CHADEMA: Kipaumbele cha Rais Magufuli ni kununua ndege? Hali ya Uchumi inazorota!

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,814
11,991
Heshima kwenu wakuu,

Bonyeza hii link kuaangalia video kupitia Youtube


na Facebook angalia hapa chini


Leo kuna Mkutano wa CHADEMA na Wanahabari unaofanyika Upanga kwenye Hotel ya Courtyard, Protea.

Huu ni Mkutano wa Uongozi wa Juu wa Chama na Wahariri pamoja na Waandishi wa Habari waandamizi, utakafanyika kuanzia Saa 04:30 asubuhi, katika hoteli ya Protea Courtyard

Hii inatokana na uamuzi ambao Kamati Kuu ya CHADEMA imeufanya katika mkutano wake wa siku mbili; tarehe 29-30 Julai, 2017 katika Hotel ya Double Tree, jijini Dar es Salaam.

Maeneo ambayo yamejadiliwa na kuridhia kuchukuliwa kwa hatua ni;

1. Hali ya mwenendo wa siasa katika nchi na ukandamizaji wa demokrasia unaofanywa na serikali ya awamu ya tano.

2. Kuporomoka kwa uchumi na hali ngumu ya maisha kwa Watanzania

3. Kamata kamata inayoendelea kufanywa na vyombo vya dola dhidi ya viongozi, wanachama na wafuasi wa CHADEMA maeneo mbalimbali nchi nzima.

Nimefika maeneo haya, ntahakikisha nawahabarisha kila kinachojiri. Karibuni.


=====

UPDATES:

CDM1.jpeg
CDM2.jpeg


Mkutano unaanza na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe ndiye msemaji mkuu.

Kamati kuu ilikua na kikao cha siku mbili kilichotanguliwa na Mkutano maalum. Viongozi wakuu walijumuika na Viongozi wa kanda mbalimbali za CHADEMA. Tulitafakari kwa kina hali za kisiasa na kamatakamata kwa viongozi wa Upinzani na hali ya Uchumi wa taifa.

Kikao cha leo kitajadili jambo moja nalo ni Hali ya uchumi katika taifa. Tumezoea kuzungumza maswala ya kisiasa, lakini sisi kama taifa hatujajipa nafasi ya kutambua hali ya uchumi.

Rais wetu tumempa likizo sana sababu yeye na Serikali yake hawajabanwa vizuri kuhusu hali ya uchumi. Vyombo vyetu vimekua vikiangalia uchumi kutokana na kauli za Serikali na sio mbaya lakini inatakiwa tujue hali hii inatupeleka wapi.

Benki ya dunia huwa inatoa taarifa IMF na BOT. Taasisi inayotoa taarifa halisi za uchumi nchini ni Benki Kuu na kila mwezi inatoa taarifa ya kiuchumi na leo tutatumia taarifa za Benki Kuu.

Kwa Sababu ya faida ya kikao hiki nitazungumzia mambo madogo sita ili kuona Mei 2015- Mei 2017 ni mambo gani yanaendelea katika nchi.

Wataalam wetu wamefanya uchunguzi wa kinachosababisha uchumi kuporomoka.

1. CHAKULA

Chakula ndio maisha yetu na 75% ni wakulima katika nchi yetu. Rais anasema hatatoa chakula, sisi tunasema "Magufuli, hiki chakula si chako"!

2015, tukiwa chini ya Serikali ya Awamu ya nne tulikuwa na tani zaidi ya laki nne(400,000) lakini 2017 kuna tani sabini na nne elfu(74,000) ambayo ni Asilimia 18 ya chakula ukilinganisha na Awamu ya nne.

Vyakula vyote sasa vimepanda bei wakati mapato kwa wananchi yanashuka. Mishahara haijaongezwa wala rais halimsumbui hilo. Wakati mataifa mengine yanasaidia nchi zao kupata chakula sisi hatufanyi hivyo.

Sekta ya kilimo imekua kwa 1.7% tangu Rais aingie madarakani. Tume ya maji ya kuboresha kilimo cha umwagiliaji haijapewa kitu. Uchumi unakua kwenye mifuko ya watu wachache, Uchumi unakua wakati umasikini unaongezeka.

Sekta ya Kilimo ufugaji na uvuvi inasinyaa. Kipaumbele cha rais ni kununua ndege. Hii fedha ya ndege ingepelekwa kwenye kilimo, watanzania milioni 40 wangecheka.

