
Kwamba; mantiki si wingi wa shughuli ulizonazo, bali ni kwa nini una shughuli hizo. Nyuki hutukuzwa, mbu huuawa.
Lakini pia nihitimishe kwa maelezo ya mwanamuziki Stevie Wonder kwamba; kila mmoja ametunukiwa uwezo lakini tofauti miongoni mwetu ni matumizi ya tunu hiyo. “We all have ability. The difference is how we use it.”
Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika. SOURCE; RAIA MWEMA.
 
Back
Top Bottom