2. HALI YA UKATA WA NCHI

Ukata unasababishwa na usimamizi mbovu wa Uchumi. Mzunguko wa fedha umeathirika sana. Fedha iliyoingizwa kwenye mzunguko imepungua kwa asilimia tano(5%) na hali hii inasababisha mdororo wa uchumi.

Sekta binafsi ndo sekta inaongeza uchumi wa taifa lakini Rais anaamini kila mmoja kwenye sekta binafsi ni mpiga dili. Rais bado anaamini anaweza kurudisha hili taifa kwenye ujamaa.

3. UBINAFSISHAJI

Kuna ugonjwa ambao ukiusikia kama unajua biashara utajiuliza hivi sisi tuna akili? Jambo linalohusu ubinafsishaji. Tangu rais huyu aingie madarakani anasema viwanda tutavirejesha serikalini na wananchi wanapenda kauli hii. Wananshangilia na watu wakimshangilia naye anavimba kichwa.

Hii ni sera ya mtu asiyejua uchumi. Hakuna mfanyabiashara duniani ambaye atapewa kitega uchumi kinachoingiza faida akakifunga kwa sababu anaichukia Tanzania. Hivi viwanda vilibinafsishwa baada ya serikali kushindwa kuviendesha kwa kukosa ruzuku ya Serikali. Viwanda hivi vilivyobinafsishwa vilikuwa vinaendeshwa kwa hasara, wengi walijaribu kivifufua wakashindwa kwa sababu vilikuwa havipati ruzuku, vina teknolojia ya zamani au tulikuwa na soko hodhi, hapakuwa na ushindani wa biashara lakini sasa kuna soko huria.

Rais anasema tutachukua viwanda, anachukuwa viwanda anavipeleka wapi? Serikali haiwezi kujenga viwanda bali viwanda vinajengwa na watu binafsi. Kwanza serikali haina hela.

Kuwekeza nchi hii ni maumivu makubwa sana. Rais anatoa hii kauli kwa sababu ya kutokujua tu. Tunaongozwa na viongozi ambao hawajui misingi ya biashara na hawajui uzito wa wawekezaji binafsi. Serikali hii haipambani na wawekezaji wa nje, bali inapambana sana na wawekezaji wa ndani.

Serikali imejiondoa kwenye biashara na ili biashara iende lazima sekta binafsi zikope lakini ukiangalia taarifa ya Benki Kuu utaona anguko la sekta binafsi.

Watu wetu wa kilimo hawakopi nje ya nchi bali kwenye Benki zetu. Sekta ya kilimo mikopo ilikuwa inakopwa 6% ya mikopo ya kibenki lakini sasa imeshuka hadi - 8% yaani hasi ikimaanisha hakuna uwekezaji mpya kwenye kilimo.

Sekta ya biashara, Ujenzi, zote zimeshuka; hii ina maana kuna miradi imefungwa. Sekta ya viwanda ambayo Waziri wake sijui kama anajua biashara au aliwahi kuuza mkaa, 32% walikuwa wanakopa ila sasa hawajakopa chochote yaani 0%. Hivi viwanda vinavyofunguliwa ni viwanda vilivyotafutia mikopo serikali ya Kikwete, Serikali hii haijajenga kiwanda hata kimoja.

4. BIASHARA YA MAUZO NJE NA NDANI

Kuhusu Biashara ya mauzo nje na ndani. Uchumi wetu ni wa kuagiza bidhaa za nje. Bidhaa za kuagiza zimeshuka kwa asilimia kumi na nne, vifaa vya usafirishaji zimeshuka kwa asilimia kumi na tano. Malori yamelala pale bandarini hakuna kazi.

Mafuta yanayoagizwa kutoka nje, yamepungua kwa 14.3%. Kitu pekee kilichoongezeka kutoka nje ni chakula yaani katika vitu kumi, chakula ndo tunaagiza sana na imeongezeka wakati sisi ndo tulitakiwa tuuze nje. Tumeshindwa kuzalisha.


5. DENI LA TAIFA

Ili serikali ijiendeshe inabidi kukopa. Tunapolalamika tupunguze kukopa, wanasema Tanzania bado inakopesheka. Deni la taifa limekuwa jini linalonyonya Serikali damu na sasa hivi hawakopesheki tena.

Deni la nje dola bilioni 7 kwa miaka miwili, deni la ndani dola bilioni 11.7 kutoka bilioni 7.7 mwaka 2015. Wastani wa mapato ni trilioni 1.2. Deni la nje kila mwezi tunalipa bil 650-800. Makusanyo ya ndani tuliyoyataja hapa hayatoshi kulipa deni, fedha za maendeleo, na kila kitu.

6. ⁠⁠⁠MAKINIKIA

CHADEMA tumekuwa tukipiga kelele kuhusu haya maswala. Huyu jamaa karekebisha lakini alivyorekebisha sivyo.⁠ ⁠Kilichofanywa kwenye makinikia ni papara. Rais na wabunge walifanya papara na wananchi wakalishwa papara. Tulisema jambo hili lifanywe katika misingi ya kutoathiri uchumi wa Taifa. Kumkamata mwizi ni sifa ya taifa, lakini kuua mwizi bila kumuonesha ni jinsi gani umemuua ni fedheha.

Dola bilioni 190 tunawadai ACACIA. Bajeti ya serikali ni dola bilioni 13, lakini tumeitoza kampuni moja dola Bil 190. Tunaonekana machizi na tumekuwa watu wa kudhalilishwa duniani. TRA tafuteni fedha sio za kutia aibu. Kwa mwendo huu hatufiki.

Tunataka serikali iweke hadharani ripoti za makinikia wachumi wazipitie. TRA watueleze wamepataje hiyo kodi? Watueleze tujue maana hii ni mara nne ya pato la taifa.

Watu wanawekeza kwenye nchi zinazoheshimu sera na sheria. Tunajidanganya kwamba Tanzania ni nchi ya kipekee sana. Hatupingi mapambano ya kutafuta haki ya rasilimali zetu lakini mambo haya yatumie akili na busara na hekima.

Maamuzi ya Rais yanawatesa watanzania. Tunataka serikali ije na mpango wa kufufua uchumi wa nchi hii. Tanzania tulikuwa tunaenda katika hali ya kuridhisha lakini sasa tumerudi nyuma. Tutaanza kukosa hata sabuni.

Mbowe amemaliza na amezungumza kwa niaba ya chama taifa. Ametoa tamko kwa niaba ya Kamati Kuu ya CHADEMA.


MASWALI

1. Je, hamuoni kuna haja ya kutokukimbia bajeti kama mnavyofanya Bungeni ili msimamie haya mambo?
2. Je, hela inayokopwa inakwenda wapi?
3. Je, hawa wafanyabiashara hawakuwa na uzoefu wa viwanda?
4. Je, kamati ya bajeti inapewa ushirikiano na Serikali?
5. Leo unamlaumu Rais kunyang'anya watu viwanda ambavyo mlikuwa mnalalamika zamani wanyang'anywe. Je kulikoni?

MAJIBU

Halima Mdee (Mbunge wa Kawe) anajibu ni kwanini wanapiga kura ya hapana kwenye swala la Bajeti.

Anasema, "Ndani ya Bunge kuna kura za ndio, hapana au hayupo kotekote. Hii ni haki ya mbunge. Serikali wao kwa mtazamo wao wanaona ni mambo ya kipaumbele lakini sisi tunaona sio kipaumbele. Pale Bungeni tunajadiliana ni nini kianze kama kipaumbele. Tulipiga hapana sababu tunaamini haiwezekani ukaja na utekelezaji wa bajeti wa 34%, halafu unakuja kuleta bajeti ya trilioni 32. IMF juzi wamesema bajeti ya Tanzania ni ya hovyo na haitekelezeki."

Anaendelea, "Wizara inayoongoza fedha nyingi haigusi wananchi moja kwa moja. Tukiwekeza kwenye Elimu, kilimo ndio tungefanikiwa kuliko Viwanda. Ununuzi wa ndege sio kipaumbele ndo maana hatujaiunga mkono bajeti. Tulipelekwa bungeni kuisimamia serikali na kutoa mawazo mbadala"
⁠⁠⁠⁠
Mbowe anajibu baadhi ya maswali

⁠⁠⁠⁠Jipeni muda wa kusoma bajeti mbadala. Sisi hatupo pale kuunga mkono kila kitu cha Serikali. Ikifanya vizuri tutaiunga mkono. Kama wabunge tungekuwa na umoja, hii bajeti isingepita. Ndio maana kabla ya bajeti, wabunge wa chama fulani walipewa milioni kumi kumi Bajeti ikapita. Wakati sisi tumeandaa hotuba makini, ukatengenezwa mkakati wa makinikia. Watu hawakujua wapinzani wana hoja gani.

Deni la taifa hili nyongeza imeenda wapi? Anayeisimamia hii nyongeza sio kambi ipinzani bali ni BoT. Hii ni ripoti ya CAG, alisema sheria inayosimamia deni imepitwa na wakati. Na hili deni linakwenda wapi? Tuliomba kabla ya kukopa Bunge tuambiwe.

Viwanda vilivyobinafsishwa vipo vya aina mbalimbali. Vipo vinavyoendeshwa kwa faida kama kiwanda cha bia na Sigara. Hivi vilibinafsishwa kwa bei ya kutupa na ubinafsishaji ulifanyika kwa upendeleo na haukuwa wa wazi. Ninachokipinga sio zoezi zima kwa ujumla. Ukinipa kiwanda nikaona godown inalipa kuliko kiwanda ntakifanya godown huo ndo ukweli. Mfanyabiashara anatafuta faida na biashara ni kubadilika.

Bunge leo ni mateka wa serikali, ambacho kinatoka serikali Kuu Bunge leo haliwezi kukataa. Kamati ya bajeti haiwezi kupinga kitu. Uhuru wa Bunge kufanya mambo yake haupo. Bunge linaangalia maslahi ya Rais, Chama halafu ndio Taifa.

Sijasema namlaumu rais kurejesha viwanda, nimesema kwenye biashara ni kitu cha kawaida mtu kubadilisha biashara.

Sheria za madini zimepitishwa harakaharaka na bado tunarudia kosa lile lile. Tumepitisha sheria tatu kwa muda siku tatu tu

=======

CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA)

TAMKO LA KAMATI KUU YA CHAMA KUHUSU KUPOROMOKA KWA UCHUMI WA TAIFA TANGU SERIKALI YA AWAMU YA TANO CHINI YA RAIS JOHN POMBE MAGUFULI KUINGIA MADARAKANI

UTANGULIZI

Ndugu Wahariri,

Kamati Kuu ya Chama chetu ilikutana Jijini Dar Es Salaam katika kikao chake cha dharura tarehe 29-30 Juni, 2017 katika ukumbi wa hoteli ya Double tree.

Kikao hiki kilitanguliwa na kikao cha siku 2 cha Sekretariat ya Taifa na Viongozi wote waandamizi kutoka Makao Makuu ya Kanda zote kumi (10) za Chama. Kanda hizo ni Victoria (Kagera, Geita na Mwanza), Serengeti (Shinyanga, Simiyu na Mara), Magharibi (Kigoma, Tabora na Katavi), Kati (Dodoma, Singida na Morogoro), Kaskazini (Tanga, Kilimanjaro, Manyara na Arusha), Pwani (Dar Es Salaam na Pwani), Kusini (Lindi, Mtwara na Ruvuma), Nyasa (Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe na Rukwa), Pemba (Kaskazini Pemba na Kusini Pemba) pamoja na Unguja (Kaskazini, Kusini na Mjini Magharibi).

Katika kikao hicho ajenda zilizojadiliwa ni pamoja na ;

  1. Taarifa ya Hali ya siasa Nchini
  2. Taarifa ya hali ya uchumi ya Nchi
  3. Kamatakamata ya viongozi wetu kunakofanywa na vyombo vya dola
Leo tumewaita hapa kwa ajili ya kuzungumzia jambo moja mahususi la mwenendo wa hali ya uchumi tangu Serikali ya Awamu ya tano iingie madarakani mwaka 2015.

Ndugu Wahariri,
Mnafahamu Taasisi mbalimbali kitaifa na kimataifa zimekuwa zikichapisha ripoti zao kuhusu mwenendo wa Uchumi wetu. Baadhi ya Taasisi hizo ni Pamoja na Benki Kuu (BoT) kupitia Monthly, quarterly and annual economic review , Kituo cha Takwimu Tanzania (NBS), Benki ya Dunia (WB), Mfuko wa Fedha Kimataifa (IMF), Economic Intelligency Unit na zingine nyingi duniani.
Leo tutawashirikisha zaidi katika ripoti ya hali ya Uchumi inayotolewa kila mwezi na Benki Kuu (Monthly Economic Review) kama ilivyotolewa Julai14, 2017 na nitagusia kidogo baadhi ya ripoti zingine. Mnafahamu BoT huchapisha tathimini ya mwenendo wa uchumi kwa kila mwezi na kila robo ya mwaka kuonesha mwenendo wa uchumi kwa mwezi husika (Monthly Economic Review) kwa kulinganisha na mwezi uliotangulia na pia mwaka uliotangulia.
Aidha kwa ripoti hizo unaweza kulinganisha hali ya Uchumi ya mwaka kufikia mwezi huo husika dhidi ya hali ya miaka iliyotangulia katika kipindi kama hicho.

Julai14, 2017, BoT ilitoa ripoti ya Mwezi June inayohusu tathimini ya mwezi May 2017. Kwa kuzingatia umuhimu wake, tumefanya uchambuzi mfupi wa ripoti hii kwa kuangalia hali ya mwaka kufikia May 2017 dhidi ya hali ya mwaka ilivyokuwa May2015 ikiwa ndio mwaka wa mwisho wa awamu ya nne. Ulinganisho wa hali ya uchumi May 2015 dhidi ya May 2017 ni muhimu ili kuona mwelekeo (trend) wa Hali ya Uchumi na athari zake, chanya au hasi kwa mustakabali wetu kama Taifa.

HALI YA UCHUMI NA MAHUSIANO YAKE NA MAISHA YA WANANCHI

Uchumi hupimwa kwa vigezo vingi, hata hivyo, umuhimu wa vigezo husika huwa na maana kutegemeana na namna vinavyoadhiri maisha ya wananchi. Katika uchambuzi wetu, tutaangalia vigezo vichache ambavyp vina mahusiano ya moja kwa moja (direct impact) kwenye maisha ya wananchi.

1. AKIBA YA CHAKULA NA BEI ZA VYAKULA MUHIMU

  • Kipindi cha Mei,2015, kiasi cha akiba ya chakula kwenye ghala la Taifa (NFRA) kilifikia tani 406,846 ukilinganisha na tani 74,826 May 2017; sawa na asilimia 18.3% tu ya kiasi cha chakula katika kipindi kama hicho mwaka 2015.
  • Bei za jumla kwa vyakula muhimu kama mahindi, May 2015 ilikuwa Tsh 47,163/ kwa gunia wakati mwaka huu May 2017, bei ya zao hilo gunia imefikia Tsh 90,149.9/ sawa na ongezeko la bei kwa asilimia 92%. Aidha bei ya mchele gunia Mei 2015 ilikuwa Tsh 162,701/ wakati Mei 2017 gunia la mchele bei ni 176,330/=
  • Mazao mengine yote ya chakula, ikiwamo maharage, viazi na sukari nayo yamepanda bei kwa wastani wa asilimia kati ya 40 na 60 kutegemea na msimu lakini trend imekuwa ni kupanda tu.
  • Sekta ya kilimo imekua kwa asilimia 1.7% mwaka 2016/17, kiwango ambacho ni cha chini kupata kutokea kwa zaidi ya miongo mitatu.
  • Wakati mataifa yote duniani yanasaidia wakulima kuongeza tija katika kilimo kwa kuwasaidia ruzuku ya mbolea, Tanzania ambayo asilimia 75% wanatagemea kilimo, 2015 ilikuwa 78 bn wakati mwaka 2016/17 ruzuku hii ilikuwa 10bn tu.
  • Tume ya maji iliyoanzishwa kwa mujibu wa sheria 2015 kwa lengo la kuhakikisha tunaongeza kilimo cha umwagiliaji katika bajeti ya mwaka 2016/17 ilipata Tsh 0 (zero) katika bajeti yake ya maendeleo.
2. HALI YA UKATA NCHINI.

Wakati bei zikiwa juu sasa kuliko mwa 2015 kabla ya awamu ya tano kuingia madarakani, hali ya ujazo wa fedha imekua kinyume chake na hivyo kuathiri biashara, uzalishalishaji, thamani ya mali (assets kama ardhi na mali zingine). Ujazo wa fedha katika dhana pana kwa mwaka kwenye uchumi (M3) uliongezeka kwa asilimia 15% May 2015 ukilinganisha na ongezeko la asilimia 5.2% May2017 kwa mwaka.

Aidha, Mzunguko wa fedha kwa maana ya kiasi cha fedha katika matumizi kwa mwaka, inaonesha Mei 2015 kiliongezeka kwa asilimia 15.2% wakati Mei 2017 kilikuwa na ongezeko hasi kwa asilimia -3%. Hiki ni kielelezo cha usimamizi hafifu wa uchumi na ndio msingi wa ukata unaoendelea nchini.

Athari za kushuka kwa ujazo wa fedha na mzunguko wa fedha kwenye uchumi katika vipindi hivyo tofauti wakati kiasi cha mfumuko wa bei kikiwa na tofauti ndogo, kwa maana kutoka asilimia 5% mwaka 2015 mpaka asilimia 6% mwaka 2017 ni pamoja na zifuatazo;

  • Pesa kuwa vigumu kupatikana japo inashuka thamani. Ndio maana pamoja na mwaka 2017 pesa kuwa ngumu kuliko mwaka 2015 kwa mujibu wa takwimu hizi za BoT, lakini thamani ya bei ya chakula kama mahindi na maharage vimepanda karibu mara mbili kwa ulinganisho wa miaka hiyo miwili.
  • Gharama ya uzalishaji kwa sehemu kubwa inabaki kuwa juu kwasababu bidhaa za mtaji na mashine sehemu kubwa zinanunuliwa nje na hivyo bei yake haiamuliwi na hali ya ndani. Kwa sababu wateja kipato kimeshuka soko la bidhaa zinazozalishwa hushuka na kusababisha mdororo wa biashara.
  • Kwa sababu ya mdororo wa biashara, wafanyabiashara wanashindwa kulipa mikopo na hivyo kuongeza presha kwenye kasi ya mikopo isiyolipika (Non Performing loans -NPL). Mpaka sasa kwa mujibu wa ripoti mbalimbali mikopo isiyolipika imeongezeka kutoka chini ya asilimia 5 mwaka 2015 mpaka asilimia zaidi ya 8 mwaka 2017. Hali hii inapunguza imani ya benki za biashara kukopesha sekta binafsi.
  • Ukata huo unasababisha kushuka kwa thamani ya asset kama ardhi, nyumba au mashine au mitambo iliyowekwa dhamana benki kwa jili ya kupata mikopo kwa sababu uwezo wa watu kununua umeshuka, na ndio sababu viwanja ambavyo viliuzwa milioni 100 sasa ukitangaza bei ya milioni 50 hupati mteja. Gari au mashine ambayo mwaka 2015 ungeuza kwa milioni 50 leo huwezi kupata nusu yake kwasababu ya ukata.
  • Uwezo wa Serikali na watu kujitegemea unapungua kwa sababu wigo wa makusanyo unapungua kutokana na biashara nyingi na ajira kupotea. Kwa sababu serikali inahitaji mapato kujiendesha na biashara zinapukutika, ni wazi mvutano wa serikali na wafanyabiashara huongezeka.
  • Ni kwasababu hiyo, maamuzi ya kisera na kisheria ya kushinikiza kampuni za simu ziorodheshwe soko la mitaji DSE, yamekuwa na mafanikio hafifu hata kuhitajika kubadilisha sheria kwa sababu sera mbovu za kiuchumi zimepunguza uwezo wa Watanzania kutumia fursa hizo kuwekeza. Ndio sababu majuzi kampuni ya Vodacom imejaribu kuongeza muda kwa IPO pamoja na sasa kuruhusu wasio wazawa kununua hisa hizo.
3. KUPUNGUA KWA MIKOPO YA BENKI ZA BIASHARA KWA SEKTA MUHIMU ZA KIUCHUMI.

Sekta binafsi kama injini ya Uchumi inategemea zaidi mikopo kugharamia uwekezaji. Hata hivyo, takwimu za BoT kuhusu mwenendo wa mikopo kwa sekta binafsi kwa ulinganisho wa mwaka 2015 dhidi ya 2017, ni kielelezo tosha kwamba uchumi umevurugwa.

Ndani ya miaka miwili kiwango cha mikopo isiyolipika (Non Performing Loans – NPL) kilivuka wastani wa asilimia 5% na kufikia asilimia 8%. Bank kadhaa zilifungwa kutokana na tatizo la mikopo isiyolipika na zilizobaki kuyumba vibaya kutokana na mdodoro wa biashara uliosababisha ongezeko la mikopo isiyolipika.

Ni hali hii ilisiyosababisha wawekezaji na wafanyabiashara kuhofu kuchukua mikopo ya kibiashara kwa upande mmoja na bank nazo kuhofu kutoa mikopo kwa wafanyabiashara na hivyo kuongeza vikwazo vya upatikanaji mikopo kwa sekta binafsi kama njia ya kukabili tatizo la uwepo wa wimbi la mikopo isiyolipika kutokana na kuyumba kwa biashara .

Takwimu hapa chini ambazo chanzo chake ni BoT ni ushahidi wa wazi wa namna sekta binafsi inavyoangamia.

ULINGANISHO WA KIASI CHA MIKOPO KWA MWAKA 2015 VS 2017
chade2.png

Chanzo: BoT Monthly Economic Review June 2015 & June 2017.

  1. MANUNUZI NA MAUZO YA KIBIASHARA NJE YA NCHI.
4.1 Manunuzi Nje (Imports)
Manunuzi ya bidhaa na huduma nje yalifikia $13,305.2M mwisho wa Mei 2015 ukilinganisha na manunuzi ya $9738.8M Mei 2017 sawa na tofauti ya $3566.4 (sawa na Tsh 7,489.44bn.)
chade.png

Chanzo: BOT monthly economic review; June 2015 & June 2017

4.2 Mauzo ya Bidhaa Nje (Exports)

Mauzo jumla ya bidhaa na huduma nje ni kigezo muhimu katika kupima Uchumi unaokuwa au kusinyaa. Kipindi cha Mei 2017, mauzo jumla yalikuwa $ 8,774.9M ukilinganisha na mauzo ya $9,454.5M kipindi kama hicho mwaka 2015. Hii ni sawa na tofauti ya $679.9M au Shilingi Trilioni 1.5
Hivyo biashara ya nje kwa ujumla (import & export) imeanguka kwa takribani shilingi Trilioni 10. Hiki ndicho IMF imesisitiza kuwa uchumi wa Tanzania unapita katika kipindi wataalamu wa uchumi wanaita SOFT PATCH, yaani unachechemea.

Mwenendo huu unathibitisha msimamo wa taasisi ya ujasusi kiuchumi ya Economic Intelligency Unit kwenye ripoti yao kwa Tanzania Julai 2017 inayoonesha kwamba uchumi wa Tanzania unatarajiwa kuporomoka ukuaji wake na kufikia asilimia 5.2% ifikapo mwaka 2021.

5.0 DENI LA TAIFA

5.1 DENI LA NJE
Deni la nje kufikia Mei 2017 lilifikia $17,907.2M kutoka deni la $14,762.7M sawa na ongezeko la deni la nje kwa kiasi cha $3,144 au shilingi Billion 6,916bn kwa miaka miwili tu.

  1. DENI LA NDANI
Deni la ndani kufikia Mei 2017 lilifikia 11,353bn kutoka 7,707.3bn mwaka 2015 sawa na ongezeko la shilingi 3,645.7bn
Kwa ujumla kwa miaka miwili, kuanzia Mei 2015 mpaka Mei 2017, deni la taifa limeongezeka kwa zaidi ya shilingi 11,493bn. (Trilioni 11.5).
Serikali imeendelea kudai kuwa deni ni himilivu. Badala ya kuelekeza nguvu na mikakati mikubwa kwenye uwekezaji, Serikali ya Magufuli inapambana na wawekezaji, wote wa nje na ndani. Mahusiano baina ya sekta binafsi na Serikali yako mashakani zaidi kuliko wakati mwingine wowote.

Investors Confidence inatoweka kwa kasi. Ni vigumu sana hata kwa wawekezaji wa ndani kuchukua “Risk” kuwekeza katika nchi isiyoheshimu demokrasia, Katiba, Utawala wa Sheria, Kanuni, mikataba na hata utu. Tunakimbiwa na tutakimbiwa zaidi, huku tukimpongeza “Bwana Mkubwa” kuwa anainyoosha nchi!

Bila kuongeza uzalishaji, deni hili litaielemea Serikali kama hadi sasa halijailemea. Kwa sasa, tunatumia asilimia 80 ya makusanyo yote ya kodi kulipa mishahara na deni la Taifa tu. Tunabakia na asilimia kama ishirini ya makusanyo kuendesha Serikali na kutekeleza miradi ya maendeleo. Hali hii haikubaliki na ni muujiza kutoka kwenye umasikini.

6.0 MAKENIKIA

Rais Magufuli aliunda Kamati Mbili maarufu kama ‘kamati za Makenikia 1&2. Taarifa za Kamati hizi zimezua sintofahamu kubwa ya uchumi na uwekezaji katika Taifa.

Kwa lengo jema la kuwa wawazi “Transparent” katika sakata hili, ni vyema Serikali ikaweka wazi taarifa hizi kwa ujumla wake na siyo vipande vipande.

Ni jambo jema kulinda rasilimali za nchi, hata hivyo ulindaji huo hauhitaji kuwa wa pupa na papara. Unahitaji kufanywa kwa umakini na tahadhari kubwa ili faida yake kwa nchi iweze kuwa ya uhakika.

Ripoti hizi zimeweka rekodi za kidunia za uzalishaji madini hususan dhahabu, na hasa baada ya TRA kuiandikia ACACIA madai ya kodi yanayofikia kiwango cha shilingi Trilioni 425 au Dola za Marekani bilioni 190.

Taarifa hizi zimesambazwa katika vyombo mbali mbali vya habari vya kimataifa, ikiwemo BBC, CNN, Bloomberg n.k sambamba na mitandao kadhaa ya kimataifa yakiwemo majarida na magazeti makubwa duniani. Kutangazwa huku ni kwa misingi ya kejeli zaidi, ikihoji kuna uwezekano gani wa kampuni kudaiwa kodi ambayo ni zaidi ya mara 10 ya bajeti ya Taifa husika?

Serikali isikae kimya. Kukaa kimya ni kukubali kebehi hizi. Kama ilivyokuwa na ujasiri wa kutangazia Taifa riport zilipotoka, iwe tayari kuitangazia hata na dunia kwa kuweka hadharani hiyo siri yenye sifa ya kuingia kwenye “Guiness Book of Records”.

  1. HITIMISHO
Kwa ujumla mwendo wa uchumi (economic trend) wetu ni mbaya. Mauzo ya nje yameporomoka, Manunuzi kutoka nje yameporomoka, Mikopo sekta binafsi imeporomoka, Deni la Taifa linapaa kuliko kipindi chochote, Biashara zinafungwa kuliko kipindi chochote, Bado Serikali inasema Uchumi unakua, ni wito kwa wachumi kufanya uchunguzi wa kina tusiingie kwenye mkumbo wa kupika takwimu za uchumi ili kupata umashuhuri wa kisiasa.

Siku zote tukumbuke kuwa mficha ugonjwa, kifo humuumbua. Wananchi sasa wanaumizwa kihakika na hali ngumu ya maisha. Serikali inapashwa kuelewa hili na kuweka haraka mpango mkakati wa muda mfupi wa kurekebisha mserereko huu.

Taifa halipaswi kubweteka na matukio kama ya Makenikia, Ufisadi wa Escrow account na mengineyo. Aidha kupambana na ufisadi pekee hakuwezi kuwa tiba ya uchumi unaoporomoka.

Kwa miaka miwili ya Rais Magufuli ameangusha biashara yenye thamani ya zaidi ya shilingi Trilioni10.
 
Heshima kwenu wakuu,

Leo kuna Mkutano wa CHADEMA na Wanahabari unaofanyika Upanga kwenye Hotel ya Courtyard, Protea.

Huu ni Mkutano wa Uongozi wa Juu wa Chama na Wahariri pamoja na Waandishi wa Habari waandamizi, utakafanyika kuanzia Saa 04:30 asubuhi, katika hoteli ya Protea Courtyard

Hii inatokana na uamuzi ambao Kamati Kuu ya CHADEMA imeufanya katika mkutano wake wa siku mbili; tarehe 29-30 Julai, 2017 katika Hotel ya Double Tree, jijini Dar es Salaam.

Maeneo ambayo yamejadiliwa na kuridhia kuchukuliwa kwa hatua ni;

1. Hali ya mwenendo wa siasa katika nchi na ukandamizaji wa demokrasia unaofanywa na serikali ya awamu ya tano.

2. Kuporomoka kwa uchumi na hali ngumu ya maisha kwa Watanzania

3. Kamata kamata inayoendelea kufanywa na vyombo vya dola dhidi ya viongozi, wanachama na wafuasi wa CHADEMA maeneo mbalimbali nchi nzima.

Nimefika maeneo haya, ntahakikisha nawahabarisha kila kinachojiri. Karibuni.
c7368ec9834a876b61e07dd40c93ac9e.jpg


=====

UPDATES:
Mungu ibariki chadema
 
Asante Mkuu tupe full info....tuko tuned hapa hatubanduki. Wenye nchi wako protea courtyard.
Heshima kwenu wakuu,

Leo kuna Mkutano wa CHADEMA na Wanahabari unaofanyika Upanga kwenye Hotel ya Courtyard, Protea.

Huu ni Mkutano wa Uongozi wa Juu wa Chama na Wahariri pamoja na Waandishi wa Habari waandamizi, utakafanyika kuanzia Saa 04:30 asubuhi, katika hoteli ya Protea Courtyard

Hii inatokana na uamuzi ambao Kamati Kuu ya CHADEMA imeufanya katika mkutano wake wa siku mbili; tarehe 29-30 Julai, 2017 katika Hotel ya Double Tree, jijini Dar es Salaam.

Maeneo ambayo yamejadiliwa na kuridhia kuchukuliwa kwa hatua ni;

1. Hali ya mwenendo wa siasa katika nchi na ukandamizaji wa demokrasia unaofanywa na serikali ya awamu ya tano.

2. Kuporomoka kwa uchumi na hali ngumu ya maisha kwa Watanzania

3. Kamata kamata inayoendelea kufanywa na vyombo vya dola dhidi ya viongozi, wanachama na wafuasi wa CHADEMA maeneo mbalimbali nchi nzima.

Nimefika maeneo haya, ntahakikisha nawahabarisha kila kinachojiri. Karibuni.
c7368ec9834a876b61e07dd40c93ac9e.jpg


=====

UPDATES:
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